Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Janja ya Al Masry yashtukiwa, Fadlu ajipanga

MASRY Pict

Muktasari:

  • Wekundu hao wa Msimbazi walitua nchini humo wiki iliyopita, ambako sikukuu ya Eid el Fitr waliila wakijiwinda kwa ajili ya mchezo huo unaotarajiwa kupigwa leo, majira ya usiku kipute kikianza saa 1:00 usiku.

Kuna mambo kibao yanaendelea hapa nchini katika anga la michezo, wakati Ligi Kuu Bara inaporejea leo, lakini kule Misri, Simba itakuwa uwanjani dhidi ya Al Masry kuwania kutinga nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Wekundu hao wa Msimbazi walitua nchini humo wiki iliyopita, ambako sikukuu ya Eid el Fitr waliila wakijiwinda kwa ajili ya mchezo huo unaotarajiwa kupigwa leo, majira ya usiku kipute kikianza saa 1:00 usiku.

Lakini, tathmini ya kiufundi ya Simba na Al Masry inatafsiri kwamba mechi dhidi yao Jumatano hii huenda ikaamuliwa kuanzia dakika ya 20 mpaka 30.

Mtihani wa kwanza alionao Kocha Fadlu Davids ni kuivusha Simba kutoka hatua ya robo fainali kwenda nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, kwenye Uwanja wa New Suez uliopo Misri.

Mchezo huo wa mkondo wa kwanza hatua ya robo fainali ya michuano hiyo, utapigwa kuanzia saa 1:00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki.


KWANINI DAKIKA 20?

Kocha wa zamani Simba, Abdelhak Benchikha, ambaye yupo nchini Misri akiifundisha Modern Sport, amewasisitiza Simba kuwa imara kwenye safu yao ya ulinzi ndani ya dakika 20 za mwanzo bila kuruhusu makosa yoyote na waongeze umakini kwenye mipira yote ya krosi inayopigwa dhidi yao kwani Waarabu hao ni wajanja.

Akizungumza na Mwanaspoti kwa njia ya simu akiwa Misri alisema; “Lazima wawe imara kwenye ulinzi haswa dakika 20 za kwanza ambazo wenyeji wao huwa wanatafuta bao kwa nguvu ili wamiliki mchezo. “Hapo ni lazima kocha wa Simba apange safu yake ya kiungo imara, lakini pia ukuta wake ujue kucheza krosi na wasiruhusu sana wapinzani wao, wawashambulie ndani ya eneo la hatari."


SIMBA NA DAKIKA 30

Takwimu zinaonesha kwamba Simba katika mechi sita za hatua ya makundi zilizowapa tiketi ya kucheza robo fainali, imefunga mabao manane na kuruhusu manne huku yote ikiyagawa kwa usawa kila kipindi.

Katika mabao manane ya kufunga, manne yamepatikana kipindi cha kwanza na mengine cha pili, huku yale manne ya kufungwa pia mawili kipindi cha kwanza na yaliyobaki kipindi cha pili.

Kwa yale mabao manne ya kipindi cha kwanza, matatu yamepatikana dakika 30 za kwanza, hivyo inaonesha Simba ndani ya muda huo inacheza kwa nguvu kubwa sana kusaka matokeo bora mapema lakini pia imeshuhudiwa ikiruhusu mabao mawili katika muda huo.

Pia mabao mengine mawili iliyoruhusu yalitokea dakika tano za kipindi cha pili tangu kuanza yote yakifungwa dhidi ya CS Constantine katika mchezo wa pili. Kwa ujumla, Simba imeruhusu mabao matatu katika dakika tano za kwanza kwa vipindi viwili tofauti kwani dhidi ya CS Sfaxien iliruhusu bao dakika ya tatu tangu kuanza kwa mchezo.

Al Masry kati ya mabao yake saba iliyofunga hatua ya makundi, sita yamepatikana kipindi cha kwanza hali inayodhihirisha mchezo huu utachezwa kwa tahadhari kubwa sana kipindi hicho. Ni bao moja pekee Al Masry imefunga kipindi cha pili dakika ya 74 dhidi ya Enyimba.

Waarabu hao pia wapo vizuri katika kufunga mabao ya mapema kwani matatu yamepatikana ndani ya dakika 10 za kwanza, huku matatu mengine yakipatikana dakika tano za mwisho kuelekea kumalizika kipindi cha kwanza, hii ni kuanzia dakika ya 41 hadi 45.

Yale mabao manne iliyoruhusu, yote ni kipindi cha pili ambapo kama Simba itakuwa makini zaidi kipindi hicho, inaweza kuwapa matokeo bora kwani kikosi chao kimeonekana kuwa na uwezo wa kufunga vipindi vyote tofauti na wapinzani wao.


FADLU ANA MATUMAINI

Licha ya kwamba ni mtihani mgumu kwa Simba, lakini Fadlu ana matumaini ya kufanya vizuri huku akisema kuna vitu wanavifahamu kuhusu wapinzani wao hao na wamefanyia kazi ili kupata matokeo mazuri ingawa amekiri Al Masry wana timu nzuri na itakuwa changamoto kubwa kukabiliana nao.

"Kukabiliana na Al Masry sio rahisi, lakini tulikuwa na maandalizi ya msimu nchini Misri, hivyo tunafahamu nini tunachotarajia kupata katika mchezo wa kwanza," alisema Fadlu.

