Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kwa hili la makocha... Wakubwa wamezoea

Wakubwa Pict

Muktasari:

  • Msemo huu unamaanisha kwamba maisha ya makocha kwenye timu hayana uhakika wa kuwa marefu, hiyo inabebwa zaidi na matokeo yanapoenda vibaya tu, mtu wa kwanza kutupiwa jicho huwa ni kocha, na kinachofuata baada ya hapo ni kutupiwa virago.

KUNA msemo maarufu kwenye ulimwengu wa idara ya ufundi katika soka kwamba “makocha huajiriwa ili wafukuzwe.”

Msemo huu unamaanisha kwamba maisha ya makocha kwenye timu hayana uhakika wa kuwa marefu, hiyo inabebwa zaidi na matokeo yanapoenda vibaya tu, mtu wa kwanza kutupiwa jicho huwa ni kocha, na kinachofuata baada ya hapo ni kutupiwa virago.

Lakini kwa Tanzania kufukuza makocha hakutokani tu na matokeo mabaya pekee, bali ni kama fasheni kwani unaweza kuona kocha anafanya vizuri, lakini ghafla anaondolewa.

Imeshuhudiwa kwa klabu mbalimbali hapa nchini hasa hizi kubwa za Simba, Yanga na Azam kuachana na makocha hata wanapopata matokeo mazuri.

Lakini wakati mwingine kocha anaweza kufanya mazuri mengi, upepo mbaya ukimpitia hata mechi mbili tatu pekee, basi safari inamuita.

Msimu huu umeshuhudia Yanga ikifikia makubaliano ya kuachana na Kocha Miguel Gamondi ikiwa ni siku chache baada ya kutoka kupoteza mechi mbili mfululizo za ligi. Kabla ya hapo, nyuma kidogo Muargentina huyo aliifanya Yanga kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa msimu uliopita ikiwa ni rekodi mpya.

Gamondi mbali na kuipeleka Yanga makundi, pia mwanzoni mwa msimu alizifunga Simba na Azam na kubeba Ngao ya Jamii. Msimu uliopita alishinda taji la Ligi Kuu Bara na Kombe la FA, pia akaipeleka Yanga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Kocha huyo alitua Yanga msimu uliopita ambapo aliiongoza timu kwa msimu mzima, kabla ya msimu huu safari yake kuishia njiani.

Achana na stori za klabu hizo kuachana na makocha kwa staili hiyo, kuna ishu nyingine ya namna makocha muda waliokaa ukizingatia kwamba juzi tu Yanga imetangaza kufikia makubaliano ya kuachana na Kocha Sead Ramovic baada ya kudumu kwa siku 82.

Mbali na Ramovic, kuna makocha wengine waliowahi kufundisha Simba, Yanga na Azam na kukaa muda mfupi. Rekodi hizi ni kwa miaka ya hivi karibuni.

Kabla hatujaenda mbali, timu zingine ambazo msimu huu zimeachana na makocha wake ambao hawakukaa muda mrefu, baadhi yao ni Patrick Aussems (Singida Black Stars), Goran Kopunovic (Pamba Jiji) na Paul Nkata (Kagera Sugar).

WK 01

AZAM FC

NI timu ambayo tangu imeanza kushiriki Ligi Kuu Bara 2008, imefundishwa na makocha zaidi ya 15 tofauti, wapo waliokwenda na kurudi, wengine wakipewa kazi mara moja tu.


DENIS LAVAGNE   (siku 47)

Kocha raia wa Ufaransa, alisaini mkataba Septemba 6, 2022, akaondolewa Oktoba 22, 2022 ikiwa ni siku 47 pekee akikaa klabuni hapo sawa na mwezi mmoja na siku 17.


BORIS BUNJAK (siku 81)

Ni raia wa Serbia ambaye alikaa kwa takribani miezi miwili kabla ya kuondolewa ikiwa ni baada ya Azam kupata kipigo cha mabao 3-1 dhidi ya Simba mchezo uliofanyika Oktoba 27, 2012.

Kocha huyo alitambulishwa Agosti 8, 2012 akipewa mkataba wa miaka miwili, lakini aliutumikia kwa siku 81 sawa na miezi miwili na siku 20, kichapo cha Oktoba 27, 2012 kilihitimisha safari yake.

Kabla ya kuondoka, aliiongoza Azam kucheza mechi tisa za Ligi Kuu Bara msimu wa 2013-2014 akishinda tano, sare tatu na kupoteza moja.


ETIENNE NDAYIRAGIJE (siku 134)

Kocha raia wa Burundi ambaye Juni 12, 2019 alisaini mkataba wa miaka miwili kuifundisha Azam FC.

Aliondoka Azam FC akaenda kuifundisha Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars ambapo Oktoba 23, 2019 aliaga klabuni hapo. Nafasi yake ikachukuliwa na Aristica Cioaba.

Kutoka Juni 12, 2019 hadi Oktoba 23, 2019, ni siku 134, sawa na miezi minne na siku 12.


ZEBEN HERNANDEZ (siku 224)

Raia huyu wa Hispania alianza msimu wa 2016-2017 kwa kubeba Ngao ya Jamii, lakini mambo yalibadilika kwenye ligi na mwisho wa siku Desemba 2016 safari yake ikafikia kikomo.

