Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

JICHO LA MWEWE: Kuzama na kuibuka tena kwa Kapombe 'Baba Easter'

JICHO Pict

Muktasari:

  • Mlinzi ambaye anapaswa kuwa mfano wa kuigwa katika kupiga krosi zinazofika katika kichwa au mguu wa mchezaji mwenzake uwanjani ni  alikuwa ni Juma Abdul 'Mnyamani'. Si ajabu Amissi Tambwe aliwahi kuibuka kuwa mfungaji bora mara mbili akiwa katika jezi ya Yanga.

WAKATI fulani Liverpool ilikuwa ya moto sana. Kule mbele kulikuwa na watu watatu hatari. Sadio Mane upande wa kushoto, Mo Salah upande wa kulia. Roberto Firmino alikuwa anacheza katikati. Walikuwa wa moto hasa chini ya yule Mjerumani, Jurgen Klopp.

Nilipenda staili yao ya mpira wa kisasa. Kukabia juu kabisa. Lugha ya wachambuzi wetu huwa wanaita 'high pressing'. Liverpool walikuwa wanakaba wote. Hawataki ukae na mpira hata sekunde tatu. Mane, Salah na Firmino wangekabia kule kule. Mpira ungewapita bado wangegeuka. Lakini hapo kwa nyuma kina Fabinho pia walikuwa wanakaba vilivyo.

Baada ya kuupata mpira wangeupeleka mbele kwa kasi. Muda mwingi Liverpool walikuwa bora. Walikuwa bora kitimu na kwa mchezaji mmoja mmoja. Hatukujua kama wengine walikuwa bora lakini ubora wa timu ulikuwa unawasaidia pia kuwa bora. Mmojawapo alikuwa Trent Alexander-Arnold. Kumbe katika ukabaji alikuwa mweupe. Hakuwa bora sana. Katika kwenda mbele alikuwa bora sana.

Tulikuja kugundua madhaifu ya Trent wakati Liverpool ilipopoteza ubora. Ile pressing ilipotea. Kina Mane na Firmino wakaanza kuchoka na kukimbilia zao kuchukua noti za Saudi Arabia. Trent akapwaya vilivyo kwa sababu Liverpool haikuwa tena ilipokuwa na mpira na wakati haina mpira. Ungeweza kumuonea huruma rafiki yetu namna alivyokuwa anahaha na kina Gabriel Martinelli.

JC 05

Kumbe kocha wake wa timu ya taifa, Gareth Southgate alishaujua mapema udhaifu wake Trent. Katika timu ya taifa Trent hakutamba. Hakuwa na namba na badala yake alikuwa anacheza Kyle Walker ambaye ni mkabaji mzuri na ana kasi nzuri uwanjani. England hawakuwa bora kuliko Liverpool kwa hiyo Southgate alimhitaji zaidi Walker kuliko Trent. Wengine hawakulielewa hili.

Nimeikumbuka hii habari ya Trent baada ya kuona kiwango cha staa wa Simba, Shomari Kapombe 'Baba Easter' katika siku za karibuni. Kwa sasa amerudi katika ubora wake kuliko wakati mwingine wowote katika miaka ya karibuni. Shomari ni bora kama alivyo na yeye ni bora katika vyote tofauti na Trent. Yeye ni bora katika kukaba, pia ni bora katika kushambulia.

Hata hivyo, miaka ya karibuni wakati Simba ikiwa imeshuka katika ubora wake Shomari alionekana kwenda chini. Yeye na Mohamed Hussein 'Tshabalala' katika mbavu nyingine ya Simba mashabiki walizusha maneno mengi. Kwamba wamechoka. Kwamba ulikuwa muda sahihi wa kutafuta wabadala wao. Wenye busara kidogo walitaka wapumzishwe katika mechi mbili tatu ili wazipashe moto betri zao.

JC 01

Hata usajili wa Israel Mwenda na Duchu Kameta ulilenga katika kuipora namba ya Shomari na siyo kuwa wasaidizi wake. Ni vile tu ubora ambao Shomari alikuwa ameuweka baina yake na walinzi wengine wa pembeni ndani na nje ya timu yake ulikuwa mkubwa kiasi kwamba ilikuwa ngumu kuipora namba yake hata wakati kiwango chake kilipoonekana kuchechemea.

Hata hivyo, kiwango chake duni kilikuja na ukweli kiwango cha timu kilikuwa kinamuelemea Shomari kutimiza majukumu yake. Lakini sasa Simba inawaka na Shomari anarudi katika ubora wake kwa sababu muda mwingi Simba inakuwa bora ikiwa na mpira na isipokuwa na mpira. Ni rahisi kwa mchezaji wa aina yake kuonyesha ubora wake.

