Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mastaa Yanga, Simba waliowahi kushuka daraja

MASTAA Pict

Muktasari:

  • Sasa wakati hayo yakiendelea, wapo mastaa wakali kibao waliowahi kutamba na timu kubwa nchini za Yanga, Simba na hata Azam ambao wamewahi kushuka daraja na klabu walizokuwa wanazichezea kama Mwanaspoti linavyowaelezea baadhi yao.

WAKATI Ligi Kuu Bara ikitarajiwa kumalizika Juni 25, 2025 kwa mechi ya Dabi ya Kariakoo  kati ya wenyeji Yanga dhidi ya Simba, lakini tayari timu mbili za KenGold na Kagera Sugar zimeshuka daraja baada ya kutokuwa na mwendelezo mzuri katika ligi.

Sasa wakati hayo yakiendelea, wapo mastaa wakali kibao waliowahi kutamba na timu kubwa nchini za Yanga, Simba na hata Azam ambao wamewahi kushuka daraja na klabu walizokuwa wanazichezea kama Mwanaspoti linavyowaelezea baadhi yao.


OBREY CHIRWA

Raia huyo wa Zambia amewika na timu mbalimbali hapa nchini zikiwemo Yanga iliyomsajili kwa mara ya kwanza Julai 1, 2016, akitokea FC Platinum ya Zimbabwe, kisha akajiunga na matajiri wa Jiji la Dar es Salaam, Azam na baadaye akatua Namungo.

Nyota huyo amekuwa na bahati mbaya kwa sababu msimu huu alikuwa akiichezea Kagera Sugar, ingawa dirisha dogo la Januari 2025 alijiunga na KenGold kwa mkopo ili kuongeza nguvu, lakini jambo la kusikitisha timu zote alizocheza zimeshuka.


BERNARD MORRISON

Morrison ni miongoni mwa nyota waliojizoelea umaarufu tangu alipojiunga na Yanga, Januari 15, 2020, akiwa mchezaji huru baada ya kuachana na DC Motema Pembe ya DR Congo akiwahi kuwachezea pia mahasimu wao wakubwa hapa nchini, timu ya Simba.

Nyota huyo ameshuka daraja na KenGold aliyojiunga nayo dirisha dogo la Januari akiwa mchezaji huru baada ya kukaa nje ya uwanja kwa zaidi ya miezi sita kutokana na majeraha tangu alipoachana na FAR Rabat ya Morocco, Julai 1, 2024.

MAST 01

KELVIN YONDANI

Beki huyo mkongwe aliyewika na timu mbalimbali ikiwamo Simba na Yanga huku akifananishwa na aliyewahi kuwa nyota wa zamani wa Manchester United ya England, Nemanja Vidic ameendeleza rekodi nyingine mbaya baada ya kushuka daraja akiwa na KenGold.

Yondani aliyeichezea pia Polisi Tanzani, ameandika rekodi mbaya kwa misimu miwili mfululizo ya Ligi Kuu, kwani uliopita alishuka daraja na Geita Gold na huu ameshuka na KenGold aliyojiunga nayo dirisha dogo la Januari 2025.


ERICK KABAMBA

Wengi wanamkumbuka nyota huyu wakati alipojiunga na Yanga msimu wa 2019-2020, akitokea Buildcon ya kwao Zambia, japo safari hii alirejea tena hapa nchini na kujiunga na KenGold dirisha dogo la Januari 2025, ambayo tayari imeshuka daraja.

Kabamba alijiunga na KenGold kwa ajili ya kuongeza nguvu katika kikosi hicho baada ya kuachana na Wakiso Giants ya Uganda, ingawa licha ya matarajio makubwa yaliyobebwa kwake, lakini mambo yameenda tofauti na timu hiyo kushuka pia daraja.

MAST 02

DEOGRATIUS MUNISHI ‘DIDA’

Kipa huyo aliyewika na timu mbalimbali kubwa hapa nchini zikiwemo za Yanga, Simba na Azam kwa sasa anaichezea Geita Gold inayoshiriki Ligi ya Championship, ingawa ni miongoni pia mwa nyota walioshuka daraja akiwa na timu mbili.

Dida aliyezichezea pia Mtibwa Sugar na University of Pretoria ya Afrika Kusini, alishuka daraja akiwa na Lipuli  ya Iringa msimu wa 2019-2020, kisha msimu wa 2020-2021 akashuka tena na Ihefu ambayo kwa sasa ni Singida Black Stars.


