Masau Bwire: Simu 9, Magrupu 286 ya WhatsApp

KATIKA watu wenye mbwembwe kwenye soka la Tanzania kwa sasa ni Ofisa Habari wa Ruvu Shooting, Masau Bwire. Ni miongoni mwa watu wenye vitu adhimu ambavyo vimetokea kuwakosha mashabiki wengi nje ya uwanja na hata kunogesha ushindani wa Ligi Kuu hasa kwa mechi zinazohusisha timu yake.

Mwanaspoti limefanya naye mahojiano maalumu na kueleza mambo mengi kuhusiana na yeye, timu yake pamoja na Ligi Kuu msimu huu. Hivi unajua ana simu ngapi?

Msemaji huyo anasema kumiliki kwake simu tisa kumetokana na waandishi wa habari, hivyo aliona achukue uamuzi huo ili iwe rahisi kwao kufanya naye mawasiliano.

“Ujue kuna muda wanahabari walikuwa wakinipigia simu na kuuliza swali sasa wakati nafafanua unakuta simu yake inakatika kiasi cha kushindwa kumaliza mazungumzo yetu. Nililichukua hilo na kuona ufumbuzi wake ni kuwa na kila laini ya mtandao.

“Nina laini tisa za mitandao tofauti, sasa mwanahabari akiwa mtandao fulani nampa namba inayoendana na yeye ili tumzungumze mpaka atakapotosheka,” anasema.

Licha ya kumiliki simu tisa, Bwire anasema ni ngumu kuishiwa bando kwenye simu hizo na amekuwa akiweka la kutosha, “siwezi kukueleza natumia bei gani kwa sababu kila mtandao una vifurushi vya gharama tofauti labda nianze kupiga hesabu.”

Hivi karibuni, Bwire anasema amepoteza simu karibu tatu kwenye mazingira tofauti.

“Bahati nzuri namba huwa nahifadhi kwenye google, hivyo nikiibiwa nanunua nyingine na mawasiliano yanaendelea bila tatizo lolote. Kuna moja niliibiwa barabarani kibaka alikwapua, nyingine uwanjani kwenye msongamano na mashabiki ambao walinizonga mpaka nikafikia kuwatishia.”


MAGRUPU WHATSAPP

Kati ya simu tisa za Bwire zipo nne ambazo ni za kisasa na moja kati ya hizo ipo yenye magrupu 286 ya Whatsapp.

“Huwa sizimi data, muda wote simu zangu huwa na chaji ni mara chache kukuta zimezima na zikizima zinazima zote kwa pamoja,” anasema.

“Nimekuwa nikijitahidi kupitia meseji na kujibu kila ambayo inahitaji ufafanuzi wangu japo muda mwingine huwa changamoto kutoka na wingi wake. Mara nyingi usiku nikiwa kitandani ndio napata muda wa kuzitazama meseji katika hayo magrupu na hata jambo langu tulivu nalifanya usiku mnene.”


NAFASI YAO KWENYE LIGI

Akizungumzia timu yake kwenye msimamo wa Ligi Kuu, Bwire anasema: “Kama sisi ni upepo mbaya tu tunaupitia, lakini timu yetu ni nzuri sana na ukishinda mechi moja unapanda juu, hivyo mpaka sasa hakuna ambaye ana uhakika wa ubingwa. Mechi bado nyingi sana.

Bwire anasema Ruvu Shooting ina uwezo wa kumaliza nafasi tano za juu na kushiriki kimataifa kwa kuwa uwezo huo inao.

Anasema yeye sio muumini wa mapro wengi katika timu za Ligi Kuu kwa kuwa hasara kubwa inakuja katika nchi.

“Ukiangalia wachezaji ambao wanaitwa Taifa Stars asilimia kubwa ni wale wa Simba, Yanga na Azam ambazo ndizo timu zenye mapro kibao, sasa shida inakuja timu ya Taifa tunakosa wachezaji kwa kuwa hata hao wazawa wa hizo timu wengi hawapati nafasi,” anasema Bwire.

Anasema Ruvu Shooting wana imani ipo siku watapata uwakilishi wa michuano ya kimataifa na wataiwakilisha vyema nchi wakiwa na nyota wazawa.


UBAGUZI WACHEZAJI

“Timu za Taifa zikiitwa unajiuliza wanatumia vigezo gani kuwaita? Maana wachezaji wakiwa timu ndogo hawaonekani, lakini huku wanakuwa bora ila wakienda Simba na Yanga tu siku hiyo hiyo wanaitwa Stars nashindwa kupata jibu,” anasema.

“Mfano halisi Oscar Joshua alitokea kwetu kwenda Yanga, lakini alivyotua tu Jangwani akaanza kuitwa timu ya Taifa na Hassan Dilunga naye alikuwa kwetu alipoenda Yanga sasa Simba akaanza kuitwa. Sasa najiuliza wanaochagua wachezaji wanatazama mechi za Simba na Yanga pekee au inakuwaje?”


GSM KUJITOA LIGI KUU

Hivi karibuni Bilionea Gharib Said ‘GSM’ alijiondoa kudhamini ligi licha ya timu kuanza kuvaa nembo yake katika mabega ya jezi zao isi-pokuwa Simba pekee ambayo iligomea udhamini huo.

