Kocha Coastal: Yanga imenipa mjengo

Muktasari:
- Katika uchezaji alicheza kama beki na aliiwakilisha Tanzania katika michuano ya Shirikisho la Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) 1990
Joseph Lazaro ni kocha wa soka ambaye kwa sasa anahudumu kama kocha mkuu wa Coastal Union ya Tanga. Kabla ya kuwa kocha, Lazaro aliwahi kuzichezea timu kadhaa nchini zikiwemo Coastal Union na African Sports za Tanga pamoja na Yanga.
Katika uchezaji alicheza kama beki na aliiwakilisha Tanzania katika michuano ya Shirikisho la Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) 1990
Baada ya kustaafu kucheza Lazaro alijiingiza katika ukocha na amekuwa na mchango mkubwa katika kukuza vipaji vya wachezaji chipukizi akisisitiza umuhimu wa nidhamu na kujituma ili kufikia mafanikio ya muda mrefu katika soka.
Katika majukumu ya ukocha amekuwa akiiongoza Coastal Union katika mechi mbalimbali za Ligi Kuu Bara, akionyesha uongozi thabiti na kujitolea kwa ajili ya maendeleo ya timu.

ALIANZAJE KUKIPIGA?
akizungumzia alivyoanza kucheza, Lazaro anasema: “Nilianza kuchezea mtaani kwanza baada ya kutoka shule, mwaka 1980 kuna timu ilikuwa inaitwa Mzalendo, ila hiki kikosi kilikuwa na wachezaji ambao ni waajiriwa wa Kampuni ya Saruji.
“Nilikuwa nakimbia umbali wa kilomita tatu, basi siku moja wale jamaa wamerudisha timu yao ikabidi na niingie huko kuichezea. Baada ya hapo nikaenda timu ya mkoa (wa Tanga).”
MKATABA WA KWANZA
Lazaro anasema kuwa awali alicheza timu nyingi, lakini mkataba wake wa kwanza kusaini ni pale alipojiunga na Coastal Union ya mjini humo.
“Mkataba wangu wa kwanza nilisaini Coastal Union 1990. Baada ya hapo nikasajiliwa na timu ya Bandari kwenda kuchezea Mtwara na kwa sababu kipaumbele changu kilikuwa kazi nikaondoka haraka. Kumbe Coastal hawakuridhika, mimi najua nimeshaondoka zangu Tanga, akaja Said Sudi akatembea kwa ndugu zangu wote akiwalalamikia kuwa Joseph anataka kuhama timu na sisi tunamtegemea,” anasema.
“Ndugu wakajaa dada na mama yangu ambao ni marehemu, basi Coastal ikamchukua dada yangu kutoka Tanga mpaka Dar ambapo tulikuwa kwenye kambi ya timu ya Taifa kwa ajili ya kunishawishi ili tu niachane na Bandari. Akaniambia nibaki kwa ndugu zangu Coastal, kipindi hicho nimeshasaini Bandari, lakini wakaniambia hata nikisajiliwa timu 10 nitacheza hapo tu.
“Nikasema sitaki matatizo ndio nikachukua fomu nikajaza tena Coastal Union, Bandari kule hana taarifa uongozi unapewa taarifa nimebadili uamuzi, ila bahati nzuri walinielewa.”

AFRICAN SPORTS, COASTAL UNION
Akizungumzia enzi za Coastal Union na African Sports zilivyoteka soka la Tanga, mkongwe huyo anasema: “Sisi zamani tulikuwa tunataka kazi sio pesa. Kwa hiyo African Sports walivyokuja kwangu ikabidi niwaulize kama watanipa ajira, nilivyoona siwaelewi nikarudi zangu Saruji, hapo ni Mwaka 1986.
“African Sports nimecheza, ila niliondoka baada ya kutokuona mpango wa kazi. Tulivyotoka kambini Kigoma nikawaambia mimi mwisho wa kukaa katika timu yao umefika maana nilikuwa nataka ajira sio pesa. Kumbe wakati sekeseke hilo likiendelea Coastal Union nao walikuwa wananivizia na wanajua kinachoendelea baina yangu na African Sports.
“Niko njiani kurudi ndio Coastal wakanichukua hata Saruji sikufika. Ilikuwa kesi kubwa wakati huo kutoka timu moja kwenda nyingine unaonekana kama muasi hivi. African Sports walikataa kabisa kupokea hela ya kuniuza, wao wakawaambia Coastal Union kwamba wanahitaji mtu sio pesa. Basi kibunda kilichukuliwa na FAT (Chama cha Soka Tanzania) na sio wao na sikufahamu ni shilingi ngapi maana mshahara wangu ulikuwa 9000.
“Kipindi hicho African Sports ilikuwa masikini, kwa hiyo hatumwi kiongozi kufanya mazungumzo anakuja mdhamini kabisa au unapewa taarifa ukiwa nyumbani kwamba unaitwa klabu fulani.”
YANGA ILIANZA NA MITEGO
Kuhusu dili lake kwenda Yanga, Lazaro anasema: “Niko timu ya Taifa sasa tunatoka kambini Dar es Salaam tunakuja huku Tanga mechi inayofuata ni Yanga na Coastal Union, upinzani ulikuwa mkubwa kwani wakati huo ni kama Simba na Yanga zinakutana. Mara naona gari naitwa na kiongozi wa Yanga. Kumbe viongozi walikuwa wananitega niuze mechi, kipindi hicho mtu akichukua pesa akijulikana ana kesi ila ikawa mgumu ili nisiuze mechi, kwa hiyo wakaniona muadilifu.
“Lakini huku Tanga skendo ikawa nimechukua hela ya Yanga ili watufunge Coastal Union. Cha kushangaza tuliwafunga mabao 3-1 kocha wao Mzungu akafukuzwa baada ya mechi.”

