JICHO LA MWEWE: Yanga wanajitekenya na kucheka wenyewe

Muktasari:

  • Kifupi ni kwamba Yanga haikuwa na sababu ya kumbakisha Pluijm kwa ajili ya kuwaridhisha baadhi ya watu wachache ambao wamechukia kuondolewa kwake

WATU wengine wanalipwa mabilioni ya pesa kwa ajili ya kutoa ushauri tu. Watu wengine tunashauri burebure tu, hatulipwi. Na leo naweza kufanya kazi nyigine ya bure ya kumshauri kocha aliyefukuzwa kidiplomasia Yanga, Hans van der Pluijm.

Nasikia amepewa kilemba cha ukoka. Amechaguliwa kuwa mkurugenzi wa ufundi. Ni cheo cha kisasa sana katika soka. Waingereza hawakipendi na hawakitumii. Hispania na Italia huwa wanakitumia. Uliwahi kusikia mkurugenzi wa ufundi wa Arsenal, au Manchester United, au Liverpool au Chelsea? Hakuna.

Mkurugenzi wa ufundi ni kama vile bosi wa kocha mkuu. Ndiye anayesimamia programu za timu. Kocha mkuu, kama ilivyo kwa huyo George Lwandamina anabakia kuwa kocha wa kikosi cha kwanza. Ndivyo ilivyo.

Waingereza wanakiogopa hiki cheo kwa sababu mara nyingi kimekuwa kikizusha migongano kati ya kocha na mkurugenzi wa ufundi. Mipaka ya majukumu inakuwa migumu na wakati mwingine ni vigumu kujua timu inashinda au inafungwa kwa sababu ya nani kati ya kocha au mkurugenzi wa ufundi. Sasa sikia hili. Yanga wamemuondoa Pluijm kwa sababu hawajafurahishwa na maendeleo ya timu. Wamekerwa na kitendo cha kutolewa katika robo fainali ya michuano ya Afrika. Walidhani wangefika mbali.

Halafu hapohapo wameona kama timu yao haisongi mbele. Pambano dhidi ya Simba, huku Simba ikicheza pungufu lilionekana kuwakera sana watu wa Yanga kwa jinsi Simba ilivyotawala mechi hadi Shiza Kichuya kusawazisha kwa kona iliyopigwa kwa mguu wa dhahabu.Baada ya hapo walimuondoa, wakamrudisha kisiasa, wakamuondoa tena, na sasa wamempa cheo cha kisiasa. Katika mioyo ya mabosi wa Yanga, imani kubwa ipo kwa kocha mpya Mzambia. Hii ina maana Yanga watakuwa na kocha wanayemuamini kuliko bosi wake.

Mgongano utaanza kutokea pale ambapo Yanga itakapokuwa haifanyi vizuri chini ya Mzambia. Kuna ambao wataamini kuwa Pluijm anaihujumu timu kwa sababu hakufurahishwa na jinsi alivyoondolewa na nafasi yake kupewa Mwafrika.

Achilia hilo, Pluijm alishashindwa katika baadhi ya kazi zake ambazo sasa ataenda kuzifanya kama mkurugenzi wa ufundi. Siamini kama hakuwa na muda kabisa wa kuangalia soka la vijana. Yanga ni moja kati ya timu kubwa nchini ambazo zina timu mbovu za vijana. Miaka ya karibuni walikuwa wameachwa mbali na Azam, Coastal Union, Simba na Ruvu Shooting. Pluijm alisaidia lolote?

Miaka ya karibuni timu hizi zimepandisha wachezaji wengi vijana kama Abdi Banda, Gadiel Michael, Ramadhani Singano, Farid Mussa, Hamad Juma, Ibrahim Twaha na wengineo. Ulisikia kuna kinda hatari amevuma akitokea Yanga?

Pluijm kwa kutumia pesa za tajiri mwenyekiti wa Yanga alikuwa anatimiziwa mahitaji yote katika programu zake kama vile kuiandaa timu nje ya nchi. Hata hivyo, Yanga wameona bado ziara za maandalizi za Uturuki hazikufanya kazi na ndio maana wamemuondoa. Ataandaa kitu gani ambacho Yanga wanaweza kumuona mpya na anawasaidia?

Nafasi ya mkurugenzi wa ufundi katika timu ni nzuri. Lakini Yanga walipaswa kumpa mtu mpya na si yule ambaye wamemuondoa katika timu kwa kumuona alikuwa hatimizi vema jukumu lake la ukocha na ameshindwa kuwavusha kimataifa.

Tatizo kubwa katika hii habari ya Pluijm ni kwamba pande mbili zimegawanyika kuhusu kutimuliwa kwake. Kuna watu wameona sio sahihi na kuna watu wameona ni sahihi. Kuepusha mgawanyiko ndio maana wamemtafutia cheo ambacho kinaweza kuleta mvurugano katika timu kuliko inavyodhaniwa.

Jaribu kufikiria Lwandamina atajisikiaje kupokea maagizo au amri kutoka kwa mtu ambaye aliondolewa na alionekana hafai katika nafasi yake. Iko wapi nidhamu ya kazi? Hapa ndipo ninapoamini kuwa Yanga walihitajika kutafuta mtu mpya mwenye wasifu wa kazi ambao unaweza kusimama juu ya Lwandamina.

Tunaishi katika dunia ya majivuno ambayo Lwandamina tayari ameshaifika Zesco katika hatua ya nusu fainali michuano ya Afrika na Pluijm hajawahi kufika katika nafasi hiyo. Kudhihirisha kwamba tunaishi katika dunia ya majivuno, tayari kocha huyu Mzambia amekaririwa akiwaambia waandishi wa habari kwamba amekiona kikosi cha Yanga kina mapungufu mengi. Tutegemee mengi siku za usoni.

Kifupi ni kwamba Yanga haikuwa na sababu ya kumbakisha Pluijm kwa ajili ya kuwaridhisha baadhi ya watu wachache ambao wamechukia kuondolewa kwake. Au haikutakiwa kumbakisha kwa kuhofia kuwa anaweza kuchukuliwa na Azam FC. Wakati mwingine soka ni mchezo wa kikatili zaidi duniani pengine kuliko ule wa kucheza na dume la ng’ombe unaofanyika Hispania. Jose Mourinho ndiye kocha bora wa muda wote Chelsea. Hakuna kocha mwenye mafanikio kama yeye. Lakini Disemba mwaka jana, Roman Abramovich alilazimika kumpigia simu na kumwambia amefukuzwa kazi. Huyu ndiye kocha mwenye mafanikio kuliko wote pale Chelsea.

Hakudanganywa kwa cheo chochote kile. Aliondoka na watu wake na maisha mengine yakaendelea. Watu wa Yanga wangepaswa kuchunguza kwanza kazi za mkurugenzi wa ufundi halafu wakajiridhisha kama Pluijm anafaa. Kwa mtazamo wangu sioni kama anawafaa kwa sababu hakuweza kuigusa hata moja akiwa kocha mkuu. Kim Poulsen au Marcio Maximo wanaweza kuifanya kazi hii.