Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

JICHO LA MWEWE: Morrison kutoka Sandton, Johannesburg hadi Chunya

Muktasari:

  • Kutoka Soweto hadi Chunya. Kutoka uzunguni mwa Jiji la Johannesburg pale Sandton kisha hadi Chunya, Mbeya. Nadhani ni maisha ambayo Morrison amejichagulia mwenyewe. Tusimuingilie sana. Tusimvurugie sana alichopanga maishani. Kupanga ni kuchagua. Nadhani yeye amechagua kuwa kama alivyo na kuishi kama anavyotaka.

BERNARD Morrison alikuwa kwenye Uwanja wa Ndege wa Songwe wikiendi iliyopita akisaini katika klabu ya KenGold ya pale Chunya. Hapana shaka baada ya kutua viwanja vya Songwe alipita kando ya Uwanja wa Sokoine na kuanza kupandisha vile vilima vya kuelekea Wilaya ya Chunya.

Kutoka Soweto hadi Chunya. Kutoka uzunguni mwa Jiji la Johannesburg pale Sandton kisha hadi Chunya, Mbeya. Nadhani ni maisha ambayo Morrison amejichagulia mwenyewe. Tusimuingilie sana. Tusimvurugie sana alichopanga maishani. Kupanga ni kuchagua. Nadhani yeye amechagua kuwa kama alivyo na kuishi kama anavyotaka.

Aliondoka Orlando Pirates ya Afrika Kusini akiwa na kipaji maridhawa akaacha kesi ya gari la wizi ikimuandama. Akaenda zake Congo kucheza AS Vita kwa muda mfupi. Akarudi zake Ghana ambako Injinia Hersi Said alimfuata mpaka kijijini kwao kwa ajili ya kuja kucheza Yanga. Alionyesha kipaji maridhawa. Jina lilibadilika na kuwa BM33 kutokana na jezi aliyokuwa akivaa.

Baadaye wote tunajua kilichotokea akiwa Yanga. Ile kesi yake ya CAS akalazimisha kuondoka Yanga kwenda kwa watani wao Simba, huku akiwa amejenga urafiki mkubwa na marehemu Zacharia Hans Poppe. Yanga waliachwa na maumivu makubwa kifuani. Wasingeweza kusamehe wala kusahau. Kule alipewa jina jipya la BM3, kwani alikuwa akivaa jezi namba tatu iliyowahi kuvalia na Haruna Moshi ‘Boban’. Jina linabadilika.

Alipoenda Simba, kama ilivyokuwa Yanga, alionyesha kipaji kikubwa lakini usumbufu ukawa mkubwa zaidi ya kipaji. Ni kama msichana mrembo aliyevaa sketi fupi. Kuna kitu unatamani kukiona zaidi kutoka kwake lakini haukioni. Unaishia katika matamanio tu. Ben alikuwa kama yule yule wa siku za mwisho wakati anakaribia kuondoka Yanga.

Ilifikia wakati Barbara Gonzalez aliyekuwa CEO wa Simba aliamua kumfungia kwa utovu wa nidhamu. Yanga wakawacheka Simba. Wakawakejeli kwamba kunguru alikuwa hafugiki. Baadae Ben akafanya vituko akamaliza mkataba wake huku Yanga wakimsubiri kwa lengo ya kumrudisha mtoto nyumbani huku wakiwakejeli Simba.

Hatimaye akarudi Yanga. Akarudi nyumbani. Kama kawaida yake alionyesha dalili ya kipaji maridhawa lakini kipaji hicho kilizidiwa nguvu na vituko maridhawa. Kuna wakati alikwenda kwao Ghana akakaa miezi miwili wakati Ligi inaendelea. Safari hii ikawa zamu ya Simba kuwacheka Yanga. Waswahili wanasema ‘muosha huoshwa’ wakati wazungu wanasema ‘what goes around comes around’.

Alipomaliza mkataba wake Yanga hawakuwa na hamu naye. Na hapo hapo Simba hawakuwa na hamu naye. Na hapa ndipo Morrison alipozichanganya karata zake vibaya. Aliweza kuwafanya Yanga wajinga mara mbili lakini asingeweza kuwafanya Simba wajinga mara mbili. Angekuwa na akili angejua kwamba kurudi kwake Yanga kulikuwa kunamaanisha hiyo ilikuwa kete yake ya mwisho kwa hizi timu.

Simba walijua kwamba huo ndio ungekuwa mchezo wa Morrison. Unaharibu huku ukiwa na imani utarudi kule. Simba hawakutaka kufanywa wajinga mara mbili. Wakafunga milango. Akiwa Yanga katika ujio wake wa pili Morrison alipaswa kujituma na kupambana kwa ajili ya mambo mawili.

