Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mapigo matano yaliyoipasua hisia Simba

Muktasari:

  • Hii ilitokana na kuruhusu sare ya bao 1-1 dhidi RS Berkane ya Morocco katika mchezo wa pili wa fainali wa michuano hiyo.

JIONI ya Jumapili kwenye Uwanja wa Amaan Complex, Zanzibar ilikuwa ni huzuni kwa Watanzania baada ya Simba kushindwa kunyakua ubingwa wa michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Hii ilitokana na kuruhusu sare ya bao 1-1 dhidi RS Berkane ya Morocco katika mchezo wa pili wa fainali wa michuano hiyo.

Mashabiki wa Simba na wadau wote wa kandanda nchini walikuwa na ndoto ya kutwaa ubingwa wa Afrika katika ardhi ya Tanzania, lakini ilififia na kupasua hisia za wana Msimbazi.

Katika mchezo wa awali uliochezwa wiki mbili zilizopita nchini Morocco Simba ilichapwa mabao 2-0 na lihitajika mchezo wa pili wa fainali kushinda 3-0 ili kuwa bingwa au 2-0 na  kumalizana kwa penalti.

Simba ilipambana kwa ujasiri na mashambulizi mengi yaliyopangwa kiufundi na kwa uangalifu, lakini ilifanikiwa mara moja kupata bao kupitia kwa Joseph Mutale dakika ya 17.

Jicho la kitabibu liliona vyema ubora wa Simba katika utimamu wa miili ya wachezaji ilikuwa vizuri kuweza kucheza kwa kiwango, huku pia wakiwa imara kisaikolojia na kihisia.

Walikuwa wameandaliwa vyema kiakili na pia wakiwa na hisia chanya ambayo ilikuwa ni faida iliyoweza kuwapa ari ya ushindi hatimaye kupata bao kipindi cha kwanza.

Vilevile waliweza kupata bao dakika 72, lakini baadaye lilikataliwa baada ya kuonekana kuwa mfungaji Stephen Mutwala aliotea.

Ishara nyingine kuwa Simba ilikuwa timamu kila kona ilipiga vyena na pia ilicheza dakika 40 ikiwa na wachezaji 10 uwanjani  baada ya Yusuph Kagoma  kupewa kadi nyekundu dakika 50. Endapo wachezaji wangekuwa hawana ustahimilivu wa juu wasingeweza kucheza kwa nguvu na kasi huku wakiwa pungufu wakipambana na timu ngumu yenye uzoefu na mashindano hayo. Utulivu wa kimwili na kiakili wa Simba kuweza kuwakabili vizuri wapinzani wao ulichangiwa na shangwe kubwa toka kwa mashabiki ambao walijipanga vizuri kila eneo la uwanja.

Yote haya yaliwafanya wachezaji kucheza kwa hamasa na ari kubwa hata pale walipokuwa pungufu kwao ni kama vile walikuwa wamekamilika.

Kama vile haitoshi kulikuwa na motisha kubwa kwa wachezaji toka katika kwa viongozi wa Serikali na wadau wa michezo.

Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi alizibeba gharama zote za maandalizi katika uwanja wa Amaan.

Wakati Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo, Gerson Msigwa alikuwa na fuko la mamilioni ya Rais Samia Suluhu kama motisha ya zawadi ya goli la mama. Mchezaji anapopata motisha za klabu pamoja na za wadau wengine wa soka zinamfanya kuwa na morali ya hali ya juu. Hii inawafanya kujituma kucheza kwa nguvu na kasi kubwa. Vitu vyote hivyo vilikuwa vinamsukuma mchezaji kucheza kwa ari ya ushindi pasipo kujali ataumia kiasi gani. Kama siyo kucheza pungufu bila shaka kungelikuwa na matokeo mazuri.

Leo jicho la kitabibu limeyatupia mapigo matano ambayo yalipasua hisia za mashabiki na wachezaji. Mapigo hayo ndio ambayo yaliwapa huzuni hatimaye kuifanya wiki hii kuwa ngumu kwao.


