Kiduku: Niliruka ukuta, nikadakwa na Polisi

HAIKUWA rahisi kuwakwepa polisi, ingawa ailazimika kutumia akili ya ziada ili kuondoka mikononi mwao na safari ya bondia Twaha 'Kiduku' Kassim kupenda ngumi ikaanzia kwenye tuko hilo.
Anasema alilazimika kuruka sen'genge ya uwanja wa Jamhuri, mjini Dodoma ili kukwepa kipigo cha polisi hao ambao kama wangemtia mikononi, hajui nini kingemkuta.
"Kulikuwa na pambano kubwa wakati huo Morogoro na Deo Njiku na mtu mmmoja alikuwa akijiita Afande Kidila, nikajiuliza hivi hasira za mabondia kupigana huwa zinatoka wapi.
"Nikasema ngoja niende Jamhuri nishuhudie watu wanawezaje kupigana bila kuwa na ugomvi, nimefika uwanjani, kiingilio ilikuwa ni Sh 500 na hiyo pesa sina.
"Niliomba getini, walinzi wakanikazia, nikaishia kukaa nje kwa muda mrefu, nikiwa nimekata tamaa natoka, nikaona watu wakubwa naruka ukuta kuingia uwanjani, nikasema na mimi napita nao hapa hapa," anasimulia Kiduku.
Anasema alipojiridhisha ni salama, akadandia ukuta na kutumbukia ndani ya uwanja, ile anashuka tu ndani, askari tayari wamepata taarifa na kuwa mbele yake.
"Uwanja wa Jamhuri kulikuwa na nyavu zimezunguka eneo la uwanja (pitch) ambako ndiko mashabiki walikuwa wamekaa kuangalia ngumi.
"Wale askari walikuwa mbele yangu, siwezi kuchomoka, nikapata akili ya haraka haraka nikaruka zile nyavu za Jamhuri nikajichanganya na mashabiki wengine.
"Wale askari walinisaka, nilikuwa mdogo mdogo, nikajichanga katikati ya watu, hawakunipata, nikasema asante Mungu, maana wangenikamata sijui nini kingenikuta," anasema.
Anasema siku hiyo ndiyo ilikuwa mara yake ya kwanza kuangalia ngumi na kutokea kuupenda mchezo huo.
"Niligeuka shabiki wa Deo Njiku, nikaanza kumshangilia mwanzo mwisho, lakini ghafla nilijikuta nimekuwa kimya hata yale makelele ya mashabiki sikuyasikia, nilikuwa nawaza kwamba hata mimi nikifanya mazoezi, mbona kama naweza kufanya kile ambacho Njiku anakifanya pale.
Anasema wakati ule, Njiku alikuwa ni bondia mkubwa Morogoro, ukimuondoa Francis Cheka aliyekuwa bondia wake wa kwanza kumfahamu.
"Cheka nilimfahamu ikiwa nyumbani, wakati huo ni mdogo nikasikia makelele nje, nikatoka nikakuta kundi kubwa la watu barabarani wakiimba na kucheza, nikualiza kuna nini, wakanijibu kuna bondia anaitwa Francis Cheka ndiyo mapokezi yake ametoka kumpiga mtu Dar es Salaam.
"Hata hivyo sikushughulika nao sana, hadi ilipotokea hili pambano la Deo Njiku ambaye baadae ndiye bondia niliyekuja kumpiga na kuchukua mkanda wa ubingwa wangu wa kwanza kwake,".
AJIFANYA KOCHA, MAOMBI YAMUOKOA
Kiduku anasema baada ya kukoswa koswa na Polisi Jamhuri, aliporudi mtaani kutokana na kuwa na shauku na ndondi, alianza kujifanya ni kocha wa mchezo huo.
"Sikuwa nafahamu lolote kuhusu ngumi, nikajikuta tu nawakamata vijana wangu kama watatu mtaani na kuanza kuwafundisha.
"Nilikuwa na shauku tu ya ngumi, siku moja akatokea bondia anataka sparing (mazoezi ya kuzichapa ana kwa ana) hapo ndipo kimbembe kilianza.
