MASTORI YA OSCAR: Huu uchawa na ushujaa unasaidia mpira wetu?

SIKU hizi mtu yeyote anayesifia serikali anaitwa chawa. Na mtu yeyote anayepinga serikali anageuka kuwa shujaa. Siku hizi kila mtu anayesifia tabaka la juu anaitwa chawa. Wakati yule anayetetea tabaka la chini anaitwa shujaa. Ndiyo maisha tunakoyapeleka. Ndiyo uandishi wetu unakoelekea.

Ukisimama na kutetea uongozi wa Barbara Gonzalez pale Simba na Mohammed Dewji wewe ni chawa wao. Ukijitokeza na kutetea uongozi wa Hersi Said na udhamini wa Ghalib Said Mohammed pale Yanga wewe ni chawa wao. Shujaa ni yule anayekosoa kila kitu na wakati mwingine bila hata ushahidi wa kutosha. Ndiko uandishi na utangazaji wa mpira hapa nchini unakoelekea.

Uandishi wa michezo na utangazaji siku hizi ni ama ukubali kuwa chawa au shujaa. Kumekuwa na viashiria vya chuki baina ya watawala na watawaliwa. Kumekuwa na viashiria vya chuki baina ya walio juu na wengi ambao wako chini. Chuki imekuwa kubwaa.

Ukitaka kumtetea hata kwenye ukweli Mohammed Dewji kila mtu anakuona chawa. Tunawachukia wakati mwingine viongozi wetu na watu waliotuzidi bila sababu yoyote.

Tunajificha kwenye kivuli cha uzalendo. Tunajificha kwenye kivuli cha ushujaa. Tunaacha taratibu miiko ya uandishi na kuwa wanaharakati. Kuwachukia bila sababu watu waliofanikiwa hakutabadilisha chochote kwenye maisha yako.

Tukubaliane kutokubaliana. Mpira una ‘engo’ nyingi. Unaweza kutoa maoni yako kuwa bao la kwanza la Aziz KI lilikuwa bora kuliko lile la Pape Ousmane Sakho na ukawa sawa tu. Hakuna tatizo. Lakini akitokea mwingine na kusema bao la Moses Phiri ndilo bora zaidi anaitwa chawa. Uandishi na utangazaji wa mpira wetu ndivyo ulivyo kwa sasa. Wapo baadhi ya waandishi wa habari za michezo ambao wamechagua kutetea mashabiki tu na kuwaumiza viongozi. Sioni tatizo hata kidogo kama kuna ukweli. Lakini ni kundi hilohilo ambalo halitaki kuona mtu akitetea viongozi. Ukitetea unaitwa chawa. Tufike mahali tukubali kutokubaliana. Mchezo wa mpira wa miguu ni mchezo wa maoni. Tukubali kupokea maoni ya wenzetu hata kama hayakubaliani na yale yetu. Mitandao ya kijamii ni mizuri sana. Kuna maisha mazuri ikitumika vizuri. Siku hizi baadhi yetu pia tunaitumia vibaya. Watu wanajaribu kuwasema watu wengine ovyo ili wapate umaarufu. Kujulikana kunakuja kwa kufanya kazi kwa bidii na weledi mkubwa. Ukifanya kazi kwa bidii na weledi mkubwa watu watakutambua tu.

Hata ukitazama kwa picha kubwa unaona namna mafanikio yanavyoleta chuki. Leo ukisifia kitu kilichofanywa na serikali kundi kubwa la tabaka la chini litakuona umekuwa chawa. Kundi kubwa la watu wa chini wataona unatafuta uteuzi. Tumekuwa waandishi na watangazaji ambao tunapotosha mtazamo chanya wa jamii juu ya watu waliofanikiwa. Siku hizi hata ukisema Yanga ndiyo bingwa mara 28 wa Ligi Kuu Bara unaitwa chawa. Siku hizi hata ukisema Mohammed Dewji ndiye tajiri mwenye mafanikio makubwa uwanjani kuliko mtu mwingine yeyote baadhi ya watu wanakuona chawa tu. Ushujaa kwenye uandishi na utangazaji wa zama hizi umekuwa ni kwenye kutukana watu na kuwavunjia heshima. Ushujaa siku hizi ni kupinga kila kitu. Soka letu litachelewa sana kama uandishi na mitazamo yetu itaendelea kuwa ya “mashujaa na machawa”. Hakuna dunia yoyote watu wanakokubalina kwenye kila mtazamo. Hakuna. Mitazamo tofauti yenye nia njema ya kujenga itaisaidia sana mpira wetu. Kutetea serikali mahali ilipofanya vizuri sio dhambi. Kukosea TFF mahali walipokosea sio dhambi. Kusifia Yanga mahali walipopatia sio dhambi.

Wachambuzi, waandishi, wanaharakati, mashujaa na machawa ni lazima watu wapeane heshima na nafasi. Tukubali kusikiliza maoni ya watu wengine hata kama hatuyapendi. Mpira ndiyo unataka hivyo. Tukubali kutofautiana. Uandishi mzuri utasaidia kuwaleta mashabiki karibu. Simba na Yanga wanaendelea kuwa watani.

Hakuna kosa lolote kwa kuwakosoa matajiri na tabaka la juu. Wakikosea mahali bila shaka yoyote wanatakiwa kuambiwa ukweli. Lakini tusijenge chuki kwa watawala. Tusiwachukie watu wenye mawazo tofauti na yetu. Mpira una ‘engo’ nyingi sana za kuelezewa. Tukubaliane kutokubaliana.

Mitandao ya kijamii isitufanye kuwehuka na kuwakosea watu kwa sababu tu ya kutaka ‘komenti’ nyingi. Misingi ya taaluma yetu haitutaki kufanya hivyo. Mtazamo wako hauwezi kuwa mtazamo wa dunia. Mtu leo akisifia serikali watu wa chini watamuona kama anajipendekeza. Watamuona kama chawa tu. Sio kweli.

Ni lazima waandishi wenzangu tubadilike kidogo. Kuwasema kila siku kwa mabaya Simba hakukufanyi kuwa mzalendo. Kuwasema kila siku GSM haupewi cheti mahali popote. Sifa kubwa ya uandishi ni kutafuta ukweli na sio kuona kila siku maoni yako ni kitabu kitakatifu.