HISIA ZANGU: Mkude anavyoimarisha kikosi cha Uganda

Tuesday February 16 2021
lwanga pic
By Edo Kumwembe

MMOJA kati ya wachezaji bora uwanjani pambano la Ijumaa usiku kati ya As Vita dhidi ya Simba pale Kinshasa alikuwa Taddeo Lwanga. Alicheza vizuri sana na kutimiza majukumu yake. Ilituacha mdomo wazi hasa ukizingatia kwamba katika michuano ya kombe la mapinduzi wiki chache zilizopita hakuwa fiti kiasi hiki.

Taddeo alicheza katika nafasi ya staa wetu wa Tanzania, Jonas Mkude ambaye alisimamishwa kwa matatizo ya utovu wa nidhamu. Simba haikupata matatizo yoyote katika nafasi hiyo na waliondoka na ushindi muhimu ugenini. Inasemwa kwamba wachezaji wenyewe wa Simba hawataki Mkude acheze kwa sasa.

Mchezo wa mpira wa miguu unakwenda kasi kama ambavyo maisha yetu yanavyokwenda. Ghafla nafasi ya Mkude huyu Taddeo ameitendea haki. Kabla hata Taddeo hajafika tayari Simba waliiibabua Platinum ya Zimbabwe bila ya Mkude.

mkude pic

Kuna madhara ya aina mbili wakati mchezaji kama Mkude anapokuwa hachezi katika kikosi cha Simba. Hii nchi haina wachezaji wengi mastaa wanaocheza nje. Tunawategemea akina Mbwana Samatta, Simon Msuva, Thomas Ulimwengu waje waungane na mastaa wanaocheza timu kubwa nchini kwa ajili ya kutengeneza kikosi kizuri cha timu ya taifa.

Majuzi kocha wa zamani wa timu ya Taifa, Ettiene Ndayiragije alibebeshwa lawama zisizo zake katika uteuzi wa timu ya taifa. Achilia mbali kumuacha, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ ambaye wengi hatukuhafiki, ukweli ni kwamba wengine walistahili kuachwa kwa sababu hawapati nafasi katika vikosi vya timu kubwa.

Advertisement

Unatazamia mastaa wetu watambe katika timu kubwa za Simba, Yanga na Azam lakini ukweli ni kwamba nafasi muhimu zimeshikiliwa zaidi na wachezaji wa kigeni. Mfano mzuri ni pale Simba ambapo wamekuwa wakishiriki michuano ya kimataifa mara nyingi.

Ni wachezaji watano tu ndio ambao wamekuwa na uhakika wa kupata nafasi mara kwa mara. Jonas Mkude, John Bocco, Shomari Kapombe, Tshabalala na Aishi ambaye nafasi yake haina mchezaji wa kigeni. Hawa wana uhakika wa nafasi zao katika timu yenye wachezaji zaidi ya 30 kwa sasa.

Inapotokea mchezaji kama Mkude akakosekana katika kikosi kinachoanza Simba basi Taifa kama taifa linapata pigo. Simba inacheza mechi nyingi za kimataifa ambazo zinamuimarisha mchezaji kuliko Biashara Musoma. Kama Jonas anajipunguza katika nafasi yake halafu inakwenda kwa Mganda basi Uganda inaimarika zaidi.

Kwa sasa Waganda wana nafasi ya kumtazama Taddeo aking’ara na kuimarika zaidi katika mechi sita za michuano ya Ligi ya mabingwa barani Afrika. Ni faida kwao kwa kiasi kikubwa. Hawawezi kuchagua wachezaji 25 wakamuacha kikosini. Najua alishakuwepo katika kikosi cha The Cranes lakini sasa atajihakikishia nafasi yake zaidi.

Wakati huo huo Ndayiragije alishindwa kwenda na Mkude kule Cameroon kwa sababu ya matatizo yake ya nidhamu na klabu yake. Akaenda na Baraka Majogoro na bado Ettiene akalaumiwa. Angeenda na nani mwingine wakati tayari alishakuwa na Fey Toto kutoka Yanga?? Pale Azam wanaotamba kwa sasa ni akina Ally Niyonzima.

