Prime
Mambo matano mazito Simba ikivaana na Berkane

Muktasari:
- Kikosi cha Simba kitashuka uwanjani kesho Jumapili kuikabili RS Berkane ya Morocco katika mechi ya pili ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika itakayopigwa kuanzia saa 10:00 jioni.
HAKUNA kitu kingine ila ni ushindi tu. Ndio, hakuna kitu kinachosubiriwa kwa hamu na mashabiki, wapenzi na wanachama wa klabu ya Simba ila ni kuona chama lao la Msimbazi linabakisha kombe la Shirikisho Afrika kesho Jumapili kwenye Uwanja wa New Amaan, uliopo Unguja visiwani Zanzibar.
Kikosi cha Simba kitashuka uwanjani kesho Jumapili kuikabili RS Berkane ya Morocco katika mechi ya pili ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika itakayopigwa kuanzia saa 10:00 jioni.
Simba inawakabili The Orange Boys ikiwa na deni la kupoteza ugenini kwa mabao 2-0 katika mechi ya kwanza iliyopigwa Jumamosi iliyopita kwenye Uwanja wa Manispaa ya Berkane, Morocco.
Hii ina maana kwamba iwe jua, iwe mvua, Simba kesho inahitaji ushindi usiopungua mabao 2-0 ili kulipa kisasi dhidi ya RS Berkane na kujiweka katika nafasi nzuri ya kubeba ubingwa wa CAF.
Mechi hiyo itakayochezeshwa na mwamuzi Dahane Beida kutoka Mauritania inasubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka hususani wa Wekundu wa Msimbazi wanaotamani kuona timu hiyo ikipindua meza kwa timu ya Morocco na kubeba ubingwa taji hilo la Afrika kwa mara ya kwanza katika historia ya klabu na Tanzania.

Simba inacheza fainali hiyo ya pili ya kombe uwanjani ikiwa nyumbani, zikiwa zimeshapita siku 11,502 (sawa na miaka 31, miezi mitano na siku 28) tangu ilipopoteza kwa mabao 2-0 dhidi ya Stella Abidjan ya Ivory Coast mbele ya aliyekuwa Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi.
Kuna kila sababu inayoilazimisha Simba kupambana na kubeba taji la michuano hiyo mbele ya Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi, ambaye ni mtoto wa Hayati Ali Hassan Mwinyi aliyekuwa mgeni rasmi wa fainali ya Kombe la CAF ya 1993.
Licha ya kucheza kwenye uwanja wa nyumbani huku kombe likiwa uwanjani kwa mara nyingine, Simba ina kila sababu ya kubeba ubingwa mbele ya RS Berkane kama ilivyoainishwa hapa chini.
HESHIMA
Simba ni moja ya klabu kubwa Tanzania na ukanda wa Afrika Mashariki, ikitajwa kufanya vizuri katika michuano ya kimataifa.
Ndio klabu ya kwanza ya Tanzania kufika nusu fainali ya Klabu Bingwa Afrika (sasa Ligi ya Mabingwa Afrika) 1974 na ya kwanza pia kucheza fainali ya CAF 1993 huku hii ikiwa ni mara ya pili katika michuano iliyozaliwa baada ya kuunganishwa kwa Kombe la CAF na Kombe la Washindi 2004.
Wekundu hao wanalisaka taji la kwanza ili kuifikia rekodi ya ukanda huu wa Afrika Mashariki iliwekwa na Gor Mahia ya Kenya ilipotwaa Kombe la Washindi mwaka 1987 kwa faida ya bao la ugenini dhidi ya Esperance ya Tunisia baada ya kupata sare ya 2-2 ugenini na kisha kutoka ya 1-1 jijini Nairobi na kutwaa kombe hilo.

