Kagoma awataja Chama, Mayele

KWA soka la kisasa, kushinda mechi yoyote unahitaji kuwa na nguvu zaidi kwenye sehemu ya kiungo ya timu yako.
Timu yenye wachezaji mahiri katikati ya uwanja, ndiyo hasa mara nyingi imekuwa ikipata matokeo mazuri kwenye mechi zake. Jambo hilo linafanya thamani ya wachezaji viungo kuwa kubwa kwa kadiri siku zinavyokwenda.
Sasa viungo pamoja na kuwa na jukumu la kuwatengenezea nafasi za kutupia washambuliaji wa timu zao na wao wameingia kwenye rekodi za kupachika mabao huku jukumu la kutoa pasi za mwisho pia wakilifanya.
Mwanaspoti limefanya makala na kiungo wa Singida Big Stars, Yusuph Kagoma ambaye amejiunga na timu hiyo dirisha dogo la usajili akitokea Geita Gold amefunguka mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutoa utofauti wa ubora wa viungo wazawa na wageni.
Utofauti ni ubora
"Tanzania imebarikiwa kuwa na vipaji vya wachezaji wengi hasa nafasi ya kiungo hata ukifuatilia Ligi Kuu Bara unaweza kukubaliana na mimi kwani wachezaji wengi wanaofanya vizuri ni nafasi ya kiungo," anasema na kuongeza;
"Pamoja na timu kubwa za Simba na Yanga kuwa na wachezaji wa kigeni kwenye nafasi hizo bado wanawachanganya na wazawa ambao pia wameonyesha uwezo mkubwa na wa kuvutia huku wakitajwa zaidi midomoni mwa watu."
Kagoma anasema kuna wageni ni wazuri hata ukiwafuatilia unabaini kuwa kuna utofauti lakini hicho hakiondoi ukweli kwamba na wao ni bora na wamekuwa wakitoa changamoto kwa wageni huku akimtaja Feisal Salum 'Fei Toto' kuwa pamoja na kupewa wachezaji wengi wa kigeni kwenye nafasi yake bado ameonyesha kuwa na uhitaji kikosini na kucheza.
"Sio Fei Toto pekee, pia ukiangalia Simba kuna Jonas Mkude na Mzamiru Yassini ni viungo ambao wameonyesha changamoto kwa mastaa wa kigeni wamekuwa bora na wanapata nafasi ya kucheza hii ni ishara tosha kuwa wazawa pia ni bora utofauti ni uraia tu."
Anasema utofauti upo kwasababu binadamu wanatofautiana anaweza kuwa na kitu mguuni na mwingine akakosa lakini kwa asilimia kubwa anakiri kuwa wazawa pia wameamka na kuonyesha kuwa wanaweza.
Sababu ya washambuliaji kupotea
"Waafrika ni wepesi wa kuridhika hii ndiyo sababu kubwa ya washambuliaji wetu wengi kushindwa kuwa na muendelezo wa ubora, uwezo wanao lakini wakishafunga mabao yao kumi wanaona wameshamaliza," alisema na kuongeza;
"Washambuliaji wengi wa kizawa wakipata mafanikio msimu mmoja msimu unaopfuata huoni wakiendeleza kile walichokifanya msimu uliopita hii ni kwasababu wanaridhika haraka na kujisahau."
Kagoma anasema hawashangai ni kawaida ya watu wenye ngozi nyeusi tofauti na wachezaji wa mataifa mengine makubwa ambao wanaamini katika kuendeleza ubora wao.
Sio kiungo tu hadi beki anakiwasha
“Nimezoeleka na kufahamina kutokana na kutumika zaidi kucheza nafasi ya kiungo lakini mimi ni mchezaji ambaye nimepata nafasi ya kucheza nafasi tatu uwanjani na zote kwa ubora,” anasema na kuongeza;
“Naweza kucheza kwa ubora kabisa nafasi ya beki wa kati na beki namba mbili ni nafasi ambazo nimepata nafasi ya kucheza nikiwa kwenye kikosi ambacho kinashiriki Ligi Kuu Bara sio kwamba nimecheza nikiwa madaraja ya chini.”
Kagoma anasema hata sasa ikitokea kocha wake akamiamimi na kumpanga nafasi hizo anaweza kucheza kwa ufanisi kwasababu soka ni mchezo ambao anaupenda na hachezi kwasababu ya kufundishwa anakipaji.
