Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Shakira anazeeka na utamu wake

Muktasari:

  • Pengine kwa vijana wa Gen Z, ambao hawajafaidi vizuri kazi za muimbaji huyo alizoachia katika ujana wake, ni mkali anayejua kuimba na kunengua na ukitaka kufananisha zama zile na hizi, unaweza kufananisha vaibu lake la stejini na la nyota wa Afrika Kusini, Tyla.

AKIWA na umri wa miaka 48 sasa, Shakira Isabel Mebarak Ripoll maarufu Shakira, bado anatamba katika gemu ya muziki ikiwa ni miaka 35 tangu alipoanza maisha ya sanaa.

Pengine kwa vijana wa Gen Z, ambao hawajafaidi vizuri kazi za muimbaji huyo alizoachia katika ujana wake, ni mkali anayejua kuimba na kunengua na ukitaka kufananisha zama zile na hizi, unaweza kufananisha vaibu lake la stejini na la nyota wa Afrika Kusini, Tyla.

Kwa miaka zaidi ya ishirini, jina la Shakira limekuwa likiendelea kuzungumziwa kutokana na aina ya muziki wake unaovuka mipaka ya lugha na tamaduni.

Mwanamuziki huyo wa asili ya Colombia maarufu kwa nywele zake za dhahabu na uchezaji wa kipekee wa tumbo (belly dance), amekuwa nembo ya ubunifu, mvuto na nguvu ya mwanamke kwenye jukwaa la kimataifa.

Amebakisha miaka miwili tu kufikisha umri wa miaka 48, lakini Shakira bado anapendwa, anasikilizwa na anatazamwa zaidi ya vijana wengi waliokuja baada yake. Unaweza kusema mkali huyo wa kibao cha Wakawaka anazeeka na utamu wake.

Ingawa anaendelea kutoa ngoma, lakini nyimbo za Hips Don’t Lie na Wakawaka zimeweka rekodi ya kipekee kwenye sanaa yake na kumtambulisha duniani kama nyota inayong’ara.

Wiki zilizopita Shakira alikuwa mmoja ya wasanii waliopata nafasi ya kutumbuiza kwenye sherehe za kuhitimisha miaka 20 ya mtandao wa Spotify na kati ya wasanii waliofanya vizuri siku hiyo jina lake lilikuwapo akiwasha moto kwa ngoma yake ya Hips Don’t Lie na kuwashangaza watazamaji.

Mshangao huo si kwa sababu aliimba live vizuri, la hasha, bali ni namna alivyocheza wimbo huo kana kwamba ndio kwanza anaanza muziki kumbe ni wa kitambo sana.


SAFARI YAKE

Shakira alianza safari yake ya muziki akiwa msichana mdogo kutoka mji wa Barranquilla, Colombia. Wazazi wake walitambua kipaji chake mapema, hasa uwezo wake wa kuimba, kucheza na kuandika mashairi.

Albamu yake ya kwanza Magia ilitoka akiwa na umri wa miaka 13, ikafuatiwa na Peligro (1993), ingawa hazikufanya vizuri sana kibiashara.

Lakini mambo yalianza kubadilika mwaka 1996 kupitia albamu Pies Descalzos na baadaye Dónde Están los Ladrones?, ambazo zilimfanya awe nyota barani Amerika Kusini na mwaka 2001 aliachia Laundry Service iliyokuwa na wimbo maarufu Whenever, Wherever, dunia nzima ikaianza kumtambua rasmi.

Mchanganyiko wake wa muziki wa Kilatini, Pop, na mitindo ya Kiarabu ulimtofautisha na wengine.


REKODI

Mafanikio hayakuishia kwenye muziki wa Kilatini pekee. Shakira aliendelea kupenya katika soko la kimataifa na kubaki hapo kwa zaidi ya miongo miwili.

Nyimbo kama Chantaje akimshirikisha Mkolombia mwenzake Maluma ulipata zaidi ya watazamaji bilioni tatu, Hips Don’t Lie (2006) ulivunja rekodi kwa kuongoza chati katika nchi zaidi ya 50 na kwa sasa una watazamaji zaidi ya bilioni 1.5 kwenye YouTube.

