Samatta amesoma Cuba sisi tumemuelewa
Muktasari:
- Huu ni uamuzi mgumu sana lakini kwa sisi watu wa mpira ambao tunafahamu mchango na mahangaiko ya Samatta kwa timu yetu ya taifa, tunamuelewa Kapteni.
Jana Mbwana Samatta ametangaza kustaafu rasmi kuichezea Taifa Stars.
Huu ni uamuzi mgumu sana lakini kwa sisi watu wa mpira ambao tunafahamu mchango na mahangaiko ya Samatta kwa timu yetu ya taifa, tunamuelewa Kapteni.
Kwa hapa kijiweni, uamuzi huo wa Samatta tunautafsiri kama ametumia elimu ya Cuba, kwa maana kwamba ameufanya kwa akili kubwa sana.
Japo wengi wanatamani Mbwana angestaafu baada ya AFCON 2027. sisi tuliomuelewa tunaamini kuna mambo ameyaepuka ambayo pengine yangepelekea asiwe na mwisho mzuri katika kikosi cha Stars.
Leo sisi ambao tunamuomba Samatta atengue uamuzi wake wa kujiuzulu, kesho tunaweza kuwa wa kwanza kumshambulia iwapo Taifa Stars haitofanya vizuri.
Kwa vile AFCON itachezwa hapa nyumbani, wengi tutakuwa na matarajio makubwa na ikiwa hayatotimia, tutahamishia mashambulizi yetu kwa Samatta.
Hii haijatokea mara moja bali mara nyingi na hatukuwahi kubadilika katika hilo.
Samatta kucheza timu na Ligi kubwa Ulaya imekuwa kama fimbo ambayo tumekuwa tukiitumia mara kwa mara kumchapia pale tunapokwama.