1. KUKATALIWA BAO

Tukio la kwanza la maumivu ilikuwa ni kukataliwa kwa bao la pili katika dakika ya 72 lililofungwa na Stephen Mukwala. Mwamuzi alikataa bao ikidaiwa nyota huyo kuwa alikuwa ameotea. Haijalishi uamuzi huo wa refa ni sahihi au si sahihi, lakini pigo hilo liliwapa hisia mbaya ikiwamo hasira, huzuni na majonzi.


2. KADI YA KAGOMA

Kama vile haitoshi likaja pigo lingine dakika 50 baada ya Kagoma kuonyeshwa kadi nyekundu kutokana na mchezo aliomfanyia mchezaji wa Berkane. Tukio hili si tu liliumiza watazamaji, bali hata wachezaji wa Simba walionekana kufaraka. Kipa Moussa Camara na kiungo Fabrice Ngoma walionekana kumshambuliana kwa maneno kiasi cha kutaka kushikana mashati. Ilikuwa ni vigumu kwa shabiki anayetaka timu yake kushinda kukubaliana na uamuzi huo. Lakini ndio mchezo wa soka ulivyo, refa ndiye mwamuzi wa mwisho hata kama VAR imeshauri.

Kadi nyekundu aliyopewa Kagoma katika mchezo muhimu kama ule ni mzigo mkubwa kwa timu. Ni kawaida kwa baadhi kushindwa kudhibiti hisia na hatimaye kujaa hasira na kufanya matendo ya ovyo.


3. BAO LA JIONI

Pigo la tatu lililokuja kipindi kibaya kwani mashabiki walikuwa wameshakata tamaa, ilikuwa ni mara baada ya Berkane kupata bao dakika za nyongeza kupitia mshambuliaji Soumaila Sidibe dakika ya 90+3.

Hamu ya kushangilia ilikatika ghafla na uwanja ulipoa. Zile kelele za kuhamasisha zilipungua. Ilikuwa ni dhahiri hakuna namna yoyote ya kupata mabao dakika zizobaki.


4. FILIMBI YA MWISHO

Pigo la nne ambalo ni kawaida kuumiza hisia za mashabiki na wachezaji ni pale kile kipyenga cha mwisho kinapopulizwa kuashiria kuwa mchezo umekwisha, huku matokeo ni faida kwa Berkane.

Hapa ndipo uliona wachezaji wakikaa, kulala au kusimama na kushika viuno kutoamini kilichotokea. Ni dakika zenye maumivu makali katika hisia za mwanadamu.


5. BERKANE KUBEBA KOMBE

Pigo la tano na la mwisho ni pale unapoona kombe hilo linalabidhiwa kwa timu isiyo ya kwako. Katika hatua hii wachezaji na Mashabiki huathirika kiakili kiasi cha kwamba wengine hudiriki kuitoa medali shingoni na kuweka mfukoni. Huu ndio mpira, mchezo ambao unakupa burudani lakini matokeo yake yanaweza kukupa hisia chanya yaani furaha au hisia hasi yaani huzuni.

Hali hiyo inaweza kuwaganda wachezaji na mashabiki wengine ikapita hata wiki hisia zinakuwa haziko sawa. Ndio maana baadhi ya vijiweni na ofisi kuna baadhi hawana furaha.


CHUKUA HII

Adui aliyekuwa anapambana na Simba si mdogo, RS Berkane - hiyo ni fainali ya tano katika kipindi cha miaka saba kwake. Na imeweka rekodi ya kubeba kombe hilo mara tatu. Licha ya kushindwa kuwafunga, Simba ilionyesha ukomavu na ubora wa hali ya juu. Hii inaleta matumaini katika misimu ijayo si tu kwa Simba hata kwa timu za Tanzania kwa ujumla kung’ara kwenye ramani ya soka la Afrika.

Mchezaji hajengwi tu kwa mazoezi na mafunzo, bali pia anajengwa kisaikolojia na kihisia. Vitu hivi vinamfanya mchezaji kutoa matokeo makubwa bila kutarajia.