Ligi ya mkwanja washika usukani
Muktasari:
- Katika mchezo maarufu wa mbio za magari unaosimamiwa na Formula One (F1), kuna wababe kadhaa waliovuka mwaka wakicheka, wakiwa ni madereva walioutumikia kwa miaka mingi na wale waliostaafu kitambo, lakini kipato walichokusanya na kukiwekeza kinaendelea kuwalipa wakifurahia siku zao duniani.
NEW YORK, MAREKANI: MWAKA 2025 ulimalizika takriban siku kadhaa zilizopita na sasa dunia inaelea ndani ya 2026, na kama ilivyo kila sekta ikiwamo ile ya michezo watu wanahesabu walichovuna, huku kukiwa na wale wanaopiga hesabu kutokana na hasara za aina mbalimbali.
Katika mchezo maarufu wa mbio za magari unaosimamiwa na Formula One (F1), kuna wababe kadhaa waliovuka mwaka wakicheka, wakiwa ni madereva walioutumikia kwa miaka mingi na wale waliostaafu kitambo, lakini kipato walichokusanya na kukiwekeza kinaendelea kuwalipa wakifurahia siku zao duniani.
Hii hapa ni orodha ya washika usukani waliokuja mzigo wa maana tu na mwaka umeanza wakiwa ndio vinara wa utajiri miongoni mwa mastaa wa kushika usukani na kusukuma ndinga za mashindano hayo yenye mashabiki wengi duniani.
1. Michael Schumacher (Dola 600 milioni)
Mwamba yupo mahututi kitandani kwa zaidi ya miaka 13 sasa, baada ya ajali aliyoipata katika mchezo wa kuteleza kwenye barafu huko Uswisi, ambao umemuacha akiwa hajitambui kwa muda mrefu sasa. Bingwa huyo mara saba alipata mamilioni kupitia mishahara, udhamini na biashara.
Hata hivyo, jina na ubalozi aliouacha pamoja an ule ambao familia yake imekuwa ikiingia mikataba mbalimbali umeendeleza utajiri alioujenga wakati akishika usukani katika mbio za magari kati ya 1992 hadi 2012. Schumacher alipata ajali hiyo miezi michache baada ya kutangaza kustaafu kuendesha magari ya mbio hizo.
2. Lewis Hamilton (Dola 520 milioni)
Huyu ndiye dereva tajiri zaidi anayeendelea kushiriki mashindano hayo. Utajiri wa Hamilton unatokana na mishahara pamoja na bonasi za Formula One za miaka mingi, udhamini na leseni, umiliki wa biashara na mali isiyohamishika.
Mwaka 2025 Hamilton alihamia Ferrari akitokea Mercedes, ambapo uhamisho huo umeongeza thamani ya chapa yake kimataifa na gharama za mialiko kwenye matukio mbalimbali.
3. Fernando Alonso (Dola 260 milioni)
Kwa kifupi Alonso anakadiriwa kuwa na takriban Dola 260 milioni akinufaika na mishahara, ubalozi na biashara zake katika nchi mbalimbali huko Ulaya, na zaidi urefu wa muda aliotumikia F1 kuanzia 2018.
Mkali huyo wa usukani amevuna malipo makubwa ya mishahara kutoka kampuni za mbio za magari za Renault, Ferrari, McLaren na Aston Martin.
4. Kimi Raikkonen (Dola 250 milioni)
Utajiri wa Kimi unatokana na mishahara ya enzi zake Ferrari, bonasi za Lotus na udhamini wa muda mrefu .
Baada ya F1, amekuwa na uwekezaji kwenye mali isiyohamishika na miradi ya mbio za magari.
5. Max Verstappen (Dola 245 milioni)
Gazeti la Quote la linadai kwamba Verstappen ana utajiri wa Dola 210 milioni, lakini Forbes imethibitisha kwamba utajiri ana mzigo unaofikia Dola 245 milioni.
Utajiri wake unatokana na msururu wa mataji, mishahara mikubwa, bonasi za kazi pamoja na mikataba ya ubalozi wa kimataifa.
Makazi yake Monaco pia yanamsaidia katika uhifadhi wa kipato kisichotozwa kodi kubwa.
6. Niki Lauda (Dola 200 milioni)
Mali ya Niki Lauda inakadiriwa kuwa Dola 200 milioni katika taratibu za kifedha za Ujerumani, mkwanja alioupata kutokana na zawadi za mataji matatu ya F1. Ana mikataba mbalimba na kampuni za kibiashara na mashirika ya ndege. Kwa miaka mingi alikuwa staa wa magari na dereva wa Mercedes katika mashindano hayo.
7. Jenson Button (Dola 150 milioni)
Button ana utajiri uliothibitishwa kufikia Dola 150 milioni kutokana na mikataba ya McLaren, taji la Brawn GP, kazi ya utangazaji, na uwekezaji mbalimbali alioufanya.
8. Sebastian Vettel (Dola 140 milioni)
Vettel anakadiriwa kuwa na takriban Dola 140 milioni hadi kufikia mwishoni mwa mwaka jana.
Dereva huyo ana mataji manne akiwa na kampuni ya Red Bull, mishahara mikubwa aliyolipwa na Ferrari pamoja na udhamini.
Tangu alipostaafu 2022 amejikita kwenye miradi ya mazingira, lakini akiendesha pia biashara zake mbalimbali huko Amerika.
9. Mario Andretti (Dola 130 milioni)
Andretti ana utajiri wa Dola 130 milioni alioupata kutokana na biashara, bidhaa zenye chapa ya jina lake katika masoko ya Ulaya pamoja na mialiko katika matukio mbalimbali anayoalijkwa ambavyo bado vinamuingizia mapato hata baada ya miaka mingi kupita.
10. Eddie Irvine (Dola 120–126 milioni)
Irvine mara nyingi hukadiriwa kuwa na kati ya Dola 120 milioni na 130. Makisio ya halisi ya watalaamu wa masuala ya fedha Ulaya ni kwamba ana mkwanja unaofikia Dola 126 milioni.
Utajiri huo unatokana na mishahara enzi zake akiitumia Ferrari, bonasi na uwekezaji katika mali isiyohamishika yakiwamo majumba na ardhi.
ZAIDI...
Madereva hao wanaongoza kwa utajiri kutokana na kutumikia timu zinazolipa vizuri kwa muda mrefu, huku chapa zao binafsi zikiwapa udhamini wa kiwango cha juu katika biashara na bidhaa mbalimbali za thamani duniani ikiwa saa, mitindo na magari.
Pia, wababe hao wamekusanya utajiri kutokana na mikataba ya miaka mingi. Wakati Schumacher na Lauda walinufaika na mwanzo wa biashara ya kimataifa ya F1, kizazi kipya kinaongezewa nguvu na mitandao ya kijamii na bonasi kubwa.