Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Jaja kachota dola kaishia, sasa zamu ya Emerson

Muktasari:

Imekuwa na ushabiki fulani wa ndani na nje ya uwanja ambao kwa mchezaji mjanja na anayejua anachokifanya kuwa tajiri ni kitu rahisi. Angalia mtu kama Emmanuel Okwi ndani ya kipindi kisichozidi miaka mitano ameshapiga zaidi ya Milioni 250 kwenye klabu za Simba na Yanga.

KATIKA Ligi za Afrika Mashariki, hii ya Tanzania inaonekana kulipa zaidi kwa takribani miaka mitano mfululizo sasa. Ni ligi ambayo mchezaji wa Kenya, Rwanda, Burundi na Uganda anapenda kucheza.

Imekuwa na ushabiki fulani wa ndani na nje ya uwanja ambao kwa mchezaji mjanja na anayejua anachokifanya kuwa tajiri ni kitu rahisi. Angalia mtu kama Emmanuel Okwi ndani ya kipindi kisichozidi miaka mitano ameshapiga zaidi ya Milioni 250 kwenye klabu za Simba na Yanga.

Hizo ni zile fedha halali alizopata kwenye usajili achana na hizi anazopewa na mashabiki huku mtaani pamoja na zawadi za hapa na pale. Sisi tuna hamasa kubwa lakini bado tuna matatizo makubwa kwenye uendeshaji na ndio maana wageni wameona hapa ndio sehemu ya kuponea.

Wameshaona hatuna uelekeo na tunataka mambo ya haraka kwa mafanikio ya leo tu si kesho.

Na mifumo ya klabu zetu wanaijua na akili za viongozi na mashabiki wanazijua, kwahiyo wanachofanya wakija ni kucheza na akili za viongozi ambao wanafanya kazi kishabiki halafu wanahamia kwa mashabiki.

Yanga imemuajiri Kocha Mbrazil, Marcio Maximo akaja na msaidizi wake Mbrazil na wachezaji wawili Wabrazil ambao ni straika Geilson Santos ‘Jaja’ na Andrey Coutinho anacheza kama kiungo.

Wakati dirisha dogo linaanza Maximo akatangaza kumchomoa Jaja huku akimlinda kwa visingizio mbalimbali, nafasi yake ameiziba kwa kumleta Mbrazil mwingine Emerson Rouqe, yeye ni kiungo.

Kama alivyomnadi Jaja, Maximo ameishawishi Yanga kwamba Emerson ni suluhisho kwenye kiungo na viongozi wameridhia muda wowote atapewa dola zake asaini mkataba. Inabidi kumuamini Maximo hivyohivyo kwavile hakuna kiongozi mwenye uwezo wa kiufundi wa kusoma uwezo wa mchezaji na kuelewa kiundani.

Hapa ndipo umuhimu wa Mkurugenzi wa Ufundi wa klabu unapokuja. Kama Yanga ilikuwa na Mkurugenzi wa Ufundi ndiye angeweza kujadiliana na Maximo na kumkosoa kitaalamu kuhusu hali halisi na aina ya wachezaji wanaoweza kuisaidia Yanga kwa wakati huu kwenye ligi na Kombe la Shirikisho kwa kuzingatia gharama na mwenendo wa uchumi wa klabu.

Mkurugenzi wa ufundi angeshaangalia ligi za Afrika Mashariki na kumwambia kwamba kuliko kutumia Milioni 50 kununua kiungo wa Brazil, timu ingesajili kijana mdogo hapo Uganda au Kenya kwa milioni 20 na angekuwa na manufaa zaidi. Hata Yanga wakija kujua kwamba Emerson ni kama Jaja tayari watakuwa wameshampa mkataba mpaka mwisho wa msimu atakula chake na msimu utaisha Mei ataondoka.

Hata Simba haina Mkurugenzi wa Ufundi mambo yanaenda kwa mazoea vilevile, umefika wakati kwa klabu zetu kubadilika na kujiweka kwenye misingi ya soka ambayo itaendana na ukongwe wake. Kuwa na Mkurugenzi wa ufundi kutasaidia klabu kuwa na mifumo inayoeleweka ndani na nje ya uwanja, kutapunguza gharama na vilevile anaweza kufanya kazi kama kocha endapo kocha mkuu hatakuwepo au akiacha kazi.

Huu mfumo wa kusajili hovyohovyo kwa kuangalia majina na kurundika mafungu ya noti mezani usingekuwepo kama klabu ingekuwa na mkurugenzi wa ufundi, mambo yanavyofanyika kwa sasa ni kishabiki zaidi na si profeshno. Kwa hali hiyo watu kama kina Emerson watakuja wengi tu, watakula fedha na kuondoka zao.