Kina Nyembera wanavyopambana na zigo la TPBRC
Muktasari:
- Mbuya aliwahi kufanya kazi akiwa na kituo cha Clouds Media kwa kipindi kirefu kabla ya kujiunga na tasisi nyingine, lakini Nyembera ameendelea hadi sasa katika kituo cha Azam Media.
MAJINA ya Patrick Nyembera na Jacob Mbuya si mageni katika tasnia ya habari za michezo nchini kutokana na kuwa wanataaluma kwa kipindi kirefu wakihudumu kuhabarisha michezo mbalimbali.
Mbuya aliwahi kufanya kazi akiwa na kituo cha Clouds Media kwa kipindi kirefu kabla ya kujiunga na tasisi nyingine, lakini Nyembera ameendelea hadi sasa katika kituo cha Azam Media.
Wote wawili wamepita katika maeneo tofauti kuripoti habari za michezo, lakini ilikuwa ngumu kuwaachanisha na mchezo wa ngumi za kulipwa nchini.
Siyo mara moja, Mwanaspoti imekuwa ikukutana nao katika matukio tofauti yanayohusisha mchezo wa ngumi hata kabla ya kuanza kuonekana moja kwa moja kupitia runinga, na mara zote wamekuwa wakiufuatilia na wanaujua vyema mchezo huo.
Kitu cha kufurahisha na kuvutia ni kuona serikali inatambua mchango wa wanahabari katika meneo tofauti ya ngazi za uongozi wa kitaifa kutoka kwenye tasnia ya habari kwa kipindi kirefu.
Tasnia imetoa viongozi wengi akiwemo Rais wa Awamu ya Tatu, hayati Benjamin Mkapa.
Lakini katika upande wa mchezo wa ngumi za kulipwa Julai, mwaka huu, Waziri wa Habari Sanaa, Utamaduni na Michezo, Profesa Palamagamba Kabudi alimteua mtangazaji wa Azam Media, Patrick Nyembera kuwa mwenyekiti wa Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBRC), baada ya kamati ya awali kumaliza muda wake.
Nyembera ataiongoza kamati hiyo kwa kipindi cha miezi mitatu yaani siku 90 kuanzia Julai 29 hadi Oktoba 29, sambamba na makamu mwenyekiti Jacob Mbuya huku wajumbe wengine wakiwa ni Gordon Nsajigwa (katibu) na wajumbe Shafii Dauda, Irene Mwasanga na Ibrahim Abbas Kamwe.
Mwanaspoti limefanya mahojiano maalumu na makamu mwenyekiti wa TPBRC, Mbuya ambaye ameeleza mipango ya kakati hiyo inayoongozwa na Nyembera.
Mbuya ambaye anaanza kwa kuishukuru serikali kutokana na jukumu hilo walilopewa, lakini ni sehemu ya kuona naye ametambulika kuwa katika eneo la mabadiliko kwenye mchezo wa ngumi za kulipwa kupitia Kamisheni ya Kusimamia Ngumi za Kulipwa.
“Binafsi nashukuru kwa hii nafasi lakini wakati napata hii teuzi nilikuwa najiuliza kwamba waliopita wamefanya nini na kwa nini mimi nimeonekana,” anasema Mbuya.
“Nimeona nina uwezo wa kuishauri kamisheni na kuipeleka mbele.
“Nadhani unafahamu kwa miaka ya nyuma ukiwa miongoni mwa watu waliokuwa wakiufuatilia kwa muda mrefu na tulikuwa tunakutana na changamoto nyingi sana.
“Miongoni mwa changamoto za mabondia kuwa wezi wakabaji, mabondia kutuhumiwa kubebeshwa dawa ya kulevya, lakini sasa tunavyozungumza asilimia 50 ya mabondia wa ngumi za kulipwa wameanza kuwa smati hata kama baadhi yao hawana elimu au uwezo mkubwa wa kifedha lakini wapo vizuri kichwani na kimuonekano.
“Kitu hicho pekee kinatuonyesha picha kwamba ngumi zinaelekea wapi na jukumu letu kubwa sisi vijana pamoja mwenyekiti wangu, Patrick Nyembera ni kubeba maono ya vijana wengi ambao wanahisi uongozi wa ngumi hauna mchango kwao.
“Sasa hivi kumekuwa na mtindo wa bondia anakwenda nje kupigana kwa ajili ya kuuza pambano, hayo ni mambo ambayo tunayatazama ili kuyapunguza au kuondoa kabisa.
“Lakini tuna jukumu mama ambalo lipo mbele yetu kuandaa katiba ipitishwe, kuitisha uchaguzi utakaowaweka viongozi wapya madarakani na kukabidhi ofisi. Hayo ndiyo majukumu yaliyotuweka hapa.
“Naamini kwa viongozi tuliopo tunaweza kufikia malengo kwa pamoja kwa sababu tushakamilisha mchakato wa katiba ambao kwa sasa tunajipanga kuipeleka kwa wadau kwa ajili kupitia kabla ya kuipeleka Baraza (la Michezo la Taifa) kuisajili iwe katiba rasmi ya Shirikisho la Ngumi za Kulipwa na siyo kamisheni tena.
SWALI: Lakini bado tukiangalia kamisheni ambayo inaenda kuwa shirikisho haina meno, shida ipo wapi?