Kwanza ni kuhakikisha anaishika Yanga mfukoni ili wasipumue. Wapigane kuhakikisha wanambakiza baada ya mkataba wake kumalizika. Lakini pili kama angepambana bila ya vituko huku akionyesha kipaji chake maridhawa basi Simba wangeweza kushawishika kupigania saini yake wakiamini kwamba amebadilika kitabia. Hakuweza kufanya hivyo.

Akakimbilia zake FAR Rabat ya Morocco. Nilijua asingetoboa. Hata kama asingepata majeraha lakini asingepata raha ya kuishi Morocco. Nimefika mara tatu pale Morocco. Napafahamu. Wana starehe zao lakini kwa mtu ambaye ulizoea starehe na sifa za jiji la Dar es Salaam kama ilivyokuwa kwa Morrison basi ingekuwa vigumu kwake kuishi Morocco.

Haishangazi kuona hata Clatous Chama na Tuisila Kisinda walipopata bahati ya kurudi tena Dar es Salaam kucheza Simba na Yanga hawakusita mara mbili. Dar ina utamu wake. Mtazame namna Aziz Ki anavyoishi. Asingeweza kuondoka kirahisi Dar es Salaam. Jiji ambalo linakufanya uwe mfalme kiurahisi tu.

Na sasa Morrison amerudi Tanzania. Angekwenda wapi zaidi? Hapa anapendwa. Amefanya vituko vingi lakini anapendwa. Akipita mitaani watu wanamuita kwa nguvu. Kipenzi cha mashabiki wa pande zote mbili. Simba na Yanga. Hata hivyo, wameishia kumpenda tu  ingawa wanajua ameshindikana. Kile ambacho amewaonyesha hawawezi kusahau.

KenGold amesaini mkataba wa miezi sita tu. Ni mkataba ambao umetupa shaka. Ni KenGold ndio wametaka hivyo au Morrison ndio ametaka hivyo. Hili la kwanza ndio linashawashi zaidi. Labda KenGold wanataka kwanza kumpima tabia zake kabla hawajaamua kuwa naye kwa muda mrefu. Tayari walishaziona tabia zake akiwa pale Kariakoo. Huenda wanapima maji kwa kidole kabla ya kuamua kuogelea.

Lakini kitu kingine kigumu kwetu ni kukaa katika upande wa Morrison. Haujui anawaza nini? Labda anawaza kufanya makubwa pale Chunya kwa ajili ya kuzivuta tena mezani zile timu mbili za Kariakoo. Hata hivyo, si ajabu wala hawazi hivyo. Kama angekuwa na mawazo hayo ya kupania kufanya kazi nzuri si ajabu mpaka leo angekuwa katika timu moja kati ya Simba au Yanga.

Nadhani alichokifanya Kariakoo kimesababisha hata miamba mingine yenye pesa Azam na Singida wasifikirie kumchukua. Labda hii miezi sita anaweza kuwa amepania kufanya makubwa kiasi cha kuwafikirisha na miamba hiyo kitu tofauti? Hatuwezi kujua. Kama angekuwa na kifua hicho basi nyakati ni hizi.

Ni nyakati ambazo pia tungeweza kufikiria kama taifa kwenda naye Morocco katika michuano ya Afcon. Si anatamani kuwa Mtanzania na kuichezea Taifa Stars? Katika ubora wake, hakuna winga wa Taifa Stars ambaye anaweza kufikia ubora wa Bernard Morrison. Wakati analilia pasipoti yetu watu wengi tulikuwa upande wake kwa maana ya kipaji lakini hatukuwa upande wake kwa maana ya nidhamu yake.

Pamoja na kila kitu Morrison anatufundisha namna maisha yanavyokwenda kasi katika mpira wa Tanzania. Kutoka Sandton hadi Chunya. Kutoka Simba na Yanga hadi Chunya. Kutoka Rabat Morocco hadi Chunya. Wazungu wanaita ‘falling from the grace’. Kutoka katika ufalme hadi kuwa raia wa kawaida tu. Ndicho kinachoweza kumtokea mwanadamu au mwanasoka anayecheza Tanzania.

Watazame Yannick Bangala na Djuma Shaban. Namna walivyopokewa nchini. Namna walivyokuwa Wafalme. Sasa hivi mmoja ameachwa na Azam na mwingine ameachwa na Namungo. Inathibitisha uamuzi sahihi kutoka kwa wakubwa wa Kariakoo. Kuna vitu tunaviangalia kama mashabiki na kuna vitu wale viongozi wa Kariakoo wanaviangalia kama hali halisi. Huwa wanaishi na hawa wachezaji. Tusubiri kumuona Morrison. Natamani kumuona akiwa katika ubora wake. Aonyeshe kile anachokiweza. Na kama akionyesha kile anachokiweza nataka kuona kama mabosi wetu wa Kariakoo wanaweza kutamani kuogelea tena katika bwawa lake la kina kirefu ambalo kila siku wanatamani kuogelea lakini maji yanawashinda.