Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tamu, chungu kwenye ngumi wababe wakicheka, kulia

Muktasari:

  • Pambano hilo la kimataifa ambalo liliandaliwa na Mafia Boxing Promotion, huku likiwakutanisha mabondia kutoka Venezuela, Ghana, Pakistan, India, Uganda, Malawi na Ufilipino.

WAKATI maisha katika michezo kama soka yakiwekwa kando kwa muda jijini Dar es Salaam kutokana na kutokuwapo kwa mechi zozote za mashindano, Ijumaa ya juzi, Watanzania walishuhudia mapambano makali ya kimataifa ya ngumi yaliyofanyika kwenye Viwanja vya Posta - Kijitonyama.

Pambano hilo la kimataifa ambalo liliandaliwa na Mafia Boxing Promotion, huku likiwakutanisha mabondia kutoka Venezuela, Ghana, Pakistan, India, Uganda, Malawi na Ufilipino.

Pambano hilo ni msimu wake wa sita kufanyika chini ya Mafia Boxing Promotion ambapo mabondia kadhaa wamefanikiwa kuchota fedha za zawadi ya ushindi wa ‘Knockout ya Mama’ kutokana kushinda mapambano waliyocheza.

Mabondia kama Dullah Mbabe, Issa Nampepeche, Mchanja Yohana, Idd Pialali, Salmini Mizinga ni miongoni mwa waliobahatika kupata zawadi hiyo ambayo imekuwa ikitolewa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa lengo la kuendelea kuhamasisha mchezo wa ngumi za kulipwa.

Lakini, katika mapambabno ya Ijumaa wapo baadhi ya mabondia waliondoka wakiwa na furaha ya kuweza kushinda mapambano, lakini pia wapo ambao usiku wa Oktoba 10, mwaka huu, ulikuwa mchungu kwao kutokana kutoshinda mapambano yao.


WAHINDI NA VICHAPO

Achana na stori zile katika filamu za kihindi zilizokuwa zikitazamwa katika vibandaumiza lakini siku zote mabondia kutoka India wamekuwa wakichukuliwa poa kwa kuonekana wepesi na wengi wao kuitwa ndizi kwa maana ya wepesi kupigwa pale walipopanda ulingoni.


KATO NDO HIVYO

Bondia wa kwanza kupoteza alikuwa ni Kato Machemba ambaye alicheza dhidi ya Akshay Chahal, raia wa India katika pambano la ubingwa wa PST ambalo lilipigwa kwa raundi nane.

Machemba licha ya kujitutumua kutaka kuonyesha ubora wake, lakini haikuwa rahisi kutokana na mpinzani wake kuwa imara na kuweza kuchafua rekodi ya Machemba kutokana na kumchapa kwa pointi.


KALOLO NAYE KAKWAMA

Bondia mwingine ambaye aliwaumiza mashabiki wengi katika pambano la Knockout ya Mama alikuwa  Kalolo Amiri baada ya kupata pigo tena la kupoteza pambano la kuwania mkanda wa ubingwa wa WBO Afrika, alijikuta akipoteza kwa mara ya pili mfululizo dhidi ya Rama Krishnan kutoka India.

Uamuzi wa pambano la Kalolo haukuwafurahisha mashabiki wengi kutokana na kiwango alichoonyesha bondia huyo ambaye alipata wakati mgumu kutokana na urefu wa mpinzani wake ambao ulichangia kupoteza kutokana na muda mwingi kuwekwa mbali.


MASTER ALIVYOPOTEZWA

Upepo uliendelea kusalia upande wa Tanzania baada ya nahodha wa Mafia Boxing Promotion, Ibrahim Mafia kupigwa kwa knockout ya raundi ya nne na Alvin Camique, raia wa Ufilipino katika pambano la raundi 10 ambalo lilikuwa la kwanza kwake kupoteza. Mafia amekuwa maarufu kutokana na kuwafumua wapinzani wake kwa knockout.

Katika pambano hilo, Mafia alianza kwa kasi kuendeleza rekodi ya ushindi, lakini alikutana na kigingi kizito kutoka kwa mpinzani wake kutokana na kutumia nguvu na kupigana muda wote

Lakini, ilipofika raundi ya nne mambo yalikuwa mabaya kwa Mafia ambaye aliruhusu ngumi ambayo ilimfanya kupoteza mwelekeo kutokana na kosa alilolifanya baada ya kuanguka kutokana na kuinuka haraka akiwa bado hajaweza kukaa sawa.


