Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hussein Kazi beki aliyeandika rekodi ya kipekee 2025-2026

Muktasari:

  • Msimu uliomalizika wa 2025-2026, amekuwa mchezaji aliyecheza mechi zote za Ligi Kuu Bara ya NBC akiwa na kikosi cha Namungo bila ya kukosa hata dakika moja. Katika mechi 30, Kazi ametumika kwa dakika 2700, hakuna mchezaji mwingine aliyefanya hivyo.

BEKI wa kati wa Namungo FC, Hussein Kazi amekuwa sio mtu wa kukata tamaa na badala yake anatumia nyakati ngumu kama fursa ya kuonyesha upekee wa kufanya vitu vigumu vya kumtambulisha na kumpa heshima.

Msimu uliomalizika wa 2025-2026, amekuwa mchezaji aliyecheza mechi zote za Ligi Kuu Bara ya NBC akiwa na kikosi cha Namungo bila ya kukosa hata dakika moja. Katika mechi 30, Kazi ametumika kwa dakika 2700, hakuna mchezaji mwingine aliyefanya hivyo.

Katika mahojiano yake na Mwanaspoti, Kazi anasema haijawahi kutokea kucheza mechi zote za msimu katika kila mchezo dakika 90, jambo analoliona kwake limekuwa la mafanikio.

"Kwangu ni kitu kikubwa kwa benchi la ufundi kuamini katika huduma yangu, baada ya kuona wananiamini niliongeza bidii na kuzidisha nidhamu ya hali ya juu," anasema na kuongeza;

"Vya msingi nilivyovifanya nilipunguza baadhi ya vitu ili kuupa mwili nguvu za kuitumikia timu, mfano badala ya kulala saa 6 au 7 usiku basi nilikuwa nalala saa 3 usiku," anasema na kuongeza;

"Ujue kama kijana kuna mambo ya kuchati na kupitapita mitandao, vyote hivyo nilivipunguza baada ya kugundua natakiwa kuisaidia timu, nimejifunza kurekebisha makosa na kuwa bora zaidi kwani kila mechi ilikuwa funzo kwangu."


FUNZO ALILOPATA

Kazi alikuwa hana nafasi kubwa ya kucheza katika kipindi cha misimu miwili aliyokuwa Simba, lakini 2025-2026 alipotua Namungo, amekuwa beki tegemeo la benchi la ufundi chini ya Juma Mgunda.

Beki huyo anafichua kitu kilichomsaidia wakati anakalia benchi Simba hadi sasa kutegemewa Namungo ni bidii aliyonayo na si kukata tamaa.

"Kwanza ukicheza timu kongwe na zenye utajiri wa mashabiki inahitajika akili kubwa kwa mchezaji kusimama katika majukumu yake.

"Mtazamo huo ulinibeba kwani nilijua kukosa nafasi ya kucheza Simba siyo mwisho wa kipaji changu, bali niliamini kupata timu ambayo nitapata nafasi ya kucheza, ndiyo maana nilipofika Namungo niliweka mbali ustaa nikaamua kufanya kazi," anasema Kazi huku akikumbuka aliyekuwa kocha wa Simba, Abdelhak Benchikha aliwahi kumwambia yeye ni beki mwenye kipaji, hivyo ili kionekane kwa ukubwa inabidi aonyeshe bidii na kutokukata tamaa.

Kazi alijiunga na Simba msimu wa 2023-2024 akitokea Geita Gold na msimu wa kwanza alipata zaidi nafasi ya kucheza Kombe la Mapinduzi chini ya Kocha Benchikha baada ya kuwa na nafasi finyu katika mechi za Ligi Kuu.

"Benchikha alikuwa anaamni katika vijana, alitaka kila mtu aonyeshe uwezo wake Kombe la Mapinduzi,  hilo lilinipa faraja kubwa ya kuendelea kupambana," anasema.

Lakini msimu wake wa mwisho Simba 2024-2025 alicheza mechi moja dakika 10 dhidi ya KMC, timu ilikuwa chini ya kocha Fadlu Davids. Wakati yeye akiwa nje, Abdulrazack Hamza na Che Malone Fondoh ndio waliokuwa wakicheza eneo la beki wa kati.