"Wale vijana wangu waliulizwa kocha wenu yuko wapi? wakanionyesha ni mimi, ukizingatia sijawahi hata kupigana, kifupi nilikuwa sijui lolote kuhusu ngumi.
"Sikutaka kuwa mnyonge, nilijitutumua mbele ya wanafunzi wangu, nikawambia nyie tulieni, huyu nitamuonyesha mimi ni nani, lakini moyoni ni tofauti kabisa.
"Sasa kama hivi kesho ndiyo siku ya sparing, nilikuwa nasujudu namuomba Mwenyezi Mungu anisaidie nisidhalilike mbele ya wanafunzi wangu ambao wakati ule walikuwa wakijua mimi ni kocha kweli wa ngumi, wakati sina lolote,".
Anasema, hofu yake kubwa ilikuwa ni kama atapigwa namna ambavyo heshima yake itashuka, hivyo kwa kuamini Mungu ndiyo kila kitu alikuwa akiomba kweli kweli, licha ya kwamba alikuwa na presha kubwa kuhusu sapring hiyo.
"Mungu alinisaidia kwenye sparing nikampiga yule bondia, pale ndipo jina langu likaanza kukuwa na wanafunzi kuongezeka walifika hadi 30, kumbuka wakati huo sijawahi kucheza ngumi, lakini nawafundisha hivyo hivyo na wananiamini balaa.
"Mwisho wa siku pale mazoezi kwetu wakaanza kuja mabondia wenye renki na kuomba sparing, nikawa nawagonga, ndipo watu wakanishawishi kwanini Kiduku usipigane ulingoni, nikasema mimi hapana, ngumi zangu ni za mtaani tu, hizo za ulingoni sizitaki,".
Anasema alishawishiwa mara kwa mara, lakini mwisho wa siku akasema isiwe kesi, ngoja aende ili kuwaridhisha.
AKUTANA NA KOCHA
Anasema siku moja alikwenda kwenye klabu ya DDC, Morogoro ambako kocha wake wa sasa, Pawa Ilanda ndiye alikuwa akifundisha.
"Walinipokea wakijua ni bondia natokeo kwenye gym nyingine, wakanipa sparing na Kudra Tamim ambaye kule kwenye timu yangu nilikuwa namfundisha pia, hivyo nikawa namgusa gusa tu.
"Nikapewa bondia mwingine naitwa Mwanafyale nikafanya hivyo hivyo, kwenye ile klabu bondia mkubwa alikuwa Cosmas Cheka, wakaniuliza vipi pumzi bado ipo tukupe mwingine, nikasema ndiyo, wakaniambia basi cheza na huyu (Cheka).
"Pale ndipo nilisema natokea, nikajiapiza kumuwashia moto, raundi ya kwanza tu akapaniki, mazoezi yalivyoisha Pawa Ilanda akaniuliza wewe unatokea gym gani? nikamwambia nipo tu mtaani, akaniuliza kuhusu kocha wangu, nikamwambia sina.
"Kila mmoja pale alishangaa, hawakuamini kama sina gym wala kocha kwa jinsi nilivyofanya, wakasema kwa namna nilivyofanya, nikipata kocha nitafika mbali, huo ndio ukawa mwanzo wa kuanza kufundishwa na kocha Ilanda,".
MESEJI YA VITISHO
Kiduku anasema akiwa kwenye gym hiyo, alipata pambano la kwanza kabisa, lakini wakati huo mkono wake wa kulia ulikuwa mbovu.
"Uliteguka mazoezini na kuvimba sana, lakini kwa kuwa ndiyo lilikuwa pambano langu la kwanza, nilisema nitakomaa na kupigana hivyo hivyo.
"Siku ya pambano, nikiwa ukumbini nafanya warm up (kupasha) nilikuwa na simu ndogo mkononi, meseji ikaingia na hadi leo sikuwahi kufahamu ile meseji ilitumwa na nani kwangu.
"Ilininyong'onyesha sana, kwa dakika kadhaa nilisimama na kuangalia jukwaani, hata hamu ya kuendelea kupasha nilikosa, lakini sikumfahamu aliyeituma.
