Imefichuka… Kaze aanika ishu yake na Simba #1
KOCHA wa Yanga, Cedrick Kaze amefanya mahojiano maalumu na Mwanaspoti nyumbani kwake Jijini Dar es Salaam na kufunguka mambo mengi mazito ikiwemo ishu yake ya kutakiwa na Simba.
Ameweka wazi ishu hiyo ilivyokuwa na jinsi walivyokuwa wanamsaka kwa kitita kikubwa, na masharti aliyowapa mpaka akageuza gari na kutua Jangwani, Oktoba mwaka jana, kuchukua nafasi ya Luc Eymael.
Kocha Kaze ambaye ni raia wa Burundi anaeleza kuwa: “Niliwahi kuwa na mazungumzo na Simba kwa vipindi tofauti, kwanza ilikuwa ni mwaka 2015 nilikuja Tanzania na kuongea na uongozi ambao walitaka niwe kocha msaidizi wa Dylan Kerr.”
“Nilikataa ofa yao niliwaambia sitaweza kwa kuwa sikutaka kuwa kocha msaidizi, kwani nilipokuja nikaangalia mazingira na muundo wa timu niliona kwa nafasi ya kocha msaidizi sitaweza kuisaidia timu kwa namna nilivyotaka, ndipo wakamleta Jackson Mayanja,” anasema Kaze ambaye ameiongoza Yanga bila kupoteza mchezo.
Anasema mwaka 2017 wakati walipomfukuza Patrick Aussems kulikuwa na mazungumzo mengine baina yake na Simba, lakini hayakufikia hatua za mwisho.
“Hicho ndicho kipindi mimi na klabu ya Simba tulizungumza, tofauti na hapo hakukuwa na mazungumzo mengine yoyote. Walikuwa wananitaka sana,” anasema kocha huyo na kuongeza kuwa tangu atue Yanga hakuwahi kufuatwa wala kufanya nao mazungumzo kwa namna yoyote ile wala hafikirii.
Kaze anasema kwamba awali mwaka jana alizungumza na Yanga na baadaye akawaomba wampe muda, lakini wakabadili mawazo na kwenda kwa kocha mwingine ila hakuamini kama wangemrudia tena.
“Wakati ule ilikuwa ndio ligi imeanza na wameajiri kocha mpya, hivyo niliona mimi na Yanga tena basi,” anaeleza kocha huyo katika mahojiano haya.
“Nilikuwa na matatizo ya familia, siku ambayo nilitakiwa kuja nikawaomba Yanga, lakini wakati huo walionekana kuwa na uhitaji wa haraka wa kocha, hivyo wakaajiri kocha mwingine na mimi nikaendelea na mipango mingine.”
“Baada ya miezi kadhaa Yanga walikuja tena, kipindi hicho Covid 19 ilikuwa imepamba moto, ligi zimesimama hivyo nilikuwa nafundisha tu akademi yangu kule,” anasema akiwa anapanga mipango mingine, Yanga walimfuata tena wakionyesha nia ya kumuajiri.
“Nikasema kama mwanzo haikuwezekana wacha nifanye kitu kinawezekana nijiunge na klabu hii, mazungumzo yetu yalifanyika haraka na ndani ya siku mbili tatu yakawa yamekamilika na nikabeba mizigo kuja Tanzania,” anasimulia kocha huyo mwenye malengo makubwa Jangwani msimu huu.
NDANI YA YANGA
Kaze tangu ametua Yanga amefanya usajili wa nyota watatu ambao ni Saido Ntibanzonkiza, Fiston Abdul Razak na Dickson Job.
“Nilipofika kitu cha kwanza ilikuwa ni kuboresha timu, kuongeza chalenji na niliona kuna haja ya kuongeza wachezaji katika ushambuliaji.
“Wakati huo tulikuwa na Michael Sarpong, Wazir Junior na Yacouba Sogne ambaye aliletwa kama mshambuliaji wa kati, timu ilipofanya tathmini ya wachezaji nikamuona ni mzuri zaidi akitokea pembeni,” anasema Kaze na kuongeza kuwa aliona kuna shida katika nafasi ya namba 10 ndiyo maana akaamua kufanya usajili .
