Makata ni sawa na makocha saba Simba, Yanga

Muktasari:
- Kocha Mbwana wa Dodoma Jiji, Makata aanika siri yake na Dodoma Jiji, kupandisha timu Ligi Kuu.
MBEYA. HUENDA Mbwana Makata akawa Kocha pekee ambaye amedumu kwa muda mrefu katika kikosi cha Dodoma Jiji kuliko makocha wote hapa nchini tangu alipoipandisha Ligi Kuu msimu uliopita.
Hadi sasa ni msimu wake wa tatu akiinoa timu hiyo aliyoanza nayo ikiwa Ligi ya Championship (zamani Ligi Daraja la Kwanza) alipoiongoza na kuibuka kinara Kundi A.
Wakati huo Dodoma Jiji ilipanda sambamba na timu za Gwambina FC ya mkoani Mwanza na Ihefu ya Mbeya, kwa sasa timu hizo mbili zinashiriki Championship.
Hata hivyo hadi sasa hakuna timu yoyote kwenye Ligi Kuu iliyokaa na Kocha wake tangu msimu uliopita, na kwa timu kama Simba na Yanga wamepishana wengi kwa muda huo.
Tangu msimu uliopita, Yanga imebadili makocha watatu, ikiwa ni Zlatco Krmpotic, akaja Cedric Kaze na baadaye kumleta Nassredin Nabi, huku Simba ikinolewa na watatu ambao ni Sven Vanderbroek kisha Didier Gomes kabla ya kuwaleta Hitimana Thiery na Pablo Franco.
Mbali na vigogo hao wa soka nchini, lakini makocha waliozipandisha Gwambina na Ihefu zimefanya mabadiliko mengi kwenye benchi la ufundi huku zikishindwa kuhimili Ligi Kuu.
Gwambina tangu ipande Ligi Kuu, imenolewa na makocha watatu, ikianza na Novatus Fulgence aliyesaidiana na Athuman Bilali ‘Billo’ kisha akaja Mohamed Badru na baadaye Mellis Medo.
Ihefu wao ambao ilipanda kupitia mchujo ‘play off’ chini ya Maka Mwalwisi iliachana naye na kumpa kibarua Zuberi Katwila aliyepo hadi sasa Championship.
Mwanaspoti imezungumza na Makata ambaye ameelezea sababu za kudumu hadi sasa klabuni hapo pamoja na rekodi yake ya kupandisha timu kadhaa Ligi Kuu.
Anasema ushirikiano alionao ndani na nje ya uwanja, uvumilivu, maelewano yake na wachezaji na kuaminiwa na mabosi wake ni sababu zilizomuweka hadi sasa ndani ya timu hiyo.
Anasema ikiwa sasa ni msimu wa tatu kwake kuwapo kikosini, yapo mafanikio mengi ikiwa ni kuiwezesha timu hiyo kuendelea kubaki kwenye Ligi Kuu, lakini kuwa timu ya ushindani muda wote.
Kocha huyo anasema pamoja na kuzikosa nafasi tatu za juu msimu uliopita, bado timu hiyo haikukata tamaa na wanaendelea kujiwinda kujiweka nafasi nzuri.
“Ni mafanikio kwa sababu niliopandisha nao kwa sasa hawapo na timu zote zilishuka daraja, lakini sisi tumeendelea kuwepo na kuonesha ushindani, kikubwa ni ushirikiano wa timu kwa ujumla” anasema Makata.
Kocha huyo ambaye amepandisha timu tano Ligi Kuu kwa nyakati tofauti ikiwa ni Mji Mpwapwa, Twiga Sports, Alliance, Polisi Tanzania na Dodoma Jiji anasema siri kubwa ni kupambana bila kujali ugumu wa ligi.
Anasema rekodi na heshima hiyo ni moja ya furaha yake katika kazi yake ya mpira na kwamba bado vita inaendelea huku akiahidi makubwa ndani ya Dodoma Jiji msimu huu.
“Tunaendelea kupambana, tunataka msimu huu tumalize nafasi tatu za juu, tayari dirisha dogo tumeanza na usajili wa Waziri Junior, bado wengine kama watatu eneo la kiungo, beki na winga ili kukamilisha malengo” anasema na kuongeza
“Siwezi kusema tunaacha yeyote kwa sababu mpira wa sasa unaendeshwa kitaalamu kwa sababu wachezaji wana mikataba lazima aidha kuvunja au kuwatoa kwa mkopo,” anasema Makata.
Kwa upande wa Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Johnson Fortunatus anasema kuwa na Kocha huyo kwa muda mrefu ni kutokana na uvumilivu kwani si kwamba anayo mazuri pekee isipokuwa ni kumpa nafasi na kumuamini.
“Kikubwa ni kuvumilia kwa sababu si kwamba mtu anaweza kuwa na mazuri tu, hata mabaya yapo ila tunashukuru matokeo si mabaya sana na tunaendelea kupambana kuipa mafanikio zaidi,” anasema Johnson.