"Ilisema hivi, wewe 'mbwa' nakuona hapo kudadeki zako unavyoruka ruka, leo unapigwa vibaya sana, nilistuka na kuishia kuangalia jukwaa labda nimuone mtu ambaye amenitumia ile meseji lakini wapi na hadi leo sikumfahamu.
"Hata hivyo haikunitoa mchezoni, ila nilisikitika, nikasema ngoja nimuonyeshe huyu jamaa mimi ni nani, kipindi hicho natembea sana ulingoni, nikipiga jabu, left upper cut lazima ukae, na ndicho nilifanya,".
MAPAMBANO MATANO BURE
Licha ya kucheza akiwa na maumivu na bado akashinda pambano hilo, Kiduku anasema aliambulia malipo ya Sh 20,000 ambayo ilikuwa ni pesa yake ya kwanza kubwa kuipata kwenye ngumi.
"Malipo ilikuwa ni changamoto kubwa, wakati mwingine nilitamani kuachana na mchezo wenyewe, kuna watu waliniambia usikate tamaa, tengeneza jina kwanza.
"Mapambano matano yaliyofuata nilipigana bure, ilifikia kipindi huelewi, unafanya mazoezi makali, ukitoka unaishia kunywa chai na maandazi matatu, wakati mwingine mchana ni hayo hayo na kama siku haiko vizuri ndiyo inakuwa hivyo hivyo hadi usiku.
"Nilimuomba Mungu sana anisimamie, maana kwenye ngumi hupati kitu, ilifikia kipindi nikawa naona napigana tu, lakini nilijiambia sitakiwi kukataa tamaa.
"Nilitamani kucheza pambano ambalo litanitambulisha kwanza Morogoro, ndipo nikapata la Deo Njiku, ambalo nililipwa laki nane ambayo ilikuwa ni pesa nyingi sana kwangu, ingawa sikumbuki niliifanyia nini ile pesa, lakini ndipo mkanda wangu wa kwanza niliupatia kwake,".
MBABE AMUACHIA ALAMA
Kiduku bondia namba moja nchini kwenye uzani wa super middle na wa 73 kati ya 1441 duniani amepigana mapambano 30, lakini yaliyomtesa ni mawili pekee.
"Kuna moja nilishinda kwa KO (Knock out) huko Zambia dhidi ya Mbiya Kanku, ili pambano nilipigana kweli kweli, lakini la Dullah Mbabe (Abdallah Pazi) ni pambano ambalo lina historia kwangu,".
Ilikuwa ni Agosti 20,2021, Mbabe alipochapwa kwa mara ya pili na Kiduku, baada ya awali, 2017 kuruhusu kipigo, mapambano yote yakiwa kwa pointi.
Kwenye marudiano, raundi ya kwanza, Kiduku alichapwa konde lililompeleka chini, Mbabe akiamini ameshinda kwa Knock Out, lakini ikawa tofauti na kibao kikageuka raundi zilizofuatia.
"Ni pambano langu la kwanza katika historia ya maisha yangu ya ngumi kwenda chini kwa punch, haikuwahi kutokea kabla tangu, kwa mara ya kwanza ilinitokea kwa Dullah.
"Mimi ni mbishi, lakini siku ile nilienda chini, nilikutana na Champion (Dullah) aliyenipiga punch (konde) nikaenda chini.
"Namshukuru Mungu alinipa subira, nikapata uvumilivu na kusimama tena nikapambana hadi kushinda kwani ni mabondia wachache sana kaa wanaoweza kukalishwa raundi ya kwanza kisha akasimama na kupambana tena," anasema.
Anasema kocha wake alimuweka sawa, alimwambia Twaha umeangushwa, lakini bado una nafasi ya kuwa sawa.
"Bado nilikuwa na wenge, akaniambia raundi bado ziko nyingi, rudi kapigane, ni heri upigwe KO, lakini kapigane naye mwanzo mwisho usimuachie nafasi, ile kauli ilinipa nguvu.
"Nilivyorudi ilikuwa kama kafungulia nyuki, nikasema kama Dullah unataka kunipiga, basi nipige KO na si vinginevyo, ikawa mi tit for tat (piga nikupige), sikurudi nyuma hadi pambano likaisha na kushinda,".
