Mandonga Kutoka kupiga debe hadi ubondia

Safari ya kujitafuta hadi kujipata ya Karim ‘Mandonga’ Said, haikuwa nyepesi, japo alifanya vitu vingi, lakini wengi walianza kumfahamu kwenye masumbwi ikiwa ni baada ya kutundika glovu kwa miaka mitatu, tangu Julai 2015, alipochapwa kwa TKO na Benki Mwakalebela kwa mara ya kwanza, hakurudi tena ulingoni hadi 2018, akapigwa tena na Juma Misumali.
Aliporejea kwa mara nyingine, Agosti 2021 na kumchapa Omari Mgoa na kutoka sare na Mohamed Mkude, Desemba 2022, bado hakuwa kwenye nyoyo za mashabiki.
Maneno na tambo zake kabla na baada ya pambano la Machi 26, 2022 dhidi ya Magambo Christopher ndivyo vilipendwa na mashabiki, kabla ya pambano hilo, wengi walitaka kuona kama maneno yatakuwa vitendo, ikawa kinyume baada ya kupigwa kwa KO.
Hata hivyo, hakujali matokeo yale, aliendelea na tambo, mashabiki wakimpenda hivyo hivyo na kuanzia hapo 'gari likawaka', miezi minne baadae alichapwa KO nyingine na Shaban Kaoneka.
'Mandonga Mtu Kazi', jina lake hilo la utani linayaangazia maisha yake halisi, anasema hakubagua kazi, alifanya vitu vingi, yote hiyo ikiwa ni kujitafuta katika maisha, alifanya hayo akipambana na haso za mtaani.
“Nimefanya vitu vingi sana hadi kufika hapa, nilikuwa na vipaji tofauti vya Sanaa, lakini sikujua nitasaidiwa na nani katika kutimiza ndoto zangu, hadi nilipopata uelekeo kupitia ngumi," anasema.
Aibukia Msamvu kupiga debe
Anasema baada ya udansa kutokuwa fursa kwake wakati ule, alipata kibarua cha kupiga debe na kupokea wageni kwenye stendi kuu ya mabasi mkoani Morogoro ya Msamvu.
“Nimepiga debe kwa miaka mingi sana, asilimia kubwa ya maisha yangu niliyawekeza pale stendi katika kazi hii, ilikuwa ni kazi ambayo baadae imekuja kunipa chaneli nyingine ya maisha,” anasema.
Anasema akiwa pale, alijiunga kwenye gym ya Msamvu ambayo ilikuwa ikifundisha masumbwi ndipo alikoanzia kujifunza mchezo huo unaompa maisha hivi sasa.
“Nilikuwa na ratiba maalumu ya kazi, asubuhi naingia kwenye kibarua stendi, jioni nakwenda kufanya mazoezi, haikunipa wakati mgumu kwa kuwa gym ilikuwa jirani kabisa na kituo changu cha kazi.
Anasema kazi yake ya kupiga debe aliifanya kwa muda mrefu hadi pale Mwenyezi Mungu alipomuonyesha mwanga wa kujikita kwenye ngumi.
“Ni Mungu tu, naona alitaka kunionyesha kuliko kung’ang’ania sehemu moja, natakiwa sasa nitoke kwenye kupiga debe nijikite kwenye ngumi na sasa ninafanya na filamu ,” anasema na kufafanua.
“Nilikuwa comedian (mchekeshaji), baunsa lakini kabla ya yote nilikuwa dansa.
"Siku moja yalifanyika mashindano ya Afrika Mashariki pale Morogoro, nikajitosa na kuwa dansa bora, hata hivyo hakukuwa na maslahi, nikatoka, nimefanya vitu vingi hadi sasa napigana na kufanya filamu.
Dau lake liko hivi
Mandonga ambaye alipata bahati ya kukubalika kwa mashabiki licha ya kupigwa, na kila alipoendelea kupigwa ndipo aliendelea kufuatiliwa na mashabiki anasema hana dau maalumu.
“Huwa sitangazi dau langu, akitokea promota anataka nipigane kwenye pambano, tutakaa chini na kukubaliana, likinilipa nacheza, hata kwenye filamu nilivyoingia ndivyo vivyo hivyo, sijawahi kusema nalipwa kiasi gani kwenye kazi ninazofanya, japo zote zinanipa maslahi mazuri,”.
Hajawatupa ‘wana’ wa Msamvu
Licha ya umaarufu wa sasa, anasema stendi ya Msamvu ndiko nyumbani kwake, hawezi kwenda Morogoro bila kushuka kuwapa salamu watu aliopiga nao debe kitambo.
“Nikifika Morogoro lazima nishuke pale nakusalimia, Msamvu ni nyumbani, gym ya pale ndiyo ilinipa muongozo ni gym ya utoto wangu.
