Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

KIJIWE CHA SALIM SAIDI SALIM: Myrtle Alice Cook Mwanamama wa Canada

MACHI 18, karibu katika kila mji wa Canada palifanyika bonanza la kumuenzi mwanamama Myrtle Alice Cook, anayejulikana kama Mama wa Kwanza wa Michezo wa nchi hio aliyefariki miaka 38 iliopita.

Mwanamama huyu aliacha historia ya aina yake kwenye mchezo wa riadha kwao Canada na duniani na kwa miaka 20 kuanzia 1932 hadi 1972, alishiriki kila michezo ya Olimpiki na kuwa kivutio cha watazamaji na waliofuatilia michezo.
Alianza kushiriki kama mwanariadha, kabbla ya kuwa mwalimu wa wanariadha wanawake wa Canada na alipostaafu kufundisha alikuwa meneja wa timu hiyo katika mashindano ya kimataifa.

Mwishowe alishiriki michezo kwa kutumia kalamu na sauti yake kama mwandishi na msimuliaji wa habari za michezo.
Uchambuzi wake wa michezo, hasa riadha, uliwavutia wasomaji magazeti, wasikilizaji wa redio na walioangalia runinga. Vile vile alizitumikia Kamati za Kimataifa za michezo ya Olimpiki na Jumuiya ya Madola.

Siku moja aliiudhi timu ya soka ya Peru ilipofungwa 2-0 na Uruguay kwa kusema labda Peru walikuwa hawajui mshindi hupatikana kwa kufunga mabao na sio kuhesabu chenga na kona.
Hii ilitokana na kutoa takwimu za chenga zilizoonyesha Peru waliwazidi Uruguay mara mbili na kuwataka walioandaa mashindano kutoa zawadi maalum kwa Peru kwa vile wachezaji wake walikuwa wapigaji chenga wazuri.

Alifanya utani kwa kusema Peru hawakutaka kuwaudhi Uruguay kwa kuwatikisia nyavu yao na kuongeza sio kila mimba huzaa mtoto na zile walizozitunga Peru hazikuzaa mabao kwa vile ziliharibika zikiwa changa.
Wachezaji wa Peru walipomtaka aombe radhi, aliwaambia wakirudi kwao wawaombe radhi wananchi wa Peru kwa kujali zaidi chenga badala ya kutafuta mabao. Lakini baadaye alikwenda Peru kuomba radhi.

Myrtle Alice Cook, alikuwa mmoja wa wasichana sita waliounda  kikosi cha mauaji cha wanariadha wa Canada kilichotamba miaka ya 1920 na kung’ara katika Olimpiki ya 1928 iliyofanyika Amsterdam, Uholanzi.

Mwanamama huyu pia alitoa mchango mkubwa katika harakati za kupigania haki za wanawake katika michezo.
Mnamo 1928 wanawake walipopewa nafasi ya kushiriki kwa mara ya kwanza katika Olimpiki kule Amsterdam, Cook alikuwa mmoja wa washiriki, licha ya kelele nyingi Canada za kupinga kupeleka wanawake katika michezo hiyo.

Hali ilibadilika baada ya michezo kwa kikosi walioitwa wauaji kufanya vizuri  na kupokewa kama mashujaa waliporudi nyumbani.
Watu wapatao 200,000 walifika stesheni ya treni ya Toronto kuwapokea na wapatao 100,000 walijipanga barabarani kuwashangilia.
Dada huyu alikwenda kwenye Olimpiki akitumainiwa kunyakua medali ya dhahabu katika mbio za mita 100 kwa vile wiki chache kabla aliweka rekodi ya dunia ya mbio hizo katika Jiji la Halifax, Canada.

Hata hivyo, katika Olimpiki alipambana na mkosi ambao kwa miaka mingi hadi alipofariki dunia aliuzungumzia kwa masikitiko na kusisitiza alionewa.
Alitolewa katika fainali kwa madai mara mbili alichomoka kuanza mbio kabla ya fataki haijafyatuliwa.

Hata hivyo, alikuwemo katika kikosi cha mbio za kupokezana vijiti za mita 100x4 na alipangwa kuwa wa kwanza, lakini alikataa na kuomba amalizie kwa kuhofia atatolewa tena katika mashindano.
Viongozi wa timu yake walipomtaka abadili uamuzi wake aliwaambia watafute kamusi na wapekue neno 'Sitaki' ili wafahamu maana ya neno hili na ndipo wangelielewa alichokuwa anasema na hatimaye ombi lake lilikubaliwa.                  

Cook alipopewa kijiti wakimbiaji wawili walikuwa mbele yake, lakini alitimka kama swala aliyekuwa anawindwa na chui na kuwa wa kwanza kufika kwenye kamba na Canada kunyakua medali ya dhahabu, huku ikifuatiwa na Marekani.
Wakati watazamaji wakishangilia Cook alikwenda kwa mwamuzi aliyemtoa kwenye mbio za mita 100 na kumuuliza je, lipo kosa alilofanya ili anyimwe medali ya dhahabu?

Alipokabidhiwa medali alimpelekea yule mwamuzi na kumwambia alimzawadia, tukio ambalo lilizusha kasheshe na baada ya kubembelezwa aliondoka na medali yake huku akitabasamu.
Myrtle Alice Cook alizaliwa Toronto tarehe 5 Januari, 1902 na tangu akiwa mdogo alipenda michezo na wakati mwingine alishindana na wanaume. Alikuwa hodari kwa tenisi, mpira wa magongo kwenye barafu, mpira wa kikapu, mbio za baiskeli, riadha na ngalawa.

Alipotimia miaka 15 aliingizwa katika kikosi cha taifa cha riadha na alishiriki mbio za mita 100 na yadi 60 na kuweka rekodi za Canada, Marekani na dunia.
Katika mwaka 1923 alianzisha klabu ya riadha ya wanawake wa Toronto na baadaye kufungua tawi katika mji wa Montreal.
Baada ya kushiriki mashindano aliwafundisha riadha wasichana na akawa kocha wa baseball wa klabu ya  Royal ya Montreal. Hii ilikuwa klabu pekee ya wanaume ya mchezo huu kuwa na kocha mwanamke.

Wakati wa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia (1938-45) aliajiriwa kutoa mafunzo ya kijeshi kwa wanawake na wakati huo alikuwa ameanza kuandika habari za michezo, kazi ambayo aliyoifanya kwa miaka 40 hadi 1969.
Wakati mmoja alikuwa na gazeti la Montreal Star ambalo mumewe naye aliliandikia akiwa mwandishi wa habari za michezo na mara nyingi aliulaumu uchambuzi wa mumewe.
Mwanamama huyu alikuwa karibu na mashindano ya riadha ya kimatifa katika maisha yake yoyote kwa kuwemo  kila kamati ya michezo ya Jumuiya ya Madola na Olimpiki kutoka 1932 hadi 1972 alipostaafu.
Aliiaga dunia Machi 18, 1985 akiwa na miaka 83 akiacha kumbukumbu nzuri katika riadha na ya uandishi wa habari za michezo.

Jina lake limeingizwa katika Ukumbi wa Wanamichezo Mashuhuri wa Canada na vitabu vingi vimeandikwa kuelezea maisha yake.
Mchango wa mama huyu kama mwanariadha mzuri na mwenye maudhi, mwalimu na mshiriki katika michezo mbalimbali, meneja na kiongozi wa kamati za kimataifa za riadha hautasahaulika.
Ataendelea kukumbukwa kwa heshima na vichekesho vya tabia yake kwao Canada na nje na zaidi katika michezo ya Jumuiya ya Madola na Olimpiki.