Simba ina kila sababu ya kupata ushindi kesho na kisha kubebea taji hili ili kuifikia rekodi hiyo ya Gor Mahia ambayo pia mwaka 1979 ilicheza fainali nyingine dhidi ya Canon Yaounde ya Cameroon na kukumbana na aibu ya kufungwa mabao 8-0, ikilazwa 2-0 nyumbani kisha kupigwa 6-0 ugenini, huku timu nyingine ya Cecafa kufika fainali za CAF ni SC Villa ya Uganda iliyocheza Kombe la CAF 1992, ikiwa ni mwaka mmoja tu tangu ilipocheza fainali ya Klabu Bingwa Afrika 1991 ikiwa klabu pekee ya ukanda huo.
Kubeba ubingwa kwa Simba kutadhihirisha ukubwa wa klabu hiyo kwa sasa katika ukanda wa Cecafa, kwani ndio inayoongoza kwa ubora ikishika nafasi ya nne kwa ubora wa Klabu za Afrika, huku pia ikitaka kuweka heshima mbele ya watani wao wa jadi, Yanga waliofika fainali kama hiyo ya Shirikisho msimu wa 2022-23 na kulikosa taji kwa kanuni ya faida ya bao la ugenini.
Yanga ilikosa taji licha ya matokeo ya jumla kuwa sare ya 2-2, ikipoteza nyumbani 2-1 na kushinda ugenini 1-0 dhidi ya USM Alger ya Algeria, na imekuwa ikiwatambia watani wao kwamba ilibeba medali za CAF bila ya kupoteza mchezo, hivyo Simba itapenda kubeba kabisa kombe kumaliza udhia.
Hata hivyo, ni lazima Simba ipambane kwelikweli mbele ya Berkane iliyowahi kubeba taji la michuano hiyo misimu miwili tofauti, huku ikitoka kubeba ubingwa wa Ligi Kuu ya Morocco kwa mara ya kwanza msimu huu, na ikiwa mbele kwa mabao 2-0 dhidi ya mnyama.
UKUBWA WA KLABU
Katika orodha ya klabu bora za Afrika, Simba ipo juu ya Berkane ikishika nafasi ya nne wakati timu hiyo ya Morocco iko katika nafasi ya tisa, huku vinara wakiwa ni Al Ahly ya Misri, Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, Esperance ya Tunisia zilizopo katika Tatu Bora.
Baada ya Simba kuwa ya tano, klabu zinazofuata kukamilisha 10 Bora ni Zamalek ya Misri, Wydad Casablanca ya Morocco, Pyramids ya Misri, USM Alger, RS Berkane na CR Belouizdad ya Algeria.

Hii ina maana kwamba Berkane kubeba ubingwa huo mbele yao ni kudhalilisha nafasi ya nne iliyonayo dhidi ya wapinzani wao hao walio nafasi ya tisa.
Hivyo ni wazi wachezaji watakuwa na kazi ya kuipigania Simba kurudisha mabao mawili iliyofungwa ugenini na kupindua meza kama ilivyofanya dhidi ya Al Masry ya Misri katika mechi ya robo fainali, kwani ilipoteza ugenini 2-0 na kushinda nyumbani kama hivyo na mshindi kupatikana kwa penalti.
Hata hivyo, ubora wa nafasi ilizonazo timu hizo haiwezi kuwa kigezo cha mmoja wao kupata matokeo, isipokuwa ni namna timu itakavyopambana ndani ya dakika 90 za pambano hilo, lakini Simba ikiwa na kazi kubwa ya kuonyesha ukubwa wa klabu hiyo mbele ya Berkane.
Lakini kombe kuwepo uwanjani tena mbele ya mashabiki wa klabu hiyo wanaotarajiwa kuujaza Uwanja wa New Amaan, ni sababu nyingine inayoifanya Simba ipanie kushinda mechi hiyo, ili kutorudia tukio la mwaka 1993 ilipoliacha Kombe la CAF likitwaliwa na Stella Abidjan ya Boli Zozo aliyefunga mabao yote mawili Wekundu wakilala 2-0 kwenye Uwanja wa Taifa.
