JICHO LA MWEWE: Yanga iende robo fainali au igeuke kichekesho

Muktasari:
- Naam, ratiba ya mechi za makundi ya Ligi ya Mabingwa na ile ya Kombe la Shirikisho Afrika, ilifanyika Oktoba 7 mwaka huu, huku Yanga ikipangwa kundi moja sambamba na TP Mazembe ya DR Congo, MC Alger ya Algeria na Al Hilal ya Sudan.
MBWANA Samatta, Rainford Kalaba, Stopilla Sunzu, Robert Kidiaba, Tresor Mputu, Andrew Sinkala, kama wangekuwa katika jezi ya TP Mazembe kwa sasa huenda Yanga wangekuwa katika kundi gumu la michuano ya CAF.
Naam, ratiba ya mechi za makundi ya Ligi ya Mabingwa na ile ya Kombe la Shirikisho Afrika, ilifanyika Oktoba 7 mwaka huu, huku Yanga ikipangwa kundi moja sambamba na TP Mazembe ya DR Congo, MC Alger ya Algeria na Al Hilal ya Sudan.
Ghafla hakuna hofu kwa mashabiki wa Yanga. Hata watani zao, Simba ambao wenyewe wamepangwa kundi moja la Kombe la Shirikisho la timu za Bravos dos Maquis ya Angola, CS Sfaxien ya Tunisia na CS Constantine ya Algeria wanaamini Yanga wapo katika kundi ambalo wanaweza kupita.
Zamani hilo lingekuwa kundi gumu kwa Yanga. Kucheza na mabingwa wa DR Congo, Sudan na Algeria.

Kwa Mazembe kuna maswali mawili. Yanga wamepanda juu au Mazembe wameshuka. Yote yapo sawa. Zamani wachezaji wa aina ya kina Pacome Zouzoua, Stephane Aziz Ki na Clatous Chama wangecheza TP Mazembe. Wangeonwa na kununuliwa na Moise Katumbi tajiri wa TP Mazembe. Hasa Chama.
Moise alikuwa anachukua wachezaji bora wa Ligi ya Zambia. Asingemkosa Chama. Leo Chama yupo Tanzania. Alianzia Simba na sasa anacheza Yanga. Kitu kizuri kwa mpira wetu. Kina GSM wametia hela ambayo imeanza kufanga kundi kama la Yanga lionekane rahisi.
Wakati huo huo, Moise Katumbi hatii pesa sana kama zamani. Amejitumbukiza zaidi katika siasa.
Hapa karibuni Yanga ilicheza mechi mbili na Mazembe katika kundi kama hili, lakini ikiwa ni mechi za Kombe la Shirikisho Afrika. Ikashinda Temeke halafu ikaenda kushinda Lubumbashi. Mechi ambazo kwa kiasi kikubwa zilitoa taswira ya uhamisho wa nguvu (shifting of power) kwa soka la klabu kati ya DR Congo na Tanzania.

Sidhani kama kutakuwa na mabadiliko zaidi katika mechi mbili za Mazembe na Yanga hasa ukizingatia wachezaji bora wa DR Congo wanakuja kucheza Yanga badala ha kwenda Mazembe.
Hawa kina Chadrack Boka na Maxi Nzingeli walipaswa kwenda Mazembe, lakini ndio kwanza Mazembe ikahangaika na mchezaji ambaye Yanga ilianza kumuona hafai, Mukoko Tonombe.
Yanga dhidi ya MC Alger? Inanikumbusha mechi ya Yanga na Club Africain. Inanikumbusha pia mechi za Simba na Wydad Casablanca. Yanga ilishinda kwa Waarabu kwa bao la Aziz Ki katika mechi ambayo iliupiga mpira mwingi. Lakini tazama mechi za Simba na Wydad. Kuanzia Temeke hadi Casablanca hazikuwa ngumu.
Waarabu wana mashabiki wanaotisha, lakini kwa sasa wana timu za kawaida tu uwanjani. Bingwa wao aliyepita kabla ya huyu USMA Alger alipata wakati mgumu kwa Yanga katika mechi zote mbili za fainali ya Kombe la Shirikisho.

