HISIA ZANGU: Ni wakati wa kumsaidia Samatta msalaba alioubeba

SIDHANI kama mambo yanaenda sawa kwa staa wa soka wa Taifa letu, Mbwana Samatta ‘Poppa. Sidhani kama yupo mahala ambapo yeye mwenyewe angeweza kudhania angekuwepo nyakati hizi. Hata hivyo, maisha ya soka yanakwenda kasi.

Kuondoka Aston Villa, kisha kwenda Fenerbahce ambako ilionekana angerudisha nyota, halafu kurudi tena Ubelgiji kucheza klabu ya Royal Antwerp sio jambo ambalo unaweza kusema limemsogeza mbele Samatta ambaye miaka michache iliyopita alikuwa lulu kwa klabu nyingi za Ujerumani, England na Ufaransa.

Nini kimetokea? Hatujui. Sidhani hata kama Mbwana mwenyewe anafurahishwa na habari hii ya kurudi Ubelgiji lakini katika maisha kuna mambo mengi yanatokea kwa haraka. Hakuna ajuaye vema lakini ukweli unabakia pale pale kwamba huku mwishoni mambo hayakwenda kama tulivyotarajia.

Umri? Hapana. Nasoma mitandaoni watu wanakazana kwamba Samatta alidanganya umri. Labda mwili unachoka. Kwa mtazamo wangu, hata kama Samatta alidanganya umri kidogo bado hawafikii wanasoka wengi wa Afrika Magharibi ambao wanadanganya umri kwa tofauti kubwa ya miaka.

Nilienda Ghana mwaka 2007 na nikakaa na washkaji vijiweni. Kule waliniambia kwamba kuna wanasoka wamedanganya umri kwa miaka 10 zaidi. Wanapofikisha miaka 32 ya Pasipoti ndio wanaanza kuchoka. Hata hivyo huwa wanacheza soka kwa kiwango cha juu kwa muda mrefu.

Ukiondoa Ubelgiji alikokaa miaka minne, Samatta hajacheza kwa kiwango cha juu kwingine alikokwenda. Alipaswa kudumu katika fomu yake kwa muda mrefu zaidi lakini haikuwa hivyo. Hakuwa na majeraha makubwa ya kutisha sana.

Vyovyote ilivyo, kuna mambo matatu katika suala hili la Samagoal. Kwanza kabisa lazima tuelewe kwamba Samagoal bado anazurura Ulaya na hajarudi nyumbani. Haijalishi kama unamuona amerudi nyuma kwa kurudi tena Ubelgiji. Samatta yuko Ulaya na bado ameendelea kuwa na hadhi ya Ulaya.

Ni tofauti na wachezaji wetu ambao wanakwenda nje na kurudi ghafla. Anakwenda katika klabu hiyo hiyo, anashindwa akiwa katika klabu hiyo hiyo, na anakatiwa tiketi ya kurudi nyumbani ghafla akiwa katika klabu hiyo hiyo. Samatta bado yupo Ulaya.

Kitu cha pili ambacho tunapaswa kukumbuka ni kwamba Samatta ameendelea kukusanya pesa. Kila anapokwenda huwa anapata pesa ya shukrani ya kusaini mkataba (signing –on fee) pamoja na ukweli kwamba mshahara wake unabakia kuwa juu kuliko wachezaji wengi wa Afrika Mashariki. Labda anazidiwa na Victor Wanyama tu wa Kenya.

Kitu kingine ambacho tunakumbushwa ni kutengeneza kina Samatta wengi. Tumemshushia mzigo mkubwa sana kijana huyu kutoka Mbagala ambaye aliamua kupambana kivyake mpaka kufika alipofika. Ni wakati sasa wa kumsaidia Samatta kubeba msalaba huu.

Husda dhidi yake imekuwa kubwa na tulipaswa kutengeneza mgawanyiko wa husda au mapenzi kwa mastaa wengine. Wakati fulani nilikuwa nasisitiza kwamba kama mwanadamu huenda pia Samatta akafeli mahali. Wenzetu wanakuwa na nafasi ya kuchepuka kwingine kama staa wao mmoja akifika mwisho au akishuka.

Uwezekano wa yai moja kuvunjika ni mkubwa lakini uwezekano wa mayai kadhaa kubaki salama pindi kapu linapoanguka bado unakuwepo. Samatta tulikuwa tumemshikilia kama yai moja tu. Kama tunadhani kurudi kwake Ubelgiji yai hilo limevunjika, basi hatuna mayai mengine.

Kama Ibrahim Ajibu angekuwa anacheza Stuttgart ya Ujerumani, Simon Msuva anacheza Napoli, Reliant Lusajo anacheza Montepellier ya Ufaransa, John Bocco anacheza PSV, huenda leo tusingekuwa na maumivu makali kwa kile tunachoona kushuka kwa Samatta.

Wanigeria wapo hivi. Kuna wachezaji ambao hata haifahamu kama wapo Ulaya na wanacheza timu za maana. Pale Leicester City tu wanao wawili. Wilfred Ndidi na Kelechi Iheanacho. Akifeli mmoja akaenda kwingineko atabakia mwingine.

Sisi wimbo umebakia kuwa Samatta tu. Kila siku tunacheza wimbo wa Samatta. Umekuwa mzigo mzito kwake. Hata katika timu ya taifa analazimika kubeba lawama nyingi tu. Anakuwa muathirika wa mafanikio yake mwenyewe. Anapofunga bao Simon Msuva unasikia Samatta anaandamwa kama vile Msuva sio Mtanzania.

Kitu kingine ambacho tunapaswa kukumbuka katika sakata hili ni ukweli kwamba licha ya kila kitu kilichotokea katika maisha ya soka ya Samatta, kama anashuka au hapana, bado Samatta atabakia kuwa alama ya soka letu kwa miaka yote iliyobaki.

Anaweza kutokea staa mwingine akafika mbali zaidi ya Samatta lakini ukweli ni kwamba Samatta ndiye aliyefanikisha ndoto zetu. Ndoto za kumuona Mtanzania wa kwanza akicheza kwa mafanikio makubwa barani Ulaya. Ni Samatta pekee.

Mtanzania wa kwanza kucheza Ligi Kuu ya England. Haitafutika. Mtanzania wa kwanza kufunga Ligi Kuu ya England. Haitafuika. Mtanzania wa kwanza kufunga bao Wembley haitafutika. Mtanzania wa kwanza kuzifunga Liverpool na Manchester City, tena zikiwa katika ubora wao, haitafutika. Haya yote ni alama.

Wakati mwingine unasoma mitandaoni na unahisi baadhi ya Watanzania hawamtendei haki Samatta. Kuna watu wanaandika kejeli. Unaishia kusononeka. Moyo unashikwa na ganzi. Samatta anastahili heshima. Amefanya watoto wetu waamini ndoto zao.