Mambo ya kuangalia wakati wa usajili

Dirisha kubwa la usajili la wachezaji limefunguliwa juzi Jumamosi Julai Mosi ili kutoa nafasi kwa timu za Ligi Kuu, Ligi ya Championship na Ligi Kuu ya Wanawake kuimarisha vikosi vyao.

Tayari tumeshuhudia mabadiliko makubwa kwenye timu kwa kuachana na wachezaji baadhi ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya soka hasa kwa msimu ujao wa ligi kulingana na lengo la kila mmoja.

Kufunguliwa kwa dirisha la usajili ndio maandalizi ya msimu wa mwaka 2023/24 ndio inatoa taswira ya kile unacholenga kuvuna msimu ujao.

Simba, Azam tayari zimeachana na wachezaji zaidi ya 10 wakiwemo wakongwe ndani ya vikosi hivyo kama vile, Erasto Nyoni, Beno Kakolanya, Victor Akpan Jonas Mkunde, Gadiel Michael (Simba), Oscar Paul (Prisons), Abdallah Shaibu 'Ninja' (Yanga), Yusuph Kisongo Yusuph Athuman (Coastal Union) hao ni baadhi tu ya wachezaji waliotemwa.

Hata hivyo tumeshuhudia mara kadhaa viongozi wa timu wakipata shida baada ya kusajili wachezaji lakini mwisho wa siku wanageuka kuwa watalii sababu ya majeraha wanayowasumbua.

Mara kadhaa wachezaji wamesajiliwa lakini hawakutumika na mwisho wa siku wanaachwa kwa kutokupona vyema majeraha yao na kushindwa kuzitumika vyema timu zao.

Mwananchi kwa kushirikiana na madaktari wa michezo ambao wengi wapo kwenye timu za Ligi Kuu wametoa ushauri kwa uongozi kwamba wanaposajili wasiangalie kiwango pekee cha mchezaji bila kuona afya na matatizo ya mara kwa mara kwa wachezaji ambao hata wakisajiliwa hawawezi kuwa msaada kwa timu.

Usajili wa mazoea
Aliyekuwa daktari wa Yanga na timu ya Taifa, Shecky Mngazija anasema uongozi wa timu pamoja na wachezaji wanapaswa kutambua afya ndio mtaji kwa kila mchezaji.

"Wachezaji wengi wanasajiliwa hawafanyiwi vipimo kwa kuficha uhalisia wa mambo sababu kiongozi anahofia atachukuliwaje pale unasema mchezaji fulani anaachwa kwa sababu ya kufeli vipimo.

Anasema timu chache ndio husajili wachezaji na kuwapima afya lakini nyingi huwa hazifanyi hivyo wanafanya mambo kwa mazoea na mwisho wa siku wanaishia hospitalini kuwatibu.

"Timu iwe na kituo maalumu kwaajili ya wachezaji wao kuangaliwa afya na kuwekeza fedha eneo hilo na mchezaji lazima apimwe na kuangaliwa mapigo ya moyo na utimamu wa mwili."

Daktari wa timu ya Tanzania Prisons, Kilulu Masuga anasema usajili wetu umekuwa wa kukimbizana kwa uongozi kila mmoja akitaka kuwahi huku wakisahau eleo muhimu la afya.

"Mchezaji anapotoka sehemu moja lazima uanze kujua kule alikokuwepo historia yake sio tu kiwango na tabia, afya yake ndio muhimu zaidi kuliko kiwango.

Daktari Samweli Shita mtaalam wa mambo ya michezo ambaye anaukurasa wake wa mambo ya afya katika gazeti la Mwanaspoti anasema wachezaji wengi wanasajiliwa kama kamari.

Anasema tatizo la kwanza linaanza kwa uongozi wa timu katika mambo ya usajili la wachezaji kwa kufanya mambo bila kushirikisha wataalamu wa afya.

"Hadi unapofikia hatua ya kumsajili mchezaji unakuwa umejua kiwango chake na kumfuatilia kwa karibu hata afya yake ili mwisho wa siku aweze kuzaa matunda kwenye timu yako.

"Unaweza kupata mchezaji mzuri lakini tatizo lake kubwa ni majeraha ya mara kwa mara ambapo hawezi kukusaidia kitu na hatimaye mnavunja mkataba maana kila baada ya michezo miwili anauguza jeraha.

Daktari wa timu ya Polisi Tanzania, Richard Yomba anasema kuna mchezaji (jina tunalihifadhi) alisajiliwa dirisha dogo lakini hakuweza kutumika sababu alikuwa na majeraha.

"Wachezaji kutoka mataifa ya nje kidogo wamekuwa wawazi kwenye afya yao atakuambia ninatatizo la goti au nyama za paja lakini hapa kwetu uongo mwingi sana ndio maana vipimo wengi hawafanyi.

Hakuna ushirikishwaji
Masuga anasema viongozi wengi huwasahau madaktari wanapofikia hatua ya kutaka kumsajili mchezaji na wanakumbuka eneo la afya baadaye wakati wameshamaliza kusajili

"Labda sababu ya kukua kwa ligi yetu ndio maana mambo mengi yanafanyika kwa siri huku daktari anakuja kupewa taarifa baadaye baada ya kukamilika kwa mambo yote.

"Tulimsajili Mussa Mbise lakini kila tulipofika wakati wa mazoezi alitakiwa kutumia dawa hivyo ikanipasa nimuulize nini tatizo lake na nilipouliza kwa daktari alikokuwa (Coastal Union) akaniambia mambo mengi ambayo ikanibidi nitoe taarifa kwa uongozi.

