HISIA ZANGU: Wakati wa kuipima akili ya Chama ndio sasa

WATANZANIA wameiweka majaribuni akili ya Clatous Chotta Chama. Kiungo wa zamani wa Simba ambaye ameacha jina kubwa nchini. Nchi ambayo inakugeuza kuwa Mfalme ambaye unajiona haustaili kwingine zaidi ya Tanzania. Mashabiki wa hapa wakikupenda wanakupenda kweli.

Kwa sasa jina la Chama linatajwa kila mahali hapa nchini. Anahusishwa kurudi klabu yake ya zamani Simba. Anahusishwa pia kwenda kwa wapinzani wa Simba, Yanga ambao wameanza kuhusishwa na Chama tangu akiwa nchini miaka miwili iliyopita. Yanga hawajawahi kuacha kumuandama Chama.

Nafikiria Chama anavyojisikia sasa. Nilikuwa Morocco wiki chache zilizopita. Jinsi Chama alivyokuwa anafurahia maisha ya Tanzania. Haiwezi kutokea vile Morocco kwa sasa. Ndani na nje ya uwanja. Haiwezi kutokea. Nje ya uwanja Tanzania kuna raha zake na hasa unapopendwa katika kiwango ambacho Chama alifikia.

Kila anapokwenda Chama ni Mfalme. Ataombwa kupigwa picha na mashabiki wa pande zote mbili. Atanunuliwa kinywaji na chakula na mashabiki wa pande zote mbili bila ya kujali itikadi zao. Chama ni mfalme nchi hii. Amechukua nafasi ya Emmanuel Okwi. Kuzungumziwa hata kama hayupo.

Ndani ya uwanja pia Chama ameacha ufalme wake. Nafasi yake ipo wazi kwa timu zote tatu kubwa nchini. Simba, Yanga na Azam. Na atakaporudi kuna nafasi kubwa akaendelea kuwa staa wa timu yoyote ambayo atakuwepo. Huu ndio ufalme aliouacha Chama nchini.

Ni kitu cha kawaida kwamba nafasi ya Chama ni ya kusuasua katika klabu yake ya sasa Berkane pale Morocco. Lile ni taifa ambalo lipo mbele kisoka. Lina uwezo mkubwa wa kuzalisha vijana wenye vipaji na lina uwezo mkubwa wa kununua wachezaji wa bei mbaya kama ambavyo Chama alinunuliwa.

Haishangazi kuona wakati mwingine tunamuona Chama akiwa benchi. Mara akiingia kipindi cha pili. Mara akitolewa nje. Hatujui wachezaji wanaocheza nafasi yake wana uwezo gani. Hatujui pia kama amepewa muda wa kuzoea mazingira kabla ya kupewa nafasi yake. Hatujasikia habari nyingi kutoka Morocco.

Vyovyote ilivyo hizi ndizo nyakati ambazo unapima tabia za mchezaji ndani na nje ya uwanja. Unapima kama mchezaji ana kiu ya mafanikio au hapana. Hizi ndizo nyakati ambazo wachezaji wetu wengi wa kizawa waliamua kurudi nchini pale walipofikiria ufalme waliouacha Tanzania.

Sio wachezaji wazawa tu, hata wachezaji wa kigeni waliowahi kuionja ladha ya ufalme Bongo mara nyingi walijikuta wakienda na kurudi. Tanzania ina raha yake. Waulize kina Okwi. Waulize kina Obrey Chirwa na wengineo. Walikwenda wakarudi. Kuna raha yake ndani na nje ya uwanja.

Kichwa cha Chama kwa sasa nadhani kipo katika hali hiyo. Anauhisi ufalme wake. Katika mtandao wake wa Instagram ana wafuasi zaidi ya laki tano. Asilimia 99 ya wafuasi hao ni Watanzania. Wote wanamsihi arudi nchini. Kuna wanaomsihi arudi Simba na kuna wale mashabiki wachokozi wa Yanga wanaomtaka akirudi abadilishe mtaa.

