Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Akrama: Hii ’hatuchezi' ni mtego

AKRAMA Pict

Muktasari:

  • Katika mahojiano baina yake na Mwanaspoti,Akram anasema heshima ya mwamuzi inatokana na kusimamia kikamilifu sheria 17 za mpira wa miguu bila kujali nani atafurahia na kuchukia, kikubwa anachokiamini ni haki inaishi.

NI vigumu kuona waamuzi nchini wanapewa maua yao na mashabiki, viongozi, wakati mwingine na wachezaji, nadra hiyo ameipata refa wa zamani Mathew Akrama ambaye kwa sasa ni mchungaji wa Kanisa la EAGT Lumala lilipo mkoani Mwanza.

Katika mahojiano baina yake na Mwanaspoti,Akram anasema heshima ya mwamuzi inatokana na kusimamia kikamilifu sheria 17 za mpira wa miguu bila kujali nani atafurahia na kuchukia, kikubwa anachokiamini ni haki inaishi.

Anasema mwamuzi aliyenyooka dakika 90 za uwanjani, timu inayofungwa mashabiki wanaweza wakawa wanamlaumu, lakani baada ya mechi wakienda kuangalia marudio watauona ukweli na heshima yake itabakia palepale.

"Hakuna njia ya mkato itakayompa mwamuzi heshima ni yeye kuzingatia muongozo wa sheria 17 na kuepukana na mambo yasiyo ya kimpira,"anasema.

AKRA 02

MAJERAHA NI SABABU YA UAMUZI

Anasema sababu iliyomshawishi kusomea uamuzi, alipata majeraha ya goti wakati anaichezea timu ya Air Force ilikuwa Daraja la Tatu, hivyo akaona njia pekee ya kusalia na furaha ya kuupenda mpira wa miguu ni kuwepo kiwanjani kivingine.

"Nilianza kuchezesha mechi za Ligi Kuu 2006 nikiwa kama refa wa msaidizi na baada kustaafu  mwamuzi Issarow Chacha mwaka 2007 nikashauriwa nibadilishe nafasi hiyo ili niwe refa wa kati na ndiye aliyenikabidhi filimbi na kunibariki," anasema na kuongeza:

"Mwaka 2008 nikaanza kuchezesha kama mwamuzi wa kati mchezo wangu wa kwanza niliuona  mgumu ni dhidi ya Kagera Sugar na Mtibwa Sugar kipindi hicho Mecky Maxime alikuwa nahodha, wale watu ni ndugu nje ya uwanjani ila siyo dakika 90."

Mechi nyingine anayoiona ni miongoni mwa zile zilizobakia kumbukumbu kwake ni Simba dhidi ya Yanga ya mwaka 2013 ambapo Haruna Moshi 'Boban' alimchezea rafu mchezaji wa upinzani badala ya kumpa kadi nyekundu akatoa ya njano, jambo lililomfanya mashabiki kumshambulia na kumkejeli.

"Ilikuwa mechi yangu ya kwanza ya dabi  kama mwamuzi wa kati, presha ilikuwa kubwa, ingawa baada ya hapo viongozi wa timu hizo waliona unyoofu wa maamuzi yangu na wao ni shuhuda wa hilo," anasema.

AKRA 01

KUCHUKIWA KISA RUSHWA

Anasema kuna baadhi ya waamuzi wenzake walikuwa hawapendi kupangwa naye, kutokana na kukosa mianya ya kupewa chochote kutoka kwa viongozi (rushwa), alichokuwa anakisimamia ni kuinyoosha  haki.

"Kuna baadhi ya timu  zinakuwa zinawatafuta waamuzi kuwapa chochote ili kuzipindisha sheria 17 za mpira wa miguu, binafsi nilikuwa nawaambia wacheze mpira wa haki na waandae timu kwa ushindani wa kweli, sasa baadhi ya waliyokuwa wasaidizi wangu wa pembeni walikuwa wananichukia maana nilikuwa siwapi nafasi ya kufanya vitu vya hovyo," anasema Akrama na kuongeza:

"Kuna wakati timu ambazo hazipendi unyoofu zinawatumia wachezaji baadhi ambao wanaanza kuwavuruga waamuzi kwa kuwachezea rafu wenzao ama kutukana marefa ili akipewa kadi nyekundu awe na sababu ya kutolaumiwa na wenzake.

"Kwa upande wangu baadhi nilikuwa nawaambia waache ujinga wanapaswa kuheshimu vipaji vyao na timu zilizowapa ajira, ingawa siwezi kuwataja kutokana na mabadiliko ya kimaisha."

Anasema wakati mwingine ni rahisi kuwatambua wachezaji wanaokuwa wamezisaliti timu zao kwa kuangalia matukio wanayoyafanya uwanjani, akitolea mfano tempa zisizo na sababu, makosa ya makusudi na kucheza chini ya kiwango ingawa katika hilo inaweza ikatokea mchezaji akawa hayupo sawa.