"Msimu wa kwanza ambaye alikuwa anacheza zaidi alikuwa ni Henock Inonga na Che Malone pamoja na Juma Kennedy, licha ya kwamba nilikuwa sichezi lakini niliendelea kufanya bidii na kujifunza na matunda yake yameonekana Namungo," anasema.


MABEKI ANAOWAKUBALI

Kazi anasema pamoja na ushindani wa namba alioupata Simba, Hamza ni kati ya mabeki anaowakubali, wengine ni Dickson Job, Ibrahim Bacca na Bakari Mwanyeto.

ALICHOVUNA SIMBA

Kazi anasema japokuwa alijenga kabla ya kujiunga na klabu ya Simba, kiuchumi akiwa na Wanamsimbazi hao kuna hatua alizipiga, ikiwemo kuwasaidia ndugu, jamaa na marafiki zake.

"Pia wakati nipo Simba nilijifunza kutumia mitandao kwa faida, kwani nimewahi kushuhudia marafiki zangu wakipata dili ya timu za nje kupitia mitandaoni, binafsi nimekutana na watu tofauti, hata wale waliokuwa wananiponda walinipa  nguvu ya kujituma.


MWAKA 2010 ULIKUWA MGUMU

Anasema wakati anacheza timu ya Makumbusho FC, alihama nyumbani kwa wazazi wake Goba jijini Dar es Salaam na kwenda kuishi na bibi mzaa mama yake aitwaye Khadija aliyekuwa anaishi Manzese.

"Bibi alikuwa hana uwezo, hivyo kwenda uwanjani bila kula ilikuwa jambo la kawaida, wakati mwingine kocha aliniona kama mvivu na mtu anayechoka sana kumbe ilikuwa njaa, kipindi hicho kilinikomaza kupambana," anasema na kuongeza;

"Kabla ya mwaka 2010 nilikuwa nasoma Shule ya Msingi Victoria, ilipakana na Makumbusho, wakati nakwenda kucheza na wanafunzi wa shule hiyo, mlinzi wa getini alikuwa anaitwa Baba Maki ndiye aliyegundua kipaji changu.

"Akaniita na kuniambia niweke nguvu kwenye soka nina kipaji kikubwa, akawa ananisaidia sana, nasikitika alifariki mapema kabla hajala matunda yangu," anasema.

Kazi ambaye mbali na kucheza beki wa kati pia anamudu namba 2, 6 na 7, aliwahi kufanya hivyo akiwa Polisi Tanzania, anasema: "Kila kocha anamtazama mchezaji anavyoweza kumtumia."

"Niliwahi kucheza Simba B mwaka 2015, kikosi cha wakubwa kilikuwa kimeweka kambi Zanzibar, sasa kuna beki aliumia, ndipo nikapandishwa ndege na kwenda kuziba pengo, kiukweli nilikuwa nahofia sana kupanda ndege na ndiyo ilikuwa mara ya kwanza," anasema.


WAKALA ALIVYOZIMA DILI LAKE

Wachezaji wamekuwa wakitamani kucheza soka nje ya nchi, inapotokea nafasi hiyo, huchangamkia. Hali hiyo ilimtokea Kazi lakini anasema alifelishwa na wakala wake.

Kazi anasema, kwanza safari yake kutoka Tanzania kwenda kufanya majaribio nchini DR Congo ilikuwa ya kuungaunga kwani alisafiri kwa gari ambayo ilikuwa ikitokea bandarini Dar es Salaam kwenda DR Congo.

Gari hilo lilikuwa linapelekwa kwa mteja aliyelinunua, hivyo akalazimika kuzungumza na dereva aliyekuwa akilipeleka baada ya kukosa pesa za usafiri wa ndege.

"Timu ambayo nilikwenda kufanya majaribio hayo ni St Lupopo, nilifuzu, changamoto ikaja kwa wakala wangu alikuwa hajaridhika na pesa aliyotakiwa apate yeye, ikabidi alikate dili hilo, niliumia sana kwani nilikuwa na hamu ya kucheza nje," anasema.