Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kiapo cha mapambano Algeria 'NGUVU MOJA'

Simba Pict

Muktasari:

  • UKIKUTANA na shabiki yeyote wa Simba, wee mwambie tu; ‘Nguvu Moja’. Hapo utaukosha moyo wake, kwani hiyo ndio kauli mbiu ya klabu, ikiwa na maana ya kuunganisha nguvu katika mapambano yao kisoka, likiwamo la leo likiwa la kwanza ugenini kwa mechi za makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.

UKIKUTANA na shabiki yeyote wa Simba, wee mwambie tu; ‘Nguvu Moja’. Hapo utaukosha moyo wake, kwani hiyo ndio kauli mbiu ya klabu, ikiwa na maana ya kuunganisha nguvu katika mapambano yao kisoka, likiwamo la leo likiwa la kwanza ugenini kwa mechi za makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Ili kukoleza mzuka wa kauli mbiu hiyo ni kwamba kila mwanasimba atakuwa anaomba dua njema kimyakimya kutaka kuona Simba ikitoka na ushindi mbele ya CS Constantine ya Algeria katika mechi hiyo ya pili ya Kundi A kwa timu hizo zinazokutana kwa mara ya kwanza katika michuano hiyo ya CAF.

Simba tayari ipo katika mji wa Constantine, Algeria kukabiliana naCS Constantine ikiwa na kumbukumbu ya ushindi wa nyumbani wiki iliyopita dhidi ya Bravos do Maquis ya Angola kwa penalti ya Jean Charles Ahoua.

Timu hizo zinavaana kwenye Uwanja wa Chahid Hamlaoui kuanzia saa 1:00 usiku chini ya mwamuzi kutoka Malawi, Godfrey Nkhakananga atakayesimama pale kati kuzihukumu kwa dakika 90 za mtanange huo.


Simba 04

Hakuna namna ya kufanya kwa Simba zaidi ya kutoka na ushindi au angalau sare ikiwa ugenini kwa nia ya kuiweka pazuri kutinga makundi kutoka kundi hilo lenye vigogo wengine wa CS Sfaxien ya Tunisia ilianza michuano hiyo kwa kukandwa nyumbani bao 1-0 na Waalgeria wiki iliyopita.

Rekodi zinaonyesha, Simba ilipokwenda Algeria kucheza mechi za CAF haijawahi kuwa na matokeo mazuri, kwani kuanzia mwaka 2010 hadi sasa Simba imeenda nchini humo mara mbili na leo i ya tatu kwao dhidi ya vinara hao wa Ligi Kuu ya Algeria.

Mara ya mwisho Simba kucheza katika ardhi ya Algeria ilipoteza 2-0 mbele ya JS Saoura ikiwa ni mechi ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikipigwa Machi 9, 2019, lakini kabla ya hapo 2012 Simba ilipoteza pia kwa mabao 3-1 kwa ES Setif katika mchezo wa raundi ya kwanza Kombe la Shirikisho Afrika.

Hata hivyo licha ya kuchapwa 3-1, Simba ilisonga mbele raundi ya pili kwa faida ya bao la ugenini kufuatia ushindi wa nyumbani wa 2-0 na hivyo matokeo ya jumla kuwa  mabao 3-3.


Simba 05

BALAA LA SIMBA

Kocha wa Simba, Fadlu Davids na jeshi zima la Msimbazi wamepanga kufanya balaa katika mchezo huo, huku wakijivunia rekodi nzuri ya kufunga mabao waliyonayo msimu huu katika mashindano tofauti.

Katika Ligi Kuu, Simba imefunga mabao 22 ikiwa vinara kupitia mechi 11 ilizocheza na Ahoua amehusika kwenye mabao tisa, akifunga matano na kuasisti mara nne.

Ahoua anaonekana kuibeba zaidi Simba katika eneo la ushambuliaji sambamba na wakali wengine kama Leonel Ateba na Steven Mukwala ambao ni washambuliaji halisi pekee waliosafiri na timu hadi  Algeria.