“Nilitaka mtu mwenye mwendelezo mzuri kwenye utendaji hapo walikuwepo waliokuwa wakicheza, lakini nilitaka ambaye atatupa matokeo mazuri kila siku katika nafasi hiyo, nilitaka wachezaji wenyewe kwa wenyewe wapatiane chalenji.
“Kabla ya kufanya usajili, namba 10 ilibadilishwa sana watu kuna wakati alicheza Haruna (Niyonzima), Faridi (Mussa), Kaseke (Deus na Carlinhos)
“Hivyo mtaona ni namna gani nafasi hii ilikuwa ina shida ya kuwa na mtu sahihi, watu wanne niliwajaribu bila mafanikio, Carlinhos kwangu sikumuona kama anafaa katika hiyo nafasi,” anasema.
Anasema Carlinhos ni mzuri akitokea pembeni kama ilivyo kwa Farid Mussa, hivyo alitaka kuongeza nguvu ndiyo chanzo cha usajili wa Fiston.
“Dickson Job ni plani yetu ya muda mrefu, ni mchezaji mzuri ambaye amepitia timu ya taifa katika levo zote, ana kipaji na mipango ya klabu yetu ni kuangalia mahitaji ya timu ya sasa na baadaye, hivyo kwa Job tunaangalia mahitaji ya kesho,” anasema.
SIKU YA KWANZA
Kaze ambaye amesaini mkataba wa miaka miwili tangu Oktoba, mwaka jana, anasema siku ya kwanza alipoanza kibarua chake ndani ya klabu hiyo, aligundua kuna vitu wachezaji wanakosa kimojawapo ni kufanya vizuri kwa muda mrefu mfululizo. “Nilibaini si kwa wachezaji wa Yanga pekee, bali ni utamaduni wa soka la Tanzania mchezaji anaweza kupafomu vizuri watu wakamsifia, kesho akashuka anakuwa anabadilika badilika, leo anacheza vizuri, kesho anapotea.”
Anasema Yanga ni timu kubwa na alichokuwa akitaka ni ufanisi wa hali ya juu na sio kuwa na mtazamo wa kufunga kila siku kwani matokeo ni kitu kingine na ufanisi ni kitu kingine.
“Kwa mchezaji kuna siku kweli unaweza kuamka vibaya, hauko sawa ukacheza chini ya kiwango hiyo inatokea, lakini sio leo unakuwa na kiwango, kesho kimeshuka, haujulikani uko kundi gani.
“Mimi naangalia bidii ya kila siku ya mchezaji mazoezini, ukiamka vibaya siku hiyo ukakosa kontroo ni kitu kingine ila nataka nione juhudi, mwendelezo na kuwa siriazi kwa kila wakati hicho ndicho kikubwa nilikitaka siku yangu ya kwanza tu Yanga.”
Anasema katika kikosi chake kila mchezaji ana nafasi na hata Carlinhos ambaye amekuwa benchi muda mrefu.
“Ni kwa vile tu anaumwa, lakini ameanza kuimarika na anarudi katika hali yake ya kawaida hivyo natarajia kwenye mechi yetu ijayo ya FA nitaanza kumtumia na bila shaka ataonyesha kile ambacho watu wanakitarajia, ni mchezaji mzuri, ana tekniki, anajituma na anaelewa,” anasema.
PRESHA MECHI YA WATANI
Kaze ambaye anakiri timu kama za Gwambina, Ihefu, Prison na Azam zina wachezaji wazuri, lakini anaikumbuka mechi yake ya kwanza na Simba tangu alipoajiriwa kuwanoa mabingwa hao wa kihistoria.
“Ilinithibitishia ni mechi spesho kwa kila upande kuanzia kwenye menejimenti, wachezaji, mashabiki na hata vyombo vya habari.
