Prime
JICHO LA MWEWE: Wananchi, safari ya nchi ya ahadi imeanzia Lubumbashi?

Muktasari:
- Yanga wameanza safari yao ya kwenda nchi ya ahadi juzi pale Lubumbashi. Hatimaye wamepata pointi yao ya kwanza katika kundi lao. Hatimaye wamepata bao lao la kwanza katika michuano hii. Hatimaye Prince Dube amepata bao lake la kwanza baada ya kipindi kirefu kupita.
WAZUNGU wana msemo wao. Against all odds. Kukipata Kiswahili sahihi unaweza kusema “licha ya vikwazo vyote”. Wakati mwingine unaweza kusema ‘Dhidi ya kila pingamizi’. Baadaye unaweza kufanikiwa.
Yanga wameanza safari yao ya kwenda nchi ya ahadi juzi pale Lubumbashi. Hatimaye wamepata pointi yao ya kwanza katika kundi lao. Hatimaye wamepata bao lao la kwanza katika michuano hii. Hatimaye Prince Dube amepata bao lake la kwanza baada ya kipindi kirefu kupita.
Kuhusu mechi? Ilizikutanisha timu mbili za kushangaza ambazo zimepitia vipindi tofauti. Hawa wenyewe Mazembe wamepitia kipindi kirefu cha kutokuwa na timu ya kueleweka. Tangu Moise Katumbi alipojiingiza katika siasa na kugombana na serikali ya Congo alisahau habari za Mazembe akaruhusu wachezaji wa kawaida wajiunge na timu yake na hatimaye ikashuka kiwango.
Zamani wachezaji kama Pacome Zouzoua wangeishia Mazembe. Siku hizi wanatua uwanja wa ndege wa Mwalimu Julius Nyerere kusaini mikataba yao na timu za Kariakoo. Hawaendi tena Mazembe. Matokeo yake juzi Yanga walitarajia kushinda Lubumbashi. Mji ambao zamani hata kina Al Ahly ilikuwa lazima waache pointi.

Yanga waliruhusiwa kuota kuondoka na pointi tatu. Mara ya mwisho walipofika hapo waliifunga Mazembe na kuzoa pointi zote tatu. Kwanini wasiote kuondoka na pointi tatu? Hata hivyo, walifanikiwa kuondoka na pointi moja. Nimezungumza namna ambavyo Mazembe wamepitia kipindi cha kushangaza baada ya Moise kujiingiza katika siasa.
Lakini napaswa kuzungumzia namna ambavyo Yanga pia wamepitia kipindi cha kushangaza. Wakati Mazembe wakiwa katika kipindi kirefu cha kushangaza, Yanga wamepitia katika kipindi kifupi cha kushangaza. Ghafla wamekuwa timu ya kawaida. Mazembe halisi wangeifunga Yanga juzi. Ile Mazembe ya kina Mbwana Samatta. Lakini Yanga kamili ya msimu uliopita wangeifunga Mazembe jana.

Kulikuwa na kupoteza nafasi kutoka kwa wachezaji wa Yanga. Lakini pia walichelewa kuamka. Waliamka zaidi katika kipindi cha pili baada ya kudorora katika kipindi cha kwanza. Hata hivyo, mwishowe walifanikiwa kuondoka na pointi yao mkononi na hii inaweza kuwafanya wabadilishe kila kitu katika kundi lao. Sawa wamejiweka katika hesabu za vidole huku wakiombea mabaya kwa wengine lakini wamejiweka katika nafasi ambayo kila kitu kinawezekana upande wao. Kama wangefungwa juzi basi uwezekano ungekuwa mdogo. Lakini sasa kuna kitu wamekiamsha. Wana pointi moja mkononi. Al Hilal ana pointi tisa mkononi. Ameshinda mechi zote.
Mazembe ana pointi mbili tu. Halafu MC Alger ana pointi nne.
Kitu cha kwanza Yanga warudishe fomu yao. Warudi Dar washinde pambano linalofuata dhidi ya hawa hawa Mazembe. Kwa Mazembe hawa ni kitu kinachowezekana. Watakuwa na pointi nne mkononi na kumuacha Mazembe akiwa na ponti mbili huku akishikilia mkia katika kundi.
Wakati huo huo kama Al Ahly akimchapa MC Alger au hata akitoka naye sare basi anaweza kuwa na pointi 10 au 12. Siri kubwa ya kuwania nafasi ya pili katika mazingira kama haya ni kuhakikisha lazima unamuombea mema mtu mmoja ambaye ni mbabe wa kundi. Yanga anapaswa kumuombea mazuri Al Hilal ili amsaidie kuwanyoosha wale ambao anagombea nao nafasi ya pili.