Aidha, Waka Waka (This Time for Africa) wimbo maalumu wa Kombe la Dunia 2010 nchini Afrika Kusini ulimfanya kuwa nembo ya muziki wa dunia. Hadi leo, wimbo huo unaendelea kuwa sehemu ya kumbukumbu za mashabiki wa soka na muziki duniani kote.

Wimbo huu ndio uliomkutanisha na aliyekuja kuwa baba watoto wake, Gerard Pique, beki wa zamani wa klabu ya Barcelona na timu ya taifa ya Hispania ambaye walikutana nchini Afrika Kusini wakati wa fainali za Kombe la Dunia 2010, ambako beki huyo alitwaa Kombe la Dunia akiwa na Hispania na akamtwaa mtoto mzuri Shakira na kuzaa naye watoto Milan, 12, na Sasha, 10. Baadaye wakaachana Juni 2022.

Lakini cha kushangaza ni kwamba, licha ya miaka kupita, Shakira ameendelea kubaki kileleni. Tovuti ya YouTube Charts inaonyesha zaidi ya video kumi za Shakira zimevuka bilioni moja ya kutazamwa, jambo ambalo ni nadra hata kwa wasanii wa kizazi kipya. Hilo linathibitisha kwamba umri wake si kikwazo bali ni historia inayoendelea kuandikwa.

SIRI YA UTAMU WAKE

Shakira anabadilika kulingana na nyakati. Wakati muziki wa dunia ulipoelekea kwenye reggaeton na Afrobeat, naye aliingia kwa ustadi. Amefanya kolabo na wasanii kama Rauw Alejandro, Black Eyed Peas, Karol G, na Burna Boy akionyesha kuwa hana hofu ya kujaribu mitindo mipya.

Ukiangalia namba za ngoma zake YouTube zinafanya vizuri, wimbo wake wa mwisho kuupakia wa ‘Soltera’ umetazamwa mara milioni 200 akichanganya midundo ya aina tofauti ambayo inawachanganya mashabiki wake.

Shakira ana asili ya Kiarabu na Kihispania na hilo linaonekana wazi kwenye sauti na midundo yake. Mchanganyiko huo unamfanya awe msanii wa kipekee si wa Amerika Kusini pekee wala Ulaya na nchi nyingine.


KIZAZI KIPYA

Katika dunia ya leo yenye wasanii wengi vijana kama Rosalia, Karol G, na Anitta, wengi wangedhani Shakira angepotea kama nyota waliomtangulia. Lakini amegeuza changamoto kuwa nafasi ya kujenga urithi.

Mwaka 2023 alishirikiana na Karol G kwenye wimbo TQG, ambao ulitazamwa zaidi ya mara bilioni 1 ndani ya miezi michache. Wimbo huo uliunganisha vizazi viwili vya muziki wa Kilatini, Shakira akiwa mwalimu na Karol G kama mwanafunzi aliyeanza kung’ara.

Hata mitindo yake ya mavazi na uchezaji wake umebaki kuwa mfano wa kuigwa. Wakati wengi wanatumia mionekano yao kutengeneza kuvutia umakini, Shakira alitumia yale yale ambayo wengi wamemzoea.


KIOO WASANII WA KIKE

Huwezi kuzungumzia mafanikio ya Shakira bila kugusa nafasi yake katika kuleta usawa wa kijinsia kwenye muziki. Akiwa mwanamke kutoka nchi isiyo kubwa sana kimuziki, alifanikiwa kuweka historia na kuvutia wasanii wengi wanawake kuamini wanaweza kufanikiwa kimataifa bila kubadili utambulisho wao.

Inaelezwa Shakira ana utajiri wa zaidi ya Sh800 bilioni jambo ambalo linamuweka kwenye orodha ya wasanii wanaoendelea kuingiza zaidi mkwanja kupitia muziki wake.

Pia inaelezwa kuwa kiasi kingine cha pesa anachopata anasaidia watoto wasiojiweza kupitia taasisi yake ya Barefoot Foundation, inayosaidia watoto masikini kupata elimu. Hili linaongeza heshima kwake kama msanii mwenye moyo wa kutoa kwa jamii.

Shakira ana albamu 11, tuzo zaidi ya 400 zikiwamo Grammy na Latin Grammy na mamilioni ya mashabiki wanaoendelea kufuatilia kazi zake.