Misimu nane timu tatu
"Nimeanza kucheza Singida United ikiwa daraja la kwanza na baadaye ikapanda nikacheza misimu miwili baada ya kushuka niliondoka na kujiunga ni timu nyingine lakini ni moja ya timu ambayo nimecheza misimu mingi zaidi," anasema na kuongeza;
"Baada ya kutoka Singida United nilijiunga na Gwambina ambayo niliitumikia kwa miaka miwili uwezo niliouonyesha nikiwa na timu hiyo ndio uliwavutia Geita Gold ambao walinichukua na kunisainisha mkataba wa miaka miwili lakini nimewatumikia mwaka mmoja na nusu na baada ya hapo ndipo nilipochukuliwa na Singida Big Stars."
Kutoka kuwa dokta hadi soka
"Ndoto yangu ilikuwa ni kuwa daktari nakumbuka tangu naanza shule nikiulizwa unasoma ili uwe nani jibu lilikuwa ni kuwa Daktari ili niweze kuwatibu wagonjwa,” anasema na kuongeza;
“Lakini soka lilichukua nafasi kubwa zaidi ya masomo pamoja na kufanikiwa kumaliza kidato cha nne lakini sikuweza kutimiza ndoto yangu na kujikuta nawekeza nguvu saidi kwenye mpira ambao pia nilikuwa naupenda.”
Kagoma anasema hajaingia kwenye soka kwa kushawishiwa na mtu yeyote au kuvutiwa na mchezaji aliamua kuingia huko kutokana na mapenzi yake binafsi na mchezo huo.
“Ntakuwa muongo nikisema nilivutiwa na mchezaji kwani nimeanza kucheza nikiwa na umri mdogo na kipindi hicho ata muda wa kuangalia mpira kw runinga ulikuwa hakuna kutokana kukosa muda kutokana na kuwa na mambo mawili kwa wakati mmoja kusoma na kucheza.”
Chama, Mayele nani anatoka
Kiungo huyo anataja kikosi chake bora ambacho amekiri kuwa kikitokea kikawa pamoja na kushiriki Ligi Kuu Bara hakuna timu inaweza kuwafunga akianza na kipa Homen Abubakar, Shomari Kapombe, Shafiki Batambuz, Oscar Masai, Juma Nyosso, Yusuph Kagoma, Ayub Lyanga, Kenny Ally Mwambungu, Fiston Mayele, Clatous Chama na Pape Sakho
“Kikosi hiki ukifungwa chache tano maana kimekamilika kila idara ukuta wa chuma eneo la kiungo kuna watu ukiangalia mbele bado kuna Chama mtu wa maaudhi kwenye chenga, kuna mzee wa kutetema na Sakho mtu wa kukimbiza,” anasema na kuongeza;
“Ubora wa kikosi hiki kitaongezewa nguvu na kocha Hans Van Pluijm ambaye ni muumini wa kuchezea mpira hivyo ninaimani kubwa kuwa kikiwa chini yake hakuna timu ya kutuzuia.” anasema Kagoma.
Azitaja Gwambina na Ruvu shooting
“Hatua ya 16 bora nilikosa penalti nikiwa na Gwambina nilikosa na ilikuwa penati ya mwisho nikishinda naipeleka timu hatua inayofuata lakini nilishindwa kuibeba timu na kujikuta najutia baada ya kufanya makosa,” anasema na kuongeza;
“Tangu nimeanza kucheza soka la ushindani sijawahi kukosa penalti na nina ubora ambao huwa najivunia nikipiga mpira huwa haujawahi kufuatwa na kufikiwa na kipa, lakini siku nikiwa na Gwambina nilifanya uamuzi tofauti nikijaribu bahati na nilikosa,” Kagoma.
Minziro anapagawisha wachezaji
“Nimepita chini ya makocha wengi lakini kocha Fredy Felix ‘Minziro’ ni kocha bora sana ana anapenda sana kufurahi mafanikio,” anasema na kuongeza;
“Nimekuwa nikimfuatilia kocha wangu hata nikiwa uwanjani ni mwalimu ambaye anakuwa na mikikimikiki kama na yeye yupo uwanjani anacheza mshambuliaji akiwa kwenye harakati ya kutaka kufunga kwa mguu basi na yeye atafanya kama anapiga au ikitokea ni kichwa pia ataonyesha ishara ya kupiga kichwa.”