Makocha Walioufunga Mwaka 2024 wakitimuliwa

Muktasari:
- Mwanaspoti inakuletea makocha wote 12 walioondoka na kile walichokifanya, ikiwa ni wanne tu waliobaki wakiwemo, Abdallah Mohamed 'Baresi' wa Mashujaa FC, Ahmad Ally (JKT Tanzania), Fadlu Davids (Simba) na Mecky Maxime wa timu ya Dodoma Jiji.
WAKATI kesho tukitarajia kuingia mwaka mpya wa 2025 kwa kudra za Mwenyezi Mungu, tayari makocha 12 wa Ligi Kuu Bara kati ya timu 16 zinazoshiriki msimu wa 2024-2025, wameondoka ikiwa ndio kwanza raundi ya pili imeanza kwa baadhi ya klabu.
Mwanaspoti inakuletea makocha wote 12 walioondoka na kile walichokifanya, ikiwa ni wanne tu waliobaki wakiwemo, Abdallah Mohamed 'Baresi' wa Mashujaa FC, Ahmad Ally (JKT Tanzania), Fadlu Davids (Simba) na Mecky Maxime wa timu ya Dodoma Jiji.

DAVID OUMA (COASTAL UNION)
Raia huyu wa Kenya ndiye alikuwa wa kwanza kutimuliwa Agosti 24, 2024, ikiwa ni muda mfupi tangu timu hiyo ipoteze mabao 3-0, dhidi ya kikosi cha Bravos do Maquis kutoka Angola, katika mchezo wa awali wa Kombe la Shirikisho Barani Afrika.
Ouma alijiunga na Coastal Union Novemba 9, 2023 akichukua nafasi ya aliyekuwa kocha mkuu wa kikosi hicho na Mkurugenzi wa Programu za vijana, Mwinyi Zahera aliyejiunga na Namungo huku akizifundisha timu za Sofapaka, Mathare United na Posta Rangers.
Kocha huyo aliyetawala soka la Kenya kwa zaidi ya miaka 21, akiwa na leseni ya UEFA, CAF A na uzoefu kutoka kituo cha michezo cha Ajax Amsterdam cha Uholanzi, amewahi pia kufundisha timu ya taifa ya Kenya 'Harambee Stars' chini ya Bobby Williams.
Uzoefu wake uliiwezesha Coastal kumaliza nafasi ya nne katika Ligi Kuu Bara msimu wa 2023-2024 na kufuzu michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa mara ya kwanza tangu mara ya mwisho iliposhiriki na kuishia raundi ya kwanza mwaka 1989.

YOUSSOUPH DABO (AZAM FC)
Septemba 3, 2024, uongozi wa Azam FC uliachana na aliyekuwa kocha mkuu wa kikosi hicho, Youssouph Dabo baada ya mwenendo mbaya wa matokeo ndani ya timu hiyo uliopelekea kutolewa katika hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2024-2025.
Dabo alitimuliwa baada ya kuiongoza timu hiyo katika mchezo mmoja tu wa Ligi Kuu Bara kwa msimu wa 2024-2025, dhidi ya Maafande wa JKT Tanzania uliopigwa kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo Mbweni na kuisha kwa suluhu (0-0), Agosti 28, 2024.
Kwa msimu wa 2024-2025, Dabo aliiongoza Azam katika michezo mitano, akianza na nusu fainali ya Ngao ya Jamii na ushindi wa mabao 5-2, dhidi ya Coastal Union Agosti 8, 2024, kisha kuchapwa fainali na Yanga kwa mabao 4-1, Agosti 11, 2024.
Baada ya hapo, akaiongoza katika michezo ya Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya awali ambapo alitolewa kwa jumla ya mabao 2-1, dhidi ya APR ya Rwanda, kufuatia kushinda nyumbani bao 1-0, Agosti 18, 2024, kisha kuchapwa ugenini 2-0, Agosti 24, 2024.
Dabo alijiunga rasmi na Azam FC Mei 1, 2023, baada ya kuachana na Klabu ya ASC Jaraaf de Dakar ya kwao Senegal ambapo alitua ndani ya kikosi hicho kwa mkataba wa miaka mitatu akichukua nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa Kocha Mkuu, Kally Ongala.
Septemba 7, 2024, uongozi wa Azam FC ulimtangaza aliyekuwa Kocha Mkuu wa RS Berkane, FAR Rabat, Raja Casablanca, ES Setif, Olympique Club de Khouribga na Wydad Casablanca, Rachid Taoussi raia wa Morocco kurithi mikoba ya Yousouph Dabo.

