Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

HISIA ZANGU: Wamezaliwa mastaa wapya pale Goma, wakati utatuambia

Hisia Pict

Muktasari:

  • Mzee Mkapa aliupenda huu wimbo. Mungu amrehemu. Na kweli huwa napenda kuendesha gari langu nikizunguka hapa nchini. Tuna nchi nzuri. Inapendeza. Zaidi ya kila kitu imebarikiwa amani. Hatuna vita. Hatuna njaa.

WIMBO ambao Rais Benjamin Mkapa alikuwa anaupenda ni ule wa ‘Tazama ramani’. “Tazama ramani utaona nchi nzuri yenye mito na mabonde ya nafaka. Nasema kwa kinywa halafu kwa kufikiri. Nchi hiyo mashuhuri huitwa Tanzania.”

Mzee Mkapa aliupenda huu wimbo. Mungu amrehemu. Na kweli huwa napenda kuendesha gari langu nikizunguka hapa nchini. Tuna nchi nzuri. Inapendeza. Zaidi ya kila kitu imebarikiwa amani. Hatuna vita. Hatuna njaa.

Hatuombei vita na wala hatuombei njaa. Sio kitu kizuri. Lakini leo pale DR Congo kuna machafuko. Kupitia hayo machafuko mastaa mbalimbali wenye kiu mbalimbali wanazaliwa pale. Watoto wanahangaika wakiwa wameshikwa mikono na mama zao. Wengine wapo migongoni. Wengine historia zao zinaanzia hapo. Ukimbizi.

Kuna mastaa kibao kutoka DR Congo ambao wamejikuta nje ya nchi yao wakiwa watoto baada ya vita kama ya Goma. Kuna ambao wamejikuta wamezaliwa Ulaya na kwingineko baada ya vita kama hiyo ya Goma. Kina Vincent Kompany, Romelu Lukaku, Mitch Batshuayi, Christian Benteke na wengine wengi walijikuta wanazaliwa Ubelgiji baada ya mambo kama hayo. Kina Tresor Romana Lualua na wengineo wakajikuta wamezaliwa Uingereza.

HS 01

Wengine wamezaliwa Ufaransa. Wengine wamezaliwa Marekani. Wengine Canada. Wengine kwingineko. Wengine wametokea Burundi na wengine wametokea Rwanda wakati ule wa mauaji ya Kimbari. Vita haina faida yoyote, lakini inaleta kiu. Kwa wale watoto ambao wameiona vita hapo majuzi kule DR Congo wakipata nafasi ya kucheza mchezo wowote ambao utawaingizia kipato huwa hawachezei nafasi. Hawataki kurudi nyumbani. Wanataka kuyatoa maisha kupitia hapo. Wanapata hasira kali ya walichokishuhudia na inakuwa kama msukumo katika mioyo yao kutorudi nyuma tena.

Haishangazi kuona kuna mastaa wengi wakubwa wana asili ya DR Congo. Kwa DR Congo wala sio habari ngeni na hasa ukizingatia kwamba wanapokewa vizuri na mataifa yao koloni kama Ufaransa na Ubelgiji. Sisi tukisikia mchezaji mmoja mwenye asili ya Tanzania anayetamba Ulaya huwa inakuwa habari kubwa kweli kweli.

Na katika wachezaji wenye asili ya Kitanzania ambaye amecheza katika kiwango cha juu ni Yusuf Poulsen. Huyu anacheza RB Leipzig. Tazama namna ambavyo Watanzania waliisherekea habari yake kwa ukubwa mwingi hasa alipotua Tanga.

HS 02

Kwa DR Congo, Nigeria, Cameroon ni habari ya kawaida tu. Hakuna anayeifuatilia kwa shauku kubwa. Miaka mingi ijayo tutasikiliza historia za baadhi ya wachezaji mahiri wa DR Congo au asili ya huko na watakwambia kwamba walitokana na kukimbia vita ya Goma kati ya majeshi ya serikali na wale M23.