Kama Al Hilal akiwachapa MC Alger na Mazembe katika mechi zinazofuata basi atakuwa amefuzu kabla hajacheza pambano lake la mwisho dhidi ya Yanga. Lakini ni Yanga ndio wanaotakiwa kufanya kazi yao kwa kurudisha kiwango chao kwa kuzichapa Mazembe na Al Hilal kabla ya kucheza pambano la mwisho dhidi ya MC Alger nyumbani.
Baada ya mechi ya juzi nimeendelea kutafakari kinachowatokea Yanga katika kundi hili. Tatizo sio wapinzani wao. Tatizo ni wao wenyewe. Mechi mbili walizofungwa na mechi moja waliyotoka sare Yanga wangecheza kama walivyokuwa wanacheza miezi sita tu iliyopita wangeweza kushinda mechi zote mpaka sasa. Wapinzani wao sio wakali wa kutisha.
Wapinzani wao hawana Pacome, Aziz Ki, Clement Mzize, Khalid Aucho, Ibrahim Bacca, Clatous Chama na wachezaji wa aina hii. Tatizo ni Yanga wenyewe wameshuka. Fikiria namna walivyogawa pointi tatu kijinga tu dhidi ya Al Hilal katika pambano la kwanza. Walinyemelewa kwa mashambulizi ya kushtukiza wakafungwa.

Hata kule Algers walikuwa hawajui wanafanya nini uwanjani lakini MC Alger hawakuwa na timu ya kutisha. Haishangazi kuona na wao Waarabu wameingia katika mkumbo wa kufungwa na Florent Ibenge. Na wala haitashangaza kama MC Alger wakienda kufungwa tena na Ibenge pale kwao Mauritania. Binafsi sitashangaa.
Kinachotakiwa kwa sasa ni Yanga kufanya kazi ngumu kurudia fomu yake. Labda kocha wao Mjerumani, Sead Ramovic anajua anachokifanya. Waendelee kumpa muda kwa sababu hata mashabiki wa Yanga ambao wanamlilia Manuel Gamondi wanasahau tu kwamba timu yao ilianza kuanguka chini ya mikono ya Gamondi. Baada ya kucheza vema katika michuano ya maandalizi ya msimu mpya ghafla timu ikaanza kushuka na kupata katika ligi. Mechi ya Tabora ilikuwa hitima tu.
Na sasa ni wakati wa kusubiri na kuona kama wanaweza kufika nchi ya ahadi. Kidogo ambacho kocha wao Ramovic amenifurahisha ni kutokariri kikosi. Kennedy Musonda ameanza kucheza. Inakuwaje anafunga mabao katika kikosi cha timu ya taifa ya Zambia lakini hapangwi katika kikosi cha Yanga? Inadaiwa kwamba hakuwa mchezaji wa Gamondi.
Lakini pia iwe kwa mbinu au gharama za uzembe, Aziz Ki atakuwa amejifunza kwa kukaa katika benchi huku mchezaji kama Musonda akicheza. Ni kweli Aziz anaweza kuwa juu ya Musonda lakini ni wazi kwamba Musonda anajituma zaidi. Labda inampa Aziz kunyanyua mchezo wake. Wachezaji wakikariri kucheza huwa wanajisahau.
Prince Dube? Labda bao lake litamfanya ajiamini. Pengine urafiki wake na nyavu unaweza kuanza kurudi. Wakati mwingine bao moja tu linabadilisha kila kitu. Yanga walimsajili kwa ajili ya mechi kama ya juzi. Kama ni Ligi ya ndani washawahi kuchukua mataji na Clement Mzize.