AKRA 04

KUHUSU USHIRIKINA

Anasema asilimia kubwa wachezaji wamejengwa katika mitazamo ya kishirikina, badala ya kuzingatia miiko ya soka na kufanya   mazoezi kwa bidii ambayo yakiwaweka fiti wanakuwa na uwezo wa kucheza kwa kiwango cha juu.

"Ilikuwa inanishangaza sana ukiingia kukagua vyumba vyao vya kubadilishia nguo unakuwa wanafanya vitu hivyo wazi wazi bila kujali na wanakuwa wanajisifu kama vile ni vitu vizuri, kiukweli kama hayo mambo yapo hadi sasa wanapaswa kubadilika na kuona fursa zilizopo katika soka ambazo zitawatoa kimaisha," anasema na kuongeza:

"Nilichokuwa nakifanya kabla ya kuingia uwanjani nasali ili kama zipo nguvu za giza ziweze kuondoka na kila mtu atoke akiwa salama kuna wakati nilikuwa nawashirikisha na watumishi wa Mungu, ndiyo maana sikuwa na hofu hata nikiona wanafanya shiriki."

AKRA 03

UCHUNGAJI

Baada ya kustaafu kuchezesha Ligi Kuu mwaka 2017 akapata muda mwingi wa kuhubiri Injili na kufanya shughuli zake zingine ambazo hakutaka kuziweka wazi.

"Niliokoka mwaka 2003 hata wakati nafanya kazi ya uamuzi nilisimama na Mungu, ndiyo maana sikuwahi kuyumbishwa," anasema.

"Nimekuwa shuhuda mzuri kwa wanamichezo kuwaambia katika kazi zao ushirikina hauwezi kuwasaidia zaidi ya uharinifu na wakajikuta wanapotea katika ramani ya michezo na kupoteza pesa zao kwa waganga."

Jambo analoliomba kwa  mamlaka za soka nchini, wawape thamani waamuzi waliopo viwanjani na waliostaafu, kutokana na majukumu makubwa wanayoyafanya ambayo nyuma yake wanakumbana na changamoto kubwa.

"Naliona Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limekuwa likitoa semina elekezi za mara kwa mara kwa waamuzi jambo ambalo litawajenga na kuwafanya wawe bora katika kuzizingatia sheria 17, ingawa kwa sasa sifuatilii sana hayo, muda mwingine natumia kwa kazi ya Mungu na kazi zangu binafsi," anasema.

AKRA 05

DABI KUAHIRISHWA

Dabi ya Yanga na Simba iliyoahirishwa Machi 8 kitu kilichozua sintofahamu, mtazamo wake anaona Bodi ya Ligi Kuu isimamie kanuni zilizowekwa kama muongozo nje na hapo ngumu kutatua changamoto hiyo.

"Kila kona kuna kauli, wapo ambao wanasema hawachezi, wengine wanacheza, mpira sio siasa wala hisia unaongozwa na kanuni zilizowekwa bila kujali huyu anataka nini na  yule hataki nini," anasema na kuongeza:

"Kama soka la Tanzania likiendekeza ushabiki tujiandae kushuka thamani kwa viwango vya Afrika, hizo kauli ya hatuchezi, tunacheza ni mtego wa kuiporomosha Ligi Kuu, nashauri warudi katika kanuni waziweke wazi na siyo mashabiki wanataka nini, hilo litawapa heshima hata kama kutakuwa na upande ambao utaumia kutakuwa ndiyo kujifunza kwenyewe."


ANAIONAJE LIGI, WAAMUZI

Anasema anawaona baadhi yao wanapata nafasi ya kuchezesha mechi za kimataifa, hivyo aliipongeza TFF kwa hilo, kuhusu Ligi Kuu imetoa timu zinazofanya vizuri kimataifa akiitaja kama ni hatua nzuri inayoonyesha ukomavu na kukua kwa ligi hiyo.

"Kwa hilo niwapongeze viongozi wa TFF chini ya Wallace Karia kuhakikisha soka linakuwa siku hadi siku, wadhamini kuongezeka hilo ni jambo zuri," anasema Akrama ambaye kazi ya uamuzi aliianza mwaka 2000 akapanda kuchezesha Daraja la Kwanza 2005, kisha Ligi Kuu 2006.


BABA YAKE MSANII

"Ilikuwa  ngumu kushawishika kuigiza na baba yangu kwa sababu tuliishi maeneo tofauti mimi Mwanza yeye Dar, ila kati ya kazi zake ambazo nilikuwa nazipenda sana ni Ua Jekundu na Kabuli la Safia," anasema.