KIJIWE CHA SALIM SAIDI SALIM: Titi Camara Jina linalotesa soka la Guinea

KWA nilivyofuatilia kwa karibu klabu na timu ya taifa ya Guinea hakukosekani angalau wachezaji wawili wenye jina la Camara. Nilielewa zaidi umaarufu wa jina hilo Guinea (kwa lugha ya kwao maana yake ni mwalimu) nilipofika nchin humo 1975.
Nilichogundua ni katika kila walipokuwepo wanaume wanne au watano kulikuwa hakukosekani mtu anayeitwa Camara.
Nilipotembelea ubalozi wa Tanzania uliopo Conakry 1975, siku zile balozi akiwa Hayati Idris Abdulwakil (baadaye Rais wa Zanzibar (1985-90), nilikuta wafanyakazi wawili walioitwa Camara mkubwa na Camara mdogo pale ubalozini.
Timu ya Hafia (wanajeshi), wakati ule ikiwa chini ya usimamizi wa Rais wa nchi hiyo, Ahmed Sekou Toure (jina lake hasa ni Ahmed Tahir) niligundua ilikuwa na kina Camara wengi. Ninaowakumbuka ni kipa kerfalla Camara, Drogba Camara, Sekou Camara, Youssef Camara na Papa Camara.
Hivi karibuni tulitembelewa na klabu ya Horoya (maana yake ni uhuru kwa kukopa neno la Kiarabu Huriya) Guinea ambayo sasa kwa kiasi fulani imeipiku Hafia katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi.
Hii inatokana na mmiliki wake ambaye ni mmoja wa wafanyabiashara wakubwa wa Afrika Magharibi na ambaye ndiye rais wa Shirikisho la Kandanda la Guinea kawekeza sana katika timu hiyo, ikiwa pamoja na klabu kuwa na chuo cha michezo.
Kikosi cha Horoya ambacho kina wachezaji wanne katika timu ya taifa ya Guinea ilikuja na kina Camara saba. Nao ni Musa Camara, Mohamed Camara, Alseny Camara, Fode Camara, Ismail Camara na Doula Camara.
Kwa miaka mingi wachezaji wenye majina ya Camara waliwika sana Guinea hasa katika miaka ya 1970 na 1980 wakati nchi hii ilipokuwa kileleni katika medani ya soka Afrika. Nakumbuka Hafia ilipokuwa inacheza na Simba mwishoni mwa miaka ya 1970 kocha wa Simba, hayati Paul West Gwivaha aliwasihi mabeki wa Simba wazibe mianya ya Camara kuingia na mpira eneo la hatari.
Beki wa kati wa Simba, Chogo, akamuuliza kocha ni Camara yupi kwa sababu kikosi kilikuwa na kina Camara watano na wawili walikuwa washambuliaji.
Gwivaha akawaambia yule mrefu aliyevaa namba 10 (sikumbuki hasa jina la pili, isipokuwa ni Camara). Lakini mashabiki wa kandanda wa Guinea wanasema kina Camara wapo wengi katika soka la Guinea, lakini ni wawili tu ndio hasa walimu na wengine feki.
Hao wawili ni Naby Laye ‘Papa’ Camara aliyekuwa nahodha wa Guinea kwa zaidi ya miaka sita katika miaka ya 1970 na kuiaga dunia miaka mitatu iliyopita akiwa na miaka 66.
Mwingine ni Aboubacar Sidiki Camara ambaye ndiye nitamzungumzia hapa kwa muhtasari. Hii ni kwa sababu wakati zamani akitamba katika soka siku hizi anafanya hivyo katika siasa za Guinea.
Aboubacar Sidiki Camara, maarufu kwa jina la Titi Camara alizaliwa Novemba 17, 1972 alikuwa beki wa kutegemewa wa Guinea na baadaye kocha wa timu ya taifa na pia Waziri wa Michezo wa nchi hiyo kwa miaka karibu mitatu.
Camara alivuliwa wadhifa huo 2012 pale alipopinga kuwepo matumizi makubwa ya silaha na kutaka fedha hizo zielekezwe kwenye michezo. Alipata umaarufu mkubwa alipoondoka Guinea kwenda kuichezea Liverpool ya England 1999–2000 na kuifungia mabao 10. Kabla ya hapo Titi Camara alizichezea klabu za Saint-Étienne, Lens na Marseille za Ufaransa.
Camara ambaye tabia zake huwaacha watu wengi wakipigwa na butwaa aliwashangaza watu wetu wengi katika Uwanja wa Anfield aliposhuka akiwa na kikosi cha Liverpool kwenye mechi dhidi ya West Ham United, ikiwa ni Oktoba 1999, siku moja tu baada ya kumzika baba yake nchini kwao Guinea.
Siku iliposhuka uwanjani alipiga magoti, akasujudu huku machozi yakimtoka na kunyanyua mikono juu kumshukuru Mungu na baada ya hapo akajipanga kuichezea Liverpool.
"Baba ameshatangulia mbele ya haki. Namuombea malazi mema na mimi lazima nijitume ili wajukuu wake wawe na maisha bora. Haifai kuweka huzuni baada ya kiumbe kuzikwa," alisema Camara.
Baadaye aliichezea West Ham United baada ya kuingia mkataba wa Pauni 1.5 milioni Desemba 21 2000 na nusu ya hizo fedha akatumia kujenga msikiti na madrasa, na kutoa sadaka kwa familia masikini kijijini kwao kama sadaka ya baba yake.
Vilevile aliichezea klabu ya Al Al-Ittihad ya Saudi Arabia msimu wa 2002–03. Titi Camara alikuwa na timu ya taifa ya Guinea kuanzia mwanzo wa miaka ya 1990 hadi mwanzo wa miaka ya 2000. Mwezi Mei 2009, alichaguliwa mkurugenzi wa Ufundi wa timu ya taifa na baadaye kocha wa timu hiyo.
Desemba 28, 2010, Camara aliteuliwa Waziri wa Michezo wa Guinea na Rais Alpha Condé, akiwa mwanamichezo wa kwanza katika nchi hiyo kuteuliwa kuwa waziri. Lakini kutokana na kumshutumu Rais Conte kwamba alijali zaidi afya za askari na sio wananchi waliokuwa na shida za maisha na wanamichezo, alifukuzwa kazi.
Mara kwa mara siku hizi Titi Camara husikika akiwa amekamatwa na polisi kuhojiwa kwa tuhuma kadhaa kutokana na hotuba zake kali katika majukwaa ya kisiasa na mara chache hufika viwanjani kuangalia kandanda.