“Nilikuwa kijana mdogo wakati nainia pale na kuanza kujifunza ngumi, ilikuwa ni kabla hata ya Cheka (Francis) kuwa staa, nilicheza cheza kidogo nikaa pembeni kwa kuwa sikuwa nimezifikilia zaidi ngumi, hadi baadae kabisa niliporudi,”.
“Wakati ule akili yangu niliiweka Zaidi kwenye kupiga debe stendi na kupokea abiria waliokuwa wakisafiri kwenda mikoa mbalimbali, kama nilivyosema niliifanya kazi yangu ya kupiga debe muda mrefu hadi Mwenyezi Mungu aliponionyesha fursa nyingine kwenye ngumi.
Chanzo ilikuwa ni Mike Tyson
Mandonga anamtaja bondia nyota wa zamani na bingwa wa dunia wa uzani wa juu, Mike 'Iron' Tyson ndiye chanzo cha yeye kuanza kufuatilia mchezo wa ngumi.
Bondia huyo anayejiita nabii aliyeamua kuzitangaza ngumi za Tanzania, anasema alikuwa akimkubali bondia huyo Mmarekani .
"Ngumi zilikuwa moyoni mwake, aliufanya mchezo huo uonekane ni rahisi, akiingia ulingoni raundi za mwanzoni tu anamaliza pambano, huyu ndiye alifanya nione kila kitu kinawezekana," alisema.
Hataki kukumbuka haso za nyuma
Katika harakati za kutafuta pesa, Mandonga anasema alipitia changamoto nyingi ambazo hataki kuzikumbuka tena.
"Siku zote kama ulitoka kwenye shida, Mwenyezi Mungu akakusaidia kuingia kwenye raha huwezi kuzisimulia shida ulizopitia.
"Huo ndio msimamo wangu, nimepitia magumu mengi, lakini nashukuru Mungu kunitoa katika kupiga debe na kunipeleka katika maisha mengine yenye uhakika wa chakula," anasema.
Maneno ya mitandaoni
Kucheza mfululizo kwa Mandonga kumeibua sintofahamu iliyopelekea Kamisheni ya Ngumi za kulipwa (TPBRC) kumtaka akafanye kipimo cha MRI kabla ya kuruhusiwa kurudi tena ulingoni huku mashbiki baadhi wakimkebehi.
"Wapo wanaoniambia, Mandonga, tunakupenda hadi utakapofia ulingoni, nawafurahia kwa kuwa kwa namna moja au nyingine nao wananisapoti.
"Maneno ya mitandao hayajawahi kuniumiza, kama nimeambiwa kuscan ubongo na sijauminia, sembuse maneno ya mashabiki wangu wanaonisapoti?,".
Pambano lake gumu
Anasema hajawahi kuwa na pambano gumu, licha ya kupigwa mara sita kwenye mapambano 14 aliyopigana.
"Kwa kuthibitisha hili, mashabiki waniambie lini wamesikia Mandonga anepigwa na kudhoofika au kulazwa hospitali baada ya pambano? kwa Mtu kazi ukinipiga ni kama nimekupiga, nikikupiga nimekupiga, nimeletwa kama nabii wa kuja kuhamasisha michezo na burudani
Akiwa nyumbani anafanya haya
Bondia huyo baba wa watoto sita anasema, katika maisha yake yote, furaha yake ni kutimiza majukumu ya familia yake.
"Mimi ni baba na mume, nilianza kuwajibika hata kabla ya kuwa staa," anasema na kufafanua anachojivua ni kuwa na mji wake hata kabla ya kucheza ngumi.
"Familia yangu imekuwa na mchango mkubwa, japo wanangu watachagua njia za kupita, kama baba yao sitawachagulia, ninachokiamini ni kwamba urithi wa mtoto ni elimu.
"Vingine vitafuata, lakini kwanza ni kusoma, watafanya wanachokipenda baada ya shule, atakayependa kuwa mwanasoka, mwanamasumbwi, msanii au vinginevyo hapo sitamuingilia,".
Kustaafu ngumi! Msikie mwenyewe
Licha ya kupata umaarufu kwa kuchelewa, anasema atapigana hadi pale mwili wake utakapomgomea.
"Sina mpango wa kustaafu hadi pale nitakapoona sasa mwili umekataa ndiyo nitaacha, kwenye filamu huko hakuna umri, nitafanya hadi mwenyewe niseme sasa basi, nikiwa hai," anasema bondia huyo aliyepewa magari mawili kutokana na ngumi.
Anasema siku si nyingi ataongeza gari jingine la tatu iwe kwa kununua kwa pesa yake au kwa kupewa zawadi.
Bondia huyo anayejiandaa kupanda ulingoni Agosti 27, anasema kwake popote atakapokuwa anapiga kambi ya ngumi.
"Dar es Salaam ndipo kazi zangu nyingi nafanyia, Morogoro ni kwangu, hivyo popote nitakapokuwa naweka kambi, niko na kocha wangu, nikiwa popote package yangu," anasema.