FIKIRI ELIAS (KENGOLD)
Elias alianza msimu na kikosi hiki kilichopanda daraja msimu huu japo aliachana nacho Septemba 17, 2024, kwa makubaliano ya pande zote mbili baada ya mwenendo mbaya wa timu hiyo, tangu ilipopanda Ligi Kuu Bara kwa msimu huu wa 2024-2025.
Fikiri aliiongoza KenGold katika michezo mitatu ya Ligi Kuu Bara na kupoteza yote, akichapwa mabao 3-1, dhidi ya Singida Black Stars Agosti 18, 2024, akachapwa tena 2-1 na Fountain Gate Septemba 11, 2024, kisha kupoteza kwa bao 1-0, na KMC Septemba 16, 2024.
Baada ya hapo ikaongozwa na Jumanne Challe aliyeipandisha kama kocha wa muda kutokana na kutokidhi vigezo vya kusimamia benchi la ufundi ambapo katika michezo yake mitano ya Ligi Kuu Bara, alishinda mmoja tu, sare mmoja na kupoteza mitatu.
KenGold iliyopo mkiani mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara na pointi sita baada ya kucheza michezo yake 16, ikishinda mmoja tu, ikitoka sare mitatu na kupoteza 12, kwa sasa inaongozwa na nyota wa zamani wa Yanga na Mtibwa Sugar, Omary Kapilima.

PAUL NKATA (KAGERA SUGAR)
Oktoba 10, 2024, Klabu ya Kagera Sugar iliachana na aliyekuwa kocha mkuu wa kikosi hicho Mganda, Paul Nkata baada ya mwenendo mbaya ndani ya timu hiyo katika michezo mbalimbali ya Ligi Kuu Bara aliyoiongoza tangu msimu huu umeanza.
Nkata aliyewahi kuzifundisha timu mbalimbali zikiwemo, SC Villa na Express FC za kwao Uganda, alijiunga na Kagera Sugar Agosti 10, 2024, akichukua nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa kocha mkuu wa kikosi hicho, Fredy Felix 'Minziro'.
Tangu Nkata achukue mikoba ya 'Minziro', aliiongoza Kagera Sugar katika jumla ya michezo saba ya Ligi Kuu Bara kwa msimu huu wa 2024-2025, ambapo kati yake alishinda mmoja, sare mmoja na kupoteza mitano akiiacha nafasi ya 14 na pointi nne.
Baada ya hapo Oktoba 17, 2024, uongozi wa Kagera ukamtangaza aliyekuwa kocha wa Coastal Union, Gwambina na Dodoma Jiji, Melis Medo, baada ya kuonyesha kiwango kizuri akiwa na kikosi cha Mtibwa Sugar kinachoshiriki Ligi Kuu ya Championship.

GORAN KOPUNOVIC (PAMBA FC)
Raia huyo wa Serbia aliachana na Pamba Jiji Oktoba 16, 2024 baada ya kuiongoza timu hiyo katika michezo saba ya Ligi Kuu Bara, akitoka sare minne na kupoteza mitatu, jambo lililowapa mashaka mabosi wa kikosi hicho na kufanya maamuzi hayo.
Goran alijiunga na timu hiyo msimu wa 2023-2024, baada ya kuachana na Tabora United ambapo alikiacha kikosi hicho nafasi ya 16, katika msimamo wa Ligi Kuu Bara, kufuatia kukusanya jumla ya pointi zake nne katika michezo saba aliyokiongoza.
Hata hivyo, baada ya maamuzi ya viongozi wa Pamba kuachana na Goran, Oktoba 17, 2024, uongozi wa timu hiyo ulimtangaza aliyekuwa Kocha wa Geita Gold na Maafande wa Tanzania Prisons, Fredy Felix 'Minziro', kuchukua nafasi ya Kopunovic.