Vyovyote ilivyo Chama atajikuta anapata matamanio ya kurudi tena nchini bila ya kujalisha kiasi cha mshahara anaolipwa Morocco. Unaweza kuomba ulipwe pungufu kidogo ya kile ambacho ulikuwa unalipwa Morocco ili mradi uje kukumbana tena na starehe za ndani na nje ya uwanja hapa Tanzania.

Kufikia hapo usiiamini sana akili ya mchezaji wa ukanda huu wa SADC. Anaweza kuamua lolote. Kwa wachezaji wa Afrika Magharibi akili zao ni tofauti. Mnigeria akiondoka nyumbani hataki kurudi nyuma. Akiondoka mahali na kwenda katika timu yenye malisho mema zaidi basi hataki kurudi nyuma. Ni kitu tofauti na wachezaji wa ukanda wetu.

Ingekuwa ni mchezaji wa Nigeria au Cameroon ningesema uvumi wa Chama ni wa kijinga. Lakini kwa mchezaji wa Zambia, Tanzania, Malawi, Uganda, Kenya na maeneo mengine ya huku basi lolote linawezekana. Unaweza kusikia Chama amerudi Simba au Yanga.

Na kama hauamini hilo jiulize ilikuwaje na kipaji kama kile Chama akajikuta katika nchi ya Tanzania? Lazima kuna maeneo yalimchosha na hakutaka kuendelea kuwepo huko hata kama kwa kuendelea kuwepo kungemfungulia njia. Hatujui hasa ilikuwajekuwaje akaishia Afrika Mashariki.

Lakini hapo hapo tujiulize, ilikuwaje Okwi akarudi nchini mara mbili wakati akiwa katika ubora wake? Mara moja alirudi Simba na mara nyingine alirudi Yanga. Tuliamini kwamba angefika mbali kuliko Mbwana Samatta kutokana na maajabu aliyokuwa anatuonyesha.

Na hiki ni kipindi cha kupima akili ya Chama. Ana kiu kiasi gani katika kupata mafanikio? Ana njaa kiasi gani? Ataweza kukaza na kubakia Morocco ili afungue njia zaidi katika maisha yake ya soka? Ataweza kufuata njia za Simon Msuva ambaye alikaza zaidi kutoka Diffaa Jadida na kutua Waydad Casablanca ambayo ni klabu kubwa zaidi?

Katika kambi ya timu ya taifa ya Zambia huwa tunamuona Chama akiweka mitandaoni picha zake na za staa wa Zambia anayecheza Leicester City, Patson Daka. Nadhanj huwa wanachangia chumba kimoja wakiwa katika kambi ya Chipolopolo.

Siamini kama Chama hana wivu na mafanikio ya Daka. Hata kama umri wa Chama unesogea. Angependa kuwepo katika sehemu ambayo inampa heshima zaidi Zambia kama ilivyo kwa Daka. Hata kama sio England lakini angependa kuwa mahali panapompa heshima zaidi.

Sina uhakika kama Tanzania inampa heshima nzuri zaidi ingawa nafahamu kwamba Simba kama timu imempa heshima nzuri baada ya kufika robo fainali za michuano ya Afrika. Wakati mwingine tunaweza kutofautisha kati ya Simba na Taifa letu.

Ni wakati wa kuipima akili ya Chama kwa sasa. Akirudi pia atawavunja moyo vijana wengi wa Kitanzania ambao walikuwa wanaamini kwamba kiwango cha Chama kilikuwa hakiwezi kumfanya ashindwe Morocco. Akiendelea kuwepo alipo sio jambo baya pia.

Kwa sasa sisi yetu macho. Tunaipima tu akili yake. Ni akili zile zile za wachezaji wetu wazawa au yeye anaweza kuwa tofauti? Ni jambo la kusubiri na ingawa kama ukiniomba nicheze kamari nitakwambia Chama ana asilimia kubwa ya kurudi nchini. Tusubiri.