Anasema huyo ndiye bondia pekee katika maisha yake ya ngumi aliyempeleka chini, historia ambayo ilimuumiza na kumjenga pia.
NYUMBANI ANAFANYA HIVI
Kiduku ambaye ana mjengo wake huko Mazimbu, mjini Morogoro ni mume na baba wa watoto watatu, ingawa kati ya wanae, anasema hakuna aliyefuata nyayo zake.
"Japo kuna mmoja ni wa kike ni kauzu, ukimchapa halii, natamani roho ya huyu angeichukua kijana wangu wa kiume, labda angeingia kwenye ngumi, binafsi huwa sipendi kuona wanawake wakicheza ngumi.
"Nahisi kama wanaumia, lakini huyu binti yangu japo wanafuatilia na nikiwa nacheza wanafahamu na hata wakati ninapokwenda mazoezi huwa nawaaga kuwa nakwenda kazini, lakini hakuna anayeonyesha dalili za kufuata nyayo za ngu.
Bondia huyo anasema akiwa nyumbani anapenda zaidi kulala kwani anahitaji muda wa kutosha kupumzika.
"Lakini pia kuwa na familia, mimi ni mtu wa utani, nikikaa na mwenzangu kidogo, yaani wifi yako na wanangu utakuta tunacheza ukuti, kindumbwe ndumbwe na kutaniana sana, hayo ndiyo maisha yangu, mimi ni mtu wa masihara na utani nikiwa nyumbani," anasema baba huyo wa watoto watatu.
KAMA SIO NGUMI ANGEKUWA HUKU
Kabla ya kuingia kwenye ngumi, Kiduku anasema alipenda sana kuwa dereva wa magari makubwa au mwanajeshi.
"Ndoto zangu hazikutimia kulingana na mazingira, ila ni kazi ambazo nilizipenda kwa moyo wangu wote.
"Nilipenda udereva nilipokuwa nikiwaona wa yale magari ya zamani namna walivyokuwa wakiingiza gia, ni kazi ambayo niliipenda lakini sikupata fursa hiyo kama ilivyokuwa ya jeshi." anasema.
Anasema pamoja na kutotimiza ndoto hizo, ngumi zilikuja kuwa mkombozi wa maisha yake, zimemheshimisha.
"Zimefanya leo nikisimama mbele za watu nathaminika, kila kitu ninachomiliki kuanzia magari, saluni na nyumba yote ni kwa ajili ya ngumi, mimi kwa sasa kufanya kazi nyingine siwezi, kwangu ni ngumi tu.
"Nikiwa na wanangu huwa nawambia naenda kazini, ngumi ndiyo ofisi yangu, baada ya ngumi utanikuta saluni kwangu Kiduku Barber shop pale Mazimbu road nikisaidiana na vijana kunyoa.
"Tunanyoa staili zote, ingawa kwangu mimi najua moja tu ya kipara, niko fiti kwenye staili hiyo, ingawa nyingine zote vijana wapo wamebobea mimi huwa nawasaidia tu,".
DIET YAKE IPO HIVI
Kiduku ambaye kwa miaka kadhaa sasa amekuwa chini ya meneja wake, Ibrahim Nyange anakwambia uwezo wake ni kula kuku mzima kwa siku.
"Kwenye chakula huwa sichagui, kwani sina limit kwamba hiki usile hiki kla, hapana, nikimaliza kufanya mazoezi lazima nile sana, huo ndiyo utaratibu wangu," anasema.
Anasema akiwa na pambano, wanakubaliana na menejimenti yake kama aingie kambini au ajifue akitokea nyumbani.
"Nina nidhamu ya mazoezi sana, nikiwa na pambano, menejimenti yangu inaamua, ingawa mara nyingi najifua kwa miezi miwili au mitatu kutegemea na pambano, ingawa pia kama sina pambano la karibuni, huwa nafanya mazoezi ya kuniweka fiti tu,".
STAILI YA TATOO
Akipanda ulingoni, Kiduku ana staili ya kujichora tatoo, eneo la kifuani, mikononi na mgongoni, ambazo anasema baadhi zinabadilika na nyingine hazibadiliki.
