IDDI PIALALI: Pambano na mfaume lilikuwa na maajabu

Muktasari:
- Pialali siyo jina geni kwa wadau wa ngumi anakumbukwa kwa upinzani wake wa jadi ambao hadi sasa hajapatiwa dawa dhidi ya Mfaume Mfaume wa Mabibo, Dar es Salaam.
KAWAIDA maisha ya mwanadamu yamekuwa ya kuhangaika katika kupata mkate wa kila siku kama ilivyokuwa kwa bondia Idd Pialali ambaye ni maarufu sana mitaa ya Manzese, Dar es Salaam.
Pialali siyo jina geni kwa wadau wa ngumi anakumbukwa kwa upinzani wake wa jadi ambao hadi sasa hajapatiwa dawa dhidi ya Mfaume Mfaume wa Mabibo, Dar es Salaam.
Bondia huyo mwenye rekodi ya kucheza jumla ya mapambano 49, sawa na raundi 240, ameshinda mapambano 36, 25 kwa knockout, amepigwa mara 10, saba kwa knockout na sare mara saba.
Pialali anakamata nafasi ya pili nchini katika mabondia 56 wa uzani wa Walter, huku duniani akiwa wa 273 kati ya mabondia 2378 na ana uwezo wa kushinda kwa knockout kwa asilimia 69.44.
Pialali anaeleza sababu kubwa ya yeye kushindwa kuonekana mara kwa mara ulingoni ni imetokana na menejimenti yake kukosa watu sahihi wa kumwongoza na kuhakikisha jina lake linakuwa juu wakati wote.
“Binafsi siyo kqama sipigani, maana karibu kila wakati nimekuwa nikipigana, lakini siyo rahisi kwenda juu kwa sababu sina watu wa kunisukuma katika mambo ambayo mabondia wengi tayari wamekuwa wakifanya na wanafanikiwa.
“Siyo kwamba sina menejimenti, nataka hapa ieleweke vizuri, isipokuwa changamoto ni wao kutambua mambo makubwa ya kufanya wakati huu dunia imepiga hatua katika eneo la teknolojia.
Nje ya ngumi unafanya kazi gani?
“Zamani nilikuwa dereva wa magari ya mizigo pale Mabibo Sokoni, lakini kwa sasa menejementi yangu inayoongozwa na Salum Msangi ‘Jomba Salum’ imekuwa ikiritibu mambo yangu yote ya msingi, hivyo sifanyi tena kazi ya udereva.
“Sasa hivi ninachokifanya ni mazoezi pekee na kuangalia familia, lakini napigana na nani, familia yangu inakula nini au natakiwa kupigana na nani, hilo limebaki kuwa jukumu la menejimenti yangu ambayo ndiyo huyo mjomba Salum na kocha wangu, Edward Lyakwipa.
Pambano lako na Mfaume mara ya kwanza lilivunjika, mkasaini kurudiana lakini kimya hadi leo?
“Nataka nikuambie kabisa, sifikiri kwa sasa kupigana tena na Mfaume Mfaume, naangalia mambo mengine maana yeye sio mtu ambaye anaweza au anataka tupigane zaidi ya kupiga kelele za mitandao.
“Mfaume hana uwezo wa kupigana na mimi, anachofanya kataka Kiki kwa sababu amekuwa akikwepa mara kwa mara kupigana, ndiyo maana nakuambia hayupo kwenye mipango yangu ya kupigana.
“Kitu kingine ambacho watu wengi hawajui, viongozi wake wa Naccoz wamekuwa wakinishawishi nijiunge nao kwa sababu wenyewe hawana tena bondia mwenye mvuto na ambaye sio muoga, wameniambia nihamie kwao Mabibo, wakati naishi Manzese, ila niliwakatalia kwa sababu niliwaambia labda wanichukue na kocha wangu kitu ambacho hawawezi.
Kumekuwa na malalamiko ya mabondia wengi kudhulumiwa stahiki zao vipi wewe ushawahi kukutana nayo?
“Binafsi sijawahi kudhulumiwa kwa njia hiyo lakini nimepoteza siyo chini ya milioni 18 ambazo promote wa Namibia alinidhulumu.
“Nilienda kupigana kule pambano la ubingwa na mabondia wa kwao, ilikuwa mwaka huu lakini kwa bahati mbaya sikulipwa pesa yangu ambayo ilikuwa ndiyo hiyo milioni 18, niliumia lakini sikuwa na jinsi ya kufanya.
“Lakini kwa hapa ndani au mawakala wa ndani wakitupeleka nje, binafsi haijawahi kunitokea zaidi mwaka 2016 katika pambano langu na Twaha Kiduku ambalo nilimpiga nililipwa Sh300,000 na promota Kaike Siraju badala ya milioni mbili.
“Nakumbuka awali tulikubaliana kiasi cha shilingi milioni mbili lakini likatokea tatizo kwa Francis Cheka kukataa kupigana na Dullah Mbabe, promota akadai hakupata pesa ikabidi nichukue sikuwa na cha kufanya.
Ngumi zimekunufaisha kiasi gani?
“Ukweli namshukuru Mungu zimenisaidia sana bado sijajipata lakini leo hii naishi nyumbani kwangu na familia yangu, nimejenga nyumba hii kwa jasho langu la ndani ya ulingo.
“Mwenyewe unaona kabisa bado sijamaliza lakini hadi hapa nilipofikia sina hekaheka za kulipa kodi na familia yangu katika nyumba za kupanga.
“Mwalimu wangu na meneja wangu wamefanya kazi kubwa bila ya wao kunisimamia pengine nisingepata hii nyumba ambayo leo hii nakaa na familia yangu.
“Lakini ukiondoa hii nyumba, nimejenga fremu mbili za biashara mmoja ipo kule Kimara barabarani na nyengine ipo nje ya hii nyumba ambayo tunaishi, napambana kuweka biashara kwa sasa.
Ujenzi mpaka sasa umegharimu kiasi gani?
“Wakati mwengine wanasema uongo, lakini ujenzi wa nyumba hii hadi ulipofikia nimetumia milioni 90 ambayo imetokana na ngumi, nashukuru tu naishi kwangu hata wakidai ni mbali ila nipo kwangu.
Kumekuwa na malalamiko ya ushirikina wewe ushawahi kukutana nayo?
“Unajua atakayekuambia ushirikina hakuna huyo muongo kwa sababu hata kwenye dini hayo mambo yametajwa na nimekutana nayo sana kwenye ngumi.
“Nakumbuka wakati pambano langu na Mfaume Mfaume mwaka 2022 linakaribia tena bado naishi Manzese, katika dirisha langu nilimkuta bundi amekufa na baada ya siku mbili akafa paka katika eneo hilo.
“Sasa jambo la kujiuliza ni hapa Dar bundi anatokea wapi, lakini hata siku ya pambano lilivunjika kiajabu kwa sababu nilipigwa kichwa upande wa kulia tena kwenye upande wa shavu lakini nikachanika juu ya jicho kulia, ukifuatilia hayo unaona kabisa yalikuwa ni mambo ya kishirikina.
Huwa unakula chakula kiasi gani?
“Ulaji wangu wakati sina pambano mara nyingi huwa ni kawaida kabisa, naweza kula nusu au hata robo ya ugali lakini huwa inategemea naenda kucheza pambano la aina gani, kama natakiwa nipunguze kilo basi huwa sina muda wa kula sana ila kama natakiwa kuongeza kawaida nafikisha hadi nusu kilo ya ugali na mboga kavu kama kuku wa kuchoma na mboga za majani,” anasema Pialali.