Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Lipston Mlagulwa: Niliota kucheza taifa stars... Leo siwezi hata kutembea

MLANGULWA Pict

Muktasari:

  • Hakuwahi kufikiria kuwa maisha yake yangetawaliwa na maumivu, safari za hospitali, upasuaji na miaka ya kuishi kitandani huku akihitaji msaada wa wengine hata kufanya mambo ya msingi.

SAA chache kabla ya maisha yake kubadilika, Lipston Mlagulwa alikuwa kama maelfu ya vijana wa Kitanzania waliokuwa na ndoto kubwa za kuvaa jezi ya Taifa Stars na baadaye kucheza soka la kulipwa nje ya nchi, akiamini ipo siku angefuata nyayo za mastaa kama Mbwana Samatta na Simon Msuva.

Hakuwahi kufikiria kuwa maisha yake yangetawaliwa na maumivu, safari za hospitali, upasuaji na miaka ya kuishi kitandani huku akihitaji msaada wa wengine hata kufanya mambo ya msingi.

Kichwani mwake kulikuwa na jambo moja tu kufanya mazoezi kwa bidii, kupata nafasi ya kucheza katika ligi za ushindani, kujenga jina lake na kutimiza ndoto ya kuwakilisha Taifa Stars kabla ya kuvuka mipaka kwenda kucheza soka la kulipwa nje ya nchi.

Ndoto hiyo ilikuwa imeanza kuchukua nafasi, alikuwa amepitia akademi mbalimbali za soka hapa nchini, akachaguliwa kwenye kikosi cha timu ya taifa chini ya miaka 17 kilichoweka kambi nchini Morocco kujiandaa na fainali za AFCON 2021 kabla ya mashindano hayo kusitishwa kutokana na mlipuko wa janga la virusi vvya corona ‘Covid-19’.

Baadaye akajiunga na Mbao FC akiwa na matumaini ya kuendelea kujitengeneza hatua kwa hatua, akiamini daraja la pili lingekuwa mwanzo wa safari yake kuelekea Ligi Kuu na baadaye soka la kimataifa.

Hakujua kwamba mazoezi ya siku moja yangekuwa mwisho wa ndoto zote alizokuwa ameziishi tangu utotoni.

Leo, miaka mitano baadaye, Mlagulwa haongei tena kuhusu mechi, mabao wala ushindani wa uwanjani. Anazungumza kwa sauti ya utulivu, lakini nyuma ya kila neno kuna simulizi nzito ya maumivu, machozi na mapambano ambayo si rahisi kuisikiliza bila kuguswa.

Ni simulizi ya ndoto zilizokatishwa ghafla wakati safari ndiyo ilikuwa inaanza. Ni simulizi ya kijana aliyepoteza nguvu za mwili na kutumia mamilioni ya fedha kutafuta tiba bila mafanikio makubwa.

Lakini, zaidi ya yote, ni simulizi ya mtu ambaye licha ya yote aliyopitia, bado hajakata tamaa ya kuamini kuwa ipo siku maisha yake yatabadilika.

Mwandishi wa makala hii alisafiri kwa saa nane na dakika 23, akikatiza zaidi ya kilomita 425 kutoka Dar es Salaam hadi wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma, ambako Mlagulwa anaishi kwa sasa.

Huko alishuhudia hali yake kwa macho, kabla ya kukaa naye kwa mahojiano ya kina yaliyofichua maisha yake, siku ambayo kila kitu kilibadilika na mapambano anayopitia hadi leo.


KILA KITU KILIVYOBADILIKA

Lipston anakumbuka siku hiyo kwa uwazi kabisa kana kwamba ilikuwa imetokea jana. Ilikuwa kipindi cha maandalizi ya msimu mpya akiwa na Mbao FC, wakati kikosi hicho kilikuwa kwenye programu maalumu ya kuongeza utimamu wa mwili kabla ya kuanza kwa ligi.

Hakukuwa na dalili yoyote kwamba siku hiyo ingekuwa mwanzo wa safari ngumu ambayo ingebadilisha maisha yake. Kila kitu kilianza kawaida, wachezaji wakiwa kwenye mazoezi ya kawaida kabla ya kuendelea na programu nyingine.

“Ilikuwa siku ya kawaida kabisa. Tulikuwa tunaendelea na maandalizi ya msimu, ligi ilikuwa bado haijaanza nadhani ilikuwa 2022. Tulikuwa tunafanya mazoezi ya kawaida, hakuna kitu nilichokuwa nakihisi kwamba kuna jambo linaweza kutokea,” anasema na kuongeza.

“Tulikuwa tunakimbia tu, zile dakika za mwanzo za kujiandaa, kufanya ‘warm up’ (kupasha mwili joto). Ndipo wakati nakimbia nikahisi mgongo umeshtuka ghafla. Ulikuwa ni mshtuko ambao sikuwahi kuupata kabla.”

Anasema: “Sikugongana na mtu, sikuanguka, hakuna aliyenikanyaga. Nilikuwa nakimbia tu kawaida, lakini ghafla nikahisi kitu kimebadilika mwilini.”

Baada ya tukio hilo, mwili wake ulianza kutoa ishara ambazo hakuzielewa.

“Baada ya ule mshtuko nilihisi kama mwili umekataa. Niliona kama nguvu zimeshuka ghafla, nikajua kuna kitu hakipo sawa.”

Aliamua kumuomba ruhusa kocha na benchi la ufundi ili akae pembeni.

