Jinsi ya kupata mapenzi unayotaka katika ndoa
Muktasari:
Kila mwenye mpenzi anapaswa kujiuliza mwenyewe. Wako wanaume ni madikteta, anamburuta mke wake kadri anavyotaka, wala hajali hisia zake, kitu ambacho ni kibaya.
MKIWA kwenye uhusiano, ni suala la msingi sana kujua namna ya kufanya ili kupeana raha, kwa sababu hakuna mtu aneyeingia kwenye ndoa kusaka mtu wa kumtukana matusi au kumpiga.
Je mpenzi wako unamfanyiaje?
Kila mwenye mpenzi anapaswa kujiuliza mwenyewe. Wako wanaume ni madikteta, anamburuta mke wake kadri anavyotaka, wala hajali hisia zake, kitu ambacho ni kibaya.
Kuna wanaume wanafikiri wanawake ni kama gunia unamfanyia vituko na matusi unavyotaka, unamnyanyasa au kumsema kwa watu kadri unavyotaka, kitu ambacho si kweli. Kuna wanaume wengine licha ya kutambuliwa kama vichwa vya nyumba, akikwaruzana na mwenzi wake, anachokijua ni kununa, kususa au hata kulala sebuleni, hii ni akili ya kitoto!
Mume kama kichwa cha nyumba, anapaswa kuwa mfano wa kuigwa, je wewe ni mwanamume wa namna gani. Kila mwanamume anapaswa kujiangalia matendo yake.
Pia kila mwanamke anapaswa kuangalia matendo yake anayofanya kwa ndoa yake na kwa mumewe.
Je, matendo ni ya haki?
Kila mwenye akili timamu anapaswa kufanya vitu ambavyo yeye akifanyiwa, atajihisi kupata raha. Jiulize wewe mwenyewe, je, unayofanya ni mambo ya aina gani. Wakati mwingine tunakuwa na ndoa mbaya kwa sababu ya matendo ambayo tunatenda.
Ni lazima uwe makini kwa vitu ambavyo unafanya. Hata hivyo, ni muhimu katika uhusiano kuwa na kawaida ya kuwa na muda wa kutafakari kwa umakini mkubwa hali ya ndoa yako na kuona ni yapi yanakwenda ovyo au yanakwenda safi. Katika maisha, msingi wa kuwa na maendeleo mema ni kuwaza na kufanya mema, ndiyo kusema hata kama labda ndoa yako ina matatizo, unapaswa kuwaza namna ya kufanya mema kwa maana ya kuondoa kasoro zilizoko na kadhalika.
Ni ujinga kutarajia mazuri kwenye ndoa yako wakati hufanyi mazuri; utakuta labda mwanamume anarudi nyumbani usiku wa manane akiwa amelewa au anatokea kwenye uzinzi, halafu bado anatarajia mema kutoka kwenye ndoa yake, inawezekanaje? Ni suala lisilowezekana. Utakuta mwanamke au mwanamume ni jeuri, utakuta mwanamume halali nyumbani, labda kaporwa na shugamami, lakini bado anatarajia maisha yake yawe na faraja, kitu kisichowezekana. Kukubali kuacha ndoa yako, ni dalili kwamba huna akili.
Ni ujinga kumkimbilia mwanamke au mwanamume mwingine na kuiacha ndoa yako, kwa sababu hayupo ambaye hana kasoro. Kama unafikiri yuko mwanamke au mwanamume ambaye hana kasoro, jua kuwa fikra zako haziko sawa. Kwa ufupi ni kwamba, katika kila ndoa, kuna wakati kunatokea hitilafu, cha msingi ni kukaa chini na kuondoa kile ambacho kinaleta shida.
Cha msingi ni kwa watu kuacha dharau, kuacha majivuno, kuacha kuona kwamba aaah, nikimwomba msamaha ataona najikomba, hakuna ubaya kuitwa unajikomba ikiwa unachokitaka ni kizuri kwa ndoa yako.
Mwanzoni mwa mwenzi huu nilianzisha semina maalumu kwa wachumba na wale walio kwenye ndoa, pia kutoa ushauri wa ana kwa ana kwa wenye matatizo ya ndoa, wengi wanaokuja ni wanawake, ni sawa wanaume pia kama vichwa katika nyumba wanapaswa kujifunza zaidi ili wajue namna ya kuendesha nyumba zako.
Ndoa nyingi zinaharibika kwa sababu wanaume wanashindwa kuzingatia majukumu yao, mwanzo wa uhusiano wao kutofahamu huyu ni mwongo au mkweli.
Kwa mfano tatizo la nguvu za kiume ambalo linaonekana kusumbua wengi, linaweza kutibika kwa kutumia mchanganyiko wa vyakula kama ambavyo nimewahi kueleza mara kadhaa, huna sababu ya kulia.
Ninachotaka kusisitiza katika makala haya ni kwamba, mojawapo ya namna ya kupata unachokitaka katika mapenzi, ni kumfanyia mwenzi wako mambo mazuri. Unapaswa kujifunza zaidi ili kuwa na ndoa nzuri zaidi, unapaswa kumjua mwenzi wako anataka nini na kisha kufanya yale unafikiri kwamba ukimfanyia atakuwa mwenye furaha.Kila ndoa ina matatizo na yanaweza kufumuka wakati wowote. La muhimu ni kwamba unapokuwa umeamua kujiingiza katika maisha ya ndoa unapaswa kujifunza jinsi ya kukabiliana nayo.
ONESHA MATENDO YA KIMAHABA
Usipojishughulisha kwa lolote lile kwa ajili ya kumfurahisha mpenzi wako utasababisha mwenzako achoke na hata kufikia mahala akakasirika. Ili kuepuka haya, hakikisha kuwa unayapa kipaumbele mambo ambayo yanamfanya mpenzi wako kujihisi maalumu kwako. Na njia rahisi zaidi ni kuwekeza katika matendo madogo madogo ya kimahaba.
Kumbuka, kauli moja hasi au ya kuvunja moyo inaweza kuhitaji kauli kama ishirini chanya ili iweze kufifia (si kufutika) akilini mwa mpenzi wako. Hii ina maana kwamba, badala ya kumlaumu mpenzi wako, wekeza zaidi katika kumsifia katika mambo yake, au mambo anayoyafanya utakavyo.
Dismas Lyassa ni mtaalam wa uhusiano aliyesajiliwa na serikali. Kwa maoni na ushauri zaidi piga 0653777700