KILICHOIVUTIA YANGA, YAMPA MJENGO
Lazaro anasema baada ya kukataa bahasha na Coastal wakashinda, ndipo Yanga wakamuamini na kuanza harakati za kutaka kumsajili msimu unaofuata.
“Baada ya kuwafunga Yanga ndio waliponielewa wakaona jinsi nilivyo muadilifu, ila bado wakaendelea kunijaribu. Lakini mwisho tukasajiliwa kwenda Yanga na wenzangu saba ambao kwa majina wengine siwakumbuki ila alikuwepo George Masatu, Hussein Masha na Mwakalebela (David), ila mwisho mimi na Mwakalebela ndio tulitua Yanga wengine wakaenda Simba,” anasema na kuongeza:
“Nilisajiliwa Yanga na milioni Moja hapo nikiwa nimetoka kuchezea timu ya Taifa. Wakati huo hakuna mambo ya benki. Hivyo nikapewa pesa zangu mfukoni na nikarudi Tanga na kuwaaga Coastal Union rasmi na kurudi mjini kwa ajili ya kuendekea na majukumu mapya.
“Msimu wa 1992/93 nikiwa namalizia mkataba wangu na Yanga tulishinda michuano ya Afrika Mashariki na Kati na niliupiga mwingi sana katika mechi hizo ambazo tulicheza na timu kutoka Zanzibar, Uganda na Kenya.”
Lazaro anasema baada ya kucheza Yanga kwa mafanikio haikumuongezea mkataba mpaka alipomaliza msimu na hata alipotaka kwenda timu nyingine mabosi waligoma. Sikuamini kwa nini Yanga iliniacha kwa sababu sikufikiria kwani niliuwasha sana msimu wa mwisho, lakini nilipotaka kuondoka walinibakiza wakidai nisiondoke wakati huo dirisha la usajili lilishafungwa.
“Hata nilipoamua kubaki sikuwa na furaha kama mwanzo na sikucheza vizuri, kwani nilivunjika mkono nikiwa uwanjani hivyo nilicheza nusu msimu.”
Nyota huyo wa zamani anasema katika maisha yake ya kucheza soka timu iliyompa mafanikio zaidi ni Yanga ambayo aliichezea misimu miwili mfululizo.
“Kiukweli nyumba hii (anayoishi Tanga) niliyoijenga siri yake ni Yanga. Nimecheza pale miaka miwili nikaanza kupata hela ya kununua matofali. Kwa hiyo mimi mpira nimeishi na mpaka sasa ndio kazi yangu. Nashukuru Mungu kwamba mguu wangu umenipa mafanikio japokuwa zamani ni tofauti na sasa hivi, mtu hawezi kukaa miaka mitano au sita.”
Kuhusu soka, anasema: “Mpira siudai kwa kweli kwa sababu nimeuishi, jambo kubwa ni hili la kupata sehemu ya kuegemea nashukuru. umenipa jengo la kukaa na maisha kwa ujumla.
“Hata kujulikana na kuniheshimisha wakati mwingine najiona wa kawaida lakini watu wananifahamu. Kuna sehemu mpira umeniweka nimesafiri pia, nimecheza timu ya Taifa.

