Kila kona ni Yamal tu! kuwa kama yeye fanya hivi

Muktasari:
- Moja ya sababu ya gumzo ni kiwango alichoonyesha Jumapili kwenye Uwanja wa Lluis Companys Olympic, jijini Barcelona katika mchezo wa El Clasico dhidi ya mahasimu wao Real Madrid.
KINDA wa klabu ya Barcelona, Lamine Yamal, mwenye umri wa miaka 17 akiwa ameishacheza zaidi ya mechi 100 na kupata mafanikio makubwa, amekuwa gumzo kila kona duniani kutokana na umahiri wa kusakata kandanda.
Moja ya sababu ya gumzo ni kiwango alichoonyesha Jumapili kwenye Uwanja wa Lluis Companys Olympic, jijini Barcelona katika mchezo wa El Clasico dhidi ya mahasimu wao Real Madrid.
Katika pambano hilo Barcelona waliibuka mshindi wa mabao 4-3 ukikuwa mchezo mkali wa kuvutia huku macho mengi yakimtazama zaidi kinda huyo aliyekuwa akishirikiana vyema na Raphinha.
Barca walipoteza mechi zote tatu El Clasico msimu uliopita 2023/24, lakini msimu huu wameifunga Madrid mara nne ikiwamo mbili za LaLiga na fainali za Supercopa na Copa del Rey. Barcelona pia iliifunga Real Madrid 2-1 katika mechi ya kirafiki ya pre-season ya kujiandaa na msimu huu iliyochezwa Marekani Agosti 4, 2024, hivyo kuwabwaga wapinzani wao hao mara tano mfululizo.

Katika mechi zote hizo (ukiacha ile ya pre-season ambayo alipumzishwa), Yamal amekuwa chachu ya ushindi kwa kusaidia timu yake ikiwamo mchezo wa ligi Jumapili iliyopita ambayo Barca ilitanguliwa kwa mabao mawili kipindi cha kwanza. Kinda huyo alifunga bao na kusaidia kurudisha mabao na hatimaye kushinda.
Umri wake, udogo wa kimaumbile, uwezo wake wa kuwachambua mabeki kwa chenga adimu na mtindo wake wa kipekee wa kupiga krosi kwa upande wa funiko la mguu (maarufu kuupiga kofi mpira au trivela) vinamfanya kuhusudiwa sana na wapenda soka.
Vijiwe vya uswahili vyenye mabishano ya soka, mabanda ya kutazamia mpira, baa na mashindano ya soka ya mtaani, habari kubwa kwa wadau wa soka ni uwezo wa Yamal katika umri ule.
Uwezo wa kuwadanganya mabeki kwa chenga za aina yake na huku akitoa pasi za mwisho zinazosababisha mabao vinamtofautisha na wachezaji wa umri wake.
Kama vile haitoshi hata wanasoka wanaocheza ligi za hapa nyumbani NBC wamekuwa wakimfuatilia na kutoa maoni mazuri katika akaunti zao za mitandao ya kijamii.
Vijana wenye ndoto za kucheza soka la kimataifa ni vigumu kukwepa kuiga ufundi wa kinda huyu ambaye alijiunga katika akademia ya La Masia ya klabu ya Barcelona akiwa na miaka 7.
Akihojiwa mwishoni mwa mchezo wa El Clasico na vyombo mbalimbali, Yamal alieleza namna anavyojisikia furaha kubwa kufunga bao katika mchezo huo wa El Classico na kusaidia goli.
“Nadhani hivyo ndivyo unavyopaswa kucheza dhidi yao. Lazima ujionyeshe kama wewe ni timu bora na ufurahie, ndivyo hivyo,” alisema hayo akiwa mwenye kujiamini.
Wiki iliyopita katika mchezo wa nusu fainali UEFA dhidi Inter Milan, ubora wa kipa wa Inter ndio ulizuia mipira yake iliyoelekea nyavuni, vinginevyo yangeingia mabao mengi.
Aliyekuwa kocha wa Arsenal ambaye sasa ni Mkurugenzi Mkuu wa Maendeleo ya Soka FIFA, Arsene Wenger amenukuliwa akisema katika maisha yake ya soka hajawahi kuona mchezaji bora kama Yamal.
Safari ya mafanikio hayo imewachukua wataalam wa La Masia miaka 9 kuutengeneza utimamu wa mwili wa Yamal ambaye alitua hapo akiwa na umri wa miaka 7 akiwa tayari ana kipaji.