Ikumbukwe kwamba, kocha huyo alisaini mkataba Mei 19, 2016 na kuiongoza Azam kumalizia mechi za msimu wa 2015-16 baada ya kuondoka kwa Stewart Hall.

Kutoka Mei 19, 2016 hadi Desemba 28, 2016 ni siku 224 ambazo ni sawa na miezi saba na siku 10.


WK 02

SIMBA

Kati ya timu kongwe, hii ni ya pili iliyoanzishwa mwaka 1936 ikiwa na mataji 22 ya Ligi Kuu Bara. Pia ina rekodi ya kucheza robo fainali sita za michuano ya CAF katika misimu saba iliyopita kuanzia 2018-2019.


ZORAN MAKI (siku 56)

Siku 68 sawa na miezi miwili na siku sita, zilimtosha kocha huyo mwenye uraia pacha wa Servia na Ureno kuifundisha Simba baada ya kutambulishwa Julai Mosi 2022 na kuondoka Septemba 6, 2022 akiiongoza kucheza mechi mbili pekee za ligi na kushinda zote.


ABDELHAK BENCHIKHA (siku 157)

Kocha raia wa Algeria ambaye alitambulishwa Simba Novemba 24, 2023, kisha akaondoka Aprili 28, 2024 akiwa ameshinda Kombe la Muungano.

Kocha huyo hakuwa na matokeo mazuri sana kwenye ligi akishuhudia kichapo cha mabao 2-1 dhidi ya Yanga. Licha ya rekodi yake nzuri kwenye michuano ya CAF ikiwemo kubeba ubingwa wa Super Cup na Kombe la Shirikisho, lakini alishindwa kuiongoza vizuri Simba iliyoishia robo fainali Ligi ya Mabingwa msimu uliopita.


DYLAN KERR (siku 206)

Kocha Muingereza, hakumaliza msimu wa 2015-2016 baada ya kuondolewa Januari 2016 akiwa amejiunga na timu hiyo Juni 2015. Hadi anaondoka, alikaa kwa siku 206 kuanzia Juni 21, 2015 hadi Januari 12, 2016, ni sawa na miezi sita na siku 23.


DIDIER GOMES (siku 276)

Januari 24, 2021, Simba ilimtangaza Gomes kuwa kocha mkuu. katika mechi 6 za makundi Ligi ya Mabingwa Afrika, aliiongoza Simba kupata pointi 13 na kuongoza kundi, ikafuzu robo fainali.

Baada ya kuiongoza Simba katika michezo 37, ambapo alishinda 27, sare 5 na kupoteza 5, Oktoba 26, 2021 aliondoka kikosini hapo. Kutoka Januari 24, 2021 hadi Oktoba 26, 2021 ni siku 276 sawa na miezi tisa na siku tatu.


GORAN KOPUNOVIC (siku 181)

Januari 1, 2015 hadi Juni 30, 2015 ndiyo muda aliokaa ndani ya Simba ambapo ni siku 181 sawa na miezi sita. Alifanikiwa kubeba Kombe la Mapinduzi pekee katika muda wake ndani ya Simba.


WK 03

YANGA

Ni mabingwa wa kihistoria wa Ligi Kuu Bara wakishinda taji hilo mara 30. Klabu hiyo iliyoanzishwa mwaka 1935, imenolewa na makocha tofauti kutoka ndani na nje ya Tanzania. Katika orodha ya makocha waliofundisha Yanga, wapo waliokaa kwa muda mchache zaidi.


ZLATKO KRIMPOTIC (siku 38)

Ni kocha Mserbia aliyejiunga na Yanga Agosti 28, 2020 akasitishiwa mkataba Oktoba 4, 2020. Ndiye kocha aliyekaa kwa siku chache zaidi ambazo ni 38, sawa na mwezi mmoja na siku saba.


SEAD RAMOVIC (siku 82)

Ameondoka Yanga hivi karibuni baada ya kukaa kwa siku 81 kuanzia Novemba 15, 2024 hadi Februari 4, 2025. Hiyo ni sawa na miezi miwili na siku 21.

Ramovic ameondoka Yanga akiiongoza timu hiyo katika jumla ya mechi 13 za mashindano tofauti ambapo Ligi Kuu Bara ni sita, Ligi ya Mabingwa (6) na Kombe la FA (1).


LUC EYMAEL (siku 201)

Mbelgiji huyo alitua Yanga Januari 9, 2020 akaondoka Julai 27, 2020. Alidumu kwa siku 201 sawa na miezi sita na siku 19.

Kocha wa Mashujaa FC, Abdallah Mohamed ‘Bares’ anayeshikilia rekodi ya kuwa kocha pekee aliyebaki na timu kwenye Ligi Kuu Bara tangu msimu uliopita hadi sasa, amesema siri hiyo inatokana na imani waliyonayo viongozi wake. “Kazi yetu ya ukocha ni ngumu sana. Binafsi, nashukuru kwa imani ambayo viongozi wa Mashujaa wamekuwa nayo juu yangu, tumekuwa tukifanya kazi kwa kushirikiana kuhakikisha timu inafanya vizuri,”  alisema kocha huyo.