JICHO LA MWEWE: Mwashiuya angekuwa staa mkubwa Simba
Muktasari:
NDANI ya wiki moja unaunganisha matukio mawili na kupata jibu moja rahisi. Unahitaji kutumia akili ya kawaida tu. Nilikuwa studio nikichambua pambano la Simba na Azam wiki iliyopita. Wachezaji wa benchi la Simba walinisikitisha sana.
NDANI ya wiki moja unaunganisha matukio mawili na kupata jibu moja rahisi. Unahitaji kutumia akili ya kawaida tu. Nilikuwa studio nikichambua pambano la Simba na Azam wiki iliyopita. Wachezaji wa benchi la Simba walinisikitisha sana.
Brian Majwega, lazima atakuwa analipwa kwa Dola na si pesa yetu ya madafu. Aliingia kipindi cha pili kuweka uhai wa Simba katika mbio za kuchukua ubingwa kama Yanga ikiteleza mbele ya safari. Majwega alikuwa kichekesho tu.
Ulitokea wakati ambapo alitazamana na kipa wa Azam, Aishi Manula hatua saba kutoka alipo. Shuti alilopiga Manula alilisubiri likitembea taratibu na kulidaka. Huyu ndiye mchezaji wa kulipwa. Ameanzia benchi na unaona kuwa kocha alikuwa na kila sababu ya kumweka benchi. Baadaye akaingia Haji Ugando. Naye alikuwa kichekesho. Kuna wakati alitazamana na kipa Manula na kujikwaa mwenyewe. Kifupi hakukuwa na mchezaji wa Simba kutokea benchi ambaye angeweza kubadili matokeo. Labda kama Ibrahim Ajib angekuwepo katika benchi. Mussa Hassan Mgosi umri umempita.
Juzi nilikuwa natazama pambano la Yanga na Esperanca ya Angola pale Uwanja wa Taifa. Kinda Geoffrey Mwashiuya aliingia akitokea katika benchi na akaubadili mpira kabisa. Krosi yake ya kwanza ndiyo ambayo Simon Msuva aliitumia kupata bao zuri. Baadaye aliendelea kusumbua sana. Mwashiuya ana uwezo mkubwa wa kukokota mpira, kupiga chenga na kupiga krosi. Kifupi ana madhara kwa walinzi kwa sababu ni mwepesi na ana kasi nzuri. Huwa nawaza, ingekuwa vipi kama Simba wangefanikiwa kumnasa Mwashiuya kabla ya Yanga? Jibu ni kwamba angekuwa staa mkubwa.
Kuna sababu nyingi. Kwanza ni kwa sababu angepewa nafasi. Simba si timu ngumu kwa wachezaji vijana. Yanga ni timu ngumu kwa vijana. Kuna presha kubwa sana kwa wachezaji wa Yanga kuliko Simba na ndiyo maana vijana wengi wanachemsha.
Hata Simon Msuva mwenyewe nusura achemshe wakati akianza maisha yake Yanga. Mashabiki wa Yanga wanataka matokeo ya haraka haraka. Hawana simile. Wachezaji makinda wanahitaji kuvumiliwa kidogo kwa sababu wakati mwingine wanafanya utoto uwanjani. Simba iliwavumilia kina Ramadhan Singano, Said Ndemla, Jonas Mkude, Hassan Isihaka na wengineo. Ni sehemu ya utamaduni wao. Lakini kwa hali yao ya kiuchumi walilazimishwa kuwa na subira kwa sababu hawamudu kununua wachezaji wa bei ghali na kuwalipa mishahara mikubwa.
Pia kwa sasa Yanga imeamua kutumia mfumo wa pesa katika kujenga kikosi imara na inakuwa ngumu kwa vijana kupata nafasi pale. Ni kitu cha kawaida kwa timu ambazo zina matumizi makubwa ya pesa katika soka la kisasa. Mwashiuya anakaa nje na timu inafanya vizuri kwa sababu Yanga wana wachezaji wazuri.
Kwa Simba Mwashiuya angepata nafasi kwa sababu timu yao haijaundwa na mastaa wakubwa kama Yanga. Kwa uwezo huu wa kina Majwega sioni ni wapi Mwashiuya angeshindwa kuwa staa wa timu. Hata hivyo, hali hiyo ya kina Mwashiuya inawatokea hata vijana wengi wanaosaini katika klabu zenye matumizi makubwa ya pesa Ulaya kama Manchester City, PSG na nyinginezo. Nafasi ni ngumu kwa vijana.
Ukiachana na Mwashiuya, hata yule mfungaji wa bao la pili la Yanga, Matheo Anthony angeweza kuwa mchezaji mkubwa Simba kwa sababu zile zile ambazo nimezitoa kwa Mwashiuya.
Zaidi ya yote ni kwamba kama wangekuwa wanacheza kila wikiendi maana yake uwezo wao wa kujiamini ungekuwa mkubwa uwanjani. Kama wanaweza kupewa dakika chache na kujiamini kama wanavyojiamini basi si ajabu wangekuwa mbali kwa sasa. Kuliko hapo walipo.
Hata hivyo hakuna wanachoweza kufanya. Huwezi kuwalaumu. Wachezaji wengi wa kisasa duniani kote uamuzi wao unasukumwa zaidi na pesa.