Katwila amejiuzulu mara tatu Mtibwa

Muktasari:

  • Kutokana na hali hiyo, Mwanaspoti limefunga safari hadi Turiani kwa Kocha mkuu wa timu hiyo, Zuberi Katwila ambaye ni mwenyeji wa Tabora ili kufanya naye mahojiano maalumu na amefunguka mengi kuhusu safari yake katika maisha ya soka.

UKITAJA timu zinazopitia wakati mgumu kwenye Ligi Kuu Bara kwa sasa huwezi kuiacha Mtibwa Sugar ya Turiani mkoani hapa. Hawa jamaa wamecheza mechi 20 na wamekusanya alama 16 pekee. Wanapitia wakati mgumu kwelikweli, wamezibeba timu zingine 15 kwenye mgongo wao.

Kutokana na hali hiyo, Mwanaspoti limefunga safari hadi Turiani kwa Kocha mkuu wa timu hiyo, Zuberi Katwila ambaye ni mwenyeji wa Tabora ili kufanya naye mahojiano maalumu na amefunguka mengi kuhusu safari yake katika maisha ya soka.


ALIKOZALIWA

Amezaliwa jijini Dar es Salaam mwaka 1973 na kwa sasa ana miaka 51, akikulia Chag’ombe Kota Railway. Hata hivyo, ni mwenyeji wa mkoani Tabora na wazazi wake, baba ni Mnyamwezi na mama ni Mngoni.

Amesoma darasa la kwanza hadi la nne katika Shule ya Msingi Kibasila iliyopo jijini Dar es Salaam kabla ya kuhamia Oysterbay alikoendelea la tano hadi alipomaliza masomo ya msingi na kwenda Sekondari ya Kinondoni Muslim ya jijini hapo.

SOKA LAKE

Kama ilivyo kwa wengi, soka linaanzia utotoni hadi kufikia ngazi za juu. Katwila anasema alianzia soka lake akiwa shule ya msingi na huko walicheza mipira ya kufuma akiwa Oysterbay.

“Nilianza kucheza soka tangu nikiwa mdogo shuleni na enzi zile tulichezea Uwanja wa Oysterbay na tukitumia mipira ya makaratasi,” anasema na kuongeza hata sekondari aliendelea kucheza soka hadi kidato cha nne na kuingia la mtaani.

“Sekondari niliendelea kucheza hadi nilipomaliza kidato cha nne, nikawa nyumbani na baadae nikawa nachezea timu za mtaani. Kuna timu moja ya Beach Boys ilikua Ligi Daraja la Tatu niliuwa naichezea tukaipandisha hadi Daraja la Pili. Pia nilicheza BP ikapanda daraja na Bandari. Baadaye nilisajiliwa na Reli Morogoro kabla ya kujiunga na Mtibwa Sugar na niko hadi leo.”


ANATOKA FAMILIA YA SOKA

“Sisi kwetu ni familia ya soka, kaka zangu wote walicheza na kipindi hicho ligi haikuwa ikionyeshwa, lakini kaka zangu wakubwa wamecheza timu kubwa na wengine wamecheza nje ya nchi, hivyo sikuvutia na lolote bali nilizaliwa familia ya soka.”

ATIMKIA NJE, ARUDI GHAFLA

Anasema alipotua Reli ya Morogoro alicheza kwa miaka miwili kabla ya kupanda pipa na kwenda nje ya nchi kujaribu bahati yake kama ilivyokuwa kwa kaka zake. Licha ya kupata timu huko lakini alifelishwa na baadhi ya mambo;

“Nimecheza Reli mwaka 1996-1998, kisha nikaenda  kufanya majaribio ya soka la kulipwa ulaya. Nilianzia Australia kisha Ubelgiji nilipata timu ya kuchezea ya Gillvebrodin na kutokana na kutokuwa na makubaliano mazuri nikarudi na mwaka 1998 Mtibwa ndio wakanisajili na nimecheza hadi sasa nikiwa kocha.”


