Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kwanini ngumi hii ilimkalisha Joshua?

Muktasari:

  • Vile vile Ulaya kulikuwa na mechi kali ikiwamo ya mabingwa mara nne mfululizo wa EPL, Man City dhidi ya Arsenal zilizotoka 2-2, huku Man United ikibanwa 0-0 dhidi ya Crystal Palace, kati ya mechi nyingi zilizokuwapo.

WIKIENDI iliyopita ilianza vizuri kwa wapenda burudani mara baada ya kuangalia mechi ya Yanga iliyoshinda mabao 6-0 dhidi ya CBE SA ya Ethiopia, huku Simba ikiing’oa Al Ahli Tripoli kwa mabao 3-1.

Vile vile Ulaya kulikuwa na mechi kali ikiwamo ya mabingwa mara nne mfululizo wa EPL, Man City dhidi ya Arsenal zilizotoka 2-2, huku Man United ikibanwa 0-0 dhidi ya Crystal Palace, kati ya mechi nyingi zilizokuwapo.

Wikiendi ilipambwa pia na usiku wa masumbwi ya uzito wa juu duniani.

Ilikuwa ni Jumamosi kwenye Uwanja wa Wembley jijini London, Uingereza lilikofanyika pambano la ngumi la uzito wa juu la kuwania mkanda wa IBF kati ya bondia Anthony Joshua na Daniel Dubois.

Katika vitasa hivyo vya uzito wa juu ilishuhudiwa bondia Dubois akimkalisha chini Joshua kwa ‘KO’ katika raundi ya 5 hali iliyomfanya kushindwa kuamka kwa wakati kutokana konde zito la mkono wa kulia.

Kwa mujibu wa bondia wa zamani wa uzito wa juu Mike Tyson, aina ya ngumi hiyo inafahamika kitaalamu kama ‘right cross punch’ na kwamba ngumi cross au ya moja kwa moja ndio ngumi mbaya zaidi na yenye nguvu kubwa.

Ngumi iliyorushwa na Dubois katika raundi ya tano ilikuwa ni cross ya mkono kulia iliyotua katika taya la kushoto na kumdondosha Joshua.

Ulikuwa ni usiku mbaya kwa bingwa wa zamani wa IBF ambaye alikuwa akijaribu kutwaa ubingwa huo kwa mara ya 3 huku ikiwa ni pambano lake la 4 kwenye Uwanja wa Wembley dhidi ya Dubois ambaye alikuwa ni pambano lake la kwanza tangu awe bingwa wa IBF.

Itakumbukwa Dubois alipata ubingwa huo mara baada ya bondia Oleksandr Usyk kuachia mkanda huo bila pambano la ulingoni, hivyo pambano hili lilikuwa la kwanza kupambana ana kwa ana.

Kulikuwa na kila dalili kuwa Joshua atakalishwa chini kwani katika raundi ya 3 alichapwa makonde mfululizo yalimpeleka katika kamba ambayo kama si kuokolewa na kengele ya kumaliza raundi angeshindwa mapema.

Katika raundi ya 5 wakati Joshua akijaribu kurudi kwa kasi kujibu mashambulizi alijikuta akizidiwa maarifa mara baada ya ngumi nzito ya mkono wa kulia kutua vyema katika taya na shingo upande wa kulia.

Kwa mujibu wa wataalamu wa mchezo huo, ngumi hiyo ijulikanayo kama right cross jab ikiwa katika mwendokasi wa juu ilitua eneo hilo kiasi cha kumfanya AJ kuweweseka hatimaye refa alimhesabia mpaka 10 bila kuinuka na kuwa sawa.

Akiwa katika hali hiyo ya kuweweseka hata msaidizi wa Joshua aliingia pia na kuonyesha ishara kuwa inatosha, bondia wake hawezi kuendelea na pambano hilo.