"Najichora kwa hena ambayo inafutika, niliamua kuwa na staili hii ili kubadili muonekano, lakini alama yangu kubwa ambayo haibadiliki ni ya moto na logo ya shoo shoo (hii ni kauli mbiu yake).
"Kwa sasa ukiachana na hii alama ya moto ambayo inaashiriki Kiduku ni moto, kifuani nimeandika RIP Daddy (pumzika kwa amani baba), nilikuwa nampenda sana lakini mwenyezi Mungu amempenda zaidi.
"Pia nimechora alama ya nyota, mkononi nimechora picha ya meneja wangu, Ibrahim Nyange kwa kuwa amekuwa ni mtu anayejitoa zaidi kwangu na si vibaya kuonyesha shukrani hiyo, kabla sijamuweka yeye nilikuwa nimechora upinde.
Anasema Nyange ni miongoni mwa watu waliofanikisha kufikia kwenye renki hiyo ya ngumi hadi sasa.
"Alianza kunisapoti zamani kidogo, wakati huo hata mfukoni sielewi, alikuwa akinitia moyo mara zote na kunitaka kupambana, wakati huo bado hajawa meneja wangu.
"Nilikutana naye kwa mara ya kwanza alikuja kuangalia moja ya mapambano yangu, siku moja nikaenda gym kwao wakati huo anapiga chuma, pale nikawa karibu tukabadilishana mawasiliana, akawa ananisapoti na kunisihi nipambane kwani ngumi ndiyo maisha yangu hadi alipokuja kuwa meneja wangu mpaka sasa,".
MAPAMBANO YA NDANI YANALIPA
Kiduku ambaye tangu mwaka jana, hajatoka nje ya nchi kwenda kupigana anasema hivi sasa mapambano ya ndani yanalipa zaidi tofauti na aliyokuwa akipigana nje.
"Sioni sababu ya kutoka kama pesa ambayo naipata nchini ni zaidi ya ile ambayo nikienda kupigana nje ya nchi siipati, hivyo sina haja ya kutoka, labda niletewe dau kubwa zaidi," anasema.
Bondia huyo anasema yeye na menejimenti yake hawachagui bondia wa kupigana naye, yoyote anayekuja mbele yake yuko tayari.
"Kikubwa ni kwamba napigana na bondia wa aina gani, nikimpiga nafaidika na kitu gani? ana rekodi gani? sio nicheze kwa sifa, ikitokea renki yake ikawa bora, ndipo tunarudi sasa kwenye maslahi, kama ana faida au hana faida hapo maslahi ndiyo yataamua, ila yoyote mimi nacheza naye,".
Anasema nchini kwa sasa ngumi ziko juu na mabondia wanalipwa vizuri kulinganisha na miaka ya nyuma akijitolea mfano yeye.
"Pesa ninayoipata hapa Tanzania ni nyingi kuliko zile ambazo nimekuwa nikilipwa nikienda kupigana nje, hivyo sioni sababu ya kutoka, lazima tupigane kwa malengo, ingawa nikipata pesa nzuri zaidi ya hapa nitakwenda kupigana huko," anasema.
Anasema kwa sasa anapata riziki nzuri inayotosha kuendesha maisha yake na famiia huku vijana wanaomzunguka wakihamasika kufuata nyanyozake, wengine wakitamani kuwa kama Dullah, Class na wengineo wanaofanya vizuri hivi sasa.
MIKANDA TISA
Baada ya karibuni kutwaa mataji ya UBO na PST, Kiduku sasa aefikisha mikanda tisa ya ubingwa ukiwamo wa Afrika mashariki na kati, WBF, TPBC na WBC.
"Nina mikanda tisa, hadi ile ya kipibdi hicho imechora Simba yupo kama mtu, lakini ndiyo ilinipa chungu hadi kupata hii mizuri, naiheshimu hii mikanda,".
Anasema, hakuna mafanikio ambayo yanakosa changamoto, kwani kuna wakati alihangaika na akakosa mtu wa kumuomba chochote,
"Lakini mwisho wa siku unamuomba Mwenyezi Mungu akupe mafanikio, hautakiwi kukata tamaa, mimi binafsi nashukuru Mungu kwa kweli nimepiga hatua kupitia ngumi,".