Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kimbembe Job na kibarua jezi ya Yondani

MASHABIKI wa klabu ya Yanga hawana presha kwa sasa hata akikosekana Lamine Moro na Bakari Mwamnyeto baada ya kuwa na wingi wa wachezaji katika eneo hilo la ulinzi wa kati.

Licha ya kuwa na Said Makapu na Abdallah Shaibu ‘Ninja’, lakini Yanga waliamua kumsajili beki kijana Dickson Job kutoka Mtibwa Sugar.

Usajili huo watu wengi walihoji kutua kwake Jangwani, lakini ukiangalia umri wake unaona kwamba wamesajili mchezaji kutoka kikosi cha kwanza na kwenda kupambana au kuwa mbadala wa wachezaji wa kikosi cha kwanza huko Yanga.

Kutua kwake Yanga moja kwa moja alipewa jezi namba tano ambayo imezoeleka kuvaliwa na aliyekuwa beki kisiki wa klabu hiyo, Kelvin Yondani ambaye aliondoka baada ya kumaliza mkataba wake.

Mwanaspoti limeangalia vitu ambavyo Job anaenda kukumbana navyo akiwa na jezi hiyo mgongoni huku mchezaji aliyepita akiwa ameifanyia makubwa.

KUPENYA KWA LAMINE NA MWAMYETO

Huu ni mtihani wa kwanza ambao Job atakutana nao katika kikosi cha Yanga. Mwamnyeto na Lamine ni miongoni mwa mabeki wenye kombinesheni bora katika kikosi hicho.

Jezi namba tano ilipokuwa inavaliwa na Kelvin Yondani, beki huyo hakuwahi kukaa nje kirahisi pindi alipokuwa fiti mara zote alikuwa anaanza kikosini.

Makapu na Ninja wameshindwa kupenya katika ngome hiyo, licha ya uwezo walionao kuwa mkubwa.

Job kazi hii pia anatakiwa atambue kwamba vita yake ni kwa mabeki wanne ambao wanamzunguka na sio kitu chepesi kupata namba mbele yao.

FITI, MBISHI KWA WASHAMBULIAJI

Sifa kubwa ya Yondani akiwa na jezi namba tano mgongoni ilikuwa ni ufiti wake ndani ya dakika 90 akihakikisha lango lake linakuwa salama.

Kitu kingine ni kwamba mchezaji huyo anapokuwa uwanjani anakuwa ni mbabe kwa washambuliaji wengi hali ambayo ilimfanya aogopwe.

Hii itakuwa kama mtego kwa Job kwani uwezo wa kupambana na mabeki anao, lakini sasa anasubuliwa kuonyesha ile hali aliyokuwa nayo Yondani ya kufanya watu wasimsogelee.

Kama atashindwa kufanya hivyo, basi beki huyo ataifanya jezi ya Yondani ionekane nyepesi kwake na kushindwa kurithi mikoba ya mkongwe huyo anayekipiga Polisi Tanzania kwa sasa.

TEGEMEo TAIFA

Hapa kidogo Job anaweza kufiti kwani ameanza safari ya kucheza timu ya Taifa katika kikosi cha vijana chini ya miaka 17 mpaka 20.

Baada ya hapo alipata nafasi ya kucheza katika kikosi cha Mtibwa Sugar na baadaye alijihakikishia nafasi ya kucheza kikosi cha nje.

Mpaka hivi karibuni Job alikuwa ameitwa katika kikosi kilichoenda kushiriki Chan nchini Cameroon, lakini majeraha yalimfanya aondolewe katika msafara wa wachezaji walioondoka.

KUDUMU YANGA

Wachezaji wengi wanapokwenda katika klabu za Simba na Yanga huwa hawadumu muda mrefu na hiyo ni kutokana na namna wanavyokutana na ugumu wa namba.

Wapo mabeki wengi waliopita kwa kukaa miaka minne na wengine mitatu, kisha waliondoka na kwenda kutafuta maisha sehemu nyingine.

Yondani katika kikosi hicho amedumu kwa takriban miaka minane akiwa na jezi yake namba tano mgongoni - tena akiwa mchezaji tegemeo katika kikosi cha kwanza.

Job ana kibarua kigumu cha kuhakikisha anaendeleza hilo ambalo lilifanywa na nyota mwenzake ambaye aliondoka baada ya mkataba kumalizika.

BEKI KIONGOZI

Yondani alikuwa ni beki kiongozi ndani ya uwanja, lakini pia ni mhamasishaji mzuri kwa wachezaji wenzake pindi alipotaka timu ifanye vizuri.

Alikuwa akiiongoza timu vizuri jambo ambalo wakati mwingine alikuwa anapewa kitambaa cha unahodha kuhakikisha kwamba kila kitu kinakwenda vizuri.

Job aliwahi kuwa nahodha katika kikosi cha timu ya Taifa chini ya miaka 17, lakini pia na yeye ana chembechembe kama za Yondani.

Kwa upande huo anaweza kukutana na changamoto mbele ya Moro na Mwamnyeto ambao nao ni viongozi ndani kwa ndani.

MWENYEWE AFUNGUKA

Akizungumzia mambo hayo matano, Job anasema atajituma kwa nguvu zote ili kuhakikisha anapata nafasi ya kucheza pamoja na kuwa beki wa kudumu katika kikosi cha timu ya Taifa ‘Taifa Stars’.

“Yote yanawezekana ukizingatia mimi bado mdogo lolote linaweza kutokea, maana ndoto yangu sio kuishia hapa ila kwa sasa nazungumzia Yanga na nitawekeza nguvu zangu zote kwa Yanga.”

Akizungumzia kuhusu jezi namba tano iliyokuwa inavaliwa na Yondani, anasema ina maana kubwa kwake kutokana na kuwa anamkubali mchezaji huyo.

“Yondani ndiye mchezaji ambaye namkubali na hii jezi ndio pendwa kwangu, nitahakikisha nafanya kile kilicho bora ili kumuenzi, pia nitatenda mengi zaidi ndani ya jezi hii.”