Mayweather, Tyson kuzichapa
Muktasari:
- Wawili hao wameushtua ulimwengu wa masumbwi kwa kutangaza kuwa watazichapa ulingoni katika pambano ambalo awali mashabiki hawakuamini kama ingewezekana.
WASHINGTON, MAREKANI: MABONDIA maarufu wa ngumi za uzito wa juu duniani, Floyd Mayweather na Mike Tyson wanatarajiwa kuzichapa katika pambano la ndoto zao ambalo litakuwa la maonyesho, huku kila mmoja akianza tambo.
Wawili hao wameushtua ulimwengu wa masumbwi kwa kutangaza kuwa watazichapa ulingoni katika pambano ambalo awali mashabiki hawakuamini kama ingewezekana.
Miaka 11 inawatenganisha kwa umri kati ya Tyson aliyestaafu ndondi za kulipwa 2005 na Mayweather mwenye umri wa miaka 48 aliyestaafu 2017 akiwa na rekodi isiyo na doa ya kusinda mapambano yote 50 aliyocheza.
Katika enzi zao, Tyson aliyekuwa maarufu kama Iron alikuwa bingwa wa uzito wa juu huku Mayweather maarufu kama Money Machine akiwa bingwa katika madaraja matano tofauti ya uzito.
Uthibitisho wa pambano kati ya wawili hao licha ya tofauti ya umri na ukubwa umeibua mshangao miongoni mwa mashabiki wa ngumi ikizingatiwa hali ya Tyson iliyotia wasiwasi baada ya kuchapwa na Jake Paul, Novemba, mwaka jana katika pambano la maonyesho.
Hata hivyo, mtandao wa The Baddest Man on the Planet umefichua kuwa lilikuwa ni wazo la Mayweather kuandaa pambano la maonyesho mwaka 2026 na Tyson amethibitisha taarifa hizo kupitia Instagram, akisema pambano litafanyika mwakani, lakini kitakuwa kipindi cha majira ya kiangazi.
Tangazo hilo pia limebainisha kuwa tarehe na mahali bado haijapangwa, huku Las Vegas na Saudi Arabia zikitajwa kama chaguo mojawapo.
Tyson amesema: “Wakati CSI (waandaaji) waliponijia kuhusu kuingia ulingoni na Floyd Mayweather, nilifikiri, ‘haiwezekani hili kutokea,’ lakini Floyd alisema ‘ndiyo’.”
“Nilikuwa nafanya mambo yangu mwenyewe. Sikumsumbua mtu yeyote. Yeye tu alitaka kuanzisha pambano.”
Mayweather aliyemshinda Conor McGregor katika pambano lake la mwisho la kulipwa, amesema: “Nimekuwa nikifanya hili kwa miaka 30 na hakuna bondia hata mmoja aliyewahi kuharibu rekodi yangu. Tayari mnajua kwamba nimeshafanya kitu. Hiki kitakuwa kikubwa na cha kipekee. Mimi ndiye bora katika biashara ya masumbwi. Hili pambano la maonyesho litawapa mashabiki kile wanachotaka.”
Ameongeza kuwa, “kwa sasa, nafanya maonyesho. Nina uhakika kwa asilimia 100 kwamba sipigani tena dhidi ya mabondia. Hilo halipo mezani. Afya yangu ina maana kubwa kwangu. Pesa hainiumbi, mimi ndiye ninayeumba pesa na afya yangu ni muhimu zaidi kuliko pesa.
"Kuhusu mimi kufanya maonyesho na kupigana na wapiganaji wa mieleka, je, nitafanya hivyo ndani ya ulingo wa ndondi? Ni hakika kabisa.”