LAKI TANO TU MTIBWA

Anasema anakumbuka alivyotua Mtibwa dau lake lilikuwa Sh500,000 na wachezaji walisajiliwa kwa kiwango kimoja.

“Zamani pesa ilikuwepo, hata hivyo, wachezaji walisajiliwa kwa kiwango kimoja, kama ni mshahara ilikuwa mnalipwa 50,000 wote na kwa ninavyokumbuka nilisajiliwa kwa Sh500,000 tu mtibwa,” anasema na kuongeza wakati anaingia Mtibwa alikuta ushindani wa namba ni mkubwa kwani vijana walikuwa wengi na kumpa wakati mgumu kocha ingawa alipata nafasi na kuaminiwa.

UBINGWA LIGI KUU MARA MBILI

Anasema katika mambo anayojivunia kuwa na Mtibwa ni kubeba mataji mawili ya Ligi Kuu Bara Mwaka 1999 na 2000 na timu ilikuwa vizuri na tishio kwa miamba ya soka nchini Simba na Yanga.

“Nilipoingia mtibwa kiukweli niliingia na mguu mzuri, tulipata mafanikio sana, maana wakati naingia mwaka 1998, mwaka uliofuata tukatwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara na mwaka uliofuata tukauchukua tena baada ya kuifunga Yanga kwenye uwanja wa Jamhuri, Morogoro. Mwaka 2001 tulikosa wa tatu, timu yetu ilikua nzuri na tulikua tunashindana ipasavyo,” anasema na kuongeza Mtibwa ile iliweza kushindana na Yanga na Simba hata kwenye usajili;

“Ushindani wa Simba na Yanga kwa miaka yote ni mkubwa. Zinaweza kufanya chochote kwenye usajili. Wakati ule Mtibwa ilikuwa nguli pia katika usajili. Kama Yanga au Simba zikichukua mchezaji bora Mtibwa na Mtibwa ingejibu mapigo kwa kuchukua kifaa humo humo. Ni tofauti na sasa mchezaji mzuri akichukuliwa Mtibwa ni ngumu kusajili mchezaji mkubwa.”

“kipindi kile Mtibwa tulikuwa na ushindani mkubwa kwenye ligi, Simba na Yanga kutufunga kwao ilikuwa ni sare, sio kama sasa wanaweza kutufunga mfululizo. Wakati ule zilikuwa bora lakini hata Mtibwa ilikuwa bora Zaidi.”


MTIBWA INAFELI WAPI KUSAJILI?

Anasema tofauti na viongozi wa sasa, wa zamani walikuwa na uwezo wa kushindana kwenye usajili na walikuwa na malengo na timu.

“Sijui kwa nini, lakini kwa mawazo yangu ni, viongozi wa zamani walikuwa na uwezo wa kushindana kwenye usajili tofauti na sasa, maana zamani walikuwa na malengo na timu, walitaka timu ifike mbali na walihakikisha mahitaji muhimu ya timu yanapatikana na kwa wachezaji wa kipindi hicho.”


WALIVYOBEBA UBINGWA MARA MBILI LIGI KUU

Katwila anakumbuka Mtibwa ya kipindi hicho ilikuwa inaweka kambi hadi nje ya nchi na ni moja ya siri ya kuwa bora na kubeba ubingwa mara mbili mfululizo mwaka 1999 na 2000.

“Kusema ukweli maandalizi yetu ilikuwa tunaenda nje ya nchi kama Zambia, congo ili kuweka kambi ya maandalizi ya msimu (pre-season). Hapo timu ikirudi inakuwa sawa. Wakati mwingine tulikuwa tunakwenda kwenye mabonanza Mauritius. Yote hii ni katika kuiweka timu kiushindani tofauti na sasa hivi, ukitaka maandalizi unaishia kwenda Dar.”