Wengine ambao angeweza kwenda nao ni akina Ibrahim Ajibu, Hassan Dilunga, Miradji Athuman. Ni wachezaji wazuri lakini wana mechi chache kwa msimu. Wanaotamba ni akina Clatious Chama, Luis Miquissone, Bernard Morrison na wengineo. Bocco alikuwa majeruhi lakini nafasi yake Simba inampa nafasi katika kikosi cha Stars bila shida.

Katika ubora wake na Manchester United yake, Sir Alex Ferguson alikuwa anaipa timu ya taifa ya England wachezaji hadi nane kwa mpigo. Gary Neville, Phil Neville, Nicky Butty, Paul Scholes, David Beckham, Andy Cole, Teddy Sheringham na Jonathan Greening.

Timu kubwa uipa timu ya taifa wachezaji wengi. Hata hivyo wachezaji hawa wanapaswa kucheza mara kwa mara na pia kuhepuka hiki ambacho Mkude anafanya kwa sasa. Bahati mbaya kwake na kwa taifa ni kwamba Simba wana uwezo mkubwa wa kipesa na wana mwamko wa kufanya vema katika michuano ya kimataifa. Mzawa akilegea wanaweka staa wa kigeni katika nafasi yake.

Usitazamie kwamba kama Shomari Kapombe akipotea basi Simba watalazimisha kuweka mzawa katika nafasi hiyo. Wanaweza kwenda Kenya au Uganda wakanunua mlinzi wa kushoto. Huu ndio utamaduni wa timu kubwa kwa sasa. Hauwezi kuwalaumu Simba.

Pale Yanga Injinia Hersi Said anatafuta majawabu kupitia kwa wachezaji wa kigeni tu akina Saido Ntibanzokonza. Alijaribu kwenda katika soko la ndani na kumnasa mshambuliaji, Waziri Junior baada ya kutamba na klabu ya Mbao lakini kinachoonekana muda si mrefu Waziri atatolewa kwa mkopo kwenda kwingineko.

Mshambuliaji wa mwisho wa kizawa kutamba Yanga alikuwa Simon Msuva. Inabidi tu tumuite Mshambuliaji hata kama alikuwa anatokea pembeni. Baada ya hapo sikumbuki Mshambuliaji wa kizawa wa Yanga aliyewahi kufikisha mabao 10 baada ya Msuva kuondoka.

Haya yanayoendelea kwa Mkude sio ya kufurahisha sana kwa taifa. Faraja pekee ambayo naipata ni ukweli kwamba kwa sasa nipo Mauritania na timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20 na nimezungukwa na makinda ambao wameshaanza kutamba nje ya nchi bila ya kugusa timu zetu kubwa.


Nitazungumza kitu kuhusu ujio wa kocha mpya wa timu ya taifa, Kim Poulsen wiki ijayo lakini ukweli ni kwamba kuna mastaa wengi watapoteza nafasi zao katika kikosi cha Kim na wengi ambao wapo hapa watapata nafasi. Hapa kuna akina Ally Msengi, Novatus Dismas, Tepsi Evance na wengineo kwa tabia za Kim lazima atawapenyeza katika kikosi cha kwanza.

Na kwa Mkude mwenyewe nadhani huu ni wakati wa kujitazama upya. Hizi timu nazifahamu kwa miaka mingi. Nafasi ambayo anaicheza kwa sasa imewahi kuchezwa na mastaa wengi ambao mashabiki wa Simba wameshawasahau. Kwanza kuna kundi kubwa ambalo haliwafahamu kabisa wachezaji hao.

Wako wapi akina Nico Njohole, Hamis Gaga, Mtemi Ramadhani, Michael Paul, Hussein Marsha, Rajab Msoma, Nico Bambaga na wengine wengi ambao walicheza katika nafasi hiyo. Wote hawa walipendwa na kuonekana mastaa wakubwa kuliko Jonas. Leo hakuna anayewazungumzia.

Soka ni mchezo wa muda mfupi. Unacheza, unachukua chako unawapisha wengine. Katika umri wa miaka 31 tu katika soka unahesabika kama mzee. Akina Jonas wasichezee umri. Wacheze soka wachukue pesa wafanye maisha mengine.

Kuna wachezaji wengi mastaa wa zamani ambao leo hawaamini kinachotokea. Walikuwa mastaa wakubwa wakazichezea nyakati na leo mkondo wa maisha umewapitia pembeni. Kazi yao ni kukumbuka enzi zao tu. Wanashindwa kurudisha umri nyuma.

Advertisement