Hakutaka kufanya haraka wala kuonekana kama analalamika. Kama mchezaji aliyekuwa amezoea kupambana na maumivu madogo uwanjani, alia mini huenda hali hiyo ingeisha baada ya kupumzika.

Akiwa pembeni, aliendelea kuwatazama wenzake wakiendelea na mazoezi huku yeye akijaribu kuelewa kilichokuwa kimetokea.


USIKU WA MASWALI MENGI

Mazoezi yalipomalizika, alirejea nyumbani akiwa na mawazo mengi. Kwa mara ya kwanza tangu aanze kucheza soka, alikumbana na hali ambayo hakuwa ameifahamu.

Hakuwahi kushtuka mgongo wala kupata tatizo la kiuno. Hakuwahi kufikiria kwamba siku moja angeweza kushindwa kufanya kile alichokipenda zaidi kucheza mpira.

“Nilipofika nyumbani nilikuwa natafakari sana. Nilikuwa najiuliza, hii imekuwaje? Kwa nini leo? Na je, hali yangu itakuwaje mbele?”

Anasema kilichompa hofu zaidi ni kwamba hakukuwa na jibu lolote.

“Sikuwa najua tatizo ni nini. Hiyo ndiyo ilikuwa inanipa mawazo sana, kwa sababu toka nianze kucheza mpira sijawahi kupata hali kama ile.”

MLA 01

NGUVU ZILIANZA KUPOTEA

Baada ya siku hiyo, badala ya hali kuwa nzuri, mwili wake ulianza kubadilika taratibu.

Nguvu zilianza kupungua kila siku, mazoezi yakaanza kuwa kitu kigumu.

“Baada ya ile siku kila siku niliona tofauti. Nguvu zilikuwa zinapungua, mwili ulikuwa unachoka sana. Hata kwenda kufanya mazoezi nilikuwa naona siwezi kama zamani,” anasema.

Baada ya siku mbili au tatu ndipo alipoanza kuelewa kwamba hii haikuwa tena hali ya kawaida.

“Nikaanza kuona hapa kuna kitu kikubwa zaidi, haikuwa uchovu wa mazoezi wala maumivu ya kawaida ya mchezaji,” anasema.

Wakati huo alikuwa akiishi na rafiki yake mmoja huko Mwanza ambaye alikuwa akimchukulia kama kaka yake.

“Bro (kaka) alikuwa anatoka asubuhi kwenda kazini anarudi usiku. Mimi muda mwingi nilikuwa peke yangu. Nikajiuliza kama hali itaendelea hivi nitakuwa salama kweli? Nani atanisaidia nikizidiwa?”

MLA 02

UAMUZI MGUMU

Baada ya kuona hali ikiendelea kuwa mbaya, Lipston aliamua kuzungumza na viongozi wa Mbao FC.

“Nilikaa nikasema lazima niwaambie viongozi hali yangu ilivyo kwa sababu niliona siwezi kuendelea kukaa pale bila msaada wa karibu,” anasema.

Aliwaeleza changamoto aliyokuwa nayo na kuomba ruhusa ya kurejea nyumbani kwao Dodoma kwa ajili ya kufuatilia afya yake.

“Niliondoka nikiwa na mawazo kwamba nitakaa siku chache, nitapata matibabu halafu nitarudi. Sikuwahi kufikiria kwamba ingekuwa hivi kwa miaka mingi,” anasema.

MLA 03

SAFARI YA KUTAFUTA TIBA

Akiwa nyumbani, Lipston hakutaka kukubali kwamba safari yake ya soka ilikuwa imefikia mwisho. Bado alikuwa na matumaini kwamba mwili wake ungeweza kurejea katika hali yake ya kawaida na angeweza kurudi uwanjani kuendelea na kile alichokipenda.

Alijaribu kuanza tena mazoezi taratibu, akiamini huenda ilikuwa ni suala la muda tu kabla ya nguvu zake kurejea.

Kadiri siku zilivyopita, ndivyo alivyogundua kwamba tatizo lilikuwa kubwa zaidi kuliko alivyokuwa akifikiria mwanzo.

Hatimaye alilazimika kufanya uamuzi ambao kwa mchezaji yeyote ni mgumu kuuchukua kusimamisha mazoezi.

“Ilikuwa ngumu sana kuamua kuacha mazoezi kwa sababu mpira ndiyo maisha yangu. Nimekuwa nikifanya mazoezi muda wote, nimezoea maisha ya uwanjani. Lakini niliona hata nikienda mazoezini sifanyi kitu, mwili wenyewe umekataa,” anasema.

Baada ya hapo ndipo ilipoanza safari nyingine ambayo hakuwahi kufikiria angeipitia safari ya kutafuta tiba.

Kutoka sehemu moja kwenda nyingine, kutoka ushauri mmoja hadi mwingine, Lipston na familia yake walianza kutafuta majibu ya tatizo ambalo lilikuwa limeanza kubadilisha maisha yake taratibu.

“Tulianza kutafuta msaada kila sehemu. Tulitembea maeneo mengi sana, tukaambiwa jaribu hiki, jaribu kile. Hakuna kitu tulichopuuzia kwa sababu tulikuwa tunatafuta suluhisho,” anasema Lipston.

Katika safari hiyo, walijaribu njia mbalimbali za matibabu, ikiwemo tiba za asili ambazo watu wengi waliziamini zinaweza kumsaidia.


Itaendelea kesho