PAN AFRICAN, KUREJEA COASTAL
Lazaro anasimulia namna ilivyokuwa kimbembe kutoka Yanga kwenda Pan Africa ambapo alikwenda kwa mbinde baada ya kukaa mwaka mmoja bure ndani ya kikosi cha Jangwani.
“Baada ya kutoka Yanga nilikwenda kuichezea Pan Africa, changamoto unapotoka kuchezea Coastal Union au Afrcan Sports, kama hizi basi watu wanakuwa na wasiwasi kama wewe ni mwenzao. Nilipata tabu hiyo nilipokuwa Yanga. Watu wanahisi kama wewe ni Simba kwa sababu hizi timu zina ukaribu,” anasema.
“Kwa hiyo hata nilivyoenda Pan bado Yanga ikawa kwenye mvutano nao ikikanusha haijaniacha, lakini msimu mmoja mbele nikatimkia hapa nilicheza misimu miwili.”
Lazaro anasema baada ya kumalizana na Pan aliamua kurudi nyumbani akitua katika mikono ya Coastal Union ambayo mpaka sasa yupo nayo.
“Mwaka 1998 nikarudi Coastal ikawa imeshuka daraja baadaye ikapanda, lakini 1999 nikasema sasa basi. Ila makocha wakaniambia nikae pembeni hapo ndio kidogo kidogo nikaanza kujifunza ukocha. Mwaka 2000 nafundisha timu za mtaani tena kwa mafanikio ikiwemo Polisi, Magereza. Kwa hiyo Coastal ndio iliyonipa njia hii mpaka sasa.”
Kuhusu kurudi kwake ndani ya kikosi cha Coastal Union, anaeleza kwamba: “Mimi Coastal Union navumilia mambo mengi sana, yapo ninayostahili kufanyiwa na yapo nisiyostahili sasa nimeanza kufanana nao. Kuna ile unasema hapa ni kwangu na timu inasema huyu ni mwenzetu. Kwa hiyo unajikuta unavumilia tu mambo yaende hadi unaulizwa umerogwa, kumbe mimi sioni timu nyingine.
“Naweza nikawaambia wachezaji wachukue mshahara hata kabla yangu mimi, ila tunathubutu kufanya hivyo kwa sababu tu klabu iende na kila wakinihitaji niko hapo.”
SHIDA IPO HAPA, HAFIKIRII KUACHA
Kocha huyo anasema kuna mambo hayaendi vizuri katika kikosi hicho na timu zingine katika Ligi Kuu, akisema: “Ni kweli msimu huu haujawa mzuri na sio kwa Coastal tu hata kwa timu nyingine ambazo zinayumba. Kuna watu wamekaa hapo mbele kwenye mpira. Sio watu wa kutengeneza mpira, wanakuja wachezaji sio kama zamani ila wanaishi kwa kujuana, ndio maana unakuta kwenye timu kuna namba nane, kumi.
“Maskauti nafasi zao zinaingiliwa na hawasikilizi matakwa ya kocha kujua nini anataka, hivyo anayepata shida ni mwalimu. Mabadiliko ya makocha ndani ya msimu mmoja mchezaji kafundishwa na walimu wenye kila mbinu mpaka haelewi ashike la nani anakuja (kocha) anataka timu ishinde, mwingine ishambulie au kuzuia tu.
“Mpaka timu ielewe mfumo mzima mmebakiza mechi tisa, hata mpambane vipi tayari mmeshashuka, tunadumazwa na klabu kwa sababu hawatekelezi mahitaji ya timu.”
Lazaro ana jambo jingine analoapa kamwe hawezi kurudi nyuma akisema: “Sifikirii kuacha kufundisha hata, kama nikiacha Coastal Union, basi hata mpira wa makaratasi na nikatoa mtu akawa mchezaji mkubwa tu. Kustaafu soka labda niwe kipofu wa macho kabisa kwa sababu hii kazi iko moyoni naipenda imenikuza, imenipa maisha siwezi kuiacha kirahisi tu.”
Hata hivyo anasema, anatamani kufundisha timu zingine na amewahi kufanya hivyo, lakini Coastal Union imekuwa ikimrudisha kila mara.
“Natamani kufundisha timu nyingine na nimewahi kufundisha Mgambo, nimeanza nao (ngazi ya) wilaya mpaka Ligi Kuu, Coastal wakaja kunichukua sio hiyo tu mpaka Polisi ilileta barua Tanga hapa nikawapandisha.
“Nikafundisha Ndanda, nikaenda Kenya mwaka mmoja, nikarudi tena huku na timu zote nilizozifundisha nimeziacha kwenye mafanikio makubwa tu.”

SOKA LA SASA
Lazaro anataja kile kinacholitofautisha soka la enzi zao na sasa akiamini kuna daraja flani lililopo kati ya vizazi hivyo vya kandanda.
“Tofauti kubwa kwanza kulikuwa na ugumu wa uchezaji wetu kuanzia sheria mpaka maslahi, lakini sikukuta ugumu huo wakati naingia. Timu moja mipira mitatu, lakini watu walikuwa na juhudi sana, walimu walikuwa wanapata sana mafunzo, shida ilikuwa vifaa na pesa,” anasema ilivyokuwa enzi zao.
“Wepesi ulikuwa timu ikikutana ili ucheze lazima wakupe ajira, lakini zaidi ya hapo ilikuwa kucheza kujifurahisha kama unapenda mpira unapambana, lakini sasa watu wanasaini mikataba ya pesa nyingi.”
Na hapa mkongwe huyo anawahusia vijana wa sasa akisema: “Wanapokuwa wamecheza kwa mafanikio kipindi kifupi au kusemwa tu ujue huyo tena sio mchezaji wako hapo tayari wanakuwa wameshavimba vichwa wanajiona hawastahili kufundishwa.
“(Vijana wa sasa) hawana subira, heshima na utulivu. (Zamani) hata kama kocha hayupo nahodha anaongoza na wote wanamsikiliza, ila sio wachezaji wa sasa hivi hawawezi kuvumilia shida.
“(Siku hizi) maslahi yamewekwa mbele kama tai, mchezaji asipolipwa mwezi mmoja anagoma hachezi mpaka apewe pesa yake, wakati sisi tulikuwa tunapewa posho sio mshahara.”