“Nakumbuka siku sio nyingi kuna timu zilikuwa zinashindwa hadi kusafiri, kulipa mishahara na hata nyingine zilisafiri na ubwabwa kupunguza gharama za vyakula. Sasa anapojitokeza mtu kama huyu halafu tukampoteza ni majonzi makubwa,” anasema Bwire.Anasema wao Ruvu Shooting huo muda wote ambao walikuwa wakivaa jezi zenye nembo ya GSM na kuitangaza hawakuwahi kupata pesa na bado wataendelea kuvaa kwa kuwa jezi zao ni gharama mpaka kuagiza mpya haiwezi kuwa leo.

“Sisi jezi hatununui Kariakoo tunaagiza nje, sasa kitendo kilichotokea ni hasara kubwa kwa klabu wanatakiwa kutuangalia sisi timu za chini wanatusaidiaje hususan katika suala la jezi maana hauwezi kubandua logo begani, hapana, tunaendelea kumtangaza tu bila faida jambo ambalo sio sawa.”


SIMBA, YANGA MABATINI

Simba na Yanga wamecheza kwenye viwanja vidogo kama Manungu kule Morogoro hivyo hata Ruvu Shooting na wao wanataka mechi zao na vigogo hivyo vya soka nchini zipigwe kwao Mabatini, Pwani.

Bwire anasema anaamini hakuna kinachoshindikana kufanyika michezo hiyo Mabatini kwa kuwa kamati za ulinzi na usalama zina uwezo wa kulinda amani na mchezo ukachezwa vilivyo bila kuwa na shida yoyote.

“Tutaandika barua (TFF) ili msimu ujao tena tutumie uwanja wetu wa Mabatini ambao una sifa zaidi hata ya Manungu na sisi watu wetu wa Mlandizi wapate nafasi ya kuwaona nyota wao wakizichakaza Simba na Yanga,” anasema.


VIGOGO WANAMTAKA

Bwire anasema timu zote kubwa hapa nchini Simba, Yanga na Azam kwa nyakati tofauti zimehitaji nafasi ya yeye kuwa msemaji wao.

‘’Nakumbuka kipindi hicho nilikuwa Corefa (Chama cha Soka Pwani), Simba walinipigia (simu) nikawaambia siwezi. Ndipo nilipomsikia Haji Manara ametangazwa, niliamua kumpigia simu na kumpongeza na alifanya vizuri sana kazi hiyo,” anasema Bwire.

Baadaye Yanga wao walimtumia mwandishi mkubwa wa habari ili azungumze naye, lakini hakuwa tayari sawa na Azam FC ambao mtendaji mkuu wa zamani, Saad Kawemba alimfuata mwenyewe nako aliwagomea.

‘’Huyo mwandishi walidhani niko karibu naye, alinipigia simu na kuniambia unatakiwa kusema ndio ili leoleo utangazwe kuwa msemaji wa Yanga, nikamwambia waambie siko tayari. Siku nyingine nilikutana na Mkwasa (Charles) akiwa katibu (mkuu) wa Yanga akaniambia tena nikamwambia hapana.

‘’Nilijaribu kuwauliza waandishi wenzangu Jesse John na hayati Alex Kashasha wakanitania nenda kachukue mpunga wewe, mimi hapo akili yangu inajua inataka nini,” anaongeza Massau akisisitiza kwamba alikataa nafasi hizo kutokana na kuelewa umuhimu wake ndani ya Ruvu Shooting na alikotoka na timu hiyo ambayo ni zaidi ya fedha za harakaharaka kwa timu za Kariakoo.


JEZI/BARAKOA YA SIMBA

Bwire anasema siyo dhambi kuvaa vitu hivyo kwa kuwa mpira sio uhasama, bali ni burudani.

“Mimi nilipewa jezi ya Simba kutoka kwa Vunjabei mwenyewe, alinipatia zawadi sasa naikataaje hata Yanga wakinipa zawadi ya jezi yao nachukua tu siwezi kuikataa, halafu utasikia…sijui navaa barakoa ya Simba sasa kama kuna sehemu nimeenda inatakiwa kuvaa barakoa na ikawepo hata ya kampuni nyingine nikivaa ni kosa?

‘’Napenda sana timu ikiwa ina majukumu ya kuwakilisha nchi mimi naisapoti. Hata hao Yanga walikuwa wanacheza na moja ya timu kutoka Ethiopia nilihamasisha watu waisapoti niliandika kwa kirefu sana, nakumbuka ilikuwa mwaka 2017,” anasema Bwire.

Anasema kitendo cha mtu kupiga picha na watu fulani ikaonekana kuwa uko na watu hao sio vizuri kwa kuwa kuna maisha nje ya mpira ambayo kila mtu anayaishi.

“Nakumbuka barakoa ya Simba nilienda kwenye msiba wa Simba, kufika pale unatakiwa kuvaa barakoa na mimi sikuwa nayo ilinilazimu nivae hiyo ya Simba ambayo nilipewa msibani na nisingeweza kuikataa,” anasema.


KUMBE NI MWAMUZI

Kama hujui ndivyo Mwanaspoti linakujuza kumbe Bwire mbali na uandishi wa habari, ualimu pia ni mwamuzi.

“Mie ni mwamuzi pia. Najua vilivyo sheria sasa huwa nashangaa baadhi ya matukio ambayo waamuzi wanayafanya lakini tunanyamaza tu kwa kuwa hata sisi uwezo tunao,” anasema.


Usikose mwendelezo wa Makala hii kesho kwenye Mwanaspoti akifafanua mambo kibao matamu