Kasi ya wanasoka hawa Kombe la Dunia ni balaa
Muktasari:
- Mpaka kufikia hatua hii moja ya washambulia ambao wametia fora kwakuwa na kasi ya kipekee ni pamoja na Vinicius Jr, Lionel Messi, Kylian Mbappe na Erling Halaand.
MASHINDANO ya kombe la Dunia 2026 kule nchini Marekani, Canada na Mexico yamezidi kupamba moto, sasa uelekeo ni robo fainal. Timu zilizofanikiwa kutinga robo fainal zinatarajiwa kuanza kwa hatua hiyo leo kwa mechi ya kwanza kati ya Ufaransa na Morocco.
Mpaka kufikia hatua hii moja ya washambulia ambao wametia fora kwakuwa na kasi ya kipekee ni pamoja na Vinicius Jr, Lionel Messi, Kylian Mbappe na Erling Halaand.
Washambualiaji hawa wakimwacha beki hatua chache huwa ni vigumu kumkamata. Kutokana na kiwango cha juu cha kasi kwa wanasoka hawa ni lazima uwe na mabeki wenye kasi.
Wapo mabeki wa pembeni ambao wamekua na jukumu la kupanda kushambulia na kushuka kukaba, angalau wameonekana kuweza kuwakaba washambuliaji wenye kasi.
Kwa wanasoka wanaocheza mashindano makubwa yenye ushindani uwepo wa kasi kasi ina maana mwili wake ni imara na hauna hali ya uvivu.
Ndio maana pale mchezaji anapoonyesha kuwa na kasi bila kuchoka hufuatiliwa kwa karibu ili kujua kama kasi yake ni ya asili au ya kuchochea na dawa za kuongeza nguvu.
Tazama mazoezi binafsi ya mshambuliaji Halaand wa nchi ya Norway ambaye kabla ya mashindano haya alikuwa akifanya mazoezi ya kupanda kwa kasi katika vilima vya maeneo alipokulia.
Hii inatoa picha kuwa ili mchezaji kupata kasi ya kipekee inamlazimu kufanya mazoezi binafsi ya ziada huku akiyafanya kwa juhudi kubwa na nidhamu ya hali ya juu.
Kasi kwa mchezaji iko hivi
Hakuna uchawi katika kasi wanayochomoka nayo Wanasoka kushambulia na kuzuia, ni uwezo binafsi unaochangiwa na vitu kadhaa ikiwamo umri, mwili, nidhamu, mazoezi na juhudi binafsi.
Haishangazi mchezaji kama Halaand, Messi na Mbappe, kuwa na kasi katika mchezo wenye upinzani mkali hii ni inatokana na mashabiki, benchi la ufundi na wachezaji anaocheza nao wanamfanya kuwa na ari ya juu ya ushindi.
Kukosa ari ya ushindi ni sawa na kuwa na nyumba bila paa, ari ya ushindi inaweza kumfanya mchezaji kuwa na hisia nzuri hivyo kuweza kujituma bila kuchoka na kusaka ushindi.
Umri wa wanasoka wenye kasi ni miaka 17-24, misuli huwa ni michanga ambayo bado haijachoka hivyo kuwa myepesi kupokea mazoezi na kujijenga vyema na kuwa na utimamu imara wa mwili.
Miili ya wanasoka wenye maumbo ya wastani unawafanya kuwa wepesi mwenye uwezo wa kupanda kushambulia na kurudi kasi kuwakaba wapinzani wao.
Wanasoka wenye kasi huwa wamezoea mazoezi na kuwa sehemu ya maisha yao hivyo kushikamana mazoezi ya timu na yale binafsi ikiwamo mazoezi ya gym na viungo.
Ukimtazama mchezaji mwenye sifa ya kasi huwa si wavivu, huwa na juhudi binafsi, wanajituma bila kuchoka, wanapopoteza mpira hata kama kachoka atakaza kurudi kukaba.
Mwili wa mwanadamu una takribani zaidi ya misuli 650 ambayo kama ikijengwa vyema huweza kufanya mengi ikiwamo kuupeleka mwili kwa kasi kama vile beki wa zamani wa Yanga Shadrak Nsajigwa..
