JICHO LA MWEWE: Hakuna cha ajabu alichoongea Asukile, tuamue tu

SIJUI Watanzania wangapi wataiona pepo. Kama kweli pepo ipo basi wengi tutachomwa moto. Tazama jinsi watu walivyoigiza kushtuka baada ya beki na nahodha wa Tanzania Prisons, Benjamin Asukile kudai kwamba wachezaji wa timu yao walikuwa wakipigiwa simu na watu wa Yanga kwa ahadi ya kupewa Shilingi 40 milioni wafungishe.

Unaweza kudhani aliongea kitu kipya katika soka. Kama ingekuwa Ulaya nadhani habari hii ingekuwa kubwa maradufu. Magazeti ya Waingereza The Sun, Daily Mirror, Daily Mail na mengineyo yangeibuka na vichwa vizito vya habari. Neno SCANDAL lingetumika sana.

Ni kama ambavyo Waitaliano waliibuka na vichwa vizito vya habari wakati soka la Italia lilipokumbwa na kashfa za kupanga matokeo ambazo ziliishusha Juventus Turin. Kashfa ile ilijulikana kama Calciopoli.

Kwa Tanzania sijui tungeanzisha kashfa ngapi kama hizi. Hii ya Asukile ni moja kati ya kashfa milioni moja ambazo zingeingia katika soka letu. Rushwa katika soka ni utamaduni wetu. Wala haishtui. Tukutane mwaka mmoja baadaye tuone kama kauli ya Asukile ilipelekea mtu yeyote kuhukumiwa popote.

Tumewahi kukumbana na kashfa nyingi kama hizi. Ukizihesabu kwa vidole basi unaweza kumaliza hadi vidole vya miguuni na hauwezi kusikia kama iliwahi kutokea hukumu yoyote. Majuzi tu kipa wa Yanga, Ramadhan Kabwili alitoa kashfa kama hii.

Hapo nyuma zimekuwepo kashfa nyingi za kina Shaaban Kado, Nsa Job, Said Morad na wenzake kina Erasto Nyoni, Aggrey Morris na Deo Munishi ‘Dida’ na wengineo. Hakuna anayejali. Kutojali ni utamaduni wetu. Na tumeamua kutojali kwa ajili ya kutoa nafasi kwa matukio haya kujirudia kwa sababu wote tunajua kwamba tunahusika.

Tanzania kuna aina lukuki ya kashfa ambazo tumeamua kuzifungia macho. Kuna kashfa za waamuzi kupewa pesa. Katika vikao vya kahawa huwa tunazungumza bila ya kufichana. Utasikia tu “hatukuwaona waamuzi”. Mwingine atasema “Tungemuona mwamuzi lile bao asingekataa”.

Wakati mwingine inatisha zaidi unaposikia “Simba inapanga orodha ya waamuzi wote wa mechi zao”. Huku kwingine utasikia “Yule mwamuzi anacheza mechi za Yanga tu na lazima washinde”. Haujawahi kusikia habari kama hii?

Imefikia wakati wakubwa wenyewe kwa wenyewe wanaogopana mpaka wanafikia hatua ya kumhonga mwamuzi ili achezeshe kwa haki. Usicheke. Wenyewe wanaosoma hapa wanajua michezo hii na wala hawashtuki.

Kuna hii ya Asukile nayo sio mpya. Kuwapa pesa wachezaji wa timu pinzani. Hii wala haina aibu. Asukile amesema lakini jiulize kuna wangapi hawasemi. Na hata kama kweli hawasemi unadhani hatujui? Tunajua sana. Haujawahi kusikia inasemwa mahala; “yule golikipa mzuri sana lakini tatizo lake ni duka yule.” Inamaanisha kipa ni mzuri, lakini tatizo lake anauza sana mabao. Ni kitu cha kawaida katika soka letu na hata katika mazungumzo yetu ya kila siku.

Haujawahi kusikia hii nyingine? “yule kipa sisi Simba tunamtaka lakini tatizo lake ni duka sana. Anauza sana yule”. Huwa inasemwa hii mara nyingi tu bila ya kificho.

Ukikaa meza moja na viongozi wa TFF, Bodi ya Ligi, Simba, Yanga, Azam na wengineo haya ni maongezi ya kawaida tu kama ambavyo Wanasiasa wana maongezi yao kule bungeni na kwingineko. Rushwa ni sehemu ya mazungumzo ya kawaida kabisa.

Asukile amelisema hili watu wanajifanya kushtuka kama vile halipo. Ni kama mbuni wanapoamua kujificha kwa kufunika kichwa mchangani wakati mwili wote unaonekana wazi. Kwa sasa kila mtu atajifanya anamshangaa Asukile.

Alipoongea Kabwili watu wa Yanga walishupalia kweli kweli nikajikuta nawauliza “Mna uhakika nyinyi hamfanyi?” Ni swali lile lile ambalo tunaweza kuwauliza watani wao ambao wamelishupalia swala hili.

Muda si mrefu utasikia Asukile ameitwa TFF kujieleza. Anaweza kubadilisha maneno au kuonywa, lakini ukweli utabakia pale pale kwamba mambo haya ni ya kawaida katika soka letu. Waliomuita wanayajua na hata aliyeitwa anajua kwamba ni kweli.

Ile mechi ya Prisons ilikuwa ya FA tu. Hauwezi kujua wakubwa wanataka fainali ya namna gani mbele ya safari ili Simba na Yanga zikutane kwa ajili ya kipato. Lakini hapo hapo hauwezi kujua nani anasimama nyuma ya haya kwa sababu wakati mwingine sio TFF nzima inayofanya haya. Kuna wajanja wachache tu wanajituma.

Asukile ameongea kitu ambacho kipo katika michuano hiyo, Ligi Kuu, Daraja la Kwanza na kwingineko. Hata mechi za mtaani ni jambo la kawaida tu kwamba mtu aliyeanzisha michuano fulani anataka timu fulani na fulani zifike fainali.

Nadhani tusimng’ang’anie sana.sukile. Ameendeleza wimbi la Kabwili.