Fainali ya kwanza Yanga walijichanganya Dar es salaam wakachapwa 2-1. Lakini ikaenda kusahihisha ugenini kwa kushinda bao 1-0 pale Algiers kwa mkwaju wa penalti ya beki anayekipiga kwa sasa Namungo, Djuma Shaban. Matokeo ya jumla yakawa sare ya mabao 2-2, faida ya bao la ugenini likawapa Waalgeria taji.
Sioni kama Yanga wanatishwa na timu za Afrika Kaskazini kwa sasa. Yanga hii ya kina Pacome ni ya moto. Ina wachezaji wengi wenye maarifa mengi. Haishangazi kuona katika miaka ya karibuni Yanga ameshinda mechi nyingi ugenini kuliko klabu nyingi za ugenini kuliko klabu nyingi kubwa za Afrika.
Nusura pia amfunge Mamelodi Sundowns ya Afrika kwake kama janja janja isingefanyika kwa bao la Aziz kukataliwa na mechi kumalizika kwa suluhu na kuamuriwa kwa penalti na Wasauzi wakasonga mbele.

Yanga dhidi ya Al Hilal. Nasikia wenyewe Yanga wamepania zaidi kuchukua pointi sita kutoka kwa Waarabu wa Sudan ambao hata ligi hawana.
Wameenda kucheza zao Mauritania baada ya kushindwa kucheza Ligi Kuu Bara. Sijui wapo katika hali gani lakini uwezo wa Wasudan umepungua kwa kiasi kikubwa.
Haijulikani watacheza uwanja gani hadi sasa hivi. Wenzao Al Marreikh waliwahi kufungwa na Yanga ugenini na ‘nyumbani’ kwao Kigali ambako waliamua kuipeleka mechi hiyo.
Yanga walikuwa bora kwa mbali katika mechi zote mbili. Kwa hawa Al Hilal au wale Marreikh swali ni lile lile. Wameshuka viwango au Yanga wamepandisha kiwango chao?
Pesa wanayo, lakini bado nchi yao haipo imara katika masuala ya michezo. Yanga wametulia na wanacheza katika mechi za ushindani Ligi Kuu Bara.
Wana kila kitu na maandalizi mazuri kule Kigamboni. Wanatazamiwa kufanya jambo la msingi.
Kama ilivyo kwa Simba, Yanga nao wanalazimika kupata pointi tisa kwenye Uwanja wa Mkapa. Ni muhimu. Kitu cha kwanza katika mpira wa Afrika ni kupata pointi zote nyumbani. Yanga pia wanaweza kushinda ugenini, lakini litakuwa jambo la nyongeza. Jambo la kwanza muhimu ni kushinda mechi tatu za nyumbani. Ukipata ushindi mmoja tu ugenini unakuwa na pointi 12.

Kama ukishinda mechi tatu nyumbani na kisha kupata sare moja inamaanisha unakuwa na pointi 10 mkononi. Ni ngumu kwa timu kufikisha pointi 12 au 10 halafu usivuke kwenda katika hatua inayofuata.
Simba alikuwa anaiwezea zaidi hii ‘Kwa Mkapa hatoki mtu’. Nyakati chache waliteleza, lakini mara zote wamekuwa imara katika jambo hilo.
Yanga anatazamiwa kupita katika kundi hili. Asipopita basi kitakuwa kichekesho kwao.
Timu iliyofika fainali za Shirikisho, timu ambayo msimu uliofuata nusura itinge nusu fainali kama sio figisu za bao la Aziz KI. Wanawezaje kutolewa katika hatua ya makundi?
Katika kundi lao wamewekwa katika nafasi ya pili huku Mazembe wakiwekwa katika kundi la vigogo. Nafasi ya juu. Kama unaamini una uwezo wa kumfunga Mazembe katika mechi mbili za kundi, kwa nini ushindwe kushika nafasi mbili za juu.
Wasipofanya hivi watageuka kuwa kichekesho kama kichekesho kingine chochote kile. Hata mashabiki wa Afrika Kusini watawacheka wananchi.
Majuzi walidhulumiwa bao la Aziz. Wakarudi tena ardhi ile ile kule Afrika Kusini wakaiteketeza moja kati ya klabu kubwa nchini mule, Kaizer Chiefs.
Ukishika nafasi katika kundi la Mazembe, MC Alger na Al Hilal basi kuna kila sababu ya kugeuka kuwa kichekesho.
Hii inakuja katika wakati ambao Yanga imeongeza watu watatu muhimu msimu huu. Boka, Chama na Prince Dube. Wanaonekana ni wachezaji wa mechi hizi.
Kama Clement Mzize hajakomaa katika mechi hizi basi unamhitaji Dube ambaye anaonekana kuwa mwepesi zaidi.
Kitu cha msingi kwa Yanga ni kutovimba kichwa (complacency). Wasiingie na matokeo yao. Wajiandae vema.