Ili mchezaji wa Tanzania afanikiwe anapaswa kujiingiza katika kiu sawa na yule ambaye ameiona vita. Anapaswa ajiweke katika kiu sawa na yule ambaye ameiona njaa. Anapaswa kujiweka katika kiu sawa na yule ambaye ameuona umaskini.

Sisi tuna mito, mabonde mazuri ya mpunga na hatuna vita (kitu ambacho ni jambo jema zaidi), tuna kila kitu. Zaidi ya yote tumeongozwa na sera ya Ujamaa na kujitegemea. Kiu inatoka wapi? Tanzania ndio mahala ambapo mtu anaweza kula milo mitatu kila siku na hana kazi. Tanzania ndio mahala ambapo mtu analeweshwa pombe kila siku na marafiki zake na hana kazi. Kiu inatoka wapi?

HS 03

Haishangazi kuona wachezaji wetu hawawezi kufuata hata nyayo za Mbwana Samatta na Simon Msuva. Wakitoka nje kidogo tu huwa wanarudi. Majuzi tumempokea Gadiel Michael ambaye alikuwa anafanya vizuri pale Afrika Kusini.

Unajiuliza kuhusu Abdulrazak Hamza. Kwa kiwango hiki anachoonyesha Simba alishindwa vipi kuendelea kubaki Afrika Kusini? Wachezaji wanaorudi ni wengi kuliko wanaotoka. Tena wanarudi katika timu za kawaida tu. Pamba Jiji, Coastal Union, Singida Black Stars.

Kwamba tuna maslahi mazuri? Ndio! Lakini kwa wenzetu ni njia zaidi ya kupata maslahi mazuri kuliko kwetu. Ndio maana unaposikia Baraka Majogoro anatakiwa na Orlando Pirates ni kwa sababu alipambana na Chippa United.

Tatizo la mchezaji wa Kitanzania anacheza soka la kulipwa Afrika Kusini, lakini mawazo yake yapo Tanzania. Kisa? Hana njaa. Kwao hakuna njaa. Zaidi ni kwamba kwao hakuna vita. Katika vita kama hii ya Goma ambayo mtoto ameona mauaji mbele ya macho yake, inakuwa vigumu kwake kufikiria kurudi nyumbani.

HS 04

Wengine wameuona umaskini katika macho yao. Umaskini uliotopea (poverty stricken). Sadio Mane aliamua kwenda Saudia kwa ajili ya kusaka noti za kwenda kubadilisha kwao. Huyu ameuona umaskini na ndio maana pesa zake anazipeleka katika kujenga misikiti, hospitali na shule pale kwao. Ameuona umaskini wa Bambali pale Senegal na ndio ulimpa msukumo wa kuwa kama alivyo.

Wakati mwingine huwa tunadanganyana kwamba vijana wa nchi za wenzetu wameandaliwa. Sio kweli. Umeona ambako Andre Onana na Mane walikoanzia? Ni viwanja vya vumbi vilivyopitiliza. Tofauti yao na sisi ni kiu tu. Tusifuate mifano ya nchi za Afrika ambazo zimeendelea kama Afrika Kusini pamoja na kule Afrika Kaskazini. Nchi zao zinajitosheleza kwa mambo mengi ndio maana hata mchezaji asipokwenda nje anaona sawa tu kwa sababu ana mshahara ambao wakati mwingine unalingana na baadhi ya wachezaji wa Ulaya.

Nawahakikishieni kwamba hii vita inayoendelea Goma tayari imeshazalisha vijana wagumu ambao hawatatazama nyuma. Siku moja tutawasikia tu wakielezea katika simulizi za maisha yao. Kwani tumewasikia wangapi?

Kama tunahitaji mfano walau mmoja tu, basi tunao. Kibu Denis. Si ametoka katika kambi za wakimbizi kuja kuchezea timu ya taifa? Kuna vijana wangapi pale Ilala wameridhika? Zile nguvu za Kibu hazijaja bure. Amejengwa hasira zile katika kambi ya wakimbizi.