MEDDIE KEGERE: Ndoo ya Super Cup imetuongezea mzuka

TUNASHUKURU Mungu kwa kumaliza michuno ya Simba Super Cup kwa kutwaa ubingwa baada ya kukusanya pointi nyingi, kuonyesha malengo yetu yalitia kama tulivyotaka.
Nikiri kwamba michuano hiyo imekuwa na faida nyingi kwetu kama wachezaji, benchi la ufundi na timu kwa ujumla kutokana na ushiriki wetu na nitaanika mambo kadhaa tuliyovuna. Kwetu wachezaji unaweza ukafanya mazoezi yako binafsi kwa muda mrefu, lakini kukaa bila kucheza soka au mechi za ushindani huwezi kuwa na utimamu wa kimwili ambao unaweza kukusaidia kwenda katika mashindano.
Kabla ya michuano hiyo tulikuwa na likizo muda mrefu ambayo tulikuwa tunatumia muda mwingi kujiandaa tukiwa majumbani pamoja na familia.
Ilikuwa ngumu kurudi katika timu kufanya mazoezi halafu kwenda katika mechi za ushindani ambazo zilikuwa za ligi, kwa maana hiyo kupata muda wa kutumika katika michezo hiyo miwili kuna hali au ubora umeongezeka.
Kwa kuangalia ratiba iliyopo ndani ya Februari kwetu Simba ni ngumu kwani katika muda mfupi tunatakiwa kucheza mechi mfululizo kila baada ya siku chache, jambo ambalo ilikuwa lazima tupate muda na mechi sahihi za kujiandaa kama ambazo tumetoka kucheza katika Simba Super Cup.
Wachezaji tumepata wakati wa kukaa na kufanya mazoezi kwa pamoja ambayo tulikwenda kuyatumia katika mechi za kimashindano ambazo tulifanya vizuri na kuna mazoezi yalirudi kati yetu baada ya kuachana kwa ajili ya likizo na wengine ni wapya kikosini.
Katika upande wa benchi la ufundi, nalo ni jipya lilipata nafasi ya kuona wachezaji wake kuanzia katika mazoezi mpaka kwenye mechi na kufahamu yupi wa kutumika wakati gani na kila sifa au ubora aliokuwa nao.
Ingekuwa sio sahihi kwa benchi la ufundi jipya kwenda kucheza mechi za ligi bila kupata mechi sahihi za kiushindani kuangalia wachezaji wake ili kupata mwanga wa kwenda kuutumia katika mechi hizo.
Aina ya timu ambazo tumecheza nazo katika mashindano haya kwanza ushindani na nchi ambazo wanatoka ni kama zile mbili za AS Vita na El Marreikh ambazo tupo nazo katika hatua ya makundi kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kuna vitu ambavyo ni wazi lazima vitakuwa vinashabihiana na kukutana navyo wakati huu ina maana tukija kukutana kwa awali ya pili havitakuwa vya kushangaza, bali itakuwa sehemu ya mazoea.
Kwa maana hiyo benchi la ufundi lilipata faida katika eneo hilo kutokana na mashindano ambayo hata mashabiki nao nadhani walipata burudani ya kuona kikosi chao kikichukua ubingwa.
Ukiangalia katika kikosi chetu kuna maingizo ya wachezaji wapya ambao nao kupitia mashindano haya walipata nafasi ya kucheza na kuzoeana na wale ambao tupo katika timu kwa muda mrefu.
Unajua ni jambo jema mno kwa mfanyakazi wa taasisi wa aina yoyote unakwenda kuanza kazi na kukutana na wakati wenye furaha ikiwemo kuchukua tuzo au heshima ambayo unaipata ukiwa kazini.
Jambo hilo linaweza kuwajenga wachezaji wapya na kutambia kuwa walikuwa na mwanzo mzuri katika timu mpya ambayo wameenda kufanya kazi na kuchukua taji mbele ya timu kubwa Afrika kama TP Mazembe na Al Hilal.
Mashabiki wetu wamepata nafasi ya kuangalia timu yao kwanza ikifanya vizuri dhidi ya timu kubwa Afrika. Waliwaona wachezaji wapya wakiunganisha nguvu na tuliokuwa katika kikosi na kile ambacho tutakwenda kukifanya katika mashindano. Kwa pande wa timu kiujumla kutwaa kombe hili morali itakuwa juu kwa kila ambaye anahusika na naamini tutakwenda na mafanikio haya mpaka katika mashindano yaliyopo mbele yetu.
Kikubwa mashabiki wetu wanatakiwa kuendelea kutupa nguvu mahala popote ambapo tunacheza na tuna imani msimu huu tutafikia yale malengo ambayo tumejipangia kutokana na ubora wa kikosi kilivyo na morali ya kila mchezaji.