MABILIONI YA NOTI
Ukiachana na heshima ya kubeba kombe hilo, Simba ina kila sababu ya kukomaa kesho ili kukomba mabilioni ya fedha zinazotolewa kwa bingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika.
Kutinga fainali kwa Simba kumeifanya ijihakikishe kuzoa Dola 1 milioni (zaidi ya Sh2.7 bilioni), lakini ikibeba ubingwa wa michuano hiyo itazoa Dola 2 milioni ambazo ni sawa na Sh5.4 bilioni, fedha ambazo ni karibu bajeti nzima ya usajili ya klabu hiyo kwa msimu huu iliyotangazwa katika Mkutano Mkuu wa klabu hiyo uliofanyika Oktoba mwaka jana.

Simba inahitaji kushinda mechi hiyo ili kuizima Berkane na kubeba ubingwa, lakini kiwango hicho cha fedha ni mzuka mwingine unaowalazimisha kina Ellie Mpanzu, Kibu Denis na nyota wa timu hiyo kutokwa jasho kwani watajikikishia wa kuzoa Sh1 bilioni walizoahidiwa na mabosi wa klabu.
Mbali na fedha hizo kutoka kwa wadhamini wa michuano hiyo inayosimamiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Simba ina kila sababu ya kushinda ili kuzoa fedha za 'Goli la Mama' ambapo kila bao ni Sh30 milioni, mbali na ahadi za wadau wa klabu hiyo akiwamo Azim Dewji ambaye amekuwa akitangaza kununua kila bao na asisti kwa mamilioni.
HADHI YA KLABU
Kufanya vizuri kwa Simba katika mechi ya kesho, kutaiweka klabu hiyo katika hadhi ya hali ya juu ya kupata dili za maana kutoka kwa wadau mbalimbali.
Duniani kote, klabu zenye mafanikio ndio zimekuwa kivutio kwa wafadhili na wahisani wengine, hivyo taji la CAF litaifanya Simba kujiweka katika nafasi nzuri ya kupiga hela kutoka katika kampuni na taasisi za ndani na nje ya nchi na kuifanya iwe na hadhi ya kipekee nchini.
Taji hilo la Afrika pia linaweza kuwa kivutio kwa wachezaji wakubwa kutamani kuja kuitumikia Simba kama ilivyoitokea kwa Yanga misimu ya hivi karibuni baada ya kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Mbali na hadhi ya klabu, pia soko la wachezaji wa timu hiyo linaweza kuwa jepesi kama Simba itabeba ubingwa, kama ilivyoshuhudiwa kwa nyota wa timu hiyo walipokiwasha robo fainali misimu kadhaa nyumba kwa kuwauza Clatous Chama kwa Berkane na Luis Miquissone (Al Ahly).
Yanga ilipocheza fainali ilimrahisishia Fiston Mayele kuuzwa Pyramids na leo atakuwa uwanjani kuiongoza timu hiyo ya Misri katika mechi ya kwanza ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini mechi inayopigwa kuanzia saa 10:00 jioni huko Sauzi.
Hivyo, hata wachezaji wa Simba watakuwa wakicheza wakijua wanafuatiliwa na maskauti wa barani Afrika na nje ya bara hilo na kama watakiwasha watajiweka sokoni kujiuza barani Ulaya na mataifa mengine yenye fedha zao. Kwanini wapishane na fursa hiyo?

SAFARI ILIVYOKUWA
Simba iliyoasisiwa mwaka 1936 ilianza michuano ya msimu huu katika raundi ya pili ikivaana na Al Ahli Tripoli ya Libya iliyoifunga kwa jumla ya mabao 3-1, ikitoka suluhu ugenini mjini Tripoli kisha kushinda 3-1 nyumbani na kutinga makundi ambapo iliwekwa katika Kundi A.