Masuga anasema baada ya hapo walikuja kugundua tatizo kubwa kwa mchezaji huyo na hapo ndio ukawa mwisho wake uwanjani na hadi sasa anaendelea na matibabu.

Yomba anasema kumekuwa na changamoto kubwa sana katika ushirikishwaji wakati wa usajili kati ya kocha, uongozi na madaktari ili kuona wanafanya kitu kimoja kwa wakati.

"Madaktari wote huwa tunaambizana katika kutoa taarifa juu ya mchezaji na inapotokea anasajiliwa kabla ya vipimo unakuwa umepata ABC yake hivyo inakupa urahisi wa kujua wapi unaanzia.

"Kuna mchezaji uongozi ulimsajili dirisha dogo lakini baadaye nikapigiwa simu kuwa anatatizo fulani na hataweza kukusaidia hivyo tukaanza mchakato ili apewe vipimo lakini mwisho wa siku hakutokea na hakuitumikia timu na hapo tayari alishachukua fedha zake.

Yomba anaongeza asilimia kubwa wachezaji wanasajiliwa baada ya mawasiliano kati ya uongozi na wakala wa mchezaji kwa kumshirikisha kocha lakini daktari ambaye mtu muhimu husahurika.

Gharama za vipimo
Mngazija anasema kulingana na uzoefu wake gharama za vipimo vimetofautiana na hospitali kama vile kitengo cha Jakaya Kikwete ambapo kuna wataalamu wengi mchezaji mmoja anaweza kugharimu zaidi ya Sh1,50,000 hadi Sh250,000.

Mnazi Mmoja inaweza ikawa chini ya hapo lakini bado watu hawafanyi hivyo na mwisho wa siku matitabu baadaye yanawagharimu pesa nyingi.

"Unapofanya vipimo kwa mchezaji inakupunguzia mambo mengi, kwanza kuwa na uhakika wa mchezaji lakini hata ukigundua tatizo lakini ni rahisi kulishughulikia haraka."

Anaongeza tatizo kubwa kwa wachezaji wanakumbana na tatizo la nyama za paja, enka, misulu na magoti hivyo kupona haraka inategemea na ukubwa wa tatizo au eneo lilipo, umri wa mchezaji pamoja na lishe.

Yomba anasema kutokana na uzoefu wake timu kubwa mchezaji hugharimu kuanzia Sh1,000,000 lakini hiyo sio tatizo kwani wachezaji hulipwa zaidi ya hiyo, hivyo kutoa milioni moja sio kitu kikubwa.

"Hata timu zinazofanya vipimo sababu ya ushiriki wao kimataifa maana Caf wanahitaji ulazima wa kufanya hivyo lakini wengi wetu hapa hatufanyi kwa kuwa ufuatiliaji ni mdogo."

Masuga anasema kwa timu yake asilimia kubwa ya vipimo vinavyofanywa huwa havizidi Sh250,000 sababu wanapima vile vipimo muhimu pekee vinavyotakiwa.

Azam wameingia kambini kuanzia juzi Jumamosi na jana na leo walikuwa katika vipimo katika Hosptili ya Agakhan kabla ya kuanza mazoezi kesho.

Daktari wa Azam, Mwanandi Mwankemwa anasema wachezaji wa timu hiyo lazima wafanyiwe vipimo na moja ya vitu ambavyo amesisitiza ni uwepo wa bima kwa kila mchezaji.

"Sioni kama ghalama ni kubwa ukiamua jambo kulifanya na kuna udhamini ambao unatoa pesa hivyo kuna fungu lipo kwaajili ya eneo hilo hasa unapokuwa na watu zaidi ya 30,"

"Kuna fomu ya kujaza ambayo ndio fumu mama ikihitaji kila mchezaji wa Ligi Kuu afanyiwe vipimo kabla ya kuanza kucheza na sehemu tunayozingatia na vipimo vya moyo.

Anasema pamoja na vipimo wachezaji watapewa mafunzo maalumu ya kufanya pale inapotokea dharula uwanjani kama mchezaji ameumia au kazimia ghafla.

"Pia wachezaji wetu tunawafundisha namna ya kunyanyua mapigo ya moyo 'Cardiopulmonary resuscitation (CPR) kabla dokta hajafika uwanjani inapotokea tatizo lazima uweze kumsaidia mwenzako haraka kwa kumpa huduma ya kwanza."

Hapa tatizo
Dk Mngazija anasema kushindwa kugundua tatizo sahihi kunasababisha wacheza wengi kutopona kwa wakati sababu hata matibabu yanakuwa sio sahihi na hapa uongozi ndio unatakiwa kuwa sahihi kipindi hiki cha usajili

"Mfano mchezaji kaumia kichwani na damu inavujia ndani lakini ukaangalia nje pekee na kushughurika nalo ujue tatizo hilo halitapona kwa muda sahihi."

Anaongeza kama timu haina mtaalam wa lishe mara nyingi hutumia zaidi watu ambao wamesoma 'General medicine au Sports medicine' katika mambo mbalimbali.

Daktari wa timu ya Tanzania Prisons, Kilulu Masuga anasema kuna wakati mchezaji anashindwa kurejea uwanjani kwa wakati sababu ya aina ya matibabu anayopewa mfano kwa mwenye tatizo la mishipa 'ligament' kwa nchi kama zetu mchezaji anachukua muda mrefu sababu mazingira yetu na ukosefu wa wataalum wa kutosha.

"Mfano mchezaji anapotoka kwenye majeruhi anatakiwa kuwa na mtu maalum wa kumfanyia mazoezi na kupewa progam yake na mtaalam maalum kwaajili yake.