ALIOTWAA NAO UBINGWA

“Kwa line-ups siwezi kuwakumbuka wote kwa haraka maana ni muda mrefu umepita, lakini labda kama tungepata picha ingekuwa rahisi. Nakumbuka golini alikuwa Steven Nemesi, Mecky Maxime, Kassim Issa, Geofrey Magoli, John Mabula, Dua said, Ramadhan Hamza, Noah Kilimanjaro, Hassan Mbaruku, Geofrey Kikumbizi, Kamab Lufo, Monja Liseki, Abubakari Mkangwa, Masumbuko Hassan hawa ni baadhi na tulicheza na Yanga Morogoro na tukashinda na kutwaa ubigwa.”


ASTAAFU AIBUKIA UKOCHA

Anasema mwaka 2013 aliachana na soka la uwanjani na kuibukia ukocha kwani wakati anacheza alikuwa akisomea kozi ya ukocha na anakumbuka aliyemshauri kufanya hivyo ni Kocha wa wakati huo wa Mtibwa, Salum Mayanga;

“Nimestaafu soka mwaka 2013 maana nilikuwa nacheza wakati huo huo najifunza ukocha na wakati huo Kocha wa mtibwa alikuwa Salum Mayanga na wao ndiyo walinishauri, lakini Mecky Maxime ndiye alitangulia baada ya kupata majeraha ya goti na Kocha Maximo akamshauri kuingia kwenye ukocha na mimi nikafuata nyayo zao,” anasema na kuongeza licha ya ugumu wa kupata leseni A ya ukocha lakini kwake haikuwa kazi.

“Nina leseni A, na kuipata leseni kiukweli lazima uende shule, lakini Mkurugenzi wa ufundi wa TFF, Oscar Mirambo amesaidia kupatikana kwa leseni A maana kwa sasa watu hawatafuti tena leseni nje ya nchi kama zamani.”


ATUA IHEFU

Anasema licha ya kuwa na Mtibwa Sugar kwa muda mrefu, lakini alihitaji kupata changamoto sehemu nyingine na hivyo alivypoata dili la kuifundisha Ihefu FC hakusita.

“Yote hiyo ni kutafuta changamoto na wakati mwingine kuna mambo yanakusukuma uondoke. Kwa kifupi nilipishana na uongozi baada ya timu kukosa matokeo. Hivyo nilipowaambia naondoka wakanikubalia. Hata hivyo, wakati naondoka nilikuwa naitakia mema timu, nikajiunga na Ihefu.”


AITUNGUA YANGA

Akiwa na Ihefu msimu huu mchezo wa mzunguko wa kwanza, ndiye aliyeharibu rekodi ya kutopoteza mchezo kwenye Ligi Kuu msimu huu kwa Yanga baada ya kuitungua mabao 2-1 na anatoa siri ya kuifunga mabingwa hao wa Ligi Kuu Bara akitaja zaidi hali ya hewa.

“Kila mechi ina ujio wake. Yanga ilipokuja, tulikuwa tunajiamini na tuko nyumbani. Hali ya hewa pia iliwasumbua. Sisi tulikuwa tunaenda Kyela Mbeya kujiandaa ndio maana tuliwafunga. Hata hivyo, hali ya hewa nadhani ndiyo ilikuwa inawachanganya Yanga,” anasema na kuongeza mbali na hali ya hewa, wachezaji pia walikuwa wakipata hamasa kutoka kwa viongozi;

“Lazima tuwahamasishe na mara nyingi hamasa ilikuwa inatoka kwa viongozi, maana tukishinda tunapata pointi, pesa na heshima. Hivyo, licha ya kusuasua kwenye ligi lakini sababu ya kufanya vizuri zilikuwa nyingi na tuliifunga Yanga timu bora.”

Kuhusu utofauti wa Ihefu na Mtibwa anasema; “Nimebahatika kufundisha timu za kampuni, maana nakuwa sehemu salama kwenye maisha na hata ikitokea lolote naweza kupata haki zangu. Utofauti wake ni Ihefu wanalima mpunga na Mtibwa miwa, na Ihefu ni ndogo kuliko Mtibwa, lakini kimasilahi na huduma wako sawa.”


AREJEA MTIBWA, CHANGAMOTO KIBAO

Anasema kilichomwondoa Ihefu ni matokeo mabaya iliyokuwa ikipata timu hiyo na alimalizana nao kwa kukaa mezani na kurejea mtibwa.