Wakati Simba ikiwa hatari katika kucheka na nyavu, pia ulinzi ipo vizuri kwani imeruhusu mabao matatu ndani ya ligi, kazi kubwa ikifanywa na kipa Moussa Camara mwenye clean sheet 9, akisaidiana na mabeki, Mohamed Hussein, Shomari Kapombe, Che Malone Fondoh na Abdulrazack Hamza.

CS Constantine katika ligi yao ya ndani ikiwa inaongoza kwa pointi 19 baada ya mechi 11, imefunga mabao 12 na kuruhusu tisa ikionekana kutokuwa na makali zaidi ya kucheka na nyavu pia safu ya ulinzi ni nyeopesi na hii inaweza kuwa nafasi nzuri kwa Simba kwa takwimu zilizoko na aina ya wachezaji wenye uchu ilionao.

Simba 03

Katika mechi za Kombe la Shirikisho msimu huu, Simba iliyoanzia raundi ya pili hadi sasa imecheza mechi tatu ikishinda mbili dhidi ya Al Ahly Tripoli (3-1) na Bravos (1-0), huku ikitoka 0-0 dhidi ya Al Ahly Tripoli.

CS Constantine yenyewe ilianzia raundi ya kwanza na matokeo yake yalikuwa ushindi wa 2–0 na 2-1 dhidi ya Police Rwanda, kisha katika raundi ya pili iliishindilia Nsoatreman 0–2 na 1-0 kisha kutinga makundi na kuanza na ushindi wa 1-0 mbele ya  CS Sfaxien ugenini kwa bao la Brahim Dib anayetajwa kuwa hatari zaidi.

Mbali na Dib ambaye ni kiungo mshambuliaji, pia Zakaria Benchaâ anayecheza nafasi ya ushambuliaji ni nyota mwingine ambaye safu ya ulinzi ya Simba inapaswa kuwa naye makini.

Kocha wa zamani wa Simba, Abdelhak Benchikha ambaye hivi sasa anainoa JS Kabylie ya Algeria amefichua kwamba CS Constantine ni timu yenye njaa ya ushindi hivyo Simba inapaswa kuwa makini.

“Wanajua kuutafuta ushindi lakini Simba kama itacheza kikubwa kama nilivyowaona wakicheza na Al Ahli Tripoli naamini watafanya vizuri  japo wanatakiwa kuwa na nidhamu ya mchezo,” alisema kocha huyo ambaye aliachana na Simba Aprili 29, mwaka huu baada ya kutua Desemba 2023.

Simba 02

Fadlu analitambua hilo huku akibainisha kwamba: “Tunatambua kucheza ugenini ni tofauti na nyumbani lakini tupo hapa kwa ajili ya kufanya kile ambacho tutaweza ili kupata pointi ambazo zitatuweka kwenye mazingira mazuri.”


Simba 06

REKODI ZAO CAF

CS Constantine wanaonekana kuwa ni wageni katika michuano ya Caf kwani tangu kuanzishwa kwa klabu hiyo mwaka 1898, hii ni mara ya tano kushiriki, mbili Ligi ya Mabingwa na tatu Shirikisho. Katika Ligi ya Mabingwa 1998 iliishia raundi ya kwanza kisha 2018/19 ikafika robo fainali. Upande wa Shirikisho, mwaka 2014 iliishia raundi ya pili ikarudia tena mwaka 2016 kuishia hapo. Msimu huu imepiga hatua zaidi kwani hivi sasa ipo makundi.

Kwa upande wa Simba iliyoanzishwa 1936, michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika pekee hii ni mara ya saba huku hatua kubwa kufika ni robo fainali msimu wa 2021/22.

Katika Ligi ya Mabingwa imeshiriki mara 12, hatua kubwa kufika ni robo fainali mara nne 2018/19, 2020/21, 2022/23 na 2023/24. Pia 1993 iliwahi kucheza fainali ya Kombe la CAF ambalo baadaye michuano hiyo ikaunganishwa na Kombe la Washindi  Afrika ikaundwa Kombe la Shirikisho kuanzia 2004.


Simba 01

REKODI ZA SIMBA ALGERIA

Kombe la Shirikisho 2012

ES Sétif 3–1 Simba

Ligi ya Mabingwa 2018/19

JS Saoura 2–0 Simba