Nidhamu ya hali ya juu na tabia njema ni moja ya nyenzo kwa mwanasoka kufanikiwa kufanya mazoezi na kufuata maelekezo mbalimbali hivyo kucheza kwa kiwango cha hali ya juu akiwa na kasi.
Faida ya mchezaji mwenye kasi
Kutawala mashambulizi
Moja ya jambo kubwa ambalo kila timu inayotaka kushinda ni kuwa na wachezaji wenye kasi ya kushambulia kwa kasi, kuvunja ngome ya mpinzani, kuwazidi mbio mabeki na kufunga.
Wanasoka wote wanahitaji kuwa na kasi uwanjani, kadiri mchezaji anavyokuwa na kasi ndivyo pia anavyocheza vizuri. Ingawa kasi ya mpira wa miguu ni tofauti na michezo mingine.
Mara kwa mara Mchezaji soka anahitaji kukimbia na mpira na anaweza kuhitajika kukimbia kawaida au kufunguka kwa kasi yenye nguvu kama anavyofanya Messi na Mbappe.
Kuwahi kuzuia mashambulizi
Mara nyingi kasi katika soka huitajika mahala pasipotarajiwa, mfano mchezaji anaweza kuwa anakimbia kidogo kidogo lakini anaponyakua mpira anaweza kufunguka kwa kasi ili aweze kushambulia lakini pia lazima awe na kasi kurudi kuzuia mashambulizi anaposhambuliwa.
Vile vile mchezaji mkabaji atahitajika kufunguka ghafla kwa kasi ili kuweza kumzuia mshambuliaji ambaye si rahisi kukumkuta kama hana kasi ya ziada.
Hivyo ni kawaida kumwona mchezaji wa soka mara kwa mara kukumbana na mbio fupi fupi za kasi ambazo zinahitaji atumie nguvu kubwa kuweza kufanya hivyo.
Faida ya kimwili na kiakili
Wepesi wa kimwili kwa mchezaji kukimbia kasi kushambulia na kurudi kwa wakati kukaba huweza kuwavuruga kiakili wapinzani kiasi cha kuwapa hofu, kuwanyima nafasi ya kufikiri haraka hatimaye kuwa na maamuzi mabovu.
Kasi ya mwanasoka inajengwa kwa mazoezi tangu akiwa kinda na anahitajika kutumia akili na kutunza uwezo wake wa kuwa na kasi kwa kuzingatia programu nzima ya mazoezi anayopewa na wakufunzi.
Kuiweka mechi nzima mfukoni
Ili kuweza kudhibiti mechi nzima yaani mtaani wanasema kuiweka mfukoni timu inahitajika muunganiko wa wachezaji wenye kasi wenye ukakamavu, nguvu na stamina. Angalau nusu ya timu ikiwa na wachezaji hao inaweza kuleta matokeo makubwa.
Kwa wachezaji kama Halaand wameiva na wamekomaa kiukakamavu kitu ambacho kinawasaidia kukabiliana na ushindani na mazingira ya mechi ngumu zenye wachezaji wakali kama wao.
Unapokuwa na kasi na mwili mkakamavu ina maana kuwa mwili huo unaweza kudumu na kuvumilia mambo mengi ikiwamo kutopata majeraha ya mara kwa mara.
Kuwa hatua moja mbele zaidi
Mchezaji mwenye kasi ya ziada huwa ni mshindi wakati wa kushambulia au kuzuia, katika hali ya kubaki mchezaji mmoja kwa mmoja au wanapobaki wawili wakipambana.
Wachezaji kama Halaand, Messi na Mbappe akibaki na beki mmoja nafasi ya kufunga kwao huwa ni kubwa, kwa sababu kasi waliyonayo iko mbele zaidi ya mabeki.
Chukua hii
Kasi ya jumla katika kila timu ni mtaji mkubwa katika kushinda, kwasababu ndio inawezesha mashambulizi na kushinda, inazuia kushambuliwa hatimaye kutoruhusu magoli. Kasi inakamata zile nafasi finyu za kushtukiza na kulifikia kila eneo kirahisi.
Wachezaji hawa wenye kasi ndio wataziwezesha timu zao kwenda hatua ya nusu fainali hatimaye fainali. Kasi zao ni kutokana na utimamu thabiti wa mwili ukichangiwa na mazoezi binafsi ya ziada.