Kaze: Simba hii mbona inatoboa

WAKATI msafara wa wachezaji wa Simba ukitarajiwa kuondoka Jumatatu kwenda DR Congo, huku mabosi wa klabu wakitanguliza wenzao wawili ili kuweka mambo sawa kwa ajili ya mchezo wao wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika, Kocha Cedric Kaze wa Yanga amefunguka akidai watani zao watatoboa.
Simba itatupa karata yake ya kwanza Februari 12 dhidi ya wenyeji wao AS Vita kabla ya kuikaribisha Al Ahly nyumbani baadaye ikisaka nafasi ya kutinga robo fainali ya michuano hiyo kutoka kundi A lenye pia timu ya Al Merreikh ya Sudan.
Makamu Mwenyekiti wa Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ ameliambia Mwanaspoti kuwa timu hiyo itaondoka na wachezaji wote kuelekea DRC ambako tayari wametanguliza ‘mashushushu’ kwa ajili ya kuweka mambo sawa ikiwamo mapokezi ya timu hiyo mara itakapowasili nchini humo.
Try Again ambaye pia ni mmoja wa wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa klabu hiyo, alisema timu yao itaondoka na wachezaji karibu wote kutokana na changamoto ya janga la corona.
“Tunafanya hivi kwa tahadhari maana unaweza kufika kule ikagundulika mmoja kati yao ana corona akawekwa karantini, hivyo kwa tahadhari wachezaji watakaosafiri Februari 8 watakuwa ni wengi zaidi,” alisema Try Again na kuongeza kuwa kutokana na uzito na ukubwa wa mechi hiyo, tayari wametuma watu kuweka mazingira sawa nchini humo ikiwamo hoteli ambayo timu itafikia, uwanja wa mazoezi na taratibu nyingine.
“Siwezi kuwataja watu hao kwa kuwa tuko kwenye mapambano, hiyo itabaki kuwa siri ya klabu, lakini maandalizi ya mechi hiyo yameanza na yanaendelea,” alisema.
KAZE AIPA MCHONGO
Wakati Simba ikijipanga hivyo, Kocha Mkuu wa Yanga, Kaze amesema anaipa nafasi kubwa timu hiyo kufuzu robo fainali kama wachezaji wataamua kwenye mechi za makundi.

“Simba ina wachezaji wazuri, wenye uzoefu wa kutosha na wanajua nini wanafanya uwanjani, kama wataamua kupambana naamini watafika mbali kwenye mashindano ya kimataifa,” alisema Kaze juzi katika mahojiano maalumu na gazeti hili.
Alisema wanachotakiwa kufanya ni kujituma na kupambana kwa ajili ya kutafuta matokeo na si vinginevyo.
“Bahati nzuri kipindi kirefu cha corona nchini Tanzania walikuwa na bahati ya ligi yao kuendelea, hilo ni jambo ambalo limeendelea kuwaimarisha wachezaji wa Simba katika safari yao ya kimataifa,” alisema kocha huyo. Alisema mashabiki na Watanzania wanapaswa kuisapoti timu yao katika hatua hiyo, ingawa wenye nafasi ya kuamua matokeo ni wachezaji wenyewe kujituma.
Msome zaidi Kaze katika mfululizo wa makala zake kuanzia kesho Jumamosi. Usikose.