JIBU: Unajua kuna utamaduni ambao sisi tumeukuta na kawaida utamaduni upo katika sehemu. Hatuna muda mrefu ila tumekutana na tamaduni nyingi na hata tuliowapokea hapa wamejaribu sana kwa kiasi kikubwa kubadilisha.
Unajua ilikuwa wadau wote namaanisha makocha, mabondia, waamuzi na mapromota waone kamisheni kama mzazi wao ila kamisheni siyo mzazi bali ni mlezi na ndiyo ulikuwa utamaduni wao huko nyuma.
Walikuwa wakiishi kama ndugu na ndiyo sababu ya kuogopana kupeana adhabu iliyofanya kamisheni ikose meno. Ila tunaamini watangulizi wetu wamefanya kazi kubwa kubadilisha huo utamaduni.
Unaona mwenyewe kamisheni jinsi ilivyo, ofisi ilianzia Keko (Dar es Saalam) chumba kimoja, ikaja kuwa Magomeni tena kwa nyumba nzima ila bado hakukuwa na hadhi ya watu wanaosimamia mchezo wa ngumi ambao wanaidhinisha zaidi ya Sh600 milioni kwa mwaka.
Lakini kamati ya muda hasa watangulizi wetu walipambana na matokeo yake wamehamishia ofisi hapa Mafao House na imekuwa ofisi ya kisasa ambayo ina hadhi, inamkaribisha mdau yeyote mkubwa.
SWALI: Nimekuuliza kamisheni haina meno kwa sababu nimeona video ikionyesha mabondia wakipigana ni wa ngumi za kulipwa, ila mwamuzi hakuwa rasmi hili linakuaje maana linaleta taswira mbaya?
JIBU: Unajua sisi ni wageni hapa. Tuna mwezi mmoja tu na jukumu letu mama ni kuandaa katiba na kuitisha uchaguzi tukimaliza miezi mitatu tuweze kukabidhi ofisi, lakini wakati tunafanya haya haina maana kwamba ngumi zisichezwe.
Lakini kumbuka wakati tunaingia hapa siyo kila mtu anatupenda kuna watu hawapendi sisi tuwepo hapa, kuna watu ambao wanatujaribu kuangalia tutafanya nini.
Nikwambie tu hilo pambano halikuwa na vibali vyovyote. Tumeshangaa mabondia wazuri wenye leseni wameenda kucheza pambano ambalo halina kibali chochote. Wamecheza wenyewe kwa sababu zao binafsi wanazozijua. Wakacheza ngumi ambazo hazina mwamuzi wala kitu chochote. Niseme kwamba hayo tunayajua na muda si mrefu tutakuja na kauli kwamba tunaelekea wapi.
SWALI: Umekuwa promota na ukapitia magumu kiasi fulani ila sasa upo ndani ya taasisi iliyokuwa inakusimamia, picha gani unaipata?
JIBU: Kiukweli mambo mengi hayapo sawa nitazungumzia ishu moja. Samahani nilipokuwa promota nilikutana na watu ambao hawakuwa na elimu, wanaendesha taasisi lakini hawakuwa na elimu kwa hiyo hawakujali uamuzi wanaoufanya utamuathiri nani.
Lakini pia hawakuwa na njia mbadala ya kufanya uamuzi ili huyu mtu umdhibiti umtengenezee mazingira gani. Yapo mazingira ya moja kwa moja ya kumtengenezea mtu kuliko kumfungia au kuvunja pambano ambalo lilishawekewa fedha nyingi.
Kiukweli hayo mambo yamewafanya mapromota wengi wakakimbia. Jukumu letu sisi kwanza ni kuwaonyesha mapromota kwamba sasa hivi (kwenye ngumi) ni sehemu salama ambayo unaweza kuwekeza.
Kumbuka wakati ule naandaa pambano kulikuwa na fujo kubwa sana. Unalipia kibali ila ndani ya uongozi huohuo unaambiwa kibali hakifanyi kazi. Unatoa bajeti kwa ajili ya mabondia ila viongozi haohao wanakufanyia uhuni. Wana pesa zao kwa mabondia.
Halafu wanafika mbali wanakwenda mpaka kwa mabondia kwa kuwaambia wasicheze ili wamtikise promota. Nadhani unaona namna mazingira yalivyokuwa mabaya na changamoto zilivyokuwa nyingi.
Lakini wewe ni shahidi unaona sasa mazingira yamebadilika hata sisi tikiondoka tunatamani kuona tukiacha mtu mwenye maono ya sisi tunachokiwaza. Afikirie kamisheni kibiashara, maendeleo ya mabondia.
SWALI: Mnaipima vipi thamani ya mabondia?
JIBU: Sasa hiyo ni changamoto tasnia kwa ujumla ni ngumu nikieleza kwamba sisi tuna uwezo wa kuwabadilisha mabondia, hilo nitakudanganya. Unaona idadi (ya mabondia) inaongezeka kila kukicha ila mabondia wamewakuwa wakichukulia poa kwa kuona (ngumi ni) sehemu ya kutafutia chakula ila ukweli haupo hivyo.
Lakini kwa upande wa kujitambua angalau wameanza kuonekana tofauti bondia anapendeza akienda katika maeneo ya watu wengi.