CHANGARAWE ALIVYOZICHANGA KO

Kutoka Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Yusufu Changarawe aliendelea kuonyesha ubora katika ngumi za kulipwa kufuatia ushindi wa ‘Technical Knockout’ baada ya mpinzani wake  kutoka Uganda Kamanda Ntege kushindwa kuendelea kufuatia kona yake (wasaidizi wake) kurusha taulo.

Changarawe  ambaye hakutaka mzaha kutokana na kumshambulia mpinzani wake katika raundi nne kiasi cha kumfanya ashindwe kuendelea na pambano kwa kuacha mwenyewe na kufanya kushinda mkanda wa ubingwa wa PST


MTOTO KAMA BABA

Abdulrahman Magoma Jr alikuwa bondia mdogo zaidi kutoka Tanzania kufanikiwa kushinda mkanda wa ubingwa wa UBO International akiwa na umri wa miaka 17.

Magoma Jr ambaye baba yake aliwahi kuwa bondia mahiri nchini, hayati Magoma Shaaban, aliweka rekodi hiyo baada ya kumbonda mpinzani wake Mohamed Saqib kutoka Pakistan kwa ushindi wa pointi huku akionyesha mchezo mzuri.


PIALALI NA USHINDI WA KUDOKOA

Bondia Idd Pialali alifanikiwa kutetea mkanda wake wa ubingwa wa PST International kwa kumchapa kwa pointi Ronald Miiro wa Uganda katika pambano ambalo liliamuliwa kwa akili za kucheza na mpinzani mwenye nguvu, ambapo Mtanzania huyo alikuwa akimpiga mpinzani wake kwa staili ya ngumi za mbali za kudokoadokoa na kisha kumkimbia.

Pialali ambaye muda mwingi alicheza kwa mtindo wa kushambulia huku akitembea kwa kutotulia sehemu moja kulimfanya amsumbue mpinzani wake.


MCHANJA ALIVYOONJA KO

Mchanja Yohana wala hakutaka kufanya mambo mengi kutokana na kutumia vizuri uwezo na kasi ya mikono yake ndani ya dakika moja pekee vilivyotosha kumaliza pambano kwa ‘body punch’ iliomfanya mpinzani wake, Aldri  Portilo kutoka Venezuela kupiga goti kuashiria kwamba hawezi kuendelea na pambano.


MIZINGA NA MIZINGA YAKE WBO

Kufuatia kupigwa kwa mabondia watatu wa Mafia Boxing Promotion ambao ni Watanzania, Salmini Mizinga ndiye alibaki kuwa tegemeo pekee la kuendelea kuwatoa kimasomaso Watanzania kwenye pambano hilo.

Mizinga alitetea mkanda wake wa ubinwa wa WBO Afrika dhidi ya Canny Kotey wa Ghana katika pambano la raundi 10 ambazo zilijaa ufundi kutoka kwa mabondia wote wawili.

Mizinga ambaye alikuwa bora licha ya mwamuzi wa pambano kitoka Ghana, Rogers Barnor mara kadhaa kumkatisha na kumuonya, lakini haikumfanya ashindwe kumchapa mpinzani wake kwa majaji wote watatu.


CHOKI ALIVYOMKALISHA MTU NA TKO

Mtanzania pekee kushiriki michuano ya Kombe la Dunia la Ngumi, Juma Choki, aliendelea kuonyesha ubora katika pambano kuu kwa kumchapa mpinzani wake, Manikandan V kwa TKO ya raundi ya tano katika pambano la raundi nane ambalo halikuwa la ubingwa.

Choki ambaye alianza kwa gia kubwa alikutana na upinzani mkali kutoka kwa mpinzani wake kabla ya kuamua kuachia mwenyewe kutokana na kupokea ngumi nyingi kali.

Wengine walioshinda katika usiku huo ni Allan Kamote ambaye alimchapa Harvey Mkacha wa Malawi, Richard Mtangi akimchapa kwa pointi Wilson Phiri wa Malawi, Tano Juma aliyemzima Yamikami Mtambo kutoka Malawi huku Said Hakimu akimshinda Varum Phartyal wa India