Hata hivyo anasema alipofika Mtibwa alikutana na Kocha Habib Kondo na alimwachiwa timu ikiwa pabaya hasa kukosa matokeo mazuri.

“Ilifikia mahala Ihefu walikua na mahitaji ya kufanya vizuri lakini baadhi ya mechi hatukufanya vizuri, ikafika wakati mimi na Uongozi tukakaa chini tukakubaliana niondoke, mkataba ukavunjwa ndio nikarejea hapa mtibwa na nilimkuta Habib Kondo aliyekuwa na timu basi uongozi ukanipa majukumu na Kondo akaondoka.”

“Nilivyokuja changamoto kubwa ilikuwa ni matokeo, timu ilikuwa nzuri inacheza lakini tatizo likawa matokeo, kwa hivyo kiufundi niliingia kurekebisha na hata kocha Kondo nilikaa naye akanieleza, nikaanza kuweka ufundi lakini nikakosa tena matokeo, baadae tukaingia na imani mbovu labda kuna mambo ya kitamaduni, lakini tukakataa, tukaamua kuweka sawa saikolojia za wachezaji, nikawaambia ukifika muda tutapata matokeo. Ni muda mrefu kabla ya majuzi kupata na naamini timu itabaki Ligi Kuu.”

Kuhusu anguko la Mtibwa, Katwila anasema; “Mimi nadhani Uongozi wa timu ndio anguko la timu hii, maana timu ina pesa kweli lakini inatakiwa viongozi wa timu wawepo wasimamie timu mahitaji yapatikane na kuwe na muunganiko mkubwa ambao unaifanya timu kuwa imara, hicho kitu kimekosekana, uongozi akiwa mmoja au wawili timu kwenda ni shida, Mtibwa ni timu kubwa na inatakiwa iwe na uongozi ili iheshimike Zaidi,” anasema na kuongeza kwa sasa soka limekuwa biashara tofauti na mwanzo walikuwa wanasajiliwa wachezaji wazuri na wa gharama na hiyo ndiyo ilikuwa sera ya klabu.


AJIUZULU MARA TATU AGOMEWA

“Nimeshawahi kufikiria kujiuzulu nafasi yangu ya ukocha hapa Mtibwa Sugar ili kocha mwingine aje achukue kijiti na aiokoe timu, nimefanya majaribio hayo mara tatu lakini watu wangu walinisihi nibakie nipambane timu ibaki kwa kuwa kocha mkubwa hupimwa nyakati hizi,” anasema na kuongeza timu ikikosa matokeo mazuri kocha anaumia sana na kuwa katika kipindi kigumu ndio maana wengine huwa wanaamua kuchana na timu.

“Katika kipindi kigumu cha ukocha ni pale matokeo yanapokosekana, bora uumwe hata malaria utapata dawa, unaweza kuwa unaumwa watu wasijue kama una umwa kumbe uko hoi na kama una afya dhaifu wanaweza kukukuta chumbani umefariki, maana unaumia sana na dawa yake huwezi kuipata, kiukweli tunaokosa matokeo tunakuwa na hali mbaya.”


MECHI 10 ZA KUAMUA

“Kipindi hiki tunaenda ukingoni tunategemea tushinde  mechi nyingi ili tumalize ligi salama, moto uliwaka lakini ligi ikasimama tena tukaanza upya, nina hofu kama tutarudi na ushindi? Tukirejea kwenye morali ya ushindi kama mwanzo naamini tutabaki ligi kuu,” anasema na kuongeza;

“Tuongeze umoja na ushirikiano kama tulivyoonyesha kwenye hizi mechi zilizopita na ikaonekana kama tunaweza na tuna umoja ambao mwanzo haukuwepo. Nawaomba wale ambao walijiweka pembeni waje tupambane kuhakikisha timu inabaki maana bila umoja timu hii kubaki daraja ni kazi kubwa,” alisema Katwila ambaye baba wa watoto watatu.  Maoni: 0658-376417