Kupigwa kwa AJ si jambo la ajabu, kwani mpinzani wake naye alikuwa ni bondia mzuri mwenye rekodi ya kushinda mapambano 22, akipoteza 2 huku akishinda 21 kwa KO.

KILICHOMKALISHA

Kwa kawaida kwa wapenda vitasa kushuhudia bondia akipigwa ngumi na kushindwa kuamka tena ni jambo la kusisimua zaidi kwenye umati wa watazamaji.

Utafiti unaonyesha kwamba kupigwa kwa ‘KO’  kwa mapigo yanaweza kuwa na madhara kwa bondia na afya yake kwa muda mrefu pamoja na kuumiza hisia zao za kiakili.

Madhara ya muda mrefu ya ubongo ambayo huenda yakawa yanajirudia rudia yanaweza kuleta uharibifu ambao unaweza kujumuisha matatizo ya akili na masuala ya utu.

Joshua mwenye umri wa miaka 34, rekodi yake ni kushinda mapambano 28, kupoteza 4 na 25 kwa KO na ana uzito wa kilo 111.

Katika pambano hilo, AJ alianguka chini mara nyingi kiasi kwamba mashabiki wengine walihoji kama aliingia ulingoni akiwa amelewa au vipi?

Kitabibu eneo alilopigwa ni katika taya ambapo ni sehemu ya kichwani na shingoni. Konde alilopigwa na kutua katika taya huweza kusafirisha mawimbi ya mtetemo mpaka katika ubongo hatimaye kujeruhi.

Uzito wa ngumi ya Dubois kwa bondia kama yeye wa uzito wa juu uzito unakadiriwa kuwa kilo 10 na huku ikiwa katika kasi ya juu inatosha kusababisha mgongano mkubwa kwenye mwili.

Pigo hilo linaweza kusababisha aina ya jeraha la ubongo lijulikanalo kama concussion yaani mtikisiko wa ubongo. Hali hii inapotokea huweza kusababisha kukatika kwa mawasiliano hatimaye kuanguka.

Inaweza kuambatana na kupoteza fahamu, kuweweseka, kuyumba yumba wakati wa kusimama. Hali hii ndio ambayo ilimpata Joshua katika raundi ya 3 na ya 5 ambayo ndio ilimaliza pambano.

Wataalamu wa ngumi wanalifahamu vyema jambo hilo ndio maana wameweka uhesabuji wa mpaka 10 kama hatua muhimu za kumwokoa bondia kwani kushindwa kusimama kwa muda huo ni ishara amepata mtikisikiko mkuwa wa ubongo.

Athari ya ngumi hiyo katika taya inaweza kuambatana na mvunjiko au kuteguka kwa taya, kujeruhiwa kwa tishu laini za eneo hilo ikiwamo kuvimba, maumivu, kuchubuka na kuvuja damu kwa ndani.

Kutokana na ujirani wa eneo hilo na mdomo wa sikio, pua na koo kama majeraha yakiwa makubwa, kuvuja damu mdomoni kunaweza kuwa ni hatari kwani inaweza kuziba njia ya hewa.

Jambo jingine ambalo linachangia kwa mtu aliyepigwa eneo hilo kudondoka au kuyumba yumba na kukosa balansi ni kutokana na ngumi hiyo eneo ilipopiga kuna mshipa mkubwa wa damu unaopeleka damu katika ubongo.

Upigwaji wa eneo hilo inaweza kusababisha mtikisiko na kusababisha damu na oksijeni inayokwenda katika ubongo kubadili mwelekeo. Hii inaweza kusababisha mtu kukosa damu katika ubongo hatimaye kupoteza fahamu au kufariki kama itadumu kwa zaidi ya dakika 6.

Ieleweke kuwa ngumi yoyote katika eneo la kichwani ni hatari kwa afya ya ubongo. Bondia anapopigwa eneo hilo na kudondoka ni muhimu wasaidizi wakamuwahi haraka na kukubaliana na hali ikiwamo kumtuliza.