MAONI: Sio rahisi kumtengeneza Rulani Mokwena wetu

Mafanikio ya Mamelodi Sundowns kutwaa ubingwa wa Mashindano ya African Football League (AFL) yameonekana kuwakosha wadau wengi wa mpira wa miguu barani Afrika.

Kiwango bora ambacho miamba hiyo ya Afrika Kusini imekionyesha katika mashindano hayo, kimeonekana kuwavutia wengi hasa ukizingatia ilifanya hivyo dhidi ya timu ambazo ni bora barani Afrika na zimekuwa zikifanya vizuri.

Katika hatua ya robo fainali waliitupa nje Petro Luanda ya Angola wakaja kuwatoa Al Ahly ya Misri na katika fainali, wakamaliza shughuli kwa kutwaa ubingwa dhidi ya Wydad ya Morocco.

Na jambo kubwa zaidi, Sundowns imepata mafanikio hayo ikiwa chini ya kocha mzawa tena mwenye umri mdogo tu wa miaka 36, Rulani Mokwena akisaidiwa na mzawa mwenzake, Manqoba Mngqithi.

Mokwena na Mngqithi wametikisa Afrika katika kipindi ambacho imani ya timu nyingi kwa makocha wazawa imekuwa ndogo na nyingi zimekuwa zikiwapa kipaumbele makocha wa kigeni ambao zimekuwa tayari kulipa mamilioni ya fedha ili kupata huduma zao tofauti na wale wa nyumbani ambao gharama za kuwa nao huwa sio kubwa.

Kufuatia mafanikio hayo, hapa nyumbani Tanzania baadhi ya wadau wa soka wameonyesha kutamani timu zetu kufanya kama kile ambacho Mamelodi Sundowns wamekionyesha kwa kumtengeneza Rulani Mokwena.

Wanaamini kwamba wakati umefika kwa makocha wetu wazawa kupewa majukumu makubwa katika timu zetu ili waweze kufikia daraja kama lile ambalo Rulani Mokwena lipo la kutazamwa kama mmoja wa makocha bora na wazuri barani Afrika.

Hata hivyo ni lazima tuambizane ukweli kwamba sio jambo rahisi kwa soka la Tanzania kumpata Rulani Mokwena wake ama awe mmoja au wengi na ili itokee hivyo, kuna kazi kubwa inapaswa kufanyika kama ambayo Mamelodi Sundowns wamefanya hadi wakampata kijana huyo.

Kumtengeneza kocha mkubwa Afrika ni suala ambalo linahitaji juhudi na uwajibikaji wa kundi kubwa la watu ambao utaendana na uwekezaji mkubwa badala ya kuishia kutamani kwa maneno pasipo kuonyesha vitendo.

Kwanza inahitaji utayari binafsi wa kocha au makocha ambao wana ndoto na tamaa ya kufika daraja la juu la taaluma yao na hilo kwa kuanzia ni katika suala la elimu au taaluma ya ukocha kiujumla.

Suala la elimu ni utashi binafsi wa mtu na kufikia daraja la juu la ukocha, hakuna njia ya mkato ambayo mtu anaweza kupita ili afikie vigezo stahiki vya kumfanya awe kocha mkubwa zaidi ya kukubali kupoteza muda na fedha zake kwenye elimu ya taaluma hiyo.

Rulani Mokwena huyo ambaye amekuwa kioo cha makocha wengi wazawa hivi sasa, ana leseni ya ukocha ya daraja A ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) lakini akaona haitoshi akaamua asake leseni ya ngazi za juu ya ukocha ya Umoja wa Vyama vya Mpira wa Miguu Ulaya (UEFA) ijulikanayo kama Uefa Pro License.

Angeweza kuamua kubaki na leseni yake ya CAf tu lakini kitendo cha kuamua kuingia darasani kuitafuta ile ya Ulaya kinaashiria kwamba aliona anahitaji kupata maarifa zaidi kwa watu ambao pasipo shaka yoyote, wamepiga hatua zaidi katika soka kuliko huku Afrika.

Hii inamaanisha kwamba Rulani Mokwena leo hii anaweza kufundisha timu yoyote barani Ulaya pasipo kizuizi chochote cha kielimu au kuhitajika kuingia darasani ili akidhi vigezo.

Na haitakiwi kuishia kwenye elimu tu bali kocha anapaswa kuhakikisha anafuata misingi ya weledi katika usimamizi wa timu na kuepuka kufanya mambo ambayo yatamharibia sifa yeye na taaluma yake na kupoteza imani kwake.

Masuala kama rushwa, upangaji wa matokeo na kuwagawa wachezaji, yanapaswa kuepukwa na kocha kwa vile akiyafanya, yatamshushia heshima na hadhi yake na yatasababisha asiaminiwe.

Baada ya mhusika kuonyesha utayari wake binafsi, timu nayo inapaswa kumsaidia na kumuwezesha kwa hali na mali aweze kutimiza malengo yake.

Uwezeshaji huo kwa kocha unafanywa kwa njia nyingi tofauti na ukamilisho wake una nafasi kubwa ya kumbeba kocha na kumpa mafanikio makubwa na hilo limejidhihirisha katika nyakati na timu nyingi.

Timu inapaswa kumbeba kocha kwa kumhakikishia usajili wa wachezaji bora ambao watakuwa na uwezo mkubwa wa kutafsiri na kufanyia kazi mbinu na mipango ya mechi ya kocha.

Kocha anapokuwa na wachezaji wazuri, anakuwa na nafasi nzuri ya kuwa bora kwa vile anakuwa hatumii nguvu nyingi katika kuwajenga wachezaji na hivyo kupata fursa ya kujifunza mbinu mara kwa mara tofauti na anapokuwa anatumia muda mwingi kuelekeza wachezaji.

Hili tunalishuhudia kwa Mamelodi Sundowns ambayo kikosi chake ni kipana na kinaundwa na kundi kubwa la wachezaji wenye ubora katika kila nafasi jambo linalompa nafasi kocha na benchi lake la ufundi kupata wigo mpana wa uteuzi wa kikosi kulingana na aina ya timu wanayokutana nayo.

Njia ya pili ya timu kumsaidia kocha kupiga hatua ni kuhakikisha inampatia kwa wakati stahiki zake kama vile mishahara, posho, malazi na nyinginezo pasipo kuchelewesha.

Kocha anapopata stahiki zake kwa wakati inasaidia kumfanya awe na utulivu na akili yake kuielekeza katika utimizaji wa majukumu yake na hivyo kumfanya ajitoe zaidi kwa ajili ya timu.

Lakini pia kocha anatakiwa kusaidiwa kwa kupewa benchi bora la ufundi ambalo litamsaidia katika utekelezaji wa majukumu na kazi zake za kiufundi na benchi hilo liwe la watu ambao yeye mwenyewe anaridhia kufanya nao kazi.

Pale Mamelodi Sundowns, Rulani Mokwena ana benchi la ufundi lenye watu wasiopungua 43 ambao wamekuwa silaha kubwa ya mafanikio yake.