“Ila tunachopaswa kutambua kwenye ligi, mechi hiyo ina pointi tatu kama zilivyo tu mechi nyingine, ni kama ukicheza na Ihefu, Gwambina, Azam na nyinginezo.”
Anasema kwake japo presha ilikuwa kubwa, lakini alichoangalia ni kujiandaa kwa pointi tatu na baada ya hiyo mechi kuangalia mechi zinazofuata.
“Kabla ya mechi niliwambia neno moja tu wachezaji, hii ni mechi yenye matamanio makubwa kwa mashabiki, nilitoa picha ya mechi kama hiyo iliyopita, nikawaeleza umuhimu wa kushinda hiyo mechi, kutuliza akili na wakacheze mpira,” anasema.
Anasema hamasa ya mashabiki wa timu hizo mbili pia ilimfanya ajifunze kitu, hasa walipoifunga Simba na kutwaa ubingwa wa kombe la Mapinduzi hivi karibuni.
“Tuliposhuka kwenye boti wakati tunarudi kuna mashabiki tena wa rika na jinsia zote walionyesha furaha yao dhahiri, wengine walikuwa wakilikimbiza basi la wachezaji hadi klabuni huku wakishangilia, hii inaonyesha ni vipi mashabiki wa Yanga wanaipenda timu yao.”
“Ukiwa kocha unakwenda kwenye timu mpya, ukifika siku ya kwanza kikubwa ni kuangalia wachezaji wanachoweza,” anasimulia Kaze.
Anasema mbali na kutaka wachezaji kujituma uwanjani, alipotua Yanga alianza kwa kufanya tathimini kumuangalia mmoja mmoja, kisha akafanya kwa timu yote.
“Niliangalia video baadhi za timu za nyuma na nikawa naichunguza katika mechi tatu tangu nimefika, nikachukua muda mfupi kuzoea mazingira ya timu, kujua timu zingine zikoje na yote hayo niliyafanya ndani ya muda mfupi sana na kikubwa niliwakuta wachezaji wote waliosajiliwa Yanga wana viwango bora na wanafundishika.”
Anasema kwake hiyo ilikuwa ni faraja kwenye kibarua chake kwani makocha wakati mwingine wanakutana na changamoto ya wachezaji hawafundishiki, lakini aliowakuta Yanga wana misingi ya mpira wana uzoefu na imemsaidia kuwa timu yenye muunganiko wa haraka.
Anasema pamoja na kwamba Yanga haijapoteza mechi tangu alipoanza kunolewa na Kaze, kwake kikubwa ni nafasi watakayokuwa baada ya msimu kumalizika. “Unaweza kucheza na kumaliza Ligi bila kupoteza mechi lakini usipate unachokitarajia na ukafungwa na ukapata kile ulichokitarajia, kikubwa kwangu ni kuangalia msimamo wakati Ligi inakwisha tumepata nini, perfomance yetu ilikuwaje?.
Anasema mechi 16 walizobakisha ili kumaliza msimu ni nyingi na wakishinda zote wanapointi 48 ambazo ni pointi nyingi sana na kila timu ina uwezo wa kukaa kileleni kwenye msimamo.
“Kuna timu kama Simba tunachuana nayo sana kwenye ubingwa, lakini sio hiyo pekee kuna Azam, Biashara hazitajwi lakini haziko mbali, hivyo inahitajika muendelezo wa kufanya makubwa zaidi mzunguko wa pili na kujitofautisha na washindani wetu.
“Ila kwa sasa hakuna timu inayoweza kuzungumzia ubingwa, bado ni mapema mno na hakuna mwenye uhakika nao, ninachokitaka Yanga ni kuangalie mechi hizo na kuzipa uzito kwa kujiandaa vizuri na kucheza kwa kiwango bora ili kupata pointi ambazo mwisho zitatupeleka kwenye msimamo,” anasema Kaze.
Unajua amefunguka nini kikubwa kingine? Fuatilia mfululizo wa makala hii kesho...Kwa maonituma meseji kwa namba 0658-376417
Imeandikwa na IMANI MAKONGORO, MWANAHIBA RICHARD NA THOMAS NG’ITU