Fadlu alibainisha kuwa hata hivyo maandalizi yamefanyika vizuri ikiwa suala la kiufundi kwani benchi la ufundi limewasoma wapinzani wao kupitia mechi zao za nyuma.

Hayo yote yakiwa yanafanyika, Simba kiu yao kubwa ni kuona safari hii wanakivuka kikwazo walichonacho ambacho wamekuwa wameshindwa kukivuka katika robo fainali tano zilizopita kwenye michuano ya CAF.

Simba yenye rekodi ya kuwa timu ya Tanzania iliyocheza robo fainali nyingi za CAF kuanzia 2018-2019 ambapo hii ya sasa ni ya sita, lakini haijawahi kuvuka hapo jambo linalowaumiza kichwa wanapouendea mchezo huu.

Katika mara zote hizo tano zilizopita, Simba imekuwa ikikwama ugenini kwani hakuna hata mechi moja ya ugenini iliyoshinda zaidi ya kupoteza tatu kwa muda wa kawaida na nyingine mbili wakipoteza kwenye mikwaju ya penalti.

Wakati ugenini hali ikiwa mbaya zaidi, Simba ina uwezo wa kuutumia vizuri uwanja wa nyumbani kwani mechi tano za robo fainali zilizopita, imeshinda tatu dhidi ya Kaizer Chiefs, Orlando Pirates na Wydad, sare moja (dhidi ya TP Mazembe) na kupoteza moja (dhidi ya Al Ahly), hivyo matokeo ya kutopoteza ugenini dhidi ya Al Masry, yanaweza kuwa na faida kubwa kwao mechi ya marudiano.

Faida ya Simba itakuja kutokana na kujifunza kupitia makosa kwani hii ni mara ya pili inaanzia ugenini hatua hii baada ya msimu wa 2020-2021 kufungwa 4-0 dhidi ya Kaizer Chiefs, nyumbani ikaja kushinda 3-0 na kushindwa kuvuka kufuatia matokeo ya jumla kuwa Kaizer 4-3 Simba.

Endapo Fadlu atafanikiwa kukiongoza kikosi cha Simba kushinda mechi hii, itakuwa ni mara ya kwanza timu hiyo kufanya hivyo hatua hii baada ya watangulizi wake Patrick Aussem (2018-2019), Didier Gomes Da Rosa (2020-2021), Pablo Franco Martin (2021-2022), Roberto Oliveira 'Robertinho' (20222-2023) na Abdelhak Benchikha (2023-2024) kushindwa.

"Malengo yetu ni kucheza kwa nidhamu ugenini ili kujiwekea mazingira mazuri mechi ya nyumbani," alibainisha Fadlu.


WA KUCHUNGWA

Katika wachezaji 22 walionao Simba nchini Misri, kuna mmoja namba zake zinawafanya walinzi wa Al Masry kuwa naye macho zaidi kwenye mchezo huu kwani wakikubali kumuacha anaweza kuwadhuru muda wowote.

Jean Charles Ahoua, ndiye mchezaji ambaye amekuwa na namba nzuri zaidi kwenye kikosi cha Simba kutokana na kuwa na mchango wa mabao manne katika mechi sita za hatua ya makundi kabla ya kufuzu robo fainali. Kiungo huyo amefungua mabao mawili na kuasisti mawili.

Ukiweka kando namba za kufunga, pia kiungo huyo ametengeneza nafasi 16 hatua ya makundi na kuonekana asipofunga, ana uwezo wa kuwatengenezea wengine na kumaliza kazi. Hata hivyo, kati ya nafasi hizo, 14 hazikutumiwa vizuri na wachezaji wa Simba huku mbili pekee ndizo zilibadilishwa na kuwa mabao.

Pia upambanaji wa Kibu Denis, unaweza kuwa hatari zaidi kwa AL Masry kwani naye anafatuatia kwa mchango mkubwa wa mabao ambapo yeye ndiye kinara wao wa kufunga akiwa na mabao matatu.

Leonel Ateba naye ana mabao mawili na asisti moja, hivyo ana mchango wa mabao matatu.

Simba iliyofunga mabao manane na kuruhusu manne hatua ya makundi, inaonekana safu yake ya ushambuliaji nyota wake wana uwezo mkubwa wa kuamua matokeo kutokana na mchango wao huo wa mabao.

Hata hivyo, eneo lao la ulinzi pia lipo imara ingawa wamepata pigo kwa kumkosa Che Fondoh Malone ambaye atakosekana mechi zote mbili, hii inayochezwa Jumatano na ile ya marudiano Aprili 9.

Che Malone ni majeruhi, lakini tumaini limerejea baada ya taarifa za kuwa fiti kwa kipa namba moja wa kikosi hicho, Moussa Camara ambaye amefanya mazoezi na wenzake akitarajiwa kukaa langoni katika mechi hii.

Kwa upande wa Al Masry, mshambuliaji wao raia wa Tunisia, Fakhreddine Ben Youssef ndiye ni kama silaha yao muhimu kutokana na kufunga mabao matatu kati ya saba waliyofunga hatua ya makundi walipocheza mechi sita.

Katika eneo lao la kiungo, Al Masry ipo salama chini ya Khaled El Ghandour atakayekuwa na kazi kubwa zaidi ya kutegeneza nafasi za kufunga kwa washambuliaji wao hasa Ben Youssef.