FRANCIS KIMANZI (TABORA UNITED)
Oktoba 21, 2024, uongozi wa Tabora United ulitangaza kuachana na aliyekuwa kocha mkuu wa kikosi hicho Mkenya, Francis Kimanzi na msaidizi wake, Yusuf Chippo, baada ya mwenendo mbaya wa timu hiyo katika michezo ya Ligi Kuu Bara msimu huu.
Makocha hao wa Kenya, walijiunga na Tabora Julai 31, 2024, na kuiongoza katika jumla ya michezo minane ya Ligi Kuu Bara msimu wa 2024-2025, ambapo kati yake walishinda miwili, sare miwili na kupoteza minne wakiiacha nafasi ya 11, na pointi nane.
Hata hivyo, Novemba 2, 2024, uongozi wa timu hiyo ulimtangaza Mkongomani Anicet Kiazayidi kuchukua nafasi ya Kimanzi, huku akizifundisha timu mbalimbali zikiwemo za, AS Vita Club, FC Simba Kolwezi, FC Les Aigles du Congo na Maniema Union.

MWINYI ZAHERA (NAMUNGO FC)
Zahera ambaye kwa sasa ni mshauri wa benchi la ufundi la timu hiyo, kabla ya majukumu hayo alikuwa kocha mkuu, ingawa Oktoba 24, 2024 aliachana na Namungo na nafasi yake kuchukuliwa na Juma Mgunda aliyezifundisha Coastal Union na Simba.
Kabla ya uteuzi wa Mgunda, Zahera alikiongoza kikosi hicho katika jumla ya michezo saba ya Ligi Kuu Bara ambapo kati ya hiyo alishinda miwili tu huku akipoteza mitano, akikiacha nafasi ya 13, kwenye msimamo baada ya kukusanya pointi sita.

ABDIHAMID MOALLIN (KMC FC)
Novemba 11, 2024, uongozi wa KMC FC ulitangaza rasmi aliyekuwa kocha wa kikosi hicho, Abdihamid Moallin kujiuzulu katika nafasi hiyo, kwa makubaliano ya pande mbili baada ya kuiongoza msimu huu kwenye jumla ya michezo 11, ya Ligi Kuu Bara.
Kocha huyo wa zamani wa Azam FC, aliiongoza KMC katika michezo 11, ambapo kati ya hiyo alishinda minne, sare miwili na kupoteza mitano akiiacha nafasi ya saba na pointi 14, akiwa ni kocha wa pili kujiuzulu baada ya Fikiri Elias wa KenGold.
Baada ya hatua hiyo, Novemba 14, 2024, KMC FC ikamtangaza aliyekuwa kocha wa muda wa Azam FC, Kally Ongala aliyefanya kazi pia ya kufundisha washambuliaji ndani ya kikosi hicho, ili kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na Moallin aliyejiunga na Yanga.

MIGUEL GAMONDI (YANGA)
Novemba 15, 2024, uongozi wa Yanga uliachana na aliyekuwa kocha mkuu wa kikosi hicho, Miguel Gamondi baada ya kuiongoza timu hiyo msimu wa 2024-2025, katika michezo 10 ya Ligi Kuu Bara, ambapo kati yake alishinda minane na kupoteza miwili.
Hatua ya Gamondi kufukuzwa ilijiri baada ya timu hiyo kupoteza michezo miwili mfululizo ikianza na (1-0) v Azam FC na (3-1) v Tabora United na katika michezo 10, Yanga ilikuwa ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara na pointi zake 24.
Gamondi alijiunga na Yanga Juni 24, 2023 akichukua nafasi ya Mtunisia, Nasreddine Nabi aliyeipa mataji mawili ya Ligi Kuu, mawili ya Kombe la Shirikisho (ASFC), mawili ya Ngao ya Jamii na kuifikisha fainali ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika.
Tangu ateuliwe kukiongoza kikosi hicho, Gamondi alikiongoza katika jumla ya michezo 40 ya Ligi Kuu Bara kuanzia msimu wa 2023-2024, hadi huu wa sasa wa 2024-2025, ambapo kiujumla kati ya hiyo alishinda 34, sare miwili tu na kupoteza minne.
Katika michezo hiyo 40 ya msimu uliopita na huu wa sasa, safu ya ushambuliaji ya kikosi hicho cha Gamondi ilifunga jumla ya mabao 85 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 18, ambapo kiujumla kwa misimu miwili alikusanya pointi zake 104.
Gamondi alichukua mataji matatu na timu hiyo akianza na Ligi Kuu Bara msimu wa 2023-2024 na kuifanya Yanga kufikisha jumla ya mataji 30, tangu mwaka 1965, akachukua pia Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) na Ngao ya Jamii mwaka 2024.
Baada ya kuondoka Gamondi, Novemba 15, 2024, uongozi wa Yanga ulimtangaza aliyekuwa Kocha Mkuu wa TS Galaxy ya Afrika Kusini, Sead Ramovic raia wa Ujerumani aliyejiuzulu mwenyewe ndani ya timu hiyo kutokana na mwenendo mbaya wa matokeo.
Ramovic alijiuzulu mwenyewe baada ya kuiongoza timu hiyo katika michezo sita ya Ligi ya Afrika Kusini bila ya ushindi na kati yake alitoka sare miwili na kupoteza minne, akiiacha nafasi ya 16 kwenye msimamo kufuatia kukusanya pointi mbili tu.