WILLIAM LUCIAN

Nyota huyo alikuwa akifananishwa na beki wa zamani wa klabu za Arsenal, Chelsea na Tottenham Hotspur zinazoshiriki Ligi Kuu England na timu ya taifa ya Ufaransa, William Eric Gallas, jina alilopewa kipindi akikichezea kikosi cha Simba.

Lucian aliyetamba pia akiwa na timu mbalimbali ikiwemo Geita Gold, alikuwa ni miongoni mwa nyota walioshuka daraja kipindi hicho akiichezea Mwadui  ya mjini Shinyanga iliyoshuka msimu wa 2020-2021, baada ya kuburuza mkiani na pointi 19.

MAST 03

PAUL NGALEMA

Ngalema aliyewika na timu za Simba, Ruvu Shooting, Majimaji, Ndanda na Lipuli, aliwahi kushuka daraja msimu wa 2020-2021 wakati akiichezea JKT Tanzania kabla ya kikosi hicho kurejea tena Ligi Kuu msimu wa 2022-2023.


NOVART LUFUNGA

Beki huyo wa kati wa zamani wa Simba, aliwahi kushuka daraja msimu wa 2020-2021 akiwa na Gwambina baada ya kumaliza nafasi ya 16 na pointi 35 kufuatia kucheza mechi 34, akiwahi kuzichezea pia JKT Mgambo, African Sports na Lipuli.


MRISHO NGASSA

Winga huyo aliyejizoelea umaarufu mkubwa hapa nchini kutokana na kipaji alichokuwa nacho, aliwahi kushuka pia daraja msimu wa 2020-2021 wakati huo akikichezea kikosi cha Gwambina kilichokuwa Misungwi, Mwanza.

Ngassa aliyewahi kucheza pia Free State Stars ya Afrika Kusini, amezichezea Yanga na Simba kwa mafanikio, huku nyota huyo akikumbukwa zaidi msimu wa 2010-2011 alipoibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara akiichezea Azam alipofunga mabao 18.

MAST 04

JORAM MGEVEKE

Mgeveke aliwahi pia kuichezea Simba ingawa beki huyo wa kati alishuka daraja msimu wa 2020-2021, akiichezea Mwadui ya Shinyanga baada ya kikosi hicho kuburuza mkia na pointi 19, huku akiwa nahodha na kushindwa kukinusuru katika Ligi Kuu Bara.


JABIR AZIZ STIMA

Stima aliyeichezea Simba iliyomsajili kutoka Ashanti United ya Ilala kisha baadaye akajiunga na Azam, Mwadui, Ruvu Shooting na Ndanda alishuka daraja msimu wa 2020-2021 wakati huo akikichezea kikosi cha maafande wa JKT Tanzania.


MWINYI KAZIMOTO

Kazimoto aliyewahi kuichezea Simba kisha Al-Markhiya ya Qatar, alikuwa ni miongoni mwa viungo bora hapa nchini, japo msimu wa 2020-2021 ulikuwa mbaya kutokana na kuandamwa na majeraha, huku pia JKT Tanzania aliyoichezea ikishuka daraja.

MAST 05

RAPHAEL DAUDI LOTH

Kiungo huyo kwa sasa anaichezea Coastal Union aliyojiunga nayo Januari 2025, baada ya kuondoka Namungo, huku akiwahi kuzichezea Mbeya City na Yanga, japo alishuka daraja msimu wa 2020-2021, akiichezea Ihefu ambayo ni Singida Black Stars kwa sasa.


PAUL NONGA

Mshambuliaji huyu wa zamani wa Yanga aliyekuwa kocha wa utimamu wa mwili ‘Fitness Coach’ wa Geita Gold msimu uliopita, alishuka daraja msimu wa 2020-2021, akiwa na Gwambina aliyoifungia mabao sita ya Ligi Kuu Bara ambayo hayakusaidia.


DANNY LYANGA

Lyanga aliyeichezea Simba, kwa sasa anakichezea kikosi cha Mashujaa alichojiunga nacho dirisha dogo la Januari 2025, akitokea kwa maafande wenzao, JKT Tanzania ambayo alishuka nayo daraja msimu wa 2020-2021, licha ya kuifungia mabao 10.