YANAYOMBEBA
1. Utimamu wa mwili
Hakuna shaka juu ya stamina na ukakamavu alionao kwa umri wake ambapo bado viungo vya mwili vinaendelea kukua na kukomaa.
Kocha wa Barca, Hansi Flick alisifu uchezaji na ukomavu wake katika kusaidia timu kutoka kutanguliwa kwa mabao mawili kwa mara ya saba msimu huu, akisema “niamini, hakika yeye si mtoto.”
Maneno haya ni sahihi kabisa, ila si tu kukomaa bali kwa ujumla wake yuko timamu kiafya.
Benchi la ufundi limetimiza wajibu wake kwa kumtengeneza vyema kwa mafunzo na mazoezi mbalimbali kiasi cha kuweza kuanza kuchezea kikosi cha kwanza Aprili 29, 2023 akiwa na umri wa miaka 15 na siku 290, dhidi ya Real Betis katika Ligi Kuu Hispania.
Kwa umri wake alionao ni lazima utimamu wake ulindwe na uboreshwe kwa lishe bora ya mwanasoka, mafunzo na mazoezi.
2 .Utulivu wa kisaikolojia na kihisia
Mchezaji asiye na hofu wala woga ni ishara ya kuwa timamu kisaikolojia na kihisia. Tazama utulivu wake na kujimini anapokuwa uwanjani na huku akionekana mwenye hisia chanya. Kabla ya mechi hiyo ya Clasico, video za Yamal zilisambaa zikimuonyesha akiwa katika chumba cha kuvalia cha Barca akicheza mchezo wa kushika mdomo wa chupa yenye kinywaji kuirusha izunguke hewani na kisha itue ikiwa imesimama kwa kitako. Hiki ni kiwango cha juu kabisa cha kujiamini kuelekea mechi kubwa na yenye presha zaidi katika soka la Hispania.
Mchezaji mwenye matatizo ya kisaikolojia ikiwamo hofu au woga na shida za kihisia ikiwamo kukosa furaha huwa katika hatari ya kucheza chini ya kiwango, kukosa umakini na kufanya uamuzi mbovu mchezoni.
3. Tabia na mwenendo
Umri wa miaka 17 ndio mara nyingi umri ambao balehe huwa zinaendelea. Tabia za kikorofi huwa ni kawaida kwa umri huo, hii ni kutokana na ushawishi wa makundi wa umri huo.
Tabia na mwenendo wa Yamal ni mzuri, hajaonyesha viashiria vya ukorofi ndani na nje ya uwanja. Tazama pale anapochezewa faulo, huwa mpole haonyeshi kutukana wala kutaka kulipiza.

4. Kutumia akili na uamuzi sahihi
Utulivu wake wakati wa kucheza umemfanya kutumia akili sana pale anapokuwa na mpira hutoa aina ya pasi ambazo wachezaji wachache hutumia staili hiyo.
Umakini, uamuzi sahihi na wa haraka, uwezo wa kujiratibu wa kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja kwa usahihi ni uwezo na utulivu wa kiakili.
Anapokuwa katika eneo la adui huwa hakurupuki, anajua wapi afanye uamuzi sahihi. Alibaini kuwa kipa wa Madrid ni mzuri katika mipira ya pembeni ambapo hutumia mtindo wa ‘Banana Chop’ kufunga.
Alimgundua amezidi upande wa kushoto kwake, alipopokea pasi tu haraka akapiga mtindo huo ambao Thibaut Courtois hakuweza kudaka mpira huo licha ya urefu wake wa mwili.
5. Wepesi na kunyumbulika
Mchezaji kuwa na wepesi na kunyumbulika kila uelekeo ni ishara ya kuwa utimamu kimwili. Kuzingatia mafunzo na mazoezi ya wakufunzi hivyo kumfanya kucheza kwa kiwango cha juu.
Hali yake ya uzito wa wastani na umbile vinamwezesha kukimbia kwa kasi na kukokota mpira, kuwapiga chenga mabeki wengi na kutoa asisti ya bao au kufunga yeye mwenyewe.
Kasi na Nguvu
Sifa kubwa ya mchezaji yeyote anayecheza pembeni kama winga ni kuwa na kasi, wepesi wake humfanya kuwapita mabeki eneo la chini katika wingi ya kulia.
Unaweza ukadhani kuwa umri wake na kilo 66 hana nguvu, kumbe sivyo. Tazama pale anapoumiliki mpira huweza kuumilki na kumzuia adui kwa mwili wake ili asimpokonye.
6.Lishe, mazoezi na mapumziko
Utamaduni wa shule ya soka ya La Masia unamjenga mchezaji kupata lishe maalum tangu kwa mtaalam lishe ya wanasoka kwa ratiba maalum.
Kila mchezaji kinda hulindwa na kuhakisha anapumzika katika mazingira bora na kulala muda wa saa 10 pasipo kusumbuliwa na chochote.
Ndani ya mazingira ya Akademia hiyo kuna viburidisha akili vya kila namna ikiwamo maeneo ya kuvutia kwa ajili ya burudani.
CHUKUA HII
Kuwapata kina Yamal kunahitaji shule za soka zenye mazingira bora na wataalam mbalimbali ikiwamo wakufunzi wa soka, walimu wa fiziolojia ya michezo na watalaam wa afya.