KWAKO JESSE JOHN: Mapinduzi ilikuwa michuano ya heshima

Sunday January 16 2022
kombe pic
By Jesse John

MICHUANO ya Kombe la Mapinduzi 2022 iliyokuwa ikipigwa visiwani Zanzibar kwa siku 10 imefikia tamati juzi usiku kwa mechi ya fainali kati ya Azam FC na Simba, Wekundu wa Msimbazi wakifanikiwa kutwaa ndoo baada ya ushindi wa bao 1-0.

Azam ndio mabingwa wa kihistoria wa michuano hiyo, huku Simba ikiwafuata nyuma yao kwa kuwa timu iliyotwaa mara nne ikiwa ni nyingi zaidi katika michuano hiyo tangu ilipoasisiwa na kutumika kwa mtindo wa sasa mwaka 2007.

Fainali hiyo ya juzi ilikuwa ikihanikiza maadhimisho ya miaka 58 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar, yaliyofanyika Januari 12, 1964.

Klabu 10 zilishiriki michuano hiyo ya msimu wa 16 ilizoziruhusu Simba na Azam kufika fainali na kushuhudiwa na Rais wa Awamu ya Nane wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi. Kwa hakika ilikuwa michuano yenye heshima kubwa na iliyoandaliwa na kufanyika vyema. Hongera sana kwa Kamati ya Maandalizi Mapinduzi Cup.

Timu za Tanzania Bara yaani Simba, Yanga, Azam na Namungo ziliheshimisha michuano hiyo hasa kwa vigogo Simba na Yanga kupeleka vikosi vyao vya kwanza tofauti na miaka mingine ya nyuma wakitishia kutoshiriki na wakati mwingine kuleta vikosi vyao vya pili au timu za vijana.

Vilevile, wachezaji wapya waliosajiliwa dirisha dogo na wale wa kimataifa waliokuwa kwenye majaribio waliongeza ‘unyunyu’ wa michuano hiyo, huku baadhi yao wakipatiwa tiketi ya kusajiliwa katika timu kadhaa mfano kipa bora wa Taifa Jang’ombe, Hussein Abel Thomas aliyekuwa ‘man of the match’ siku Yanga ilipokipiga na Taifa Jang’ombe ambapo alisafiri sana kwenye nguzo, kiasi cha kuwavutia maafande wa Tanzania Prisons waliomchukua jumlajumla.

Advertisement

Kadhalika wapo wengine walioonwa na baadhi ya timu hasa za Bara na kuachia japo namba za simu ili kusubiri siku kupigiwa ili watue klabuni kwao na kumalizana nao kwa usajili.

Timu shiriki za Zanzibar, Meli 4 City, KMKMK, Mlandege, Taifa Jang’ombe, Selem View na Yosso Boys za Pemba zilionyesha ushindani mkubwa pamoja na kupoteza dhidi ya timu za Bara, kwani zilizitoa kamasi hata kama ziliishia njiani na kutofuzu nusu fainali.


UPUNGUFU

Kumalizika kwa michuano hii ni mwanzo wa michuano mingine Januari 2023, ambapo waandaaji wanatakiwa waongeze utamu kwa kuleta timu za nje kama walivyokuwa wakifanya miaka ileee.

Awali tulishuhudia Tusker ya Kenya, URA na KCCA za Uganda pia uwepo wa timu hizi za nje zitaleta tija na kipimo tosha kwa timu shiriki za Mapinduzi Cup na hasa washiriki wa michuano ya kimataifa kwa Bara na Visiwani, pamoja na kuwapa uzoefu vijana wadogo na hasa timu za Zanzibar.

Pia, suala la waamuzi; kuna mwamuzi nilishuhudia akisukumwa na mchezaji mmoja wa Zanzibar. Dhahiri shahiri ilipaswa kuwa kadi nyekundu lakini kwa uoga mwamuzi alimpa kadi ya njano. Vinginevyo waamuzi wa Visiwani waliacha rafu za waziwazi dhidi ya timu za Bara hasa Simba na Yanga bila hatua yoyote kuchukuliwa, baadaye hali iliendelea vizuri. Ushauri wangu ni kwamba wawe wanaletwa pia waamuzi wa kimataifa kutoka ukanda wa Afrika Mashariki na Kati katika kuboresha michuano hii.

Ninamalizie kwa kuelekeza mamlaka husika na hasa Shirikisho la soka Zanzibar (ZFA) na lile la Tanzania (TFF) kuyaweka katika kalenda mashindano haya na ratiba yake iwe inafahamika mapema kama walivyofanya.

Vilevile timu shiriki zichukulie kwa uzito ‘serious’ michuano hii hasa wenzetu wa Unguja ambao ligi yao bado sio bora na haina ushindani ili kuweza kuwapa nafasi wachezaji chipukizi ambao wengi wamesajiliwa Bara. Pia, ikiwezekana michuano hiyo itumike vizuri kama Ligi Kuu ya Muungano iliyoleta tija miaka ya nyuma kwa timu zilizoongoza tatu za Ligi Bara na nyingine kama hizo za Zanzibar zilizokuwa zikishindana kusaka mwakilishi wa michuano ya kimataifa ili ziwe zinawania ubingwa na sio kushiriki.

Advertisement