PATRICK AUSSEMS (SINGIDA BS)
Raia huyo wa Ubelgiji aliyetamba na timu mbalimbali zikiwemo Simba, aliachana na Singida Novemba 25, 2024 na msaidizi wake, Denis Kitambi kwa kile kilichoelezwa kufikia makubaliano ya pande zote mbili ya kusitisha kwa mikataba yao.
Hadi Aussems anaondoka alikuwa ameiongoza Singida katika jumla ya michezo 11, ya Ligi Kuu Bara na kati ya hiyo alishinda saba, sare mitatu na kupoteza mmoja tu, ambapo alikiacha kikosi hicho nafasi ya nne kwenye msimamo na pointi zake 24.
Baada ya hapo, uongozi wa timu hiyo ukamtangaza mkurugenzi wa ufundi wa kikosi hicho, Ramadhan Nswanzurimo kukiongoza kwa kushirikiana na Muhibu Kanu, huku mchezo wao wa kwanza wakapoteza kwa mabao 2-1, dhidi ya Azam FC Novemba 28, 2024.

MBWANA MAKATA (TZ PRISONS)
Kikosi hiki cha Maafande kiliachana na aliyekuwa Kocha Mkuu, Mbwana Makata na msaidizi wake, Renatus Shija Desemba 28, 2024, baada ya kutoridhishwa na mwenendo wa matokeo ya timu hiyo ya jijini Mbeya katika Ligi Kuu Bara tangu msimu huu umeanza.
Makata alikiongoza kikosi hicho katika jumla ya michezo 14 ya Ligi Kuu Bara kwa msimu wa 2024-2025, ambapo kati ya hiyo alishinda miwili tu, sare mitano na kupoteza saba, ambapo alikiacha kikiwa nafasi ya 15, kwenye msimamo na pointi 11.
Baada ya kuondoka Makata, timu hiyo ikakabidhiwa kwa Kocha Msaidizi, Shaban Mtupa aliyesimamia katika michezo miwili ya Ligi Kuu akianza na kichapo cha mabao 4-0, dhidi ya Yanga Desemba 22, kisha ushindi wa bao 1-0 na Pamba Jiji Desemba 26.

MOHAMED MUYA (FOUNTAIN GATE)
Muya ndiye kocha wa mwisho kati ya 12, waliouaga mwaka 2024 vibaya baada ya kutimuliwa Desemba 29, 2024, ikiwa ni muda mfupi tu tangu timu hiyo ikumbane na kichapo cha fedheha cha kucharazwa kwa mabao 5-0, dhidi ya mabingwa watetezi Yanga.
Hadi Muya anaondoka ndani ya kikosi hicho alikuwa amekiongoza katika jumla ya michezo 16, ya Ligi Kuu Bara ambapo kati yake alishinda sita, sare miwili na kupoteza minane, akikiacha kikiwa kwenye nafasi ya sita kwenye msimamo na pointi 20.
MSIKIE MUYA
Baada ya Fountain Gate kuachana na Muya, kocha huyo alifunguka kwa kuweka wazi haamini kama alifeli ndani ya timu hiyo, huku akieleza jambo linalompa furaha moyoni mwake ni kukiacha kikosi hicho kikiwa katika nafasi nzuri kwenye msimamo.
"Ningekuwa nimeiacha mkiani mwa msimamo kiukweli ningejutia zaidi lakini kwa hapo nilipoiacha kwangu ni mafanikio, kama kocha inauma kupoteza kwa idadi kubwa ya mabao ila muda mwingine inabidi kukubaliana na kinachotokea maishani," anasema.