Wakati mwingine kiwango cha timu na mchezaji bora huwa vinabebana. Katika umri wa miaka 33 ambao anao sasa hivi, Shomari anahitaji kucheza katika timu bora ambayo inakaa na mpira ili afurahie maisha yake ya mwisho ya soka. Kucheza katika timu ambayo kwa dakika nyingi inafukuza mpira sio jambo ambalo litaonyesha ubora wake. Haishangazi kuona kadri Simba inavyoendelea kuwaka katika simu za karibuni ndivyo Shomari anavyozidi kuwaka.

JC 04

Akigeuka nyuma Yusuf Kagoma anakaba kwa niaba yake katika eneo la katika, wakipitwa Che Malone anakaba kwa nyuma zaidi. Wakienda mbele anakutana na mpira mbele yake na anapiga krosi ambazo zinazaa mabao kama ambavyo amefanya katika siku za karibuni. Watu wakibeba majukumu kwa pamoja maisha yanakuwa mazuri kwa Shomari.

Kwa ninavyomtazama kwa sasa Shomari inabidi aendelee kujitunza tu. Kuhusu umri anapaswa kuziba masikio yake kwa sababu mashabiki wa Tanzania wana tabia ya kupenda kumtoa mchezaji mchezoni pindi wanapoanza kumchoka. Katika mpira kitu cha msingi ni kiwango na siyo umri. Ukiwasikiliza Watanzania unaweza kutangaza kustaafu soka mapema wakati bado una uwezo.

Kama Khalid Aucho angekuwa Mtanzania basi tayari ingekuwa tumeshamtoa katika mpira wetu kwa muda mrefu sasa kwa sababu ameanza kucheza soka zamani. Kina Jerry Tegete tuliwaondoa katika mpira mapema kwa kisingizio cha umri kumbe walikuwa wameanza kucheza soka mapema. Wachezaji wachache wanakomaa na kuziba masikio katika suala la umri. Mfano ni Juma Kaseja na sasa Kelvin Yondani.

JC 02

Shomari anapaswa kuendelea kujitunza tu. Ule upande wake anaocheza kule Uganda kulikuwa na mtu anaitwa, Simon Masaba. Aliitendea haki ile nafasi ya upande wa kulia katika kikosi cha timu ya taifa ya Uganda 'The Cranes' hadi alipokaribia miaka 40. Kwa nini Shomari ashindwe? Tusimbugudhi.

Kwa nini mashabiki wa Liverpool hawapigi kelele Virgil Van Dijik astaafu au aondoke wakati huu akiwa na umri wa miaka 33? Wenzetu wanaangalia zaidi kiwango kuliko umri. Sisi kitu cha kwanza tunaangalia zaidi umri kuliko kiwango cha mchezaji husika. Mchezaji anavishwa uzee ambao hana kwa sababu amekaa katika macho yetu kwa miaka mingi.

Tunahitaji ubora wa Shomari pia katika michuano ya Afcon pale Morocco Desemba mwaka huu. Kwa hali ilivyo sasa sijaona beki wa kulia ambaye anaweza kufikia ubora wake miongoni mwa wachezaji wazawa. Alivumilia kukaa nje muda mrefu katika kikosi cha Taifa Stars, huku zama zake zikionekana zimekwisha lakini aliporudi ametusaidia kufuzu kwenda Morocco.

Akijitunza zaidi tunaweza kuwa naye hata katika michuano ya Afcon ambayo itafanyika nyumbani Tanzania miezi 24 ijayo. Hakuna kisichowezekana. Awe mbishi tu na asisikilize sana maneno yetu. Hata Mbwana Samatta tulitangaza amechoka na amezeeka lakini sasa hivi ameamka kule Ugiriki na anaweza kupata mkataba mpya katika klabu yake ya PAOK.

JC 03

Hakuna beki wa kulia ambaye tumewekeza sana kwake kama Shomari. Amecheza mechi nyingi na timu za taifa za vijana na za wakubwa pamoja na Azam na Simba. Amecheza mechi nyingi za ndani na za kimataifa. Ni wachezaji wachache wa aina yake katika mpira wa Tanzania kwa sasa. Ukiwa na mchezaji kama yeye ni hazina na haupaswi kumtoa mchezoni.

Kitu pekee ambacho wakati mwingine Shomari na walinzi wetu wengi wa pembeni wananiangusha ni krosi zao. Aliwahi kuniambia staa wa zamani wa Yanga na timu ya taifa ya Tanzania, Edibily Lunyamila kwamba krosi ni pasi kama pasi nyingine yoyote ile uwanjani. Mabeki wetu wengi wa pembeni wana tatizo la kutoangalia krosi zao wanapeleka wapi. Wanapiga tu ili mradi wanaingiza mpira ndani ya boksi.

Mlinzi ambaye anapaswa kuwa mfano wa kuigwa katika kupiga krosi zinazofika katika kichwa au mguu wa mchezaji mwenzake uwanjani ni  alikuwa ni Juma Abdul 'Mnyamani'. Si ajabu Amissi Tambwe aliwahi kuibuka kuwa mfungaji bora mara mbili akiwa katika jezi ya Yanga.