Kundini humo ilianza kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Bravos kisha ikaenda kupoteza ugenini dhidi ya CS Constantine ya Algeria kwa mabao 2-1 kisha kuwafunga mabingwa wa kihistoria wa michuano hiyo, CS Sfaxien ya Tunisia kwa mabao 2-1 nyumbani na kwenda kuilaza ugenini 1-0.
Baadaye ilienda kutoka sare ya 1-1 ugenini dhidi ya Bravos na kumalizia hatua ya makundi kwa ushindi wa 2-0 dhidi ya Constantine na kutinga robo fainali ambapo iliing'oa Al Masry kwa penalti 4-1 baada ya matokeo ya jumla ya sare ya 2-2 kila timu ikishinda nyumbani kwa mabao 2-0.
Katika nusu fainali, Simba ilipangwa kuvaana na Stellenbosch ya Afrika Kusini na kuifunga kwa bao 1-0 lililopatikana katika mechi ya kwanza visiwani Zanzibar likiwekwa kimiani na Jean Charles Ahoua kisha kwenda kutoka suluhu ugenini na kutinga fainali dhidi ya Berkane.
Kwa upande wa Berkane ilianza raundi ya pili dhidi ya Dajde ya Benin iliyoishindilia jumla ya mabao 7-0, ikishinda nyumbani 5-0 na 2-0 ikiwa ugenini na kutinga makundi ikipangwa Kundi B ambapo ilizinyuka Stellenbosch nyumbani 5-0 na ugenini 3-1, pia ilitoka suluhu la CD Luanda na kushinda 2-0 nyumbani huku ikiipasua nje ndani Stede Malien ya Mali kwa bao 1-0 nyumbani na ugenini.
Katika robo fainali iliichapa Asec Mimosas ya Ivory Coast kwa bao 1-0 nyumbani na ugenini na kutinga nusu fainali ambapo ilivaana na Cs Constantine ya Algeria na kuifunga jumla ya mabao 4-1, ikishinda nyumbani 4-0 na kulala ugenini 1-0.
MSIKIE FADLU
Kocha wa Simba, Fadlu Davids amenukuliwa mapema kwamba mechi ya kesho haitakuwa rahisi kwa kila mmoja, lakini kwa upande wa Msimbazi wamepania kuingia kivingine ili kuwapa furaha mashabiki wa klabu hiyo kwa kubeba ubingwa huo wa Afrika licha ya kupoteza ugenini.
"Haitakuwa mechi nyepesi, kwani tulishagundua makosa tuliyoyafanya ugenini na kutuponza kupoteza 2-0, Jumapili tutaingia kivingine tukiwa na kazi ya kurudisha mabao hayo ya Berkane kisha kusaka mengine ya kutupa ushindi nyumbani. Mechi haijaisha kwa vile tuna dakika nyingine 90," alisema Fadlu, huku nahodha Mohammed Hussein 'Tshabalala' akisisitiza kuwa watapambana kwa kila hali.
"Kila mchezaji na Mwanasimba anataka kuweka heshima Afrika, tunapenda kuandika majina yetu kwa wino wa dhahabu na kuendelea kukumbukwa klabuni kwa kuiwezesha Simba kushinda ubingwa wa CAF," alisema Tshabalala aliyefunga bao la kufutia machozi katika mechi dhidi ya CS Constantine iliyochezwa ugenini kwa Simba kulala 2-1.
Sh 5.4 Bil- Kiwango cha fedha ambacho anapewa bingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika
00 Hakuna klabu yoyote ya Tanzania iliyowahi kubeba ubingwa wa michuano ya Afrika.
Sh 2.7 Bil- Fedha ambazo hadi sasa Simba imejihakikishia kupewa kwa kutinga fainali ya CAF
3 Idadi ya mabao ambayo Kibu Denis